Na James Truman, brotherdanny5.blogspot
Sao Paulo, Brazil
JUMLA ya
mashabiki 3,531,211 wanatarajiwa kuingia viwanjani kutazama mechi 64 za fainali
za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil kuanzia Juni 12, mwaka huu.
Mashabiki
hao watatinga kwa nyakati tofauti katika viwanja 12 vitakavyotumika katika
fainali hizo za 20, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kulinganisha na fainali za mwaka
2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini.
Hata
hivyo, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limetenga jumla ya tiketi
3,334,524 kwa ajili ya fainali hizo, lakini ikiwa mashabiki wataingia kwa idadi
halisi ya viwanja hivyo, jumla yake watakuwa 3,531,211.
Sehemu
kubwa ya tiketi zilizotengwa na FIFA zitagawiwa kwa makundi kama ya
wafanyabiashara washirika, wanahabari na wageni maalum. Tiketi zitakazouzwa
zinakadiriwa kuwa 1.1 milioni ambapo 400,000 kati yake ni kwa ajili ya
Wabrazili na 700,000 kwa mashabiki kutoka nje. Kwa kila mechi, asilimia 8 ya
mauzo ya tiketi itakwenda kwa timu zinazoshiriki.
Hadi kufikia Agosti 20, 2013 jumla ya tiketi 2.3 milioni zilikuwa
zimeuzwa ndani ya saa 24 tu na hadi kufikia Oktoba 2013 kulikuwa na maombi ya
tiketi milioni 6. Bei ya tiketi hizo inaanzia Dola 12.50 kwa mechi za awali
wakati mechi ya fainali tiketi zitauzwa kwa Dola 990.
Estadio do Maracana
Taarifa
zinaonyesha kwamba, uwanja wa Maracana ulioko jijini Rio de Janeiro
umekarabatiwa upya kwa ajili ya fainali za mwaka huu zinazofanyika miaka 64
tangu zilipofanyika nchini humo mwaka 1950. Uwanja huo unaotumiwa na klabu
kongwe nchini humo za Fluminense na Flamengo na ulifunguliwa Juni 2013 kwa
mechi baina ya Brazil na England.
Estadio
do Maracana ulitumiwa kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1950,
ambapo mashabiki 174,000 waliingia na kuishuhudia Uruguay ikiichapa Brazil 2-1.
Uwanja
huo wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 73,531 ndio utakaotumika kwa mechi ya
fainali Julai 13, 2014, lakini pia utahusisha mechi nyingine sita na hivyo
kufanya jumla ya watazamaji watakaoingia uwanjani hapo kuwa 514,717.
Mechi
nyingine zitakazochezewa hapo ni mechi za Kundi F baina ya Argentina na
Bosnia&Herzegovina (Juni 15, 2014); Hispania na Chile (Juni 18, 2014);
Ubelgiji na Russia (Juni 22, 2014); Ecuador na Ufaransa (Juni 25, 2014);
Mshindi Kundi C na Mshindi wa Pili Kundi D (Juni 28, 2014); na Robo Fainali
(Julai 4, 2014).
Arena de Sao Paulo (Corinthians)
Uwanja
huu uko jijini hapa Sao Paulo, ambako ndiko soka ilikozaliwa kwa nchi ya Brazil.
Unatumiwa na klabu kongwe ya Corinthians na una uwezo wa kuingiza watazamaji
65,000. Sao Paulo ni mji ulioko Kusini Mashariki ma Brazil na unafahamika kama
Terra da Garoa kutokana na mvua kunyesha mara kwa mara.
Katika uwanja
huu jumla ya mechi sita zitachezwa na kuingiza watazamaji 390,000 katika
fainali hizo.
Mechi
zitakazochezewa hapo ni ile ya ufunguzi baina ya wenyeji Brazil na Croatia (Juni 12, 2014); Uruguay na England (Juni 19, 2014); Uholanzi
na Chile (Juni 23, 2014); Korea Kusini na Ubelgiji (Juni 26, 2014); Mshindi
Kundi F na Mshindi wa Pili Kundi E (Julai 1, 2014); na Nusu Fainali (Julai 9,
2014).
Estadio Nacional Mane
Garrincha
Uwanja
huu wenye uwezo wa kuingiza jumla ya watazamaji 68,009 kwa wakati mmoja, uko
jijini Brasilia, mji mkuu wa Brazil tangu mwaka 1960 uliochukua nafasi ya Rio
de Janeiro.
Jina
la uwanja huo limetokana na nyota wa zamani wa klabu ya Botafogo na Brazil, Manuel
‘Mane’ Garrincha, ambaye alikuwa mmoja wa wanasoka mahiri nchini humo katika
miaka ya 1950 na 1960.
Ndani
ya uwanja huo mpya kutachezwa mechi 7 na jumla ya mashabiki 476,063 anatarajiwa
kuhudhuria mechi hizo.
Mechi
zitakazochezwa hapo ni baina ya Uswisi na Ecuador (Juni 15, 2014); Colombia na
Brazil (Juni 19, 2014); Cameroon na Brazil (Juni 23, 2014); Ureno na Ghana (Juni
26, 2014); Mshindi Kundi E na Mshindi wa Pili Kundi F (Juni 30, 2014); Robo
Fainali (Julai 5, 2014); na Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu (Julai 12, 2014).
Estadio Castelao
Uwanja
huu uko jijini Fortaleza, Kaskazini Mashariki mwa Brazil, na una uwezo wa
kuingiza watazamaji 58,704. Klabu zinazoutumia uwanja huu ni Ceara SC na
Ferroviario AC na ndio utakaotumika kwa mechi ya pili ya Brazil ya hatua ya
makundi.
Fortaleza
ni maarufu kwa utalii, fukwe nzuri na vyakula vya aina yake na unatajwa kuwa na
hali ya Kitropiki.
Jumla
ya mechi sita zitachezwa hapa na mashabiki 352,224 wanatarajiwa kuingia
uwanjani. Mechi hizo ni Uruguay na Costa Rica (Juni 14, 2014); Brazil na Mexico
(Juni 17, 2014); Ujerumani na Ghana (Juni 23, 2014); Ugiriki na Ivory Coast (Juni
24, 2014); Mshindi Kundi B na Mshindi wa Pili Kundi A (Juni 29, 2014); na Robo
Fainali (Julai 4, 2014).
Estadio Mineirao
Huu
ni uwanja unaotumiwa na klabu ya Cruzeiro. Uko katika Jiji la Belo Horizonte,
umbali wa saa moja tu kutoka Jiji la Rio de Janeiro na ni mji usio na gharama
kubwa sana kwa mashabiki wa kigeni.
Hapa
ndipo mwanasoka mahiri duniani, Ronaldo de Lima, alipoanza kung’ara akiwa na
klabu ya Cruzeiro.
Uwanja
huu una uwezo wa kuingiza watazamaji 57,483 ambao utachezewa pia mechi ya nusu
fainali.
Jumla
ya mashabiki 344,898 wanatarajiwa kuingia kwenye uwanja huu katika mechi sita
zitakazochezwa hapa.
Mechi
zitakazochezwa ni baina ya Colombia na Ugiriki (Juni 14, 2014); Ubelgiji na
Algeria (Juni 17, 2014); Argentina na Iran (Juni 21, 2014); Costa Rica na
England (Juni 24, 2014); Mshindi Kundi A na Mshindi wa Pili Kundi B (Juni 28,
2014); na Nusu Fainali (Julai 8, 2014).
Estadio Beira-Rio
Uwanja
huu uko jijini Porto Alegre na una uwezo wa kuingiza watazamaji 48,849 ambapo
pia unatumiwa na klabu mbili za Internacional na Gremio. Upo kando ya Mto
Guaiba.
Porto
Alegre ni mji wenye mvua kipindi cha Juni na Julai na visiwa kadhaa, kimojawapo
ni Lago de Patos kilichozungukwa na miti karibu milioni moja.
Hapa
patachezewa mechi tano na hivyo watazamaji 244,245 wanatarajiwa kuingia
uwanjani.
Mechi
zitakazochezewa hapo ni Ufaransa na Honduras (Juni 15, 2014); Australia na
Uholanzi (Juni 18, 2014); Korea Kusini na Algeria (Juni 22, 2014); Nigeria na
Argentina (Juni 25, 2014); na Mshindi Kundi G na Mshindi wa Pili Kundi H (Juni
30, 2014).
Arena Pernambuco
Huu
ni uwanja ulioko jijini Recife na unatumiwa na klabu maarufu za Nautico, Santa
Cruz na Port ukiwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 44,248.
Recife
ni mji ulioko kwenye Pwani ya Kaskazini Mashariki ya Brazil, ulitumika mara ya
mwisho katika mechi ya Kombe la Dunia 1950.
Huu
ni mji maarufu kwa uchumi wa Brazil, lakini wakazi wake ni mashabiki wa soka
waliopitiliza.
Jumla
ya mechi tano zitachezwa hapa na mashabiki 221,240 wanatarajiwa kushiriki.
Mechi hizo ni kati ya Ivory Coast na Japan (Juni 14, 2014); Italia na Costa
Rica (Juni 20, 2014); Croatia na Mexico (Juni 23, 2014); Marekani na Ujerumani
(Juni 26, 2014); na Mshindi Kundi D na Mshindi wa Pili Kundi C (Juni 29, 2014).
Arena Fonte Nova
Huu
uwanja uko kwenye Jiji la Salvador ukiwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 52,048
na unatumiwa na klabu za Bahia na Vitoria. Uwanja huo utashuhudia mechi sita
kwenye fainali hizo. Waandaaji wanasema uwanja huo mpya umejengwa kisasa na una
migahawa, makumbusho ya soka, maduka, hoteli na kumbi za sherehe.
Mji
wa Salvador ni uko Kaskazini mwa Brazil na ndio uliokuwa mji mkuu wa kwanza wa
nchi hiyo.
Mechi
zitakazochezwa hapo ni kati ya Hispania na Uholanzi (Juni 13, 2014); Ujerumani na Ureno (Juni
16, 2014); Uswisi na Ufaransa (Juni 20, 2014); Bosnia&Herzegovina na Iran (Juni
25, 2014); Mshindi Kundi H na Mshindi wa Pili Kundi G (Julai 1, 2014); na Robo
Fainali (Julai 5, 2014).
Jumla
ya watazamji 312,288 wanatarajiwa kushuhudia mechi hizo uwanjani hapo.
Arena Pantanal
Uwanja
huo upo kwenye mji wa Cuiaba, Magharibi mwa Brazil, Kusini mwa Misitu ya
Amazon. Unafahamika kama ‘Green City’ na ni maarufu kwa utalii licha ya kwamba
kwa kipindi cha Juni hadi Julai hali ya hewa inakuwa tatizo kutokana na joto
kufikia nyuzi 40.
Uwanja
huo uliboreshwa kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia na utatumika kwa ajili
ya mechi nne. Una uwezo wa kuingiza watazamaji 42,968. Ni nyumbani kwa klabu za
Cuiaba na Mixto.
Hapa
jumla ya mashabiki 171,872 wanatarajiwa kushuhudia mechi hizo nne za Chile na
Australia (Juni 13, 2014); Russia na Korea Kusini (Juni 17, 2014); Nigeria na
Bosnia&Herzegovina (Juni 21, 2014); na Japan na Colombia (Juni 24, 2014).
Arena Amazonia
Uwanja
huu uko mjini Manaus, mji ambao upo katikati ya misitu ya Amazon. Una uwezo wa
kuingiza watazamaji 42,374.
Mji
huo unaelezwa kwamba siyo mahali pazuri sana kwa soka kutokana na kuwa katikati
ya misitu, hata hivyo waandaaji wameamua fainali za Kombe la Dunia zichezwe
kila kona ya nchi baada ya kuzikosa kwa miaka 64.
Huenda
baada ya michuano ya Kombe la Dunia uwanja huo utageuka kuwa mahali pa wanyama.
Inatazamiwa
kwa mashabiki 169,496 watahudhuria mechi nne zitakazochezwa hapo.
Mechi hizo
ni baina ya England na Italia (Juni 14, 2014); Cameroon na Croatia (Juni 18,
2014); Marekani na Ureno (Juni 22, 2014); na Honduras na Uswisi (Juni 25, 2014).
Estadio das Dunas
Huu
ni uwanja ulioko jijini Natal ukiwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 42,086.
Unatumiwa na klabu ya America na umemalizika kujengwa kwa ajili ya Kombe la
Dunia.
Estadio
das Dunas utatumika kwa mechi nne za makundi katika fainali hizo. Natal ni mji
unaofahamika kama Cidade do Sol (Sun City) kwa sababu umekuwa na joto
linalokaribia nyuzi 28. Fukwe zilizopo Kaskazini Mashariki mwa jiji hilo zinalifanya
jiji hilo lizidi kupendeza.
Jumla
ya mashabiki 168,344 wanatarajiwa kuingia kutazama mechi baina ya Mexico na
Cameroon (Juni 13, 2014); Ghana na Marekani (Juni 16, 2014); Japan na Ugiriki (Juni
19, 2014); na Italia na Uruguay (Juni 24, 2014).
Arena da Baixada
Uwanja
huu uko jijini Curitiba ambao kwa mara ya kwanza ulijengwa mwaka 1914 lakini
ukafanyia ukarabati maka 1999 na umerekebishwa zaidi baada ya Brazil kupata
fursa ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia.
Unatumiwa
na klabu ya Atletico Paranaense na una uwezo wa kuingiza watzamaji 41,456.
Jumla
ya mechi nne zitachezwa hapa na mashabiki 165,824 wanatarajiwa kutinga.
Mechi hizo ni
Iran na Nigeria
(Juni 16, 2014); Honduras na Ecuador (Juni 20, 2014);
Australia na Hispania (Juni 23, 2014); na Algeria na Russia (Juni 26, 2014).
Curitiba
ni mji wa aina yake ndani ya Brazil na unatajwa kuwa na uchumi mkubwa. Hali
yake ya hewa inafanana na Rio de Janeiro na Belo Horizonte.
No comments:
Post a Comment