INNOCENT A. NDAYANSE
(ZAGALLO)
0755 040 520 / 0653 593
546
UTANGULIZI
Judith amekutana
na wanaume wawili ambao anatambua kwamba ni Watanzania na wako na lori la
mizigo. Anakubali kuwa nao ili tu afanikishe azma yake ya kutoroka mikononi mwa
Makella. Makella naye anazidi kuchanganyikiwa na hata anapokutana na mkuu wake
anaonekana mwenye mawazo. Je, Judith atafanikiwa kufika salama Tanzania? Vipi Makella
atachukua uamuzi gani? Ungana na msimulizi wako …
Muda mfupi baadaye walikuwa pamoja, Luteni Kasa akinywa bia na Makella
akinywa maji.
“Uko kazini?” hatimaye Luteni Kasa alimwanza.
“Ndiyo,” Makella alijibu, kisha akafuatisha hadithi nzima ya operesheni
dhidi ya Watutsi mchana kutwa lakini akiepuka kuuweka bayana ukweli wa
kilichomsibu dakika chache zilizopita.
“Ok, lakini siyo vizuri
kujiamini kiasi cha kutembea peke yako eti kwa kuwa una silaha,” Luteni Kasa
alimwonya. “Ni vyema kama mngekuwa wawili, watatu hivi. Ukiwa peke yako kama
hivi, adui akikuona na silaha atakuwahi.”
“Ni kweli, lakini kuna sababu iliyonifanya niwe peke yangu.”
“Sababu gani?”
“Namfuatilia shushushu mmoja wa
Kitutsi.”
“Shushushu?!”
“Ndiyo. Tena ni mwanamke!”
“Mwanamke?!” Luteni alimkazia macho Makella. Akairejesha mezani glasi ya
bia iliyokuwa mikononi. Kisha akaongeza, “Una hakika kapita hapa au
unabahatisha?”
“Taarifa nilizonazo zinanifanya niamini kuwa amepita hapa!” Makella
alisisitiza.
Kimya kifupi kilitawala. Luteni Kasa akamtumbulia zaidi macho, Makella.
Kisha: “Nina zaidi ya saa nzima niko hapa nje. Huyo mtu kapita muda gani?”
“Siyo zaidi ya robo saa.”
“Kavaaje?”
“Fulana ndefu ya bluu na sketi nyeusi.”
“Kichwani?”
“Ana nywele ndefu zilizomwagika hadi mabegani.”
Tabasamu la mbali likamtoka Luteni Kasa. Akasema, “Nadhani nimemwona.”
“Afande, umemwona?” Makella akamtolea macho.
“Ndiyo, na nadhani ni mwenyewe.”
“Yuko wapi?”
“Hapa hakukaa,” Luteni Kasa alijibu kwa utulivu. Akaongeza, “Kawaulize
hao madereva teksi. Nadhani watakuwa na jibu la kukuridhisha.”
Makella aligugumia maji na kuitua chupa mezani ikiwa tupu. Kisha
akanyanyuka na kutoa saluti nyingine, saluti ambayo kama ile ya awali, hii pia Luteni Kasa
alionyesha kutoijali, zaidi alitamka neno moja tu: “Asante.”
Makella akatoka. Moja kwa moja hadi kwenye teksi ambayo dereva wake
alikuwa nje, kaegemea bodi. Akazungumza naye kwa kifupi tu na kuambiwa kuwa
mwanamke huyo alikodi teksi na kuelekea mashariki mwa nchi.
“Labda anakimbia hizi vurugu,” dereva huyo alimalizia.
“Teksi hiyo imeelekea kule mpakani?”
“Inawezekana.”
Makella alifikiri kidogo kisha akauliza, “Una mafuta ya kutosha?”
“Full tank.”
“Ok, twende. Chaji yako
utaileta hapa kwa afande, Luteni Kasa. Sawa?”
Haikuwa rahisi kwa dereva huyo kupinga amri ya Makella. Kwa siku hiyo,
kila askari wa jeshi alikuwa na sauti. Kama dereva huyo angekataa, isingemwia
vigumu Makella kumshindilia risasi na kumchukua dereva mwingine. Angeweza, na
asingetokea mtu yeyote wa kumuuliza chochote!
**********
KICHWA cha Judith kilikuwa kizito. Aliuhisi uzito huo kutokana na mambo
yaliyoisumbua akili yake. Kumbukumbu ya mauaji yaliyotokea usiku huo, saa
chache zilizopita zilimganda akilini. Hakujisikia kuwa yu binadamu wa kawaida,
wala hakuwa na hamu ya kuendelea kuishi. Kuuawa kwa wazazi wake na wadogo zake
kulimwathiri kisaikolojia kwa kiwango kisichokadirika.
Isitoshe, ni muda mfupi tu uliopita alipomtoroka Makella huku akiwa
amemwibia dola 2,000 za Marekani, tendo aliloamini kuwa lingeweza kumletea
matatizo zaidi, hata kuyahatarisha maisha yake.
Kwa hali hiyo, alihitaji usalama, na usalama huo uwe wa uhakika. Hapo
alipo, bado hakujiona kuwa yu katika sehemu nzuri kwa usalama wake. Lakini
afanye nini? Hakuwa na la kufanya. Akalazimika kusubiri muda ambao Baraki
ataamua waondoke huku kimoyomoyo akiomba Mungu, Makella asitokee.
Alikunywa bia huku akiilazimisha
nafsi yake kutii utomasaji wa Baraki katika chuchu za matiti yake na wakati
mwingine mkono ukivuka hadi mapajani ambako ulitulia na kuyapapasa-papasa.
Japo eneo waliloketi halikuwa na mwanga, hata hivyo halikuwa likistahili
kuchukuliwa kuwa ni maficho kamili, eneo ambalo mtu yeyote mwingine ambaye
angefika hapo angeshindwa kuwaona. Kwa
vyovyote vile, mtu ambaye angelisogelea eneo hilo kwa umbali wa hatua tano
kutoka kwenye meza hiyo, kama anamfahamu Judith, angeweza kumtambua. Ni taswira
hiyo ambayo Judith hakuipenda, na hakuipenda kwa kuwa alihofia kukutwa hapo na
Makella.
Mara Baraki aliacha kumpapasa. Akaitazama saa yake na kusema, “Nadhani
huu ni muda mwafaka. Saa nne! Twende na bia zetu garini, na nyingine ziko
hukohuko. Sidhani kama tutazimaliza.”
Yalikuwa ni maneno ambayo Judith aliyahitaji, zaidi ya hizo bia au jambo
jingine lolote. Hakuhitaji bia, alihitaji kuwa mbali na Makella. Hakumhitaji
Baraki, alihitaji kuwa mbali na Makella! Aliyahitaji maficho!
Kwa furaha ambayo ilifurika moyoni na kufanikiwa kutoiweka hadharani,
aliitwaa chupa na kuipeleka kinywani. Safari hii hakunywa, alimimina! Alipoitua
chupa hiyo mezani, ilikuwa tupu. Sasa akamtazama Baraki kwa namna nyingine
kabisa, macho yake yakitoa shukrani za dhati.
Baraki akiwa hayajui yaliyomo moyoni mwa Judith, alivutiwa na macho
hayo, akamvuta na kumbusu shavuni. Hakuishia hapo, akajaribu kupenyeza ulimi
kinywani mwa Judith, jaribio ambalo safari hii Judith hakulizuia, akafuata ule
usemi wa ‘mtaka cha uvunguni.’
Wakakutanisha midomo yao na kudumu katika busu hilo kwa sekunde kadhaa,
Baraki akipata burudani halisi ilhali Judith akiwa katika starehe bandia.
Itaendelea kesho…
No comments:
Post a Comment