Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 29 June 2014

RIWAYA TAMU: JUDITH…JUDITH…! - 16



INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

0755 040 520 / 0653 593 546 

UTANGILIZI
Judith yuko ndani ya Fusso ambalo amepanda kama msaada kwake kutoka Rwanda kuja Tanzania. Baraki, dereva wa Fuso hilo amezama katika mapenzi ingawa Judith mwenyewe moyo wake haupo kwenye mapenzi zaidi ya kutafuta hifadhi. Wameingia Biharamulo na Baraki anachukua chumba na kumkaribisha Judith ndani. Je, nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako …

Kwa hali hiyo aliamua jambo moja kwa faida yake; kumfurahisha Baraki usiku huo. Na ndivyo ilivyokuwa; Baraki aliuona usiku huo kuwa ni mzuri kupindukia, viungo vyake vikiburudika huku nafsi ikiliwazika. Kwa upande wa Judith, yeye kwake ulikuwa ni usiku wenye adha aliyolazimika kuivumilia japo pia alilazimika kumridhisha Baraki kwa kila hali, akitoa ushirikiano wote uliohitajika.
Waliingia jijini Dar es Salaam saa 4 asubuhi, siku ya sita baada ya usiku huo. Mara tu gari lilipoegeshwa kwa tajiri wa Baraki eneo la Tabata Dampo, Baraki na Judith waliondoka pamoja hadi Magomeni Kondoa ambako Judith alipatiwa chumba katika gesti moja ya hadhi ya kati.
“Usihofu, utaishi hapa kwa muda bila matatizo yoyote,” Baraki alimwambia. “Mimi naishi mbali kidogo, na nina mke. Lakini hilo lisikutishe. Hutapata shida yoyote. Tuko pamoja baby.”
Alipokwishasema hayo, alimpatia shilingi 30,000 huku akiongeza, “Za chakula cha mchana. Kama unasikia njaa, hapo nje kuna chipsi na kuku. Nikuchukulie?”
Judith alikataa kwa kutikisa kichwa. Kisha akasema, “ Asante, mpenzi. Lakini kwa sasa sijisikii kula. Nimechoka sana, labda baadaye .”
Ok, kaoge, upumzike,” Baraki alisema huku akimbusu katika shavu la kulia. Akaongeza,  “Muda huu ngoja nirudi ofisini, usihofu kitu. Hutapata matatizo yoyote.”
Akatwaa kalamu na karatasi kisha akaandika tarakimu kadhaa na kumpatia Judith karatasi hiyo, akisema, “Hii ni namba yangu ya simu. Ukiwa na shida yoyote unipigie.  Kama leo hatutaonana, basi kesho asubuhi nitakuja. Na, nadhani inabidi uwe na simu. Suala hilo nitalishughulikia kesho hiyohiyo.”
“Nitashukuru sana, baby,” Judith alisema huku naye akimbusu shavuni.
Kisha Baraki alimfuata mhudumu wa gesti na kumwambia, “Yohana, mgeni wangu asipate shida yoyote. Nimekuachia kazi hiyo wewe. Kukiwa na tatizo lolote, unitaarifu. Sawa?”
“Poa tu, wala usikonde, msh’kaji wangu.”

******

JUDITH  aliachwa peke yake. Akawa peke yake chumbani, na akawa peke yake Magomeni. Aliketi  kitandani na kushusha pumzi ndefu, akivuta kumbukumbu ya matukio ya kutisha na kusikitisha yaliyomkuta ile siku asiyoisahau, siku ambayo baba, mama na wadogo zake watatu waliuawa kikatili mbele yake, nyumbani,  mjini Kigali, Rwanda saa 2 usiku.
Machozi yakamtoka! “Nimebaki peke yangu!” alinong’ona huku akiendelea kulia. Ndiyo,  alikuwa katika kipindi kigumu maishani. Hakujua nini kitafuata. Japo alifanikiwa kumtoroka Makella, hata hivyo hakuwa na dira yoyote mbele yake.
Dakika takriban kumi zilikatika akiwa hapo kitandani akiwaza hili na lile, mawazo ambayo hayakumpa mwanga wowote wa mafanikio mbele yake.
Hatimaye akapiga moyo konde na kujipa ujasiri, akinong’ona, “Kama ni kufa bora nifie huku. Wazazi wangu na wadogo zangu wameuawa na hata makaburi yao sitayaona, bora hata na mimi nife. Kifo changu hakitakuwa cha ajabu!”
Akasimama na kuchojoa nguo zake, na ndipo alipobaini kuwa bado alikuwa na mtihani mbele yake. Hakuwa na nguo nyingine zaidi ya hizo. Lakini alikumbuka kuwa alikuwa na dola 2,000, isitoshe, Baraki alipoondoka alimwachia shilingi 30,000 za Tanzania .
Akatwaa zile shilingi 30,000 na kuvaa tena nguo zake. Akaenda mapokezi ambako baada ya kuzungumza na mhusika, akapata msaada aliouhitaji.
“Subiri nikuitie mtu wa kukusaidia,” aliambiwa.
Muda mfupi baadaye aliondoka na binti mmoja mcheshi ambaye alimwongoza hadi soko kuu la Magomeni, eneo ambalo Judith alitarajia kupata nguo.
Wakiwa njiani, msichana yule aliyeitwa Swaumu alimdadisi, “Kwani umetokea wapi?”
Akili ya Judith ilifanya kazi haraka. Hakutaka kusema kweli kwani aliamini kuwa kwa kufanya hivyo atakuwa amejiweka katika mazingira magumu zaidi. Akaukumbuka mji wa Kahama ambako walilala siku mbili wakiwa njiani kuja Dar.
“Kahama,” alimjibu.
“Kahama?”
“Ndiyo.”
“Sasa huku umekuja kibiashara au?”
“Ndiyo,  kwa mambo ya biashara.”
“Lakini ulishakuja Dar hapo kabla?”
“Hapana. Hii ndiyo mara yangu ya kwanza.”
“Umeleta biashara gani?”
“Sikuleta biashara, nimekuja kuangalia vitu vitakavyofaa kupeleka Kahama.”
Ok,” Swaumu alionyesha kuridhika.
Kutoka hapo Magomeni Kondoa hadi sokoni ziliwachukua takriban dakika ishirini. Swaumu akampeleka hadi kwenye eneo lililotawaliwa na wauza nguo. Hapo Judith akanunua blauzi tatu, sketi mbili na nguo chache za ndani. 20,000/- zikawa zimekatika!
“Kwa nini hukuja na nguo?” Swaumu alirudia kudadisi.
Akiwa amekereka kwa maswali ya Swaumu, Judith aliachia tabasamu bandia kisha akajibu, “Ilikuwa ni safari ya ghafla.” Na katika kuhakikisha kuwa Swaumu haendelei kumsumbua kwa maswali naye alimuuliza, “Hivi huku kuna sehemu ya kubadili pesa?” 
“Pesa?” Swaumu alimtazama kwa mshangao. “Pesa gani? Una dola?”
“Ndiyo,” Judith alijibu huku kwa kiasi fulani akijilaumu kwa kuuliza hivyo. Kwa kuwa aliona kuwa ‘maji yamekwishamwagika,’ aliongeza uongo, “ Nina dola tano. Nitazibadilishaje?”
“Ni kazi ndogo sana hiyo,” Saumu alijibu. “Kariakoo au katikati ya jiji kuna maduka mengi tu ya kubadilisha pesa. Uwe na Dola, Yen, Pauni, Yuro na nyingine zote utapata tu. Wala us’konde. Vipi, twende  town?”
“Hapana,” Judith alipinga haraka. Akaongeza, “Tufanye kesho, au unaonaje?”
“Poa tu.”

Itaendelea kesho…



No comments:

Post a Comment