INNOCENT A. NDAYANSE
(ZAGALLO)
0755 040 520 / 0653 593
546
UTANGILIZI
Judith amekuingia
Tanzania baada ya kukutana na Baraki. Hakumpenda kwa dhati, lakini alihitaji
mahali pa kujificha, hivyo akakubali kwa shingo upande. Ungana na msimulizi
wako …
Dakika tano baadaye walikuwa wameshaagana na wahusika wakuu wa mpaka wa
Rwanda na Tanzania. Lori aina ya Fuso lilikuwa barabarani, ndani ya ardhi
ya Tanzania, Baraki akiwa nyuma ya usukani, kando yake kaketi Judith na
kushoto, alikuwa ni msaidizi wake, Livingstone.
Kama kuna jambo ambalo Judith alilihitaji, na likiwa ni jambo ambalo
lingemfariji kwa kiasi kikubwa, ni hilo la kuvuka mpaka na kuingia Tanzania.
“Mungu anipe nini?” alinong’ona kwa sauti ambayo haikuyafikia hata
masikio yake mwenyewe.
Akiwa na ujasiri uliosababishwa na bia alizokunywa sanjari na bangi
aliyovuta, Baraki alitumbua macho barabarani huku mwendo wa gari ukiwa mkali.
Na kila alipohisi usingizi unamnyemelea, aliegesha gari pembezoni mwa barabara,
akateremka na kwenda nyuma ya gari ambako aliwasha msokoto wake na kuvuta
kidogo. Kisha alirudi garini na
kukanyaga tena mafuta.
**********
MAKELLA aliteremka ndani ya teksi, dakika ishirini tu baada ya kuikodi.
Kimoyomoyo Makella alimsifu dereva huyo kwa umahiri wake. Akalisogelea eneo
hilo la mpakani kwa hadhari kubwa. Lilikuwa ni eneo lililochangamka kwa kiasi
kikubwa. Baa mbili maarufu zilikuwa zimefurika watu. Magari manne makubwa ya
mizigo yalikuwa kando ya baa hizo.
Makella hakujiunga na wateja hao. Alimfuata askari mmoja aliyekuwa
akizunguka-zunguka hapa na pale. Akamsalimu na kumuuliza kama ameiona teksi
yoyote katika eneo hilo.
“Teksi?” askari yule aliuliza huku akionyesha mshangao wa mbali.
“Ndiyo.”
“Saa ngapi?”
Makella alifikiri kidogo kisha akajibu, “Siyo zaidi ya nusu saa
iliyopita.”
Ukimya mfupi ukapita. Kisha yule askari akasema, “Yeah. Nadhani nimeiona. Ilipaki hapo,” akaonyesha kwa kidole. Kisha
akaongeza, “Haikukaa sana . Ilimleta mtu na kugeuza.”
Makella akashtuka. “Ulimwona mtu mwenyewe?”
“ Kama sikosei, alikuwa ni mwanamke.”
Haraka Makella akaingia katikati ya mkusanyiko wa watu katika baa
mojawapo. Humo alihaha akiangaza macho huku na kule, kwa huyu na yule hadi
akakata tamaa. Mlengwa wake hakuwemo.
Akaivaa baa ya pili ambako pia alifanya zoezi kama la awali.
Patupu!
Akazidi kuchanganyikiwa. Akaamua kumrudia yule askari.
“Vipi, umemwona?” askari yule alimuuliza huku akimtazama kwa mshangao.
Makella akakataa kwa kutikisa kichwa. Kisha naye akarusha swali,
“Unaweza kukumbuka yule mwanamke alikuwa amevaaje?”
Yule askari wa baa aliguna kidogo, kisha akasema, “Sikujali kuhusu kuvaa
kwake. Lakini alikuwa ni mrefu. Ni Mtutsi. Vipi, kuna tatizo?”
Makella alikunja uso na kuonyesha kufikiri. Kisha, badala ya kujibu kwa
mara nyingine akaibuka na swali: “Una hakika kuwa umewaona wateja wote walioingia?”
“Ndiyo!” askari alisisitiza.
“Na waliotoka?”
“Nimewaona!”
“Sasa huyo mtu atakuwa wapi, maana’ake humo ndani ya baa zote mbili
hayumo!”
Askari alishangaa. “Umeangalia vizuri?”
“Hadi vyooni!”
Askari yule aliguna na kuonekana akifikiri jambo. Kisha ghafla
akaonekana kukumbuka kitu. Akasema, “Lakini kuna watu kama wawili, watatu hivi
wameondoka muda si mrefu kwa Fuso. Mmoja wao alikuwa ni mwanamke.”
“Aaah!” Makella alitamka kwa namna ya kukata tamaa. Kisha akauliza,
“Wamekwenda wapi?”
“Lile gari ni la Watanzania. Huwa linakuja huku mara kwa mara. Na
hufanya safari zake usiku tu. Kwa vyovyote vile leo walikuwa wakirudi Tanzania
.”
“Wana muda gani tangu wameondoka?!” sauti ya Makella ilijaa kitetemeshi
cha hasira.
“ Kama nusu saa hivi.”
Makella alitikisa kichwa kwa masikitiko. Kisha ghafla akasema, “Mambo
yanazidi kuwa magumu…” akasita na kuondoka kwa hatua ndefu akizifuata ofisi za
mpakani. Jibu alilolipata huko likazidi kumchanganya.
“Wamepita hapa muda mrefu kidogo,” mhusika mkuu alimwambia.
“Unaweza kukumbuka yule mwanamke alikuwaje?”
“Ki-vipi?”
“Yaani kimavazi na mwonekano wake kwa jumla.”
“Kwani kuna tatizo gani?” mkuu yule alimbana Makella.
Ilimbidi Makella abuni uongo wa haraka alioamini kuwa ungemsaidia. “Ni mhusika katika tukio la utunguaji wa ndege
iliyomuua Rais,” alisema.
“Khaa! Kumbe…” mkuu wa ofisi hiyo alizidi kushangaa. Kisha akasema,
“Haonyeshi kuwa ni mhusika katika mpango
huo mchafu. Vaa yake na sura yake ni tofauti kabisa na hilo unalosema! Na anaonekana bado ni binti mbichi kabisa!”
“Kwa kifupi unaweza kukumbuka alivyovaa?” Makella alimkata kauli.
“ Sana tu. Alikuwa amevaa T-shirt
ya bluu na sketi nyeusi. Macho yake yamerembuka. Nywele ni nyingi, zimeshuka
hadi mabegani.”
Makella alitikisa kichwa akionyesha ishara ya kukubali. Kisha akasema, “
Ni mwenyewe.”
“I see,” yule mkuu wa ofisi alitamka kwa masikitiko. Akaongeza, “Saa hizi
watakuwa mbali.”
“Najua, lakini ipo siku atapatikana tu,” Makella alisema huku akiondoka.
“Itabidi tuwasiliane na Serikali ya Tanzania haraka iwezekanavyo. Na kwa
Tanzania atakamatwa tu. Hana ujanja!”
Ilikuwa imetimu saa 6 usiku. Kwa Makella, ulikuwa ni usiku mbaya zaidi.
Kwa namna nyingine alihisi Mungu hayuko upande wake. Hata hivyo, wakati
akiirudia teksi ili arudi mjini, moyoni alikuwa akiamini kuwa ipo siku
atakayomtia mkononi mbaya wake.
“Judith…! Judith…!” alitamka
kwa hasira wakati akifungua mlango wa teksi na kuingia.
Itaendelea kesho…
No comments:
Post a Comment