Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 30 June 2014

BRAZIL YATWAA KOMBE LA DUNIA KWA KUICHAPA UJERUMANI 2-0 JAPAN 2002

File:NISSANSTADIUM20080608.JPG
Uwanja wa International jijini Yokohama, Japan ulikofanyikia mchezo wa fainali mwaka 2002

Na Daniel Mbega

Tunaendelea kujikumbusha mambo mbalimbali ya fainali za Kombe la Dunia ambapo leo ni miaka 12 tangu Brazil ilipoichapa Ujerumani katika mchezo wa fainali na kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya tano.
Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa International, Yokohama nchini Japan mwaka 2002 ulihudhuriwa na watazamaji 69,029 na ulichezeshwa na 'Kipara' Pierluigi Collina wa Italia aliyesaidiwa na Leif Lundberg (Sweden) na Philip Sharp (England), wakati mwamuzi wa akiba alikuwa Hugh Dallas (Scotland).
Huu ndio ulikuwa mchezo wa kwanza na pekee mpaka sasa baina ya nchi hizo mbili katika historia ya Kombe la Dunia. 
Brazil ilishinda mchezo huo kwa mabao 2–0, huku mshambuliaji wake nyota Ronaldo (ambaye hakufanya vizuri katika fainali za mwaka 1998 kule Ufaransa), aliyeweka rekodi ya ufungaji mabao kwenye Kombe la Dunia mwaka 2006, alifunga mabao mawili kati ya mabao yake 15 ya Kombe la Dunia kwenye kipindi cha pili cha mchezo huo, akaiongoza Brazil kutwaa ubingwa na yeye akatwaa Kiatu cha Dhahabu. 
Pia mechi hiyo ilimfanya nahodha wa Brazil Cafu kucheza mchezo wa fainali wa tatu mfululizo, rekodi ambayo bado haijafikiwa na mchezaji mwingine yeyote katika historia ya mashindano.
Timu zote zilikuwa zimeongoza katika makundi yao kabla ya kwenda kwenye mtoano, ambako Ujerumani iliwafunga wapinzani wake wote na kufuzu fainali, wakati Brazil iliruhusu bao moja tu kwa England. 
Ujerumani iliwaondoa Marekani na wenyeji-wenza Korea Kusini, wakati Brazili iliitoa England.
Taji hilo la tano la Brazil kwenye Kombe la Dunia hakuna timu ambayo imeifikia rekodi hiyo, na katika mechi hiyo Brazil ikaweka rekodi ya kushinda mechi zote saba bila kuingia katika muda wa nyongeza au penalti. 
Ujerumani ilipoteza mchezo wa fainali kwa mara ya nne, na kuweka rekodi nyingine ya Kombe la Dunia. Walikuwa wamejiandaa kuifikia rekodi ya Brazil ya kutwaa taji hilo mara nne, kwani mpaka wakati huo ilikuwa imetwaa mara tatu.
Katika fainali hizo Ujerumani ilikuwa Kundi E pamoja na Jamhuri ya Ireland, Saudi Arabia na Cameroon na katika mechi yao ya kwanza waliichabanga Saudi Arabia mabao 8-0 kwenye Uwanja wa Sapporo Dome huku Miroslav Klose akipiga hat-trick. 
Katika mechi yao ya pili Ujerumani iliongoza kwa muda mrefu kwa bao 1-0, lakini katika dakika za majeruhi Robbie Keane akaisawazishia Ireland. Ikiwa inahitaji ushindi ili iongoze kundi hilo, Ujerumani ikaichapa Cameroon 2-0 kwenye Uwanja wa Shizuoka, huku Klose akifunga bao lake la tano la mashindano lililomfanya aibuke mfungaji bora.
Katika hatua ya mtoano Ujerumani ilipambana na Paraguay na kuifunga 1-0 kabla ya kutoa kipigo kama hicho kwa Marekani katika robo fainali.
Ujerumani ilikutana na Korea Kusini kwenye nusu fainali katika mchezo ambao ilijihami zaidi. Kabla ya kupatikana kwa bao lolote, Michael Ballack wa Ujerumani akapewa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 71 na kumfanya akose mchezo unaofuata. Lakini ni Ballack huyo aliyefunga bao la ushindi dakika nne kabla ya mchezo kumalizika.
Brazil yenyewe ilikuwa Kundi C pamoja na China, Costa Rica na Uturuki. Kufuatia kupoteza mchezo wa fainali mwaka 1998, Brazil ilikuwa na kocha mpya, Luiz Felipe Scolari, ambaye alikuja na staili ya kucheza kwa kutumia nguvu.
Katika mchezo wa kwanza na Uturuki Brazil ilishinda kwa mabao 2-1 na mchezo uliofuata dhidi ya China kwenye Uwanja wa Ulsan Munsu ikapata ushindi wamabao 5-2 yaliyofungwa na Roberto Carlos, Rivaldo, Ronaldinho, na Ronaldo akifunga mawili.
Katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Costa Rica wakapata ushindi mwingine wa mabao 5-2, Ronaldo akifunga mawili.
Kwenye hatua ya mtoano Brazil ilikumbana na washindi wa pili wa Kundi H Ubelgiji ambapo Rivaldo na Ronaldo waliipatia ushindi wa mabao 2-0 na kukumbana na kibarua cha England kwenye robo fainali. Michael Owen aliifungia England katika dakika ya 23 lakini Rivaldo na Ronaldinho wakafunga na kuipatia ushindi wa 2-1 ingawa Ronaldinho alitolewa nje.
Kwenye nusu fainali Brazil ikakutana na Uturuki kwa mara ya pili katika Uwanja wa Saitama na Ronaldo akafunga bao katika dakika ya 49 lililoisukuma Brazil fainali.
Zaidi ya nchi 200 ziliutangaza mchezo wa fainali kupitia radio na televisheni ambapo kwa ujumla wake vituo 232 vya TV viliuonyesha ikiwa ni rekodi mpya kabla haijavunjwa mwaka 2006. Zaidi ya watazamaji milioni 63 waliutazama mchezo huo kupitia kwenye luninga.
Vikosi vya siku hiyo vilikuwa; Ujerumani: Oliver Kahn (nahodha), Thomas Linke, Carsten Ramelow, Christoph Metzelder, Torsten Frings, Dietmar Hamann, Jens Jeremies/Gerald Asamoah 77', Marco Bode/Oliver Bierhoff 74', Bernd Schneider, Miroslav Klose (kadi ya njano 9')/Christian Ziege 84', Oliver Neuville. Kocha alikuwa Rudi Völler.
Brazil: Marcos, Lúcio, Edmílson, Roque Júnior (kadi ya njano 6'), Cafu (nahodha), Gilberto Silva, Kléberson, Roberto Carlos, Ronaldinho/Juninho 85', Rivaldo, Ronaldo/Denílson 90'. Kocha alikuwa Luiz Felipe Scolari, ambaye anaifundisha tena mwaka huu.

Ujerumani yalichabanga Argentina 4-2
Lakini siku kama ya leo, mwaka 2006 kule Ujerumani, wenyeji walifanikiwa kuvuka hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Argentina baada ya matokeo ya dakika 120 kuwa bao 1-1.
Huu ndio ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Argentina kufungwa kwa penalti kwenye Kombe la Dunia: mpaka kufikia mechi hiyo Argentina na Ujermnai zilikuwa zimeshiriki mara tatu katika upigaji wa penalti, na zote zikashinda.
Mjini Gelsenkirchen, England ilikumbana na Ureno na Wayne Rooney akatolewa nje, Ureno ikashinda kwa mikwaju ya penalti 3-1 baada ya matokeo ya dakika 120 kuwa 0-0 hivyo ikasonga mbele kwenye nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu zama za Eusébio miaka 40 nyuma, na kumhakikishia kocha Luiz Felipe Scolari ushindi wake wa tatu mfululizo wa robo fainali dhidi ya kikosi cha England chini ya Sven-Göran Eriksson.
Julai Mosi Italia iliifunga Ukraine 3-0 iliyofuzu kwa mara ya kwanza kwenye robo fainali. Ufaransa ikaichapa Brazil 1–0. Brazil ilipiga shutimoja tu golini katika mechi hiyo ambayo ilishuhudia 'uchawi' wa chenga kwenye kiungo wa Zinedine Zidane ambaye pasi yake ya mpira wa adhabu kwa Thierry Henry ndiyo iliyozaa bao la ushindi.

Hungary yaifunga Uruguay 4-2
Aidha, tarehe kama ya leo miaka 60 iliyopita, yaani mwaka 1954, ulichezwa mchezo wa nusu fainali baina ya Hungary na Uruguay ambapo Hungary ilishinda kwa mabao 4-2 baada ya dakika 120.
Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Stade Olympique de la Pontaise, jijini Lausanne, Uswisi na kuhudhuriwa na watazamaji 37,000, ulichezeshwa na mwamuzi Benjamin Griffiths kutoka Wales.
Mabao ya Hungary yalifungwa na Czibor 13', Hidegkuti 46', na Kocsis 111', 116' wakati yale ya Uruguay yalifungwa na Hohberg 75', 86'.
Katika nusu fainali ya pili siku hiyo, Ujerumani iliichakaza Austria kwa mabao 6-1 katika Uwanja wa St. Jakob, mjini Basel mbele ya watazamaji 58,000 huku mwamuzi akiwa Mtaliano Vincenzo Orlandini.
Mabao ya Wajerumani yalifungwa na Schäfer 31', Morlock 47', F. Walter 54' (pen.), 64' (pen.), na O. Walter 61', 89' wakati lile la Austria lilifungwa na Probst 51'.
Hatimaye Ujerumani ndiyo iliyotwaa ubingwa mwaka huo kwa kuifunga Hungary 3-2 kwenye fainali, huku mabao yake yakifungwa na Morlock 10', Rahn 18', 84', na yale ya Hungary yakifungwa na Puskás 6' na Czibor 8'.
Mchezo huo uliofanyika Julai 4 katika Uwanja wa Wankdorf mjini Bern mbele ya watazamaji 60,000 ulichezeshwa na Mwingireza William Ling.
Mfungaji bora wa mashindano hayo alikuwa Sándor Kocsis wa Hungary aliyezifumania nyavu mara 11.

Argentina 1-2 Brazil
Kwa siku kama ya leo, miaka 40 iliyopita katika fainali zilizofanyika Ujerumani Magharibi, Argentina ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Brazil katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Niedersachsenstadion, mjini Hanover na kuhudhuriwa na mashabiki 38,000.
Mchezo huu wa raundi ya pili uliochezeshwa na mwamuzi Vital Loraux wa Ubelgiji ulishuhudia Brazil ikianza kufunga kupitia kwa Rivellino katika dakika ya 32 kabla ya Brandisi kusawazisha dakika ya 35. Jairzinho aliipatia Brazil bao la ushindi dakika ya 49.
Katika mchezo mwingine wa mtoano, Ujerumani Mashariki nayo ilichapwa mabao 2-0 na Uholanzi ambayo yalifungwa na Neeskens katika dakika ya 7 na Rensenbrink dakika ya 59.
Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Parkstadion, Gelsenkirchen ukihudhuriwa na watazamaji 67,148, ambapo mwamuzi alikuwa Rudolf Scheurer wa Uswisi.
Siku hiyo Poland nayo ikicheza kwenye Uwanja wa 
Waldstadion, jijini Frankfurt mbele ya watazamaji 55,000, iliweza kuichapa Yugoslavia mabao 2-1 kupitia kwa Deyna aliyefunga kwa penalti dakika ya 24 na Lato dakika ya 62, wakati Karasi aliifungia Yugoslavia dakika ya 43. Mwamuzi alikuwa Rudi Glöckner wa Ujerumani Mashariki.
Wenyeji Ujrumani Magharibi, ambao ndio baadaye walikuja kuwa mabingwa, siku hiyo waliichabanga Sweden kwa mabao 4-2 katika Uwanja wa Rheinstadion, huko Düsseldorf mbele ya mashabiki 66,500.
Wafungaji wa Ujerumani walikuwa Overath dakika ya 51, Bonhof dakika ya 52, Grabowski dakika ya 76 na Hoeneß alifunga kwa penalti dakika ya 89, wakati yale ya Sweden yalifungwa na Edström   dakika ya 24 na Sandberg dakika ya 53. Mwamuzi alikuwa Pavel Kazakov wa Urusi.

Argentina yashinda kwa matuta
Mabingwa watetezi, Argentina, siku kama ya leo miaka 24 iliyopita (mwaka 1990) kule Italia ilijikuta ikivuka kwa mbinde hatua ya robo fainali mbele ya Yugoslavia ambayo ilicheza na watu 10 kwa dakika 90.
Baada ya dakika 120 bila bao ikabidi mikwaju ya penalti ipigwe, ndipo Argentina ikavuka kwa mikwaju 3-2, huku penalti ya Diego Maradona ikiokoloewa.
Aliyewaokoa Argentina siku hiyo ni kipa Sergio Goycochea (aliyechukua nafasi ya Nery Pumpido aliyevunjika mkuu katika hatua ya makundi) ambaye aliokoa penalti mbili za Yugoslavia huku Pedro Troglio akiwa ameikosesha Argentina penalti nyingine ambayo ingewatoa mashindanoni.
Ireland nayo ilibanjuliwa na Italia kwa bao 1-0 la Salvatore Schillaci katika hatua hiyo, wakati ambapo Ujerumani Magharibi waliichapa Czechoslovakia bao 1-0 ka mkwaju wa penalti wa Lothar Matthäus.
Mechi iliyokuwa inatazamwa na wengi siku hiyo ya Juni 30 ilikuwa baina ya England na Cameroon, ambayo ilikuwa imeonyesha maajabu makubwa kwenye fainali hizo.
Ndiyo mechi pekee ya robo fainali ambayo ilikuwa na goli zaidi ya moja, kwani England ilishinda kwa mabao 3-2 baada ya dakika 120.
Kwanza England ilipata bao kupitia kwa David Platt katika dakika ya 25. Lakini baada ya mapumziko mkongwe Roger Milla akaingizwa na kuubadili mchezo ndani ya sekunde tano ambapo Cameroon walipata penalti iliyofungwa na Emmanuel Kunde. Baadaye katika dakika ya 65, Eugene Ekeke akafunga bao la kuongoza. Waafrika wakajua wanakwenda nusu fainali, lakini wakasababisha penalti ambayo ilifungwa na Gary Lineker. Katikati ya muda wa ziada, England wakapata penalti nyingine ambayo ilifungwa na Lineker na wakauzu kwa nusu fainali.

Croatia yaicharaza Romania
Siku kama ya leo, lakini mwaka 1998 ule Ufaransa, Croatia ikishiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia iliicharaza Romania kwa bao 1-0 katika mchezo wa robo fainali baolililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Davor Šuker katika dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza. Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Parc Lescure, mjini Bordeaux mbele ya mashabiki 31,800 na ulichezeshwa na Javier Castrilli wa Argentina.
Mchezo mwingine wa siku hiyo ulikuwa baina ya Argentina na England ambazo hadi dakika 120 zinamalizika matokeo yalikuwa 2-2. Gabriel Batistuta aliifungia Agentina bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti dakika ya 6, lakini Alan Shearer akasawazisha kwa penalti dakika ya 10 kabla ya Michael Owen kuongeza la pili dakika ya 16. Zanetti alisawazisha mambo kwenye dakika ya 45, matokeo ambayo yalidumu hadi dakika 120 zinamalizika.
Katika mikwaju ya penalti, Argentina ilipata nne na England wakapata tatu, hivyo Waingereza wakatolewa. Mchezo huo ulifanyika kwenye Uwanja wa Geoffroy-Guichard, mjini Saint-Étienne mbele ya watazamaji 30,600 na ulichezeshwa na  Kim Milton Nielsen wa Denmark.


No comments:

Post a Comment