Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 29 June 2014

HOTUBA YA MHE. WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA

PG4A9702
UTANGULIZI

a)    Masuala ya Jumla

Mheshimiwa Spika,
1.    Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutupatia uzima na afya hadi kufikia siku ya leo. Tumekuwepo hapa kwa takriban miezi miwili ambapo tumeweza kupokea na kujadili Taarifa za Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na Mwelekeo kwa mwaka 2014/2015 kwa Wizara mbalimbali na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015.


2.    Napenda kutumia nafasi hii ya awali kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri ya kutukuka ambayo wameifanya kwa nidhamu na ufanisi mkubwa, hususan wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta. Kipekee niwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Bajeti chini ya Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi kwa kazi yao nzuri ya kuchambua Bajeti ya Serikali na Sheria zinazoambatana na masuala ya Bajeti. Changamoto zilikuwa nyingi,   lakini   kwa   pamoja   tumekubaliana   na   kuafikiana. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kwenda kushirikiana na Wananchi katika utekelezaji wa Bajeti hii ili kuwaletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika,
3.    Katika kipindi hiki tukiwa hapa Bungeni, yapo matukio ya kusikitisha yaliyotokea ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walipoteza Wapendwa wao. Aidha, yapo matukio ya Kitaifa yaliyosababisha kupoteza maisha ya Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia nafasi hii kuwapa pole Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote waliofikwa na misiba na majanga mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wote waliopotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki.


Mheshimiwa Spika,
4.    Kipekee niwape pole ndugu, jamaa na marafiki waliopotelewa na ndugu zao na wote waliopata majeraha wakati kulipotokea Mlipuko wa Bomu pale Darajani, Zanzibar. Tukio hili la kusikitisha halipendezi kwa Nchi yetu. Niwaombe Wananchi wote kwa umoja wetu tushirikiane kuwa Walinzi katika maeneo yetu na kuwezesha kuwatambua mapema wale wote wenye nia mbaya ya kuharibu amani na utulivu katika Taifa letu.


b)    Shughuli za Bunge
Mheshimiwa Spika,
5.    Katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kufanya uchaguzi wa Wajumbe wa Wawakilishi kwenye Bodi za Taasisi, Mabaraza na Tume za Bunge. Napenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Terezya Luoga Huvisa, Mbunge wa Viti Maalum kuwa Mjumbe katika Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere; Mheshimiwa Goodluck Joseph Ole-Medeye, Mbunge wa Arumeru Magharibi kuwa Mwakilishi wetu katika Bunge la Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC-PF); Mheshimiwa Alphaxard Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara kuwa Mjumbe katika Tume ya Utumishi wa Bunge; Mheshimiwa Henry Daffa Shekifu,  Mbunge wa Lushoto; Mheshimiwa Sylvester Massele,  Mbunge wa Dole; na Mheshimiwa Zainab Rashidi Kawawa, Mbunge wa Viti Maalum wote kuwa Wajumbe katika Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Beatrice Matumbo Shelukindo, Mbunge wa Kilindi na Mheshimiwa Dkt. Maua Abeid Daftari, Mbunge wa Viti Maalum kuwa Wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi – Muhimbili; na mwisho nimpongeze Mheshimiwa Rashid Mfutakamba, Mbunge wa Igalula kuwa Mjumbe wa Bodi ya Utawala ya Chuo cha Ufundi Arusha. Tunaamini wote waliochaguliwa watatuwakilisha vyema katika Taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika,
6.    Pamoja na kupokea, kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, jumla ya Maswali 321 ya Msingi na 879 ya Nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 37 ya Msingi na 30 ya Nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.

7.    Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza Maswali ambayo yalilenga katika kuwaletea Wananchi maendeleo katika Majimbo yetu na kwa Taifa letu kwa ujumla. Vilevile, niwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wamefanya kazi kubwa ya kuandaa majibu na maelezo ya ziada katika kila Swali lililoulizwa.
c)    Miswada, Maazimio na Kauli za Serikali
Mheshimiwa Spika,
8.    Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali na kukamilisha hatua zote ni Muswada wa Sheria wa Fedha wa Mwaka 2014 [The Finance Bill 2014]; na Muswada wa Sheria wa Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2014 [The Appropriation Bill, 2014].

Mheshimiwa Spika,
9.    Miswada ifuatayo imesomwa kwa mara ya kwanza:

i)    Muswada wa Sheria wa Kufanya Marekebisho katika Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa 2014 [The Public Private Partnership (Amendment) Act, 2014] ulisomwa kwa mara ya kwanza.
ii)    Muswada wa Sheria ya Utawala wa Kodi 2014 (The Tax Administration Act 2014);
iii)    Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali [Miscellaneous (Amendments) Bill 2014]; na
iv)    Muswada wa Sheria Mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani [The Value Added Tax Act, 2014] unaopendekeza kufuta Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani.
d)    Maazimio
Mheshimiwa Spika,
10.    Vilevile, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge pia walikubali Maazimio ya Bunge kama ifutavyo:
i)    Azimio la kuridhia kubadilisha Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kuwa Taasisi inayojitegemea kiutendaji [Tengeru Institute of Community Development (Establishment Order, 2013)];

ii)    Azimio la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Fedha na Uwekezaji (SADC Protocal on Finance and Investment);
iii)    Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki [Protocol on the Stablishment of the East African Community Monetary Union].
Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa Spika,
11.    Katika Mkutano huu pia Mawaziri waliweza kutoa Kauli za Serikali zifuatazo:
i)    Kauli ya Waziri wa Maji Kuhusu Matatizo ya Uzalishaji Maji katika Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu;

ii)    Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Dengue;
iii)    Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Hali ya Mashine za Mionzi za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).
SERIKALI ILIVYOJIPANGA KUTEKELEZA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa Spika, 
12.    Wakati wa Mjadala wa Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015; Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na kutoa maoni na ushauri kuhusu Sera na Mikakati iliyopangwa na Serikali ya kuimarisha maandalizi na usimamizi wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali. Tunashukuru kwa michango hiyo mizuri ambayo Serikali inaahidi kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika,
13.    Napenda kutumia fursa hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge wengine kuwapongeza Mheshimiwa Stephen Masato Wasira (Mb.) – Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu; na Mheshimiwa Saada Mkuya Salum (Mb.) – Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha vizuri Hotuba za Mpango na Bajeti ya Serikali na pia kutoa maelezo mazuri ya ufafanuzi wakati wa kuhitimisha Hoja hii tarehe 24 Juni 2014.  Vilevile, nawapongeza Mawaziri wa Kisekta na Naibu Mawaziri kwa kuwasilisha Bajeti za Wizara zao kwa umahiri mkubwa. Pamoja na pongezi hizo, napenda kutoa msisitizo katika maeneo machache yafuatayo:

a)    Kuimarisha utengemavu wa Viashiria vya Uchumi Jumla
Mheshimiwa Spika,
14.    Ukuaji wa uchumi jumla ulio endelevu unahitaji mazingira ya uchumi jumla yaliyotengamaa na yanayotabirika. Mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukiongezeka na kufikia wastani wa Asilimia 7 kwa mwaka licha ya changamoto za upandaji bei za chakula na mafuta ya petroli katika soko la dunia. Ili kuweza kuendeleza ukuaji huu mzuri wa uchumi hapana budi kuendelea kutengamaza vigezo muhimu vya uchumi jumla, ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuimarisha Ukuaji halisi wa Pato la Taifa na kukua kwa kiwango cha juu zaidi ya Asilimia 7.0; kudhibiti kasi ya upandaji bei kwa kuhakikisha kwamba kiwango cha mfumuko wa bei ni chini ya tarakimu moja, ikiwezekana kisichozidi Asilimia 5; na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi. Kutengamaza viashiria hivi kutaihakikishia Nchi yetu kuendelea kwa kasi katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini hasa ule wa kipato kwa Wananchi wetu wengi wa Vijijini. Tayari dalili nzuri zinaanza kujitokeza, kwani kiwango cha Watanzania walio katika umaskini kimepungua kutoka Asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi Asilimia 28.2 mwaka 2012. Aidha, wastani wa Pato la Mwananchi kwa mwaka limeongezeka kutoka Shilingi 516,000 mwaka 2007 hadi Shilingi 1,003,000 mwaka 2012.

b)    Kuimarisha utaratibu na usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
15.    Mwaka 2014/2015, ni wa Nne wa utekelezaji wa Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016). Ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango unafikia malengo yaliyokusudiwa, Serikali imeiagiza Tume ya Mipango kuendelea na utaratibu wa kukagua na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya Maendeleo ya kipaumbele na ile ya kimkakati ili kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyokubalika na inalingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali (Value for money). Vilevile, kuhakikisha kuwa Miradi hiyo inakamilika kwa wakati; na pale ambapo kuna changamoto za kiutekelezaji kutoa ushauri stahiki Serikalini wa njia za kufanikisha miradi husika. Kwa upande wa miradi inayotekelezwa katika ngazi za Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Serikali itaimarisha mfumo wa ufuatiliaji kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana katika mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” (Big Results Now – BRN).

Mheshimiwa Spika,
16.     Sambamba na hatua hizo, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali imeanza kufanya mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016). Lengo la mapitio hayo ni kupima hatua ya utekelezaji wa mpango na kubaini changamoto pamoja na kuweka mikakati ya maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021).  Taarifa ya mapitio ya Nusu ya Kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016), itatolewa Desemba 2014. Madhumuni ya Taarifa hii ni kuhakikisha kuwa maeneo ambayo hayakutekelezwa ipasavyo na maeneo mapya yaliyoibuka (emerging issues) hususan  kuiandaa nchi kwa uchumi wa gesi na umuhimu wa kuimarisha ushindani wa Tanzania katika uzalishaji na biashara ya Kimataifa.

c)    Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
17.    Kutokana na michango mizuri ya mawazo ambayo Serikali imepokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta, Serikali imejipanga vizuri zaidi kuimarisha ukusanyaji wa Mapato katika Mwaka 2014/2015. Hata hivyo, ni vyema Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa kwenye eneo la mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali ya awamu ya nne imefanikiwa kuongeza mapato hayo kutoka Wastani wa Shilingi Bilioni 117 kwa mwezi Mwaka 2005/2006 hadi Wastani wa Shilingi Bilioni 800 kwa Mwezi mwaka 2013/2014.  Ongezeko hilo ni sawa na Asilimia 351. Lengo la Serikali ni kuongeza kasi zaidi katika eneo hili hata kuzidi kiwango hiki.

Mheshimiwa Spika,
18.    Pamoja na kuipongeza TRA kwa jitihada hizo, Serikali itafanyia kazi maoni mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ya kupanua wigo wa vyanzo vya Kodi pamoja na taarifa zilizopatikana zinazoonyesha kwamba bidhaa nyingi zinapita kwenye bandari bubu au vituo vya forodha bila kulipakodi stahiki.  Hatua za kupunguza misamaha ya Kodi zitaendelea kuimarishwa. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuielekeza Mamlaka ya mapato Tanzania kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuimarisha zaidi miundo ya ukusanyaji na ulipaji kodi. Ni muhimu, Mamlaka ya Mapato kurahisisha zaidi taratibu za kukusanya Kodi kwa kuweka na kutangaza kwa uwazi Kodi zinazostahili kulipwa kulingana na aina ya bidhaa na kuondokana na utaratibu wa kufanya makadirio au kutumia mwanya wa majadiliano na walipa kodi jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa rushwa na hivyo kuikosesha Serikali Mapato yake stahiki. Vilevile, naviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoa ushirikiano wa kutosha katika kudhibiti na kuzuia ukwepaji wa kodi na ushuru katika bandari zetu na maeneo ya mipakani.

Mheshimiwa Spika,
19.    Ni imani yangu kuwa tukiweka wazi kodi zinazopaswa kulipwa na  tukirahisisha taratibu za kukusanya Mapato ya Kodi hususan Bandarini na maeneo ya mipakani tutaweza kuweka mazingira mazuri ya kusaidia kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza urasimu na vishawishi vya kudai Rushwa. Nashauri, Mamlaka ya Mapato Tanzania ijipange upya vizuri ili kuhakikisha kwamba jukumu la kukusanya kodi linatekelezwa vizuri na kwa weledi mkubwa. Tukiwa na uhakika wa makusanyo ya mapato yetu ya ndani, naamini tutakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika,
20.    Kuhusu mapato yasiyotokana na Kodi hususan Maduhuli, uzoefu wa mwaka 2013/2014 umeonesha kwamba mwenendo wa ukusanyaji wa mapato hayo hauridhishi. Kwa mfano, kuanzia Mwezi Julai, 2013 hadi Aprili, 2014; Makusanyo yasiyotokana na Kodi yalifikia Shilingi Bilioni 425.5 ikiwa ni Asilimia 57 ya lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 741.1 kwa mwaka. Aidha, kwa upande wa mapato ya Halmashauri, makusanyo yalifikia Shilingi Bilioni 252.8, sawa na Asilimia 66 ya makadirio ya mwaka.  Mwenendo huo nao hauridhishi hivyo, ni lazima sasa tujipange upya kuhakikisha malengo yanafikiwa.

Mheshimiwa Spika,
21.     Ili kuimarisha ukusanyaji wa Mapato yatokanayo na Kodi na yasiyo ya Kodi (Non-Tax Revenue) na ya Halmashauri kuanzia Mwaka ujao wa Fedha, Wizara zenye jukumu la kukusanya Kodi na Maduhuli pamoja na makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali, Idara za Serikali zinazojitegemea kuanzia sasa zitatakiwa kuandaa Mpango Mkakati na Mpango Kazi (Action Plan) wa mwaka wa kukusanya Mapato na Maduhuli yao yote na kutoa taarifa bila kukosa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu makusanyo ya kila robo mwaka; ifikapo tarehe 15 ya mwezi unaofuata kila baada ya robo mwaka ambaye atawasilisha taarifa hiyo ya utekelezaji kwenye Kamati Ndogo za Baraza la Kazi la Baraza la Mawaziri zinazohusika kwa ajili ya tafakuri na maelekezo.

Mheshimiwa Spika,
22.    Tayari Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu ameagizwa kuandaa utaratibu mzuri wa kupata Taarifa za Makusanyo ya Mapato yatokanayo na Kodi na Maduhuli kutoka Wizara na Taasisi zote za Serikali zinazojitegemea. Aidha, naagiza kila Katibu Mkuu wa Wizara, Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi, Wakala za Serikali na Idara za Serikali  zinazojitegemea kuhakikisha zinakusanya Mapato kulingana na Mpango Mkakati wa Mpango Kazi na kuwasilisha Taarifa hizo kwa wakati.

MISAMAHA YA KODI
Mheshimiwa Spika,
23.    Eneo la misamaha ya Kodi limekuwa likilalamikiwa na Wananchi wengi na Waheshimiwa Wabunge kwa muda mrefu. Katika eneo hili, ni vyema Wananchi na Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa kuna misamaha ya Kodi ya aina mbalimbali.  Kundi la Kwanza ni misamaha ya Kodi inayotolewa kwa Washirika wetu wa maendeleo wanaotoa misaada katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi linajumuisha pia misamaha ya bidhaa za Sukari, Mchele, Mafuta ya Diseli, n.k.  Kundi la Pili ni misamaha ya Kodi kwa Asasi zisizo za Kiserikali na Mashirika ya Dini yanayotoa huduma kwa Wananchi pasipo kutegemea kupata faida.  Kundi la Tatu ni misamaha ya Kodi ambayo hutolewa ikiwa ni Mkataba wa kuvutia Uwekezaji Nchini.  Kwa kawaida Misamaha ya aina hii hutolewa kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ili kuvutia Uwekezaji katika Miradi Mikubwa ambayo tunategemea kuwa manufaa yatakayopatikana kutokana na uwekezaji huo yatakuwa makubwa sana ikilinganishwa na msamaha wa kodi uliotolewa. Kwa mujibu wa Takwimu za hivi karibuni za Mamlaka ya Mapato Tanzania za Mwaka 2012/2013 zinaonesha kuwa Misamaha ya Kodi ya bidhaa za mtaji kwa Wawekezaji waliopewa Hati za Usajili na Cheti cha hadhi ya Uwekezaji mahiri kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ni Asilimia 19.7 ya Misamaha yote.

24.    Kwa mfano, utafiti uliofanywa na Kituo cha Uwekezaji TIC mwaka 2012 kwa Makampuni Makubwa 50 ya Uwekezaji yaliyosajiliwa na TIC, kiasi kilichowekezwa katika kipindi cha miaka mitano (2005 – 2010), ni Shilingi Trilioni 1.7 ambapo katika uwekezaji huo, Makampuni hayo yalilipa Kodi Shilingi Trilioni 1.1. Aidha, Makampuni hayo yalitoa ajira 981,000 za moja kwa moja na 112,070 zisizo za moja kwa moja. Misamaha ya Kodi iliyotolewa kwa Makampuni hayo ni Asilimia Saba (7) tu ya Kodi yote iliyolipwa na Makampuni hayo. Misamaha kwa makundi  mengine ikiwemo Miradi ya Wahisani mbalimbali na Asasi zisizo za Serikali (NGOs), n.k ni Asilimia 38.6; na Misamaha kwa Sekta Binafsi ni Asilimia 23.8 ya Misamaha yote iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mheshimiwa Spika,
25.    Serikali inatambua kuwa bado tuna kazi ya kubwa ya kuhakikisha kwamba misamaha ya kodi inayotolewa kwa Wawekezaji na Walengwa wengine Nchini inatumika vizuri katika miradi iliyokusudiwa, na si vinginevyo. Kwa mfano, msamaha wa kodi uliotolewa kwenye mafuta ya dieseli hatutarajii mafuta hayo yaingie sokoni badala ya kutumika kwenye mradi wa uwekezaji uliokusudiwa. Hivyo, kutokana na umuhimu wa kuvutia uwekezaji Nchini, misamaha ya kodi iiliyoidhinishwa na Bunge Kisheria itaendelea kutolewa kwa Wahusika. Nitoe wito  kwa wote watakaopata misamaha hii kuwa waadilifu  na kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote atakayetumia vibaya misamaha hii. Serikali kwa upande wake itaimarisha zaidi usimamizi wa matumizi ya misamaha hii na itahakikisha inatumika kwa lengo lililokusudiwa.

KUONDOA URASIMU KATIKA VITUO VYA FORODHA
Mheshimiwa Spika,
26.    Mwezi Februari, 2014 nilipokutana na Wafanyabiashara waliotaka kugoma kutumia Mashine za kisasa za kutoa Risiti (Electronic Fiscal Devise-EFD) walinieleza kwamba moja ya eneo linalowasumbua ni urasimu mkubwa katika maeneo mengi ya Vituo vya Forodha Mipakani na Bandarini hasa Dar es Salaam. Katika  Vituo  hivyo  vya Forodha walisema zipo Taasisi nyingi za  Serikali  zinazofanya  ukaguzi wa mizigo inayoingizwa Nchini na ile inayotoka kwenda Nje ya Nchi. Miongoni mwa Taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Idara ya Uhamiaji; Jeshi la Polisi; Wakala wa Viwango (TBS); Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA); Mkemia Mkuu wa Serikali; Tume ya Nguvu za Atomiki; Idara ya Misitu na Nyuki; Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Mimiea na Wadudu (TPRI); Kitengo cha Afya ya Mimea cha Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; na Kitengo cha Afya ya Mifugo cha Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika,
27.     Serikali iliweka Taasisi nilizozitaja hapa kwa nia njema ya kusimamia vizuri na kudhibiti uingizaji na utoaji wa mizigo bandarini na bidhaa zinazopitishwa katika mipaka ya Nchi yetu. Hata hivyo, baadhi ya Watendaji wasio waaminifu wanatumia mwanya huo kuwalazimisha Wafanyabiashara kutoa fedha zao bila kupata risiti eti kwa ajili ya kusaidia mizigo kupitishwa kwa urahisi. Aidha, nimeelezwa kuwa baadhi ya Watendaji wanatumia nafasi zao kuongeza urasimu usio na lazima ili kudai rushwa, jambo ambalo linaongeza gharama kwa Wafanyabiashara na kuleta athari za kuchelewesha utoaji wa mizigo bandarini na kuathiri sifa za bandari zetu. Naagiza Wizara husika kufuatilia utendaji kazi wa Vyombo hivyo kwa karibu na kushughulikia kwa haraka malalamiko mbalimbali na kupata ufumbuzi wa tatizo la urasimu katika Vituo vya Forodha. Yapo Makampuni ya Mawakala yapatayo 527 yanayofanya kazi za Mawakala wa kutoa bidhaa Bandarini. Tunayo taarifa kuwa, Utitiri wa Makapuni hayo nao umekuwa chanzo kikubwa cha rushwa na ukwepaji Kodi. Serikali haikubaliani na aina hii ya Utendaji wa Makampuni hayo. Utendaji huo uachwe sasa. Navitaka Vyombo husika kufuatilia kwa karibu sana mienendo ya Makampuni yote ya Mawakala wa kutoa bidhaa Bandarini na kuchukua hatua stahiki.

Mheshimiwa Spika,
28.    Pamoja na changamoto zilizopo katika bandari zetu, napenda kutumia fursa hii kumpongeza Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb.) kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia kwa karibu uboreshaji wa utendaji katika Mamlaka ya Bandari; hasa kupunguza muda wa kutoa mizigo bandarini kutokana na kuweka utaratibu wa kufanya kazi kwa saa 24. Ninamtaka aongeze juhudi zaidi ili kuimarisha utendaji kazi katika eneo hili ili kuongeza sifa kwa Bandari zetu.

UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW-BRN)
Mheshimiwa Spika,
29.    Utekelezaji wa mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa umeendelea vizuri, na licha ya matatizo ya upatikanaji wa fedha matokeo yake yameanza kuonekana kama ilivyoainishwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta husika walipowasilisha Hotuba zao katika Mkutano huu. Uzoefu tulioupata katika kipindi hiki, ni kwamba upatikanaji wa matokeo makubwa kwa muda mfupi unawezekana, ilimradi tuwe tumechagua vipaumbele vyetu kwa usahihi, tunafuatilia utekelezaji kwa karibu,   na   kutanzua   changamoto   mara   zinapojitokeza. Napenda kutumia fursa hii tena kuwashukuru Wadau wote wa Maendeleo waliowezesha kupata matokeo haya. Natoa wito kwa Viongozi na Watendaji katika ngazi zote tuendeleze kasi na umakini wa kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele ya Mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” ili tuweze kufanikiwa zaidi katika kipindi kijacho.

Mheshimiwa Spika,
30.    Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba katika Mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha mchakato wa Ajira za nafasi wazi za Watumishi wa Taasisi ya Kuratibu na Kusimamia Mfumo wa Tekeleza sasa kwa Matokeo Makubwa kilichopo Ofisi ya Rais, yaani President’s Delivery Bureu (PDB). Vilevile, Serikali itaimarisha Vitengo na Taasisi zote zinazosimamia mfumo huu, ikiwa ni pamoja na kukamilisha uundaji wa Vitengo na Kamati za kuratibu utekelezaji katika Wizara na Taasisi zinazotekeleza Programu ya Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara Nchini. Serikali pia  itaandaa na kutangaza matokeo ya utekelezaji wa mfumo huu katika mwaka wake wa kwanza wa 2013/2014, baada ya kuhakikiwa na jopo huru la Kimataifa. Hatua hii inalenga kukamilisha mfumo wa uwajibikaji ambao ni chachu muhimu ya mafanikio ya mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Vilevile, Wizara zingine, Mikoa na Halmashauri zote zinaendelea kuhimizwa kutumia mfumo huu katika kuchambua, kupanga, na kutekeleza mipango na miradi yake yote ya maendeleo kwa kuzingatia mfumo huu wa Matokeo Makubwa Sasa.
KILIMO

Hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini
Mheshimiwa Spika, 
31.    Hali ya upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia albaki ya mavuno ya msimu uliopita na matarajio ya mavuno mazuri katika msimu wa kilimo wa 2013/2014 ambayo uvunaji wake umeanza katika baadhi ya maeneo. Aidha, kufuatia mwenendo mzuri wa hali ya unyeshaji wa mvua katika msimu wa 2013/2014 katika maeneo mengi ya nchi, kuna matarajio ya uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na hivyo upatikanaji mzuri zaidi wa chakula kwa mwaka 2014/2015.

Mheshimiwa Spika, 
32.    Hali ya akiba ya chakula katika Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ni nzuri. Mwanzoni mwa mwaka 2013/2014 Akiba ya Chakula ilikuwa Tani 25,452.6 na baada ya kununua Tani 219,377.3, akiba ilifikia Tani 244,829.9. Hadi kufikia tarehe 4 Juni 2014 Serikali ilitoa Jumla ya Tani 54,845.0 kama chakula cha Msaada na Maafa ikiwemo njaa, mafuriko na operesheni mbalimbali na kubaki na akiba ya Tani 189,984.9. Aidha, Serikali ina mpango wa kuuza Tani 75,000 ili kuacha Maghala wazi kwa ajili ya mazao mapya yatakayonunuliwa katika msimu mpya wa 2014/2015 na hivyo, kuyaacha Maghala ya Serikali yakiwa na Akiba ya Tani 114,984.9 za Mahindi ifikapo Julai, 2014. Katika mwaka 2014/2015 Serikali itanunua Tani 160,000 za Nafaka na kuzijumlisha zile za akiba kutoka msimu wa 2013/2014, hivyo kuwa na hifadhi ya jumla ya Tani 274,984.9 za Nafaka.

Mheshimiwa Spika, 
33.    Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu na Wananchi kuwa Serikali kwa mara ya kwanza imefikia uamuzi wa kununua Mpunga na kuhifadhi katika Maghala ya Taifa kama Chakula cha Akiba. Uamuzi huu umefikiwa kwa kuzingatia kuwa baada ya Serikali kuruhusu wafanyabiashara kuingiza mchele kutoka nje ya Nchi kufidia pengo la upungufu wa mchele hapa Nchini, baadhi ya wafanyabiashara hao waliendelea kuingiza mchele hata baada ya muda wa vibali vyao kuisha hivyo kuwafanya Wakulima kukosa soko la mpunga baada mavuno kuongezeka. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa katika msimu huu wa mavuno, Serikali imedhamiria kuanza na hifadhi ya Tani 10,000 za mpunga kwa lengo la kujiridhisha kama hifadhi ya mpunga haitakuwa na matatizo. Baada ya kujiridhisha, katika misimu inayofuata, Serikali itaongeza kiasi cha Mpunga utakaohifadhiwa na Serikali kwa nia ya kuziba pengo la upungufu wa mchele iwapo hali hiyo itatokea badala ya kutegemea Wafanyabiashara tu kuagiza Mchele kutoka nje ya Nchi. Nitumie fursa hii kuwahimiza wakulima kuongeza uzalishaji wa zao hili kwa vile sasa Serikali imeamua kuhifadhi Mpunga kama ilivyo kwa Mahindi na Mtama. Aidha, niwaahidi Wananchi kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya kuhifadhi mpunga katika Maghala ya Taifa ili kuwawezesha Wakulima wengi kupata soko kama ilivyo kwa mazao ya Mahindi na Mtama. Ninaagiza kuanzia sasa Taasisi zote zinazotoa vibali vya kuingiza sukari, mchele na ngano kutoka nje ya nchi kuhakikisha kuwa Wafanyabiashara wenye vibali vinatumika tu kwa muda uliopangwa.

Mheshimiwa Spika, 
34.    Naagiza pia kwa Wakala wa Hifadhi Taifa ya Chakula kuanza kununua nafaka kwa wakati ili wakulima waweze kunufaika na bei nzuri zitakazotolewa. Ni matarajio yangu kuwa Wakala pamoja na kununua nafaka kwa bei ya soko na kupitia vituo vya ununuzi, vikundi vya wakulima na mawakala, watahakikisha kuwa wakulima hasa wa mahindi wanapata si chini  ya  Shilingi  500  kwa  kilo ambayo ni bei ya msimu uliopita ili kuwawezesha kurudisha gharama za uzalishaji. Aidha, nawasihi Wakulima wasikubali kuuza mazao yao chini ya bei hiyo. Lengo ni kuwawezesha kurejesha gharama za uzalishaji. Bei elekezi kwa nafaka nyingine pia zitangazwe kwa kuzingatia gharama za uzalishaji mapema kabla ya msimu wa ununuzi kuanza. Nichukue fursa hii kuwasihi Wananchi hasa katika Kanda zile wanazouza nafaka iliyo na ubora hafifu hasa uchafu kujirekebisha na kuacha tabia hiyo mara moja, kwani kwa kufanya hivyo wanavuruga jitihada za Serikali za kusaidia Wakulima Wadogo kuinua maisha yao.

Mazao ya Asili ya kuingiza Fedha za Kigeni
Mheshimiwa Spika, 
35.    Nchi yetu inayo mazao yanayotuingizia fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Tumbaku n.k. Kwa madhumuni ya Hotuba yangu ya leo nimeona nizungumzie uendelezaji wa mazao ya Korosho na Pamba. Kutokana na bei ya mazao haya kuendeea kutegemea bei katika Soko la Dunia, Wakulima wetu wameendelea kupata bei za chini na zisizokuwa na uhakika kila msimu wa mauzo unapowadia. Hivyo, ni vyema sasa tukazingatia umuhimu wa kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa soko la ndani linakuwa la uhakika kwa mazao haya. Aidha, Serikali imekuwa ikiweka mikakati ya kusindika mazao ya Pamba na Korosho hapa Nchini kwa lengo la kuyaongezea thamani na kuongeza Tija katika uzalishaji kwa eneo. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali sasa imejikita katika utafiti wa mbegu na miche bora pamoja na kufufua viwanda ambavyo vitatumia malighafi zitokanazo na mazao haya hapa Nchini.

Mapango wa kufufua Viwanda vya Korosho
Mheshimiwa Spika, 
36.    Uzalishaji wa korosho umeendelea kuwa tegemeo kubwa la wakulima wa Mikoa ya Kusini  ya Lindi na Mtwara na pia Mkoa wa Pwani. Kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali za kufufua zao hili, katika msimu wa 2013/2014, uzalishaji wa Korosho umeongezeka hadi kufikia Tani 127,939.4 ikilinganishwa na Tani 121,703.8 kwa msimu wa 2012/2013. Pamoja na ongezeko katika uzalishaji, mchango wa zao hili kwa Pato la Mkulima na Taifa umekuwa mdogo kutokana na Taifa kuendelea kuuza korosho ghafi nje ya Nchi kwa zaidi ya Asilimia 90 hivyo, kuikosesha Nchi mapato na faida nyingine nyingi kwa wakulima. Hali hii imetokana na Wawekezaji wa Viwanda 12 vya kubangua korosho vilivyojengwa na Serikali miaka ya 1980 na kubinafsishwa mwaka 2004 kushindwa kuvifufua viwanda hivyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa mitaji na kuendelea kutumia Teknolojia iliyopitwa na wakati.

Mheshimiwa Spika, 
37.     Napenda kulijulisha Bunge lako na wananchi kwamba kutokana na changamoto hizo, mwezi Februari, 2014 niliitisha Kikao kilichohusisha baadhi ya Watendaji Wakuu wa Serikali, baadhi ya Wamiliki wa Viwanda vya kubangua Korosho na baadhi ya Taasisi ya Fedha kujadili mikakati ya kufufua viwanda vya kubangua korosho hapa nchini. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau hao iliamua ifanyike tathmini ya gharama na mikakati ya kufufua Viwanda vya kubangua korosho hatua kwa hatua na kwa kuanzia Serikali kwa kushirikiana na Wamiliki itaanza kufufua Viwanda vinne (4) vyenye uwezo wa uzalishaji (Installed Capacity) wa kati ya Tani 5,000 hadi 10,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, 
38.    Kwa kuanzia Serikali iliamua tathmini ifanyike kwa viwanda vya Newala-I; Masasi; Lindi Farmers kilichopo Nachingwea; na Kiwanda cha Kampuni ya BUCCO kilichopo Lindi kwa ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni ya Oltremare ya Italy ambayo ina uzoefu mkubwa duniani katika utengenezaji wa mashine za usindikaji wa Korosho. Kampuni hii ndiyo iliyojenga baadhi ya viwanda vya kubangua korosho hapa nchini kikiwepo Kiwanda cha TANITA. Tathmini hii itaangalia hali ilivyo katika masuala ya kiufundi, usindikaji na miundombinu; uwezo na madeni ya Kifedha; Masuala ya Kisheria kuhusu Mikataba mbalimbali iliyowekwa na wawekezaji hawa, Mfumo wa upatikanaji wa malighafi; na uwezo wa Rasilimali watu wa viwanda hivyo.

Mheshimiwa Spika, 
39.    Tathmini ya awali ya gharama za kufufua viwanda hivyo vinne iliyofanywa na Kampuni ya Oltremare kwa kushirikiana na Kampuni ya Agrofocus ya hapa Tanzania ilibaini kuwa kuna njia mbili zinazoweza kutumika: Kwanza, iwapo Serikali itaamua kuvifufua Viwanda vya Newala 1; Masasi na Lindi kwa kuvijengea uwezo wa kila kimoja kubangua Tani 15,000 kwa mwaka, pamoja na cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa mwaka; kwa pamoja zitahitajika jumla ya Paundi 31,280,690. Pili, iwapo Serikali itaamua kuvifufua viwanda vya Newala 1, Masasi na Lindi kwa kuvijengea uwezo wa kila kimoja  kubangua Tani 22,000 kwa mwaka, na Kiwanda cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa mwaka, kwa pamoja zitahitajika jumla ya Paundi 44,185,022. Hata hivyo, kabla ya kuweka mikakati ya kupata fedha hizo, Serikali imeamua kupeleka kikosi kazi chake kutathmini tena gharama hizo na kuzilinganisha na hizo za awali kwa nia ya kushirikiana na vyombo vya fedha na Kampuni ya Oltremare ya Italy kufufua viwanda hivi. Aidha, Kampuni ya Oltremare ya Italy imekubali kutoa mafunzo kwa wazawa kuhusu utawala na uendeshaji wa viwanda hivyo pindi vitakapofufuliwa; na kuisaidia Tanzania kupata Soko la Korosho zitakazobanguliwa. Naamini kabisa ufufuaji wa viwanda hivi utasaidia kuboresha teknolojia, kuongeza ufanisi, ajira na mapato ya Serikali na bei ya korosho ghafi kwa mkulima badala ya kutegemea bei ya Soko la Dunia pekee.

Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika, 
40.    Zao la Pamba lina mchango mkubwa katika kukuza Uchumi wa Nchi yetu na kuondoa umaskini kwa zaidi ya Wakulima 400,000 na wategemezi wao katika Mikoa takriban 15 hapa Nchini. Hata hivyo, bado Kilimo chake kinakabiliwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na tija ndogo, matumizi kidogo ya teknolojia za kisasa na zana duni. Aidha, kuna huduma duni za ugani na utafiti, kukosa mitaji na soko la uhakika; migogoro baina ya wakulima na wafanyabiashara, na Uhaba wa Viwanda vya kuongezea Pamba thamani.

Mheshimiwa Spika,
41.    Katika msimu wa 2011/2012 Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Gatsby Charitable Foundation ya Uingereza chini ya Ufadhili wa Lord David Sainsbury ilianza majaribio ya Mfumo wa Kilimo cha Pamba cha Mkataba kupitia Program ya Kuendeleza zao la Pamba katika Mkoa wa Mara na Wilaya za Bariadi na Kibondo kwa madhumuni ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto nilizoeleza punde. Matokeo ya majaribio yalionesha kuwa, uzalishaji uliongezeka kutoka Kilo 398 kwa ekari hadi Kilo 558 kwa ekari; na ubora wa pamba uliongezeka hadi kufikia Asilimia 78 kutoka Asilimia 48 za awali.

Mheshimiwa Spika,
42.    Baada ya Serikali kupitia Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuanza mikakati ya kusimamia kilimo cha Mkataba cha pamba, takwimu za mwezi Mei, 2014 zinaonesha kuwa Wilaya Saba (7) katika Kanda ya Magharibi zilishiriki katika Kilimo cha Mkataba. Aidha, takriban wakulima 90,000 wamenufaika na mikopo ya Pembejeo ya  Kilimo cha Mkataba msimu huu kupitia Wachambuzi takriban 15, ikilinganishwa na wakulima 30,000 katika msimu uliopita. Vilevile, takwimu hizo zinaonyesha wakulima 140,000 ndani ya kilimo cha mkataba wamelima zaidi ya ekari 400,000; na kwamba katika msimu huu kati ya Makampuni 42 ya pamba, Makampuni 26, yameshiriki kwenye kilimo cha mkataba ikilinganishwa na Makampuni 12 yaliyoshiriki msimu uliopita. Kwa ujumla wakulima wengi wameelezea kunufaika kutokana na Kilimo cha Pamba cha Mkataba hasa kutokana na kuongezeka kwa kipato.

Mheshimiwa Spika, 
43.    Pamoja na mafanikio hayo, yaliyojitokeza changamoto kadhaa ikiwepo ya baadhi ya Wakulima kuuza na Makampuni kununua pamba nje ya mkataba jambo lililokwamisha Mfumo wa kurudisha mikopo ya pembejeo katika maeneo yaliyolimwa kwa mfumo wa Kilimo cha Mkataba. Hivyo, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwenye zao la pamba katika maeneo yote yanayolimwa pamba. Lengo ni kushirikisha Wadau wengine, kuainisha na kupata ufumbuzi wa kasoro zilizojitokeza katika misimu iliyopita; kupanga mikakati ya utekelezaji; kuweka utaratibu mzuri wa kulinda uwekezaji wa wachambuaji na pia kulinda haki za wakulima kwa kuzingatia mikataba inayowekwa kati ya wakulima na wachambuaji. Nitumie fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais kwa Viongozi kusimamia kikamilifu kazi hiyo ili Wakulima wanufaike na Mfumo huu wa Kilimo cha Mkataba. Njia nyepesi ya kutoa elimu juu ya Kilimo cha Mkataba ni kutumia Mashamba Darasa na Mashamba ya Mfano. Nawaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri wasimamie vema na kwa karibu utaratibu huu.

Mheshimiwa Spika, 
44.    Kutokana na tatizo lililojitokeza la baadhi ya wakulima wa pamba kuuziwa Tani 1,088 za mbegu ya pamba kipara ambayo haikuota kutoka Kampuni ya Quton, kwa niaba ya Serikali napenda kuwapa pole Wakulima hao. Kama Serikali ilivyoahidi hapo awali, tumesitisha malipo ya Shilingi Bilioni 1.7 za ruzuku kwa Kampuni ya Quton. Aidha, Serikali inaitaka Kampuni ya Quton kutorudia makosa haya katika siku zijazo. Maafisa Ugani wasimamie kwa karibu upandaji wa mbegu hizi wakati wa msimu kwa kutoa elimu stahiki.

Mheshimiwa Spika, 
45.     Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili la mbegu hafifu, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaendelea na juhudi za kukaribisha uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbegu bora kipara kutoka ndani na nje ya Nchi ili kuweka mazingira ya ushindani ambao utaleta ubora zaidi. Aidha, Taasisi zinazohudumia zao la pamba ziangalie kama kuna uwezekano wa kupata mbegu za pamba hata kutoka nje ya Nchi kwa kuzingatia masuala ya ubora na unafuu wa bei. Nichukue fursa hii kuwakumbusha Bodi ya Pamba na wagani wa zao la pamba kuhakikisha kuwa ubora wa mbegu (germination percentage) unafanyiwa tathmini kabla mbegu hazijagawiwa kwa wakulima. Aidha, Wakulima waelimishwe manufaa ya kutumia Mbegu Kipara kwamba wakati wa kuziandaa zinawekewa viuatilifu ambavyo vinaua vimelea na wadudu ambao wanatokana na mavuno ya msimu uliopita, hivyo kupunguza uwezekano wa pamba inayotokana na mbegu hizi kupata magonjwa na wadudu mapema ikilinganishwa na mbegu za manyoya.

46.    Mbegu Kipara zinaweza pia kutumika na mashine za kupandia (planter) hivyo kuwezesha mimea ya pamba kuota katika mstari na kwa nafasi stahili na kumwezesha mkulima kupata mimea mingi kwa ekari (plant population) kama inavyoshauriwa kitaalamu miche 22,222, hivyo kuongeza tija kwa ekari tofauti na mbegu za manyoya. Naamini kupitia ushirika na Kilimo cha Mkataba Wakulima wataweza kuungana kupata planter ili kupunguza sulubu ya jembe la mkono wakati wa kupanda. Ninaiagiza Bodi ya Pamba iendelee kusimamia zoezi la wakulima waliochaguliwa kuzalisha mbegu bora kwa Kampuni ya Quton ili kuwezesha ongezeko la upatikanaji wa mbegu bora kwa Wakulima.
Mheshimiwa Spika, 
47.    Pamoja na changamoto zinazoikumba tasnia ya pamba na hasa Kilimo cha mkataba cha pamba, nichukue fursa hii kuwasihi wakulima wa pamba ambao hawajajiunga na mfumo huu  kufanya  hivyo  kutokana  na  mafanikio yaliyopatikana kwa wale waliojiunga  tayari.  Napenda  kuwakumbusha  Wagani  wa Pamba kusimamia ipasavyo suala la usafi wa pamba inayouzwa na wakulima ili wakulima wapate bei nzuri. Aidha, kutokana na kilimo cha mkataba katika zao la tumbaku na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani kwa zao la korosho kuwanufaisha sana wakulima wa mazao hayo, niwatake viongozi wote wanaohusika na uimarishaji wa zao la pamba kuimarisha kilimo cha pamba na suala la kilimo cha pamba cha mkataba ili kuweka utaratibu utakaomfanya mkulima kuuza pamba kwa yule aliyemwezesha kupata pembejeo na kwa kutumia mfumo wa Ushirika.

Mheshimiwa Spika, 
48.    Kupitia Mkutano Mkuu wa Wadau wa Sekta ya Pamba wa tarehe 4 Julai 2013 Jijini Mwanza, wajumbe waliiomba Serikali kusimamia uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya zao la pamba na utengenezaji wa bidhaa za pamba hapa Nchini. Nakubaliana na azimio hilo kwa sababu hatuwezi kama nilivyoeleza kwa zao la Korosho, kuendelea kusafirisha sehemu kubwa ya pamba inayozalishwa hapa nchini kama malighafi kwa vile hakutainufaisha nchi na hata wakulima. Hivyo, narudia tena wito wangu kuitaka Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kuhimiza uwekezaji katika viwanda vingi vya kusindika na kutengeneza bidhaa za pamba hapa Nchini badala ya kuuza pamba ghafi. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu na Wananchi kuwa, katika kujiandaa na Raslimali Watu kwa ajili ya Viwanda vya Nguo hapa Nchini, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kimewezeshwa kuanzisha Kozi za Shahada mbili za Uhandisi wa Viwanda vya Nguo na Ubunifu, na Vyuo vya VETA vinatoa mafunzo hayo kwa Kada za Chini.

Mheshimiwa Spika, 
49.    Kwa kuwa msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2014/2015 umeshazinduliwa tangu tarehe 18 Juni, 2014, ninawasihi Wakuu wa Mikoa yote inayolima pamba kusimamia kwa karibu mambo yafuatavyo:

Kwanza:    Kuhakikisha kuwa bei ya chini ya kununua Pamba inakuwa Shilingi 750 kwa kilo;
Pili:    Kuhakikisha kuwa maeneo yote ambayo Bodi ya Pamba itathibitisha kwamba hakuna mnunuzi aliyetoa huduma au mkopo kwa Mkulima, yawe huru kwa mnunuzi yeyote kupewa Leseni ya kununua Pamba ili kuwapa fursa Wakulima ambao hawapo katika mfumo wa kilimo cha mkataba kuuza bila matatizo.
50.    Ni matumaini yangu kwamba, hatua hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa uboreshaji wa zao la Pamba.
UMUHIMU WA VIWANDA NA KULINDA VIWANDA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
51.    Maendelea ya Nchi yoyote ile yanategemea sana ujenzi wa viwanda.  Kwa maana hiyo, suala la ujenzi wa viwanda haliepukiki kutokana na sababu kwamba, Viwanda husaidia kuongeza thamani mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na mazao ghafi yanayozalishwa katika Sekta zingine. Aidha, Viwanda huongeza muda wa bidhaa hizo wa kutumika kabla ya kuharibika. Vilevile, mazao yaliyoongezwa thamani humpatia mkulima bei nzuri na kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa mazao. Uwepo wa viwanda pia unatusaidia kupata fedha za kigeni, kutoa ajira na hivyo kupunguza tatizo la ajira kwa watu wetu hasa Vijana. Kwa maana hiyo kuna haja ya kuwepo Sera na Sheria mahsusi zitakazohimiza na kuchagiza  uwekezaji katika Sekta ya Viwanda na pia kuondoa vikwazo vya kibiashara.

Mheshimiwa Spika,
52.    Kwa kutambua umuhimu wa viwanda Nchini, ndio maana Serikali imeanzisha Mpango wa uanzishaji wa Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje Export Processing Zones – (EPZ) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Special Economic Zones – (SEZ) kama  mkakati  mahususi  wa kuvutia Wawekezaji. Katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013 jumla ya miradi ya viwanda ipatayo 52 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 474.37 ilisajiliwa na Mamlaka ya EPZ ambapo ajira 12,347 za moja kwa moja zinatarajiwa kupatikana. Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Mei 2014, pekee jumla ya miradi 21 yenye thamani ya Dola la Kimarekani Milioni 121.4 inayotarajia kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 4,814 imesajiliwa. Katika miradi hiyo, ipo Miradi inayosajiliwa kwa utaratibu wa kushirikisha Sekta ya Umma na Binafsi (Private Public Partnership-PPP). Ujenzi wa miradi hiyo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mheshimiwa Spika,
53.    Ni kweli kwamba, Serikali imeweka juhudi kubwa katika ujenzi wa Viwanda katika sehemu mbalimbali Nchini na pia kupanua wigo wa bidhaa zinazozalishwa. Kwa mfano, hivi sasa kuna Viwanda vya Chuma takriban 17 vinavyojumuisha Viwanda vya mabati, misumari, nyaya za uzio, nyaya za umeme, bidhaa za chuma, ikiwemo nondo na mabomba ya chuma kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Lakini pia tunavyo Viwanda vya kuzalisha Saruji vipatavyo vitano (5) vya Dar es Salaam, (TPCC), Tanga (TCC), Mbeya (MCC), Pwani (Rhino Cement Mkuranga), na Lindi (Lee Building Material ya Kilwa Masoko). Vilevile, Viwanda Vipya vya Saruji vinajengwa Arusha, Dar-es-Salaam (3), Tanga (2), Lindi, Pwani na Mtwara. Upanuzi huu wa Viwanda vya Saruji vitaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa Nchi Wazalishaji Wakuu Barani Afrika na hivyo kujitosheleza Kitaifa na kuuza nje.

54.    Tunavyo pia Viwanda vikubwa vya Kusindika Ngozi Saba (7) katika Mikoa ya Arusha, Dar-es-Salaam, Kilimanjaro (2), Morogoro, Pwani na Shinyanga. Tunavyo Viwanda vya Nguo Tisa (9) katika Mikoa ya Arusha, Dar-es-Salaam (4), Mara, Morogoro, Mwanza na Tanga na tunavyo pia Viwanda vya Sukari katika Mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Morogoro ambavyo vyote kwa ujumla wao vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Spika, 
55.    Pamoja na jitihada kubwa iliyowekezwa katika ujenzi wa Viwanda hivyo Nchini, tunayo Changamoto kubwa ya namna ya kuvilinda Viwanda hivi dhidi ya ushindani usio halali (Unfair Competition) ili viweze kukua na kuimarika kiushindani, Kikanda na Kimataifa. Mathalani, zipo bidhaa au vifaa vinavyoingizwa Nchini na kuuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na bei ya bidhaa aina hiyo hiyo zinazozalishwa Nchini. Bidhaa hizo huuzwa kwa bei ya chini kutokana na wazalishaji wa Nchi zinakotoka bidhaa husika kupewa ruzuku au bidhaa hizo zinakuwa na ubora duni usiokidhi Viwango vya Ubora au kutozwa ushuru mdogo au kupewa msamaha wa ushuru. Hali hii husababisha ushindani usio wa haki katika Soko la Ndani na ni changamoto kubwa kwa Taifa letu na Afrika Mashariki kwa ujumla. Naomba uniruhusu nitoe mifano michache ambayo itatuwezesha kuona ni namna gani tunaweza kukabili changamoto hii kwa lengo la kulinda Viwanda vyetu Nchini.

Mheshimiwa Spika,
56.    Nikianza na Saruji. Kama nilivyosema tunavyo Viwanda vitano vya Saruji vyenye uwezo wa kuzalisha Saruji hadi Tani Milioni 3.8 kwa mwaka. Mahitaji ya Saruji kwa sasa ni Tani Milioni 3.9 kwa mwaka na zipo juhudi za kuongeza uzalishaji kupitia uwekezaji katika miradi tisa (9) mipya ya ujenzi wa Viwanda vya Saruji ambavyo kwa ujumla wake inatarajiwa vitazalisha Tani Milioni 8.3 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika,
57.     Pamoja na uzalishaji huo mkubwa, changamoto kubwa ni namna ya kuhimili gharama kubwa za uzalishaji wa Saruji ikiwemo umeme, gharama za usafirishaji, na ushindani mkubwa dhidi ya saruji kutoka nje ya nchi ambayo ina ruzuku, hivyo kuvuruga soko la ndani kwa Viwanda vya Saruji. Aidha, ziko taarifa za ukwepaji kodi na udanganyifu ambao umeendelea kuwa tatizo kubwa sana katika Sekta ya Saruji. Kwa kutambua changamoto hiyo, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikubaliana kuweka Ushuru wa Forodha wa Asilimia 55 mwaka 2005 na kuushusha kufikia Asilimia 35 mwaka 2010. Matarajio yalikuwa ni kuvilinda Viwanda hivi ili vijijenge kwa miaka mitano na baada ya hapo kuendelea kuvilinda kwa kuviweka chini ya kundi la bidhaa nyeti, yaani kuwa na wigo wa pamoja wa Ushuru wa Forodha wa zaidi ya Asilimia 25.

Mheshimiwa Spika,
58.    Hali iliyojitokeza katika Viwanda vya Saruji haitofautiani sana na Viwanda vya Chuma ambavyo navyo vina changamoto kubwa hasa katika uzalishaji na ubora wa bidhaa za chuma. Mathalan, ziko taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba karibu Viwanda vyote vya Nondo Nchini vinazalisha chini ya viwango, jambo ambalo halikubaliki kabisa. Nilibahatika kufanya Ziara Mkoa wa Mwanza ambapo nilikuta katika Mradi mmoja wa ujenzi wa Tanki la Maji – Mkandarasi alikuwa ananunua Nondo kutoka Uganda kwa madai kuwa Nondo zilizokuwa zinazalishwa na Viwanda vyetu kwa maelezo yake zilikuwa chini ya viwango. Kiwango stahiki kinapaswa kuwa BS 406, BS 500, n.k. lakini Viwanda vyetu vinazalisha chini ya kiwango hicho, yaani BS 400. Ni wakati muafaka sasa Viwanda vyote kuzingatia viwango vya Kimataifa ili kuepusha majanga yanayotokana na udhaifu huo na pia kuwezesha Nondo hizo kutumiwa na wahitaji wote wa hapa ndani na nje ya Nchi. Ninahimiza Shirika la Viwango Nchini liendelee kusimamia ubora wa bidhaa za Nondo kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, 
59.    Kwa sasa kuna Viwanda vya Nondo takriban 15 ambavyo vina uwezo wa kuzalisha Nondo Tani 420,000 kwa mwaka. Mahitaji ya Nondo ni Tani 200,000 kwa mwaka, ikiwa ni ziada ya Asilimia 40 zaidi ya mahitaji. Aidha, Viwanda hivi vya Nondo peke yake vinatoa ajira ya moja kwa moja ya watu 4,000 na wengine takriban 40,000 ambao siyo wa moja kwa moja.

60.    Lakini pia tuna Viwanda vikubwa vya Chuma viwili (2) vyenye uwezo wa kuzalisha Mabati Tani 150,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ni Tani 100,000 kwa mwaka ikiwa ni ziada ya Tani 50,000, sawa na  Asilimia 50 ya mahitaji. Viwanda hivi navyo vimezalisha ajira ya takriban Watu 16,000.
Mheshimiwa Spika,
61.    Mifano hiyo miwili ya Uzalishaji wa Nondo na Mabati inadhihirisha kwamba tatizo la uzalishaji kukidhi mahitaji halipo, bali tatizo ni uagizaji wa Nondo zinazoingizwa Nchini kwa kulipiwa Ushuru mdogo, naambiwa wa Asilimia 10 tu kama Kodi kwa visingizio mbalimbali na hivyo kutoa ushindani usio halali kwa Nondo zinazozalishwa Nchini. Aidha, mabati yanayoingizwa Nchini yamewekwa katika orodha ya “Deemed Capital Goods” ambayo haiwabani watekelezaji wa Miradi mbalimbali nchini kutumia mabati yanayotengenezwa na Viwanda vya Ndani.

Mheshimiwa Spika,
62.    Tunavyo Viwanda vya kusindika Ngozi takriban tisa (9). Viwanda hivi vina uwezo wa kusindika vipande vya Ngozi Milioni 13.2 kwa mwaka katika hatua ya mwanzo yaani (Wet Blue). Kati ya hivyo vipande vya ngozi za ng’ombe ni milioni 2.5 na vya mbuzi na kondoo ni Milioni 10.7. Aidha, usindikaji wa ngozi ghafi umefikia Vipande 945,596 vya Ng’ombe na Vipande 2,713,636 vya Mbuzi na Kondoo kwa mwaka 2013. Kama ilivyo kwa Viwanda vya Chuma na Saruji, changamoto kubwa ya usindikaji wa ngozi ni pamoja na ushindani usio wa haki unaosababishwa na uingizaji wa viatu vya plastiki na mitumba ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa viatu vya Ngozi na bidhaa nyingine za Ngozi Nchini.

Mheshimiwa Spika,
63.    Vilevile, tunalo tatizo kubwa katika Viwanda vya uzalishaji wa Sukari Nchini. Tunavyo Viwanda takriban Vinne vya Sukari. Uwezo wa uzalishaji Sukari Nchini ni Tani 300,000 kwa mwaka. Mahitaji ya Sukari ni Tani 590,000 kwa mwaka (Tani 420,000 ni Sukari ya Matumizi ya Kawaida na Tani 170,000 Sukari ya Matumizi ya Viwandani). Kwa maana hiyo, kuna upungufu wa Tani 290,000 sawa na Asilimia 49. Kati ya hizo Tani 170,000 (29%) ya Sukari ya matumizi ya Viwandani na Tani 120,0000 (20%) Sukari ya Matumizi ya Kawaida. Kutokana na upungufu huo, Serikali iliweka utaratibu wa kuagiza na kusambaza Sukari kutoka Nje ya Nchi ili kufidia pengo hilo kwa kuruhusu Waagizaji kulipa Ushuru wa Asilimia 25 na pia Ushuru wa Forodha Asilimia 10 kwa Viwanda vinavyotumia Sukari kwa ajili ya matumizi ya Viwandani. Vipo pia vibali vya bila ushuru kabisa vinavyotolewa wakati wa upungufu wa sukari.

Mheshimiwa Spika,
64.     Utaratibu huu pamoja na kusimamiwa na Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), umesababisha malalamiko mengi kuwa hatua hizi za kushusha Viwango vya Ushuru wa Forodha zimesababisha waingizaji Sukari kukwepa kabisa Kodi, ikiwemo Ushuru wa Forodha na VAT. Aidha, zipo hisia kuwa sukari hiyo ambayo ni nyingi zaidi ya kiasi kilichoruhusiwa kuingizwa Nchini inatokana na Wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kutumia kinyume cha Sheria vibali vya Mamlaka ya Mapato Tanzania vinavyowaruhusu kupitishia Nchini Sukari inayosafirishwa kwenda nje ya Nchi (Transit Sugar) kwa kuibakiza bidhaa hiyo hapa Nchini na sukari ya viwandani kuuzwa kama sukari ya mezani.

Mheshimiwa Spika,
65.    Sukari hii inayoingizwa nchini huathiri uzalishaji na mtiririko wa usambazaji sukari ya ndani hivyo kutishia ukuaji wa viwanda vya ndani vya Sukari na uzalishaji wa sukari kwa ujumla. Vilevile, itakumbukwa kuwa Serikali kwa nia njema, tulianzisha utaratibu wa “Outgrowers” ili Wakulima wanaoishi kandokando ya Viwanda vya Sukari kulima Miwa na kuuzia wenye Viwanda kule Kilombero, Mtibwa na Kagera ili kuboresha maisha yao kiuchumi. Hivyo, kutokana na hali ilivyo kwa sasa, Wakulima hawa wakiwemo Wakulima wa Kilombero wameshindwa kulipwa kwa wakati baada ya kuuza Miwa yao Kiwandani kwa vile Wazalishaji wamekuwa wakiuza Sukari chini ya Wastani wa mauzo ya kawaida.

Mheshimiwa Spika,
66.    Nimeamua kuongea haya yote kuhusu hali halisi ya Viwanda vyetu na bidhaa zinazozalishwa humu Nchini ili kuona umuhimu wa kujenga Viwanda na changamoto tulizonazo katika kulinda Viwanda vyetu vya ndani kwa kutumia mifano ya bidhaa za Chuma ikiwemo Mabati, Nondo, Saruji na Sukari. Yapo mambo mengi ambayo yanajitokeza katika kila moja. Lakini jambo  la  msingi  ni  namna  ya  kuangalia kama tunapokuwa na  mahitaji  yanayozidi uwezo wa uzalishaji Viwandani tuchukue  hatua  gani. Ni lazima kama Nchi pamoja na upungufu wa bidhaa uliopo, sasa tuamue kulinda Viwanda vyetu vya ndani dhidi ya Ushindani usio halali kwa nguvu zetu zote. Lazima sasa tukae tuone namna ya kudhibiti uingizaji wa bidhaa ambazo zinakwamisha maendeleo ya Viwanda vyetu. Aidha, tuangalie njia bora ya kupunguza gharama za uzalishaji, ikiwemo bei kubwa za umeme. Matarajio ni kwamba, baada ya kupatikana kwa Gesi tunaamini gharama za Umeme zitapungua na kupunguza gharama za uzalishaji Viwandani.

Mheshimiwa Spika, 
67.    Tumeona changamoto zinazokabili bidhaa za Mabati, Nondo, Sukari, Ngozi na Saruji kama mfano. Ninaagiza Taasisi zetu zikiwemo Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bodi ya Sukari, Jeshi la Polisi na Uhamiaji kukaa kwa pamoja kuangalia njia bora ya kudhibiti uingizaji kiholela wa bidhaa zinazokwamisha maendeleo ya Viwanda vyetu. Kwa maana hiyo ni vizuri sasa kuchukua hatua stahiki kulinda Viwanda vyetu kuhimiza mambo muhimu yafuatayo:

i)    Wizara ya Viwanda na Biashara ni lazima sasa kuhakikisha kwamba Viwanda vyetu vinazalisha bidhaa zenye ubora kwa Viwango vya Kimataifa. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lisaidie, lakini lazima ubora uwe unawezesha bidhaa hizo kuuzwa ndani na nje bila vikwazo;
ii)    Wizara ya Fedha ihakikishe kuwa bidhaa zilizomo katika kundi la bidhaa nyeti katika Afrika Mashariki haziondolewi katika kundi hilo katika kipindi kirefu kijacho hadi hapo suala la Ruzuku likipatiwa ufumbuzi wenye manufaa kwa Nchi changa katika Shirika la Biashara Duniani (WTO);
iii)    Wizara ya Fedha iangalie uwezekano wa watumiaji wa Industrial Sugar wanalipia Ushuru kamili na kisha baadaye wapewe Duty Drawback baada ya kuthibitishwa kuwa Sukari husika kweli ilitumika katika uzalishaji. Wizara ya Fedha pia iweke utaratibu ulio bora wa uagizaji wa Sukari kufidia upungufu huu kutumia Bulk Importation, na kisha kusambazwa kwa usimamizi madhubuti na kwa bei maalum, n.k.;
iv)    Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Bodi ya Sukari wakae na kutathmini mahitaji halisi ya Sukari, ikilinganishwa na uwezo wa Viwanda vya Sukari vilivyopo Nchini, pamoja na kukamilisha taratibu za kisheria na kimfumo za uagizaji wa Sukari kuziba upungufu pale inapobidi. Aidha, ni muhimu kuhimiza upanuzi katika uzalishaji wa Sukari kwa kuhamasisha Uwekezaji mpya katika Sekta hii;
v)    Utaratibu wa kuagiza bidhaa zitakazoingizwa Nchini kuziba pengo lililopo lazima uangaliwe upya ili uagizaji huo usiathiri Viwanda vya ndani;
vi)    Tathmini ya upungufu wa bidhaa unaojitokeza uangaliwe kwa umakini na kupanga njia bora ya kufidia upungufu huo, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa vibali vya kuruhusu kuingiza bidhaa Nchini. Vibali vihusishe muda ule wenye upungufu pekee. Aidha, utaratibu wa sasa wa kutumia Wafanyabiashara kuleta bidhaa kwa lengo la kufidia upungufu wa bidhaa husika uangaliwe upya ili kuepuka uingizaji bidhaa kwa wingi kuliko upungufu ambako kunasababisha kudumaza Viwanda vya ndani; na
vii)    Bei za bidhaa zizingatie maeneo yanayozunguka eneo la Uzalishaji. Kwa mfano, haitarajiwi bei ya Sukari kilo moja ya Sukari inayozalishwa na Kiwanda cha Sukari cha Kagera au pale Moshi TPC, au Mtibwa na Kilombero iwe kubwa sawa na Sukari hiyo inavyouzwa Mtwara au Ruvuma au Katavi.
Mheshimiwa Spika,
68.    Ipo mifano kwa baadhi ya Nchi Duniani ikiwemo India ambazo zimejaribu kuweka Nembo inayoonesha kwamba bidhaa hizi zinazalishwa Nchini na bei yake ni kiasi fulani. Lengo likiwa ni kuhakikisha kulinda watumiaji wa bidhaa hizo na kulinda pia Viwanda. Majirani zetu Kenya wameanza kuchukua hatua katika Bajeti ya 2014 kulinda Viwanda vyao. Kwa mfano, Serikali ya Kenya imeongeza Ushuru wa bidhaa za Chuma kutoka Asilimia 0-10 na kufikia Asilimia 25 na kuahidi kuweka mezani Muswada mpya wa Sheria ya Ushuru wa Forodha ili kulinda Viwanda vyake. Nasi tukidhamiria hata kama hatukufanikiwa kwa kiasi kikubwa mwaka huu, tunaweza kufikia lengo hilo kwa mwaka ujao wa Bajeti. Nina hakika Tukidhamiria tutaweza kufika!

UTOAJI WA ELIMU KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU NCHINI
Mheshimiwa Spika,
69.    Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 inasisitiza kuhusu haki ya kila raia wa Tanzania kupata Elimu wakiwemo watu Wenye Mahitaji Maalumu; Sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 1996 inayozungumzia umuhimu wa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule kwenda na kupata elimu bora; na Sera ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu ya 2004 – inasisitiza umuhimu wa Elimu ya watoto wenye Ulemavu kutolewa katika mazingira Jumuishi na rafiki. Katika kutekeleza Sera hizo, Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa elimu bora kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule, wakiwemo wenye Mahitaji Maalumu.

Mheshimiwa Spika,
70.     Kwa sasa zipo Shule za Msingi 22 ambazo ni maalum kwa ajili ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum na Shule za Msingi 354 zenye Vitengo Maalum kwa ajili ya Wanafunzi hao. Jumla ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum katika Shule za Msingi na Vitengo hivyo ni 11,689. Aidha, ipo Shule moja ya Sekondari ambayo ni maalum kwa Wanafunzi wa Sekondari wenye Mahitaji Maalum pamoja na Shule za Sekondari 61 ambazo zina Vitengo Maalum kwa ajili ya Wanafunzi wa aina hiyo. Kwa sasa, wapo Wanafunzi 1,406 wenye Mahitaji Maalum waliopo katika Shule za Sekondari Nchini.

Mheshimiwa Spika,
71.     Tarehe 3 Mei 2014 nilifungua maonesho ya Elimu yaliyokuwa yameandaliwa na Wadau mbalimbali wa Elimu kwenye Uwanja wa Jamhuri hapa Dodoma. Nilipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali yaliyokuwa yakionesha shughuli mbalimbali za elimu. Moja ya Banda nililotembelea ni lile lililokuwa likionesha hatua mbalimbali za utoaji wa elimu maalum. Katika Banda hilo nilielezwa njia zinazotumiwa kuwafundisha Wanafunzi wenye Mahitaji maalum hususan Wasioona na nilioneshwa vifaa vinavyotumika na kuelezwa changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika,
72.    Tarehe 4 Juni 2014 nilitembelea na kukagua Shule ya Msingi Bwigiri – Wasioona, Wilayani Chamwino. Katika ziara hiyo nilikagua maktaba, chumba cha kompyuta, chumba cha kutayarishia mitihani na vyoo. Niliongea pia na Wanafunzi waliokuwa wamebaki hapo shuleni baada ya wanafunzi walio wengi kuwepo kwenye likizo. Shule hiyo ni miongoni kwa Shule 120 za Msingi zilizoko kwenye Wilaya ya Chamwino ikiwa na jumla ya Watumishi 39 kati yao 25 wakiwa ni Walimu. Shule ina Wanafunzi 87, kati yao 61 ni Wasioona na 26 Wanaona. Jambo lililonifurahisha katika Shule hiyo ni kuwa Wanafunzi wanaohitimu Darasa la Saba wamekuwa wakifaulu wote (Asilimia 100) kwa muda wa miaka 13 mfululizo. Wanafunzi hao wanaofaulu wamekuwa wakijiunga na Shule Maalum za Sekondari kama vile Shule ya Sekondari Diocese of Central Tanganyika (DCT) Mvumi n.k.

Mheshimiwa Spika,
73.    Tarehe 7 Juni 2014 nilitembelea pia Shule ya Sekondari ya Mvumi DCT ambako baadhi ya Wanafunzi Wasioona wanasoma. Nilikutana na Walimu pamoja na Wanafunzi wa Kidato cha Pili na Nne ambao walikuwa wanajiandaa na mitihani ya Kitaifa ya mwaka 2014. Nilifurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Serikali, Kanisa la Anglikana Nchini na Walimu wa Shule hiyo kwa kuwawezesha Wanafunzi Wasiiona kupata haki yao ya elimu.

74.    Ziara zangu hizo zilinithibitishia kuwa Walimu Nchini wakiwemo Walimu wa Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum wanafanya kazi kubwa na ya Kizalendo ambayo inahitaji kuungwa mkono wakati wote. Nawapongeza Walimu wote Nchini kwa kazi yao muhimu ya kutoa elimu kwa Taifa letu. Nitumie fursa hii ya kipekee kabisa kuwapongeza Walimu na Wanafunzi wote wa Shule ya Msingi Bwigiri – Wasioona kwa kuwezesha mafanikio makubwa na ya kuigwa yaliyopatikana Shuleni hapo. Aidha, nawapongeza Wasimamizi wa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa usimamizi wao mzuri uliowezesha ufaulu na mafanikio hayo kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
75.    Pamoja na pongezi hizo, Ziara zangu hizo ziliniwezesha kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo Wanafunzi Wasioona wakiwa shuleni. Ni kweli changamoto ni nyingi, lakini kubwa nililoliona na ambalo limewagusa Wanafunzi hao pekee ni lile la Wanafunzi Wasioona kutofundishwa somo la Hisabati katika ngazi ya Sekondari na hivyo, kutofanya mtihani wa somo hilo wa kumaliza Kidato cha Nne na kusababisha kushushwa madaraja yao ya ufaulu sawa na Wanafunzi wa kawaida katika Shule zingine Nchini wasiofaulu somo hilo. Lakini Shule hizi zinakosa vitendea kazi muhimu kama vile Braille Printer, Embossing Photocopy Machine, Kompyuta, n.k.

Mheshimiwa Spika,
76.    Ninafahamu kuwa changamoto nyingine si za Wanafunzi wasioona tu bali zinawahusu pia Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum pamoja na Walimu wao kwa ujumla. Napenda kutoa wito kwa Watendaji wanaohusika na elimu maalum Nchini kushughulikia changamoto zonazowakabili Walimu na Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum pamoja na Majengo ya Shule zao. Ni imani yangu kuwa kila mmoja anayehusika atachukua hatua mapema ili kuwawezesha Wanafunzi Wasioona na wote Wenye Mahitaji Maalum kupata elimu stahiki katika mazingira stahiki.

AFYA
Uwiano wa Idadi ya Watu wa Vijijini na Mijini  wanaohudumiwa na Daktari
Mheshimiwa Spika,
77.    Idadi ya Watanzania inakadiriwa kuwa Milioni 48.2 kati yao wanaoishi Vijijini ni Milioni 36.6 na wanaoishi Mijini ni Milioni 11.6. Watanzania hao wanahudumiwa na Madaktari ni 2,311 waliopo Nchini kwa sasa. Madaktari wanaoishi maeneo ya Vijijini ni 523 na wanaoishi  maeneo ya Mijini ni 1,788. Mgawanyo huu wa Madaktari unafanya kuwa Daktari mmoja kitaifa anahudumia Wastani wa Watanzania  19,982. Kwa upande wa Vijijini, Daktari mmoja anahudumia Wananchi 66,211 wanaoishi Vijijini na kwa maeneo ya Mijini, Daktari mmoja anahudumia Wananchi 6,460. Hali hii inaonesha kuwa Daktari mmoja anayehudumia maeneo ya Vijijini anahudumia zaidi ya mara kumi ya idadi ya watu wanaohudumiwa na Daktari anayefanya kazi Mjini.

78.    Kiwango hiki cha Daktari mmoja kwa Watanzania 19,982 ni kikubwa sana ikilinganishwa na wastani wa kawaida wa Daktari mmoja kwa Watu 10,000. Kinahitaji kupunguzwa kwa kuongeza idadi ya Madaktari Nchini. Serikali itaendelea kugharamia elimu ya Madaktari Nchini na kuwawezesha kuwa na mazingira bora ya kazi kwa kuzingatia hali ya uchumi wa Nchi. Nia ni kuongeza idadi ya Madaktari wa ngazi na vitengo mbalimbali vya Afya na kuwasambaza Nchini hususan maeneo ya Vijijini ili Daktari mmoja ahudumie Watanzania wachache zaidi.
Saratani ya Shingo ya Kizazi
Mheshimiwa Spika,
79.    Serikali imeanzisha mpango wa kitaifa wa kukinga na kuzuia saratani ya shingo ya kizazi. Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu kujikinga na saratani ya awali, kupanua vituo vya kupima dalili za awali za saratani na kupatiwa tiba ya ugandishaji baridi kwenye Mikoa mitatu iliyobakia ya Mtwara, Rukwa na Simiyu. Huduma ya rufaa itaboreshwa kwa wagonjwa wanaofikiriwa kuwa na saratani kwa ajili ya tiba katika Taasisi ya Saratani ya Dar-es-Salaam. Aidha, chanjo ya kuwakinga Wasichana wenye umri wa miaka 9-13 dhidi ya saratani imeanza kutolewa katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kujifunza mfumo wa kutumia Shule kwa ajili ya kutoa chanjo hii nchi nzima.

HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Spika, 
80.    Kwa ujumla hali ya usalama katika Mipaka yote ya Nchi yetu inaendelea kuwa shwari licha ya kuwepo changamoto kadhaa.  Mathalani katika Mpaka wa Kaskazini ambapo Tanzania inapakana na Kenya na Uganda kumekuwepo na changamoto ya Wahamiaji haramu hususan katika Wilaya za Misenyi na Karagwe na changamoto ya uharibifu wa alama za Mipaka. Aidha, katika Mpaka wa Kusini pamekuwepo na changamoto ya utata wa Mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa na changamoto ya ujenzi holela unaofanywa na Wananchi waishio Mpakani eneo la Tunduma.

Mheshimiwa Spika, 
81.    Serikali kupitia Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti hali hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo ya pamoja baina ya Wataalamu wetu na Wataalamu wa Nchi hizo jirani kwa mfano:

i)    Tarehe 05 hadi 12 Octoba, 2013 Mjini Arusha vilifanyika Vikao vya pamoja kukagua, na kuhakiki Mpaka kati ya Tanzania na Kenya;
ii)     Mwezi Februari 2014 Jijini Dar es Salaam kilifanyika kikao cha kuboresha Mipaka ya Tanzania, Burundi, Zambia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika ziwa Tanganyika;
iii)    Mwezi Mei, 2014 kilifanyika Kikao cha TUME ya Uimarishaji na Uhakiki wa Mpaka baina ya Tanzania na Burundi Mjini Ngara.

Mheshimiwa Spika, 
82.    Pamoja na kwamba kwa ujumla hali ya usalama wa Mipaka yetu ni shwari, bado Nchi yetu kama sehemu ya Afrika Mashariki inakabiliwa na tishio la mashambulizi ya Kigaidi ambalo linawakumba Majirani zetu.  Serikali kupitia Jeshi la Wananchi Tanzania inaendelea kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Nchi jirani, Nchi Marafiki pamoja na Jumuia ya Kimataifa ili kukabili tishio hilo. Nitoe wito tena kwa Wananchi wetu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Vyombo vya Usalama katika kuhakikisha Nchi yetu inakuwa salama wakati wote.

AJALI ZA BARABARANI
Mheshimiwa Spika, 
83.    Suala la ajali za barabarani bado ni changamoto kubwa hapa Nchini likichangia vifo na majeruhi wengi na uharibifu wa mali. Pamoja na hatua mbalimbali za kisheria, bado kumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani mwaka hadi mwaka. Katika kipindi cha Januari 2011 hadi Mei 2014, jumla ya Ajali 78,654 ambazo zilisababisha Vifo 13,375 na Majeruhi 67,936 zilitokea. Hii ni idadi kubwa ya ajali, vifo na majeruhi.

Mheshimiwa Spika,
84.    Ziko sababu mbalimbali zinazochangia kuongezeka kwa ajali za barabarani zikiwemo makosa ya kibinadamu (Uzembe wa Madereva, Ulevi, Mwendokasi na Uegeshaji mbaya wa magari barabarani n.k.) ambayo kwa ujumla yanachangia Asilimia 77 ya ajali zote zinazotokea, ubovu wa vyombo vya moto unaochangia Asilimia 16, na mazingira ya barabara yaani ubovu wa miundombinu na hali ya hewa vinavyochangia Asilimia 7.

Mheshimiwa Spika,
85.    Katika kukabiliana na ajali za barabarani, Serikali kupitia Vyombo mbalimbali imechukua hatua za kuimarisha mafunzo kwa Madereva kwa kutunga Kanuni zinazowalazimisha kusoma masomo ya umahiri wa kuendesha magari ya abiria na magari makubwa ya mizigo (HDV); kudhibiti mwendokasi na kuanzisha Mfumo wa kufuatilia mwendo wa Mabasi na Malori utakaodhibiti makosa mbalimbali ya usalama barabarani. Hatua nyingine ni kuanzisha mfumo wa uwekaji nukta (Point system) katika Leseni za Madereva ili kuwaondoa barabarani madereva wanaokithiri kwa makosa, kupima kiasi cha ulevi kwa Madereva; na kupanua wigo wa elimu ya usalama barabarani kwa njia ya televisheni, redio, simu na magazeti. Kwa upande wa Usimamizi wa Sheria zilizopo, hatua stahiki zinachukuliwa kwa kuongeza usimamizi na mafunzo kwa watendaji wote wanaosimamia Sheria ili kuwaongezea ufanisi na kudhibiti nidhamu yao. Watendaji wanaokiuka maadili ya kazi wanachukuliwa hatua za kinidhamu.

Mheshimiwa Spika,
86.    Kwa upande wa ubovu wa vyombo vya moto, Serikali inaandaa Kanuni za Ukaguzi wa Lazima. Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimekamilisha ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa magari ikiwa ni pamoja na mitambo ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa. Ninatoa wito pia kwa Sekta Binafsi kujitokeza kuwekeza katika eneo hili ili mitambo hii iwepo ya kutosha. Aidha ni muhimu sasa kuanzisha Gereji maalum kwa ajili ya matengenezo yatakayokuwa yanapimwa kwa mfumo huu. Sambamba na hatua hizo, Jeshi la Polisi pia linaandaa Kanuni zitakazowalazimu Madereva kubandika mkanda ang’avu kuzunguka magari makubwa ya mizigo na mabasi ili kusaidia kuongeza muonekano wa magari hayo wakati wa giza.

Mheshimiwa Spika, 
87.    Pamoja na jitihada hizo za Serikali za kuandaa Kanuni mbalimbali, Sheria mpya ya Usalama Barabarani inaweka muundo bora wa usimamizi wa shughuli za Usalama barabarani kwa kuweka hitaji la kuundwa kwa Taasisi Kiongozi ya Usalama Barabarani (Road Safety Lead Agency). Sheria hiyo itaanisha majukumu ya Taasisi Wadau wa Usalama Barabarani na kuratibu utekelezwaji wa majukumu ya Taasisi hizo. Uwepo wa Chombo hiki utaongeza uwajibikaji wa kila Taasisi katika eneo lake tofauti na sasa ambapo suala la usalama barabarani linachukuliwa kama jukumu la Polisi pekee. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taasisi na Wadau mbalimbali wanafanya mapitio ya rasimu ya Muswada huu ambao mara utakapokamilika utawasilishwa Bungeni.

MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI NA VIKONGWE
Mheshimiwa Spika, 
88.    Nchi yetu bado inaendelea kukumbwa na tatizo la Mauaji ya Watu wenye Ulemevu wa Ngozi na Vikongwe kwa imani za ushirikina. Katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, takwimu zinaonesha kwamba jumla ya Watu 3 wenye Ulemavu wa Ngozi waliuawa katika Mikoa ya Arusha, Tabora na Simiyu na wengine 2 walijeruhiwa katika Mkoa wa Rukwa. Kufuatia matukio hayo, watuhumiwa 8 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa mauaji na wengine 4 wanashtakiwa kwa kujeruhi. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya Vikongwe 1,393 waliuawa kikatili katika Mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu, Mwanza, Tabora, Singida, Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa.

Mheshimiwa Spika, 
89.    Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hili, Serikali inachukua hatua ya kuzihusisha Kamati za Ulinzi na Usalama za ngazi mbalimbali kuanzia Vitongoji na Mitaa katika mapambano dhidi ya mauaji ya Vikongwe kwa kufanya Mauaji ya Watu wenye Ulemavu na Vikongwe kuwa Agenda ya kudumu katika Mikutano yao. Aidha, tutaendelea kutoa elimu kwa Wananchi kupitia Vyombo vya Habari, Viongozi wa Dini na Watu mashuhuri katika maeneo husika ya kuepukana na imani potofu za ushirikina. Jeshi la Polisi linaendesha Program mbalimbali kuelimisha Jamii kukabiliana na uhalifu kufanya ufuatiliaji wa matukio ya mauaji ya Vikongwe ikiwa ni pamoja na kuweka mkakati wa kuharakisha upelelezi wa kesi za matukio ya Mauaji.

MAUAJI YA WANAWAKE MKOANI MARA
Mheshimiwa Spika, 
90.    Pamoja na Mauaji ya Vikongwe na Watu wenye Ulemavu wa Ngozi katika Mkoa wa Mara kumetokea mauaji ya kinyama ya Wanawake kutokana na sababu za kishirikina katika kipindi cha Januari hadi Mei 2014 hususan katika Wilaya za Butiama na Musoma. Waathirika wa matukio haya walikuwa wakiuawa kwa kunyongwa kwa kutumia khanga nyakati za mchana wakiwa katika shughuli zao na hivyo kusababisha hofu kubwa katika Jamii. Jumla ya matukio tisa (9) ya kuuawa Wanawake yaliripotiwa katika Kata nne za Mugangwa, Etaro, Nyegina na Nyakatende.

Mheshimiwa Spika, 
91.    Kufuatia matukio hayo Serikali kupitia Jeshi la Polisi na kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imechukua hatua za haraka na jumla ya watuhumiwa 15 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa kesi za mauaji. Aidha, Kikosi Kazi cha Makosa dhidi ya Binadamu na vitendea kazi kutoka Makao Makuu ya Upelelezi kikiongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania Kamishna ISAYA MNGULU walifika Mkoani Mara kwa ajili ya ufuatilia wa karibu wa kitaalamu wa matukio haya. Timu hiyo wenye Wataalam mahiri katika eneo la Upelelezi wanaendelea kufuatilia matukio haya  sambamba na kutoa elimu juu ya Ulinzi Shirikishi  wa  namna  ya  kukabiliana  na  matukio kama haya,ikiwa ni pamoja na kutoa elimu zaidi kuhusu uhalifu huu na kufanaya Operesheni ijulikanayo kama “Zuia Mauaji ya akina Mama Wilaya ya Butiama.”

Mheshimiwa Spika, 
92.    Kutokana na juhudi hizo, hali ya Usalama katika maeneo hayo imeimarika na matukio hayo hayajajitokeza tena. Napenda kutoa wito kwa Wananchi wote kutambua kuwa jukumu la ulinzi ni la kila Mwananchi, hivyo hatuna budi kuwafichua wale wote wanaofanya uhalifu katika Jamii. Lengo ni kuwalinda Wananchi na kuhakikisha kuwa maeneo tunayoishi yanakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha ili Wananchi waendelee na shughuli zao za uzalishaji badala ya kuhofia maisha yao.

MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Mheshimiwa Spika,
93.    Kama wote tunavyofahamu, Bunge Maalum la Katiba liliaanza majukumu yake mapema mwezi Februari 2014 ambapo katika kipindi hicho Wajumbe walikamilisha kuandika na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Bunge Maalum, Wajumbe kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba hiyo na Kamati za Bunge Maalum kuwasilisha maoni yao Bungeni. Hata hivyo, na kwa masikitiko makubwa wakati tukiwa katika hatua za uwasilishaji, baadhi ya Wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba na Wananchi (UKAWA) waliamua kutoka nje ya Bunge kwa sababu ambazo hazikueleweka wakati huo.

Mheshimiwa Spika,
94.     Wote tunafahamu kuwa, Bunge Maalum la Katiba lina Wajumbe wa aina tatu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe 201 wanaotoka katika Makundi mbalimbali. Kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge hili ni sehemu ya Wajumbe wa Bunge Maalum, naomba nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa ujumbe mfupi kwa Wajumbe wa Bunge Maalum ambao naamini utaweza kuwafikia popote walipo.

Mheshimiwa Spika,
95.    Kifungu cha 26 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinatoa masharti na mamlaka ya Bunge Maalum kutunga Kanuni kwa ajili ya kuendesha  shughuli  za  Bunge Maalum. Ni kwa kupitia mamlaka kama ilivyofafanuliwa katika Kifungu hiki, Wabunge wa Bunge Maalum waliweza kutunga Kanuni za Bunge Maalum kwa maridhiano kwa muda wa takriban mwezi mmoja. Vilevile, ni kupitia Kanuni hizo, Viongozi wa Bunge Maalum waliweza kuchaguliwa na kufanya Bunge hilo kuwa Chombo Maalum chenye Uongozi na kuwa na Mamlaka yake ya Kisheria.

Mheshimiwa Spika,
96.    Kanuni ya 46 ya Bunge Maalum la Katiba inaeleza mambo yasiyoruhusiwa kwenye Bunge Maalum yakiwemo kutumia lugha ya kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au inayodhalilisha watu wengine. Aidha, Kanuni hii ya 46 inatoa utaratibu mzima wa jinsi ya kushughulikia masuala haya ndani ya Bunge Maalum. Kanuni ya 16 (3) inatoa nafasi kwa Mjumbe au Wajumbe wa Bunge hilo ambaye hakuridhika na uamuzi wa Mwenyekiti uliotolewa, kuwa atakuwa na haki ya kuwasilisha kwa maandishi malalamiko yake kwa Katibu ndani ya siku moja kuanzia tarehe ya uamuzi.

97.    Kwa muendelezo huo huo, Kanuni ya 59 (1) (d) inaelekeza kuwa, moja ya majukumu ya Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum ni kuchunguza kuhusu masuala yote ya haki, kinga na madaraka ya Bunge Maalum yatakayopelekwa kwenye Kamati hiyo na Katibu kutoa taarifa kwa Mwenyekiti baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge Maalum. Kutokana na utaratibu huo wa Kikanuni kama ilivyoainishwa katika Kanuni hizo za Bunge Maalum, ninapenda kutumia fursa hii kuwashauri “Wana UKAWA” ambao wengi wao wamo ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wenzangu wote wa Bunge Maalum ambao wamo ndani na nje ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla wetu kutumia mifumo iliyowekwa na Bunge Maalum kupeleka malalamiko yote katika Kamati ya Kanuni ya Bunge Maalum ili yapatiwe ufumbuzi ndani ya Bunge Maalum na siyo nje ya Bunge. Hilo ndilo jambo la busara!!
Mheshimiwa Spika,
98.    Mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya, ambao kimsingi ni wa Kisheria umeanza siku nyingi na kwa hatua mbalimbali shirikishi kwa makundi ya watu na Vyombo mbalimbali, kupokezana majukumu kwa lengo la kufanikisha azma ya kupata Katiba Mpya. Ninapenda kuwakumbusha Wajumbe wenzangu wa Bunge Maalum la Katiba popote walipo ndani na nje ya Bunge hili kuwa, kuwepo kwetu katika Bunge Maalum la Katiba ni jambo la Kisheria na si jambo la kawaida wala la hiari. Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, sote kwa ujumla wetu tuna wajibu wa kukamilisha sehemu yetu kama Wajumbe wa Bunge Maalum kwenye mchakato mzima wa kuandaa Katiba Mpya.

Mheshimiwa Spika,
99.    Vilevile, napenda kukumbusha kuwa Bunge Maalum la Katiba si hatua ya mwisho ya mchakato huu. Baada ya Bunge Maalum la Katiba kumaliza wajibu wake, Rasimu itakayokuwa imependekezwa na Bunge Maalum itatakiwa kuwasilishwa kwa Wananchi wote wa Tanzania waisome, waielewe na kisha waweze kuipigia kura ya maoni kuikubali au kuikataa kwa mujibu wa Sheria iliyopo ya Kura ya Maoni mwaka 2013. Hivyo, ni vyema tukaelewa vizuri suala hili na kwamba, bado kuna Wananchi wenzetu wengi kwa idadi ambao nao wanasubiri haki yao ya Kisheria katika kukamilisha mchakato huu kabla ya kupata Katiba Mpya. Hivyo tusiwanyime haki hiyo!

100.    Ninapenda kuwashauri Wajumbe wenzangu ambao wameamua kususia Vikao vya Bunge Maalum la Katiba kutafakari uamuzi na matendo yao kwa kutambua masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na wajibu wao kwa Wananchi. Sisi wote tuliopo hapa tuna wajibu huo wa kukamilisha kazi hii muhimu tuliyopewa kisheria ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata Katiba Mpya.
101.    Hivyo, natoa wito kwa Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba ambao wamesusia Vikao vya Bunge Maalum la Katiba, warejee kwenye Bunge hilo ili tuweze kuendelea na Mjadala wa Rasimu ya Katiba huku tukitumia utaratibu mzuri wa maridhiano uliowekwa Kikanuni kutatua tofauti zilizopo.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
102.    Changamoto kubwa iliyoko mbele yetu baada ya kuwepo hapa Bungeni kwa takriban miezi miwili ni kusimamia utekelezaji wa Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha. Sisi kama Wabunge tuondoke hapa kwa lengo moja la kushirikiana na Wananchi kusukuma maendeleo na Bajeti tuliyoipitisha ikiwa ndiyo kichocheo kikuu. Twendeni tukasisitize umuhimu wa kuishi kwa amani, upendo na mshikamano. Tukiwasimamia vizuri na kuwaongoza Wananchi katika matumizi ya rasilimali hata kama ni kidogo kiasi gani, Nchi yetu itasonga mbele kimaendeleo na maisha bora kwa Wananchi wetu yatapatikana.

SHUKRANI
Mheshimiwa Spika,
103.    Baada ya kusema hayo, napenda hasa nimalizie kwa kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Nikushukuru kwa namna ya pekee wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri kulingana na Kanuni za Bunge. Aidha, nimshukuru Mwenyekiti, Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala kwa kuongoza vizuri baadhi ya Vikao vya Bunge wakati wa Mkutano huu. Ninawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu ya dhati na yenye Mantiki kwa ajili ya Maendeleo ya Nchi yetu. Niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Watumishi na Wataalam wote wa Serikali waliosaidia kujibu Maswali na hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge na mambo mengine yanayohusiana na Bajeti hii. Vilevile, nawashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kuwapatia Wananchi habari kuhusu Majadiliano yaliyokuwa yanaendelea hapa Bungeni. Wote kwa ujumla wenu nawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika,
104.    Kipekee napenda kuwashukuru Madereva wote ambao wamekuwa makini katika kazi ya kuwaendesha Viongozi wote, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Wataalam kutoka shemu mbalimbali Nchini na kuwawezesha kufika hapa Dodoma kuhudhuria Mkutano huu wa Kumi na Tano. Vilevile, nawashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Dkt. Rehema Nchimbi kwa ukarimu wao kwa muda wote tuliokaa hapa Dodoma. Nivishukuru pia Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo vimehakikisha muda wote tumekaa kwa Amani na Utulivu mkubwa. Mwisho namshukuru Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah na Watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa huduma nzuri zilizowezesha kukamilisha shughuli zilizopangwa katika Mkutano huu bila matatizo.

Mheshimiwa Spika, 
105.    Nitumie fursa hii kuwaombea safari njema mnaporudi katika  maeneo  yenu  ya  kazi. Lakini  pia  niwaombee  kheri  na Baraka  tele Waislamu wote ambao wameanza na wanaendelea na Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kila atakayeamua kufanya Ibada hiyo aifanye kikamilifu na kama Kitabu cha Quran Tukufu kinavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika,
106.    Baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 04 Novemba, 2014 siku ya Jumanne, Saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 16 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika,

107.    Naomba kutoa hoja

No comments:

Post a Comment