Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 24 June 2014

UJERUMANI YAAHIDI EURO MILIONI MOJA KULIKOA PORI LA SELOUS

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII 

TAARIFA KWA UMMA 

Serikali ya Ujerumani Yaahidi Kutoa Msaada wa Euro Milioni Moja

Serikali ya Ujerumani, pamoja na ahadi ya Euro milioni moja ya kusaidia Uhifadhi wa Pori la Akiba Selous, imehimiza mataifa mengine kusaidia Uhifadhi wa Pori hilo kutokana na ujangili wa tembo uliokithiri.

Pori la Akiba Selous, lenye ukubwa wa kilometa za mraba 50,000, ni mojawapo kati ya maeneo saba yaliyo kwenye orodha ya Urithi wa Dunia nchini Tanzania. Maeneo mengine ni Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara, Michoro ya Miambani Kondoa, na Mji Mkongwe Zanzibar. Malengo makuu na faida ya kuweka eneo kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia ni pamoja na: 

  • Kuwa na nguvu ya pamoja kimataifa ya kusimamia uhifadhi wa eneo; 
  • Kujulikana kimataifa kama kivutio chenye sifa maalum cha utalii; 
  • Kutumika kwa tafiti mbali mbali za uhifadhi pamoja; na 
  • Kuvutia misaada ya kimataifa ya kiuhifadhi. 

Kamati ya Urithi wa Dunia imeainisha vigezo 10 vinavyowezesha eneo kuorodheshwa kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia.Pori la Akiba Selous liliorodheshwa mwaka 1982 kwa kukidhi vigezo viwili kati ya hivyo, ambavyo ni:

  • Eneo muhimu sana kwa bioanuai ikiwemo idadi kubwa ya tembo kuliko pori 
  • lolote duniani; na 
  • Eneo lenye aina na muingiliano mpana wa uoto wa asili ikiwemo mimea zaidi 
  • ya aina 2100 na misitu mikubwa aina ya miombo kuliko sehemu nyingine yoyote duniani. 

Katika Mkutano wa 38 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea jijini Doha-Qatar (15-26 Juni 2014), Pori la Akiba Selous ni mojawapo ya maeneo yaliyoingizwa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia ulio hatarini.

Lengo la kuingiza eneo kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia ulio hatarini ni kuongeza uelewa wa jamii kitaifa na kimataifa kuhusu matatizo yanayolikabili eneo hilo ili kuwezesha upatikanaji wa misaada ya hali na mali ilikulirejesha katika hadhi yake ya asili.

Tangu Pori la Akiba Selous liwekwa kwenye orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia, hali yake kwa ujumla iliendelea kuwa nzuri na ya kuridhisha. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2010 Pori hili pamoja na maeneo mengine nchini yamekumbwa na wimbi kubwa la ujangili, hususani wa tembo. Hali hii imesababisha kupungua kwa idadi ya tembo katika mfumo ikolojia wa Selous, kutoka tembo 70,000 mwaka 2006 hadi kufikia tembo 13,084 mwaka 2013. Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania ilichukua hatua za haraka kudhibiti hali hii katika Pori la Akiba Selous kwa :

  • Kuliongezea uwezo wa rasilimali fedha kwa kurejesha utaratibu wa awali wa kubakiza asilimia 50 ya mapato; 
  • Kuandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kuhifadhi tembo na kuunda vikosi maalum vya pamoja miongoni mwa taasisi za wanyamapori vya kupambana na ujangili katika kanda 11 nchini. Mojawapo ya kanda hizo ni kwa ajili ya mfumo wa ikolojia ya Selous; 
  • Kuboresha shughuli za uhifadhi rasilimali ya wanyamapori kwa kubadili mfumo wa usimamizi wa uhifadhi wa wanyamapori kwa kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori itakayowezesha Pori la Akiba la Selous kupata fedha za kutosha kwa ajili ya shughuli za uhifadhi; 
  • Kuongeza idadi ya wahifadhi wanyamapori 105 ambao 40 kati yao walipangiwa eneo la kazi la Pori la Akiba Selous. Aidha, usaili wa kuajiri wahifadhi wengine 437 umefanyika na kati yao 200 watapangiwa kazi katika Pori la Akiba la Selous; na 
  • Kuongeza idadi ya vitendea kazi yakiwemo magari mapya 8, helikopta moja, ukarabati wa mitambo na magari, kuboresha huduma za jamii kwa watumishi pamoja na kukarabati miundo mbinu ya barabara, nyumba za watumishi na viwanja vya ndege. 

Kutokana na hali ya ujangili mkubwa uliosababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya tembo, Kamati ya Urithi wa Dunia ilituma timu ya wataalam mwezi Desemba 2013 kwa ajili ya kufanya tathmini ya ukubwa wa tatizo na kupendekeza hatua stahili za kuchukua kunusuru hali hii. Baada ya kutembelea Pori la Akiba Selous na kupata maoni ya Serikali na wadau mbalimbali wa uhifadhi, Kamati ya Urithi wa Dunia ilipendekeza Pori la Akiba Selous liwekwe kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini kama ilivyokuwa kwa eneo la Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara mwaka 2004. Pendekezo hili limeridhiwa na Mkutano wa 38 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea Doha katika Falme ya Qatar.

Katika mkutano huu, eneo la Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara limeondolewa kutoka orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini baada ya juhudi kubwa za Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na jamii ya kimataifa kuchukua hatua stahili kurekebisha upungufu uliosababisha eneo hili kuwekwa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini. Pori la Akiba Selous kuwekwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini ni fursa ya kuweza kupata misaada kutoka jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukabili tatizo la ujangili wa tembo.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, Kamati ya Urithi wa Dunia imetoa muda wa mwaka mmoja kwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kukomesha ujangili wa tembo katika Pori la Akiba la Selous na hatimaye kuliondoa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini.Kutokana na uamuzi huu, Serikali ya Ujerumani imeahidi kutoa euro milioni moja na kuhimiza mataifa mengine yatoe misaada ya kifedha na kiufundi kwa Tanzania ili iweze kukabili tatizo hili sugu haraka iwezekanavyo. Vile vile mataifa mengine ikiwemo Ureno, Algeria, Senegali, Lebanon na Colombia yameungana na Ujerumani kuhamasisha jumuiya ya kimataifa kuisaidia Tanzania kutimiza azma yake.

IMETOLEWA NA MSEMAJI WA WIZARA 
23.06.2014 

No comments:

Post a Comment