INNOCENT A. NDAYANSE
(ZAGALLO)
0755 040 520 / 0653 593
546
UTANGILIZI
Judith ameingia
ndani ya Jiji la Dar es Salaam na Baraki anampangishia chumba cha gesti
Magomeni. Kunapokucha anamuaga kwamba anakwenda kazini lakini anamwambia wazi
kuwa ameoa ingawa anamtoa hofu asiwe na wasiwasi. Lakini baadaya Baraki
kuondoka Judith anagundua kwamba hana nguo, hivyo anatoka nje mapokezi kuomba
msaada. Je, nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako …
Judith hakutaka Swaumu awe rafiki wa karibu. Ni ugeni wake tu uliomfanya
aambatane naye. Kwa mtazamo wa haraka haraka alimwona Swaumu kuwa ni mwanamke
ambaye hajatulia. Yuko macho juu-juu. Maswali mengi, udadisi usiokoma. Kichwani
mwake hakumwona kuwa ni mtu anayefaa kwa ushirikiano wowote baina yao. Akaamua
kujihadhari naye, lakini kwa namna ambayo Swaumu mwenyewe hatamshtukia.
Jioni ilifika, usiku ukaingia. Baraki hakuonekana. Lakini ilipotimu saa
4 usiku Judith akamwona Yohana, mhudumu wa gesti akimjia na simu mkononi. “Simu
yako,” alimwambia huku akimpatia simu hiyo.
Alikuwa ni Baraki aliyepiga. Judith alipoipokea na kusikiliza, akapokea
taarifa kutoka kwa Baraki kuwa kwa siku hiyo hatafika kwa kuwa amekuta matatizo
katika familia yake.
“Kesho mchana tutawasiliana, sawa?” Baraki alimalizia.
“Sawa,” Judith alijibu kwa unyonge.
Usiku huo Judith akaamua kupiga pasi nguo zile alizonunua mchana kisha
akaziweka juu ya kiti kilichokuwa chumbani humo. Angeziweka wapi wakati hakuwa
hata na kijibegi kidogo? Baada ya hapo akalala. Usingizi haukumjia mapema.
Alikuwa akiwaza jinsi atakavyomudu kuishi katika nchi hiyo ngeni ilhali hana
hata ndugu huku pia ubalozi wa Rwanda ukiwa hauna taarifa yake. Akaendelea
kuwaza na kuwazua, jibu asilipate. Hatimaye akaamua kufumba macho na
kuulazimisha usingizi.
Dakika kumi baadaye alipitiwa na usingizi bila ya kujitambua, akazinduka
asubuhi. Sasa akapiga moyo konde na kuamua kutoka, aukague mji huo mkubwa wa
Dar es Salaam, labda huenda akapiga hatua moja nzuri katika kuhangaika huko.
Na sasa hakutaka kumshirikisha mtu yeyote hususan yule Swaumu ambaye
jana walikubaliana kuwa leo watakwenda wote kwenye maduka ya kubadilisha pesa.
Hata huyu mhudumu wa mapokezi naye hakupaswa kujua ni kipi kinachoendelea.
Hivyo, mara tu baada ya kuoga, alivaa nguo nyingine kisha akaondoka
kimya-kimya, machoni mwa wapita njia wenzake akionekana kuwa ni mwanamke wa
kuvutia. Ndani ya pochi ambayo nayo aliinunua jana kule sokoni, kulikuwa na
pesa kidogo za Tanzania, shilingi 9,000 zikiwa ni masalia ya zile 30,000/-
alizoachiwa jana na Baraki.
Alitembea huku akiwafuata watu wengine walioonekana kuwa na haraka,
wengi wao wakiwa wamevalia kinadhifu, hali iliyompa hisia kuwa huenda walikuwa
wakielekea kule ambako watu hupaita ‘mjini.’ Na wengi kati ya watu hao walikuwa
ni wanawake. Akaendelea kuwafuata.
Alikumbuka kuwa jana, wakati akiwa na Swaumu wakienda sokoni, aliyaona
mabasi madogo ya abiria yenye maandishi ubavuni: CITY BUS. Alitaka ayatumie
magari hayo kumfikisha huko panapoitwa ‘mjini.’ Akaendelea kuwafuata hao watu
wengi ambao baadhi yao walikuwa na mabegi madogo mikononi.
Robo saa baada ya kuianza safari hiyo, akajikuta akitokea Barabara ya
Rashid Kawawa. Akaivuka na kushika Barabara ya Chemchemi. Hatimaye alijikuta
akiibukia katika kituo cha daladala cha Magomeni Mapipa ambako alikuta idadi
kubwa ya watu wanaosubiri usafiri.
Daladala zilikuja, daladala zikaondoka. Yeye hakukurupuka kupanda.
Hakujua ni wapi alikopaswa kwenda na pia hakuwa na haraka. Akaendelea
kuwatazama abiria wakikimbilia kila daladala iliyoingia. Kuna zilizokwenda
Posta, nyingine Kariakoo, Muhimbili na hata Kivukoni.
Hatimaye aliamua kupanda daladala lililokwenda Posta, bila ya kupajua
huko Posta na kama atafanikiwa kutimiza malengo yake.
Aliteremkia Posta Mpya. Akavuka barabara bila ya kumuuliza mtu yeyote,
jambo lolote. Moyoni mwake alipanga kutafuta duka la kubadilisha pesa, lakini
aliamua kuwa makini kwa kuwa alijua fika kuwa thamani ya pesa alizonazo ni
kubwa hivyo kama watu wengine wangefahamu huenda ingekuwa hatari kwa upande
wake. Kuna vibaka, matapeli na majambazi. Yeyote kati ya hao anaweza kumfanyia
unyama kwa kujitwalia pesa hizo kwa njia moja au nyingine.
Akaifuata Barabara ya Jamhuri, akitembea kwa kujiamini kama vile ni
mwenyeji wa eneo hilo . Huko mbele akajikuta akikumbana na Mtaa wa Zanaki. Hapo
akasita. Sasa akajiwa na wazo la kuachana na Mtaa wa Jamhuri.
Akapinda kushoto na kufuata Mtaa wa Zanaki. Hakufika mbali, mara
akaliona duka lenye bango kubwa ukutani: SAKA BUREAU DE CHANGE. Akasimama na
kulitazama kwa sekunde chache kisha akalifuata. Dakika ishirini baadaye alikuwa
akitoka ndani ya duka hilo huku akiwa na pesa za Tanzania, shilingi 2,000,000
na ushei. Akasimama kando ya barabara akiwa hajui ni wapi alikopaswa kwenda na
kipi alichopaswa kufanya.
Akatulia kando ya barabara hiyo, nje ya duka hilo huku akiwa ameduwaa.
Dakika mbili baadaye akapata uamuzi wa kukodi teksi. Japo alikuwa mgeni, lakini
hakuwa mtu wa kushindwa kuzitambua teksi za jijini Dar, ambazo zilikuwa na
utambulisho rasmi. Akaipungia mkono teksi
ambayo ilimtii.
“Magomeni,” alimwambia dereva teksi akiwa ameshaingia garini.
“Magomeni ipi?”
Lilikuwa ni swali ambalo Judith hakulitarajia. Hakuijua vizuri Magomeni
na vitongoji vyake. Amwambie ni Magomeni ipi? Hata hivyo hakutaka kuudhihirisha
ugeni wake kwa huyu dereva. Akamjibu, “Nitakuelekeza mbele ya safari.”
Walipofika jirani na Bondeni Hotel, Judith akakikumbuka kile kituo cha
daladala alichopandia wakati anakuja Posta. Akamwambia dereva akate kulia.
Dereva akatii. Walipofika jirani na kituo hicho, akamwamuru asimame.
“Ni kiasi gani?”
“Elfu saba.”
Itaendelea kesho…
No comments:
Post a Comment