INNOCENT A. NDAYANSE
(ZAGALLO)
0755 040 520 / 0653 593
546
UTANGULIZI
Judith ametoroka
mikononi mwa Makella na amechukua teksi ili impeleke mpakani. Makella amechanganyikiwa
baada ya kuambiwa kwamba binti huyo ametoroka. Judith anafika mpakani na
kukutana na wanaume wawili ambao baadaye wanamkaribisha kinywaji. Je, nini
kitaendelea? Makella atafanya nini? Judith naye anaelekea wapi? Ungana na
msimulizi wako …
Baraki hakukubali, akanyanyuka na kumfuata. Na ni hapo sentensi hii na
ile ilipowaunganisha. Katika zungumza hiyo ndipo Baraki alipojua kuwa Judith
alikuwa ni mtoto yatima. Hakuwa na baba wala
mama, na ndugu zake wote walikwishauawa.
Lakini Judith hakusema kuwa mauaji hayo yalifanyika kwa usiku huo. Kwa
kuwa ujasiri ulikwishamwingia, alijitahidi kuwa makini kwa kila jambo sanjari
na kutoonesha bayana usoni kuwa kuna madhila yaliyomkuta.
Maongezi yao yaliponoga ndipo Judith alipogundua kuwa watu hao walikuwa
ni Watanzania na walikuwa safarini usiku
huo.
“Kumbe nyie ni Watanzania?” alimuuliza Baraki ambaye wakati huo mkono wake mmoja ulikuwa umetua kwenye bega
la Judith.
“Ndiyo, sisi ni Watanzania,” Baraki alijibu. “Tunakukaribisha kwetu
Tanzania, upaone. Hakuna fujo, ni amani
tupu. Kwani wewe ni kabila gani? Mhutu au Mtutsi?”
Judith alisita kidogo kisha kwa sauti ya chini akajibu, “Mtutsi.”
“Ok, nd’o maana ni mzuri,”
Baraki alisema huku akitabasamu na kumtazama kwa namna ya kipekee, wakati
huohuo, mkono uliogota begani sasa ukimpigapiga.
Judith aliguna na kutwaa chupa ya bia, akanywa funda moja kubwa kisha akairejesha mezani. Akahisi kitu
kikimnong’oneza kichwani: ‘Hii ndiyo
nafasi yako. Itumie kikamilifu.’ Papohapo akamtupia macho Baraki na kuachia
tabasamu la kirafiki, zaidi ya lile tabasamu la urafiki wa kawaida. Yale macho
yake yanayobembeleza na kushawishi yakamsisimua Baraki kiasi cha kumpa nguvu ya
kuendeleza hoja yake.
“Judith, twende Tanzania,” yalimtoka Baraki kwa sauti yenye kigugumizi
cha mbali.
“Siyo kwamba nakataa. Hata mimi huwa napenda sana kwenda Tanzania
kutembea. Nasikia huko kwenu hakuna mambo ya ukabila wala udini japo makabila
ni mengi sana na dini ni nyingi sana…”
“Yeah,” Baraki alimkata kauli. “Kwa kweli Tanzania ni
kisiwa cha amani na utulivu. Kuna makabila zaidi ya mia moja, lakini hayaleti
mtafaruku wowote! Nashangaa hapa kwenu kuna makabila mawili tu lakini duu!”
Judith aliinamisha kichwa kwa huzuni. Kumbukumbu ya mauaji ya wazazi
wake ikamrudia kichwani kwa nguvu kubwa kiasi cha kujikuta akibubujikwa machozi
bila ya kujitambua.
Baraki aliiona hali hiyo na haraka akamuuliza, “Kwa nini unalia Judith?
Samahani sana kama kwa kukwambia hivyo nimekuudhi.”
Judith alishtuka na kujifuta machozi haraka. Hakutaka Baraki ajue
chochote cha ziada; kwamba siku hiyo wazazi wake waliuawa na kwamba alikuwa na
Makella na akafanikiwa kumtoroka huku akiwa amemwibia dola 2,000! Ndiyo,
alipanga kuwa hiyo iwe ni siri yake!
“Judith…” Baraki alimwita huku akimwinamia.
“Baraki usijali, ” Judith alimwahi. “Nimekumbuka mbali.”
“Umekumbuka nini, Judith?”
“Mwaka jana kuna mtu aliniambia kuwa niende kujiendeleza kimasomo huko
Tanzania, nikakataa. Leo yeye mwenzangu mambo yake mazuri. Nasikia amemaliza
Chuo cha Biashara na tayari anafanya kazi.”
“Ooh pole sana,” Baraki alisema. “Sasa unasemaje mtoto mzuri. Hauko
tayari kwenda na sisi?”
Judith aliachia tabasamu la kirafiki na kumtazama Baraki kwa yale macho
yake yanayoshawishi. Kwa ujumla alikuwa akitaka kuipata nafasi hiyo muhimu ya
kwenda nje ya nchi. Amtoroke haraka Makella!
Hali hiyo ilimpa nguvu zaidi Baraki, na sasa aliutupa mkono wake juu ya
paja laini la Judith. Akautelezesha kwa namna isisimuayo. Judith akaguna na
kuushika mkono huo, akiuzuia kuendelea na ziara yake.
Lilikuwa ni zuio ambalo hata Baraki aliona kuwa ni la bandia. Hivyo,
zaidi alimsogelea na kumbusu sikioni. Judith akaguna na kuruka kidogo. “Jamaani…”
“Sema Judith, uko tayari twende wote?”
“Sawa.”
**********
KUTOROKWA, tena kutorokwa na mwanamke, kwa Makella ilikuwa ni zaidi ya
tusi la nguoni. Isitoshe, mwanamke mwenyewe katoroka huku pia akiwa amemwibia
pesa, dola 2,000 za Marekani! Lilikuwa ni tukio zito, tukio ambalo Makella
alilichukulia kwa uzito mkubwa. Hivyo, mara tu alipokuwa nje ya Kiyovu Hotel
alitembea kwa hatua ndefu akiifuata Barabara ya 17/18 ambako aliambiwa kuwa ndiko Judith alikoelekea.
Dakika tano baadaye alikuwa mbele ya duka lililomilikiwa na ofisa wa
Jeshi la Rwanda . Hapo, licha ya kuwa na huduma za bidhaa mbalimbali pia
vinywaji kama bia za aina tofauti zilipatikana.
Kulikuwa na wateja wengi waliojiburudisha kwa vinywaji. Kwa sekunde
chache alisimama akiduwaa, lakini hakuduwaa kama taahira. Alikuwa na sababu.
Alizungusha macho kwa kila mtu aliyekuwa hapo huku akilini mwake sura ya Judith
ikimjia.
Alitarajia kumwona Judith mahali hapo, lakini hakuambulia kitu. Akazidi
kuchanganyikiwa. Akasonya kwa hasira huku akijiapiza kimoyomoyo kuwa akimwona,
kwanza atamtia risasi ya kichwa kisha atainajisi maiti yake!
“Vipi, umekosa nafasi?” sauti kutoka nyuma yake ilipenya masikioni
mwake.
Akageuka haraka kumtazama muulizaji. Akashusha pumzi baada ya kumwona
Luteni Kasa, mmiliki wa duka hilo.
“Hapana, afande,” Makella alijibu huku akifuatisha saluti ambayo Luteni
Kasa hakuonyesha kuijibu. “Kuna mtu…” aliongeza na kusita.
“Subiri,” Luteni Kasa alimwahi. Papohapo akamwita kijana mmoja na
kumwamuru alete viti viwili na meza moja.
“Lete na bia mbili,” Luteni aliongeza huku akimgeukia Makella na
kumuuliza, “Bia gani?”
“ Asante . Labda maji tu.”
Sauti na mwonekano wa Makella vilitosha kumfanya Luteni Kasa ahisi kuwa
Makella ana tatizo; kuna jambo lililomkera.
Itaendelea kesho…
No comments:
Post a Comment