Dk. Salim Ahmed Salim
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim
Ahmed Salim amesema hakutarajia kusikia kauli za Rais Jakaya Kikwete
alizozitoa bungeni kukosoa Rasimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa
sababu walikuwa wanampa taarifa kwa kila hatua waliyokuwa wanafikia
kabla ya kutoa rasimu hiyo.
Dk Salim alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia kama hali ingefikia hatua
iliyofikia,” alisema Dk Salim na kuongeza: “Lakini Rais ana uamuzi wake
na anazingatia mambo mengine mengi.”
Akilihutubia Bunge maalumu la Katiba Machi 21,
mwaka huu Rais Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika
Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa
mengine hayawezekani kutekelezeka. Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa
Serikali. Alipinga waziwazi pendekezo la serikali tatu lililopendekezwa
na Tume na kuegemea katika muundo wa serikali mbili na idadi ya watu
walioupendekeza akionyesha kuwa ilikuwa ni ndogo.
Pia alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na
ubunge kama ilivyokuwa imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri
wanatakiwa kuwepo bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo lingine alilokosoa katika Rasimu ni
pendekezo la mtu kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita
mfululizo huku akisema baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa
vimekuwa na mambo mengi ambayo hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali
katika sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Katika mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema
baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya
chama chake ili aweze kufanya kazi hiyo kwa usahihi na alimtaarifu
Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais na katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba
Mpya haitapatikana, Dk Salim alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo
limeingizwa siasa na Bunge Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza
kuleta matatizo.
“Tuko katika hali ambayo si nzuri inayohitaji
uongozi thabiti, viongozi wote watambue umuhimu wa zoezi hili kwa lengo
la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho
ndicho kipimo cha uongozi kwa CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari
masilahi ya Watanzania wa leo, kesho na keshokutwa.
Nini kifanyike?
Dk Salim alisema jambo muhimu sasa ni pande mbili
zinazoshindana kuhusu idadi ya Serikali kutumia mwezi ujao wa Julai
kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao ili Bunge la Katiba liendelee bila
misuguano.
“Mwezi huu wa Julai ni muhimu sana, ni mwezi pekee uliobaki wa
kuwaweka pamoja wanaotofautiana. Kila jitihada zinatakiwa kufanyika ili
kuhakikisha Bunge Maalumu linakutana tena Agosti na wapinzani waliosusa
wanarejea ili kumaliza kazi hiyo kabla ya kutoa rasimu ya tatu kwa ajili
ya kura za maoni,” alisema na kuonya kuwa kuendelea na katiba ya sasa
kunaweza kuleta matatizo.
Neno ‘wasaliti wa Mwalimu Nyerere’ lamchefua
Aidha, Dk Salim ameeleza kusikitishwa na
kukatishwa tamaa na kauli za baadhi ya wanasiasa dhidi yake na wajumbe
wenzake wa Tume kwa kuwaita wasaliti na hasa kitendo cha kutilia shaka
uzalendo wao.
“Inakatisha tamaa sana. Mimi nina umri wa miaka
72, kati yake zaidi ya miaka 30 nimeitumikia nchi yangu, haiingii
akilini katika umri huu wa mwisho nianze kuisaliti nchi yangu,
inasikitisha sana kusikia eti hawa wasaliti wa Mwalimu Nyerere,”
alisema.
Dk Salim ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu
Nyerere (MNF), alisisitiza kuwa wajumbe hao wamekuwa wakishutumiwa na
watu wenye malengo yao, akitolea mfano kuwa hata Dk Mwesiga Baregu
aliwahi kushutumiwa na chama chake na kutakiwa ajitoe kwenye tume hiyo
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Itakumbukwa kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imekuwa ikishutumiwa na wanasiasa hasa kutoka CCM kutokana na
mapendekezo yake ya mfumo wa Muungano wa serikali tatu badala ya mbili
zinazoungwa mkono na chama hicho.
Kutokana na tofauti hiyo, wajumbe walio wengi wa
Bunge Maalumu la Katiba kutoka CCM waliamua kubadili baadhi ya vifungu
vya rasimu.
“Ni bahati mbaya sana binadamu unapotukanwa,
unatupiwa madongo, tunaonekana wapuuzi kwa kazi ya kukusanya maoni ya
wananchi, inaumiza sana,” alisema.
Kama ambavyo Jaji Warioba amesema mara nyingi, Dk
Salim aliitetea Rasimu ya Katiba, akisema kilichopendekezwa ndiyo picha
halisi ya maoni ya Watanzania.
Alisema Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi
yenye hoja nzito yakieleza hasa matatizo yao katika nyanja mbalimbali
kama afya, elimu, ardhi na mengine, ingawa hoja kuhusu muundo wa
Serikali ndizo zinaonekana kushikiwa bango na wanasiasa.
Alisema ushahidi wa watu waliohojiwa upo katika
maandishi, sauti na picha za video na idadi yao inatosha kuwakilisha
Watanzania wote.
“Wanasema hatukuhoji watu wengi, waliohojiwa ni
representative sample (sampuli), huwezi kuhoji Watanzania wote milioni
45,” alisema Dk Salim.
Alisema ni jambo la kushangaza kuwa mchakato umetekwa nyara na
wanasiasa lakini Katiba inastahili kuwa ya kitaifa ya Watanzania wote,
wenye vyama na wasio na vyama vya siasa.
Alisema hata kwenye tume, walikuwapo wajumbe zaidi
ya 12 ambao hawatokani na CCM, wakitoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi
na wote walikuwa na mawazo tofauti lakini waliamua kuyaweka kando na
kutoa rasimu inayotoa taswira ya mawazo na masilahi ya wananchi.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Dk-Salim-afichua-siri-ya-JK-na-Tume-ya-Warioba-/-/1597296/2366416/-/qlooj5/-/index.html
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Dk-Salim-afichua-siri-ya-JK-na-Tume-ya-Warioba-/-/1597296/2366416/-/qlooj5/-/index.html
No comments:
Post a Comment