Katika kutekeleza kazi ya mbunge ya kuisimamia
Serikali itakumbukwa kwamba tarehe 12 Mei 2014 nilichukua hatua bungeni
ya kutaka Serikali kutatua kwa dharura matatizo katika mtambo wa maji wa
Ruvu Juu yenye kukosesha maji kwa wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam na
Pwani.
Nilitaka kwa mujibu wa Kanuni ya 49 ya
Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la mwaka 2013, Waziri wa Maji Prof
Jumanne Maghembe atoe kauli bungeni juu ya matatizo ya maji katika
maeneo yanayohudumiwa na mabomba kutoka katika mtambo kwa kuweka bayana
iwapo kuna hujuma na kurejesha kwa haraka huduma kwa wananchi.
Kufuatia
hatua hiyo hali ya upatikanaji wa maji iliongezeka katika maeneo
machache ndani ya siku chache lakini kwa sasa katika maeneo mengi
yanayohudumiwa na mabomba kutoka katika mtambo wa Ruvu Juu katika kata
za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara, Saranga, Ubungo na
Makuburi matatizo ya maji yamejirudia.
Katika
kuendelea kutekeleza wajibu wa kibunge wa kuishauri na kuisimamia
Serikali natoa mwito wa wazi kwa wenyeviti wa bodi za Wakurugenzi na
Maafisa Watendaji Wakuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar Es
Salaam (DAWASA) na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ndani ya
siku tatu kusimamia kazi ya dharura kuhusu matatizo ya mtambo wa maji wa
Ruvu Juu yanayoendelea mpaka hivi sasa.
Aidha,
ndani ya siku hizo tatu wajitokeze mbele ya vyombo vya habari kutoa
maelezo kwa umma kueleza kwanini mpaka sasa huduma ya maji katika maeneo
mengi katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar Es Salaam kwa ujumla
yanayohudumiwa na mabomba yanayotoka katika mtambo wa Ruvu Juu hayapati
huduma ya maji inavyostahili na lini matatizo yaliyopo yatapatiwa
ufumbuzi.
Kwa upande mwingine, ndani ya muda
huo huo wa siku tatu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ajitokeze mbele ya
vyombo vya habari na kueleza umma matokeo ya uchunguzi uliopaswa
kufanyika ndani ya mwezi mmoja kubaini kama matatizo ya mara kwa mara ya
Mtambo wa maji wa Ruvu Juu yanatokana na masuala ya kiufundi,
kiuendeshaji au makosa mengine ya kibinadamu.
DAWASA,
DAWASCO na Wizara ya Maji wasipojitokeza ndani ya siku tatu mbele ya
vyombo vya habari kutoa maelezo kwa umma nitachukua hatua za kibunge
nitakazoona zinafaa dhidi ya Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kwa
kulidanganya Bunge kupitia kauli ya Serikali aliyotoa Bungeni mwezi Mei
2014.
Ikumbukwe kwamba tarehe 12 Mei 2014 ikiwa
ni sehemu ya kutimiza wajibu wa mbunge wa kuwawakilisha wananchi
nilieleza Bunge kwamba matatizo katika mtambo wa Ruvu Juu yamekuwa
yakijirudiarudia kwa nyakati mbalimbali kwa kipindi cha takribani miezi
mitatu kati ya Januari mpaka Mei 2014 katika maeneo ambayo awali
yalikuwa yakipata mgawo wa maji.
Nilichukua
hatua hiyo kwa niaba ya wananchi wanaohudumiwa na mtambo huo katika
kata za Kwembe, Kibamba, Mbezi Lois, Msigani, Kimara, Saranga, Ubungo na
Makuburi kwenye Jimbo la Ubungo; na kata mbalimbali za majimbo ya
Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Segerea nk.
Kufuatia
hatua hiyo, Mwezi Mei 2014 Waziri wa Maji Prof. Maghembe alitoa kauli
ya Serikali ya kueleza matatizo yanayoukabili mtambo wa kuzalisha maji
wa Ruvu Juu kwa ajili ya Jiji la Dar es salaam na maeneo ya DAWASA
katika mkoa wa Pwani.
Katika kauli yake Waziri Maghembe
alikiri kwamba kwa takribani siku 67 (kati ya tarehe 01.03.2014 na
tarehe 06.05.2014) mtambo ulizalisha maji chini ya kiwango na kufikia
kati ya lita milioni 8.2 na lita milioni 57.4 ikilinganishwa na lita
milioni 82 kwa siku, ambazo ndio uwezo halisi wa mtambo huo.
Katika
kauli yake bungeni, Waziri Maghembe aliorodhesha matatizo ya mtambo wa
Ruvu Juu kuwa ni: Kuharibika kwa pampu mara kwa mara kunakosababishwa na
uchakavu unaosababishwa na umri kua mkubwa miaka (60), kukatika kwa
Umeme mara kwa mara, maji kuwa na tope jingi sana (turbidity) wakati wa
mvua na mafuriko hali inayopunguza uwezo wa pampu za kusukuma maji na
husababisha kusagika kwa vifaa vya pampu na ugumu wa upatikanaji wa
vipuri halisi (genuine parts). Hata hivyo, Waziri Maghembe hakukiri wala
kukanusha juu ya madai ya kuwepo kwa udhaifu, uzembe, ufisadi na hujuma
katika mitambo ya vyanzo vya maji na mitandao ya mabomba ya maji.
Waziri
Maghembe alieleza Bunge kwamba Wizara imechukua hatua za kutatua
matatizo yaiyopo kwa kuchonga vipuri na vifaa vya pampu katika karakana
zilizopo hapa nchini kwa kuwatumia wataalamu wa jeshi, kuagiza vipuri
nje ya nchi na kutoa matangazo kwa wananchi kuhusu upungufu wa maji pale
uzalishaji unapopungua/kusimama.
Waziri
Maghembe alilieleza bunge kwamba baada ya hatua hizo uzalishaji wa Maji
wa Mtambo wa Ruvu Juu unaendelea kurudi katika hali yake ya kawaida na
kutoa mfano wa kwamba tarehe 17 Mei, 2014 uzalishaji wa maji ulikua lita
milioni 80.3 kwa siku. Aidha, Waziri Maghembe alitoa kauli Bungeni
kwamba Wizara ya Maji imeunda Kamati Maalum ambayo imeanza kufanya
tathmini ya kina juu ya chanzo cha matatizo ya mara kwa mara katika
mtambo wa kusafisha maji wa Ruvu Juu.
Waziri
Maghembe alieleza kwamba kamati hiyo itafanya uchunguzi kubaini kama
matatizo hayo yanatokana na masuala ya kiufundi, kiuendeshaji au makosa
ya binadamu na kuahidi kwamba kamati itatoa taarifa yake katika kipindi
cha mwezi mmoja. Mwezi mmoja umepita tangu nilipohoji bungeni tarehe 12
Mei 2014, hivyo ni wakati muafaka kwa mamlaka zote zinazohusika kuweza
kutoa mrejesho juu ya uchunguzi huo na hatua nyingine za haraka za
kuboresha upatikanaji wa maji safi kama nilivyozieleza katika hoja
binafsi niliyoiwasilisha bungeni kwa niaba ya wananchi tarehe 4 Februari
2013.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
No comments:
Post a Comment