Dodoma. Katibu mtendaji wa Tume ya Marekebisho ya Sheria, Japhet Sagasii amesema serikali tatu haziwezi kuvunja Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Sagasii alisema hayo kutokana na hoja inayotolewa na baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kuwa muundo wa Muungano wa serikali tatu ni hatari kwa kuwa unaweza kuvunja Muungano.
“Hoja ya kwamba Serikali tatu zitavunja Muungano hazina mashiko. Mambo yote ambayo yanaonekana kuwa yanaweza kuvunja Muungano wanayaweka katika Katiba ya Muungano,” alisema Sagasii.
Alisema baada ya kutengeneza Katiba ya Muungano na Tanganyika nayo itaunda katiba yao ambayo itaainisha masuala yatakayokuwa ya nchi zao.
Aidha, Sagasii aliyewahi kuwa mkurugenzi wa shughuli za Bunge, alisema suala la muundo wa serikali limekuwa likijitokeza mara kwa mara kuanzia mwaka 1984.
Aliwashangaa Wana-CCM kudai kuwa wazo la serikali tatu linatoka kwa vyama vya upinzani akisema “suala hilo liliibuliwa na Wabunge wa CCM waliojulikana kama G55 walipotaka kuundwa kwa Tanganyika.
Mbali na Tume ya Jaji Robert Kisanga kuonyesha mahitaji ya serikali tatu, Sagasii alisema hitaji hilo pia lilionekana wakati wa utawala wa rais wa pili wa Zanzibar, Abdul Jumbe.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ya tano kuibua suala hilo, lakini safarihii ni mwafaka zaidi kwa kuwa maoni hayo yametokana na wananchi wenyewe.
“Wanaotumia nafasi zao kwa ajili ya kuzuia serikali tatu ni sawasawa na mpira uliojazwa upepo sasa ukiuzamisha kwenye maji ukiendelea kuushikilia utabaki katika maji lakini ukiutoa mkono unaibuka hiyo ndiyo hoja ya Utanganyika,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment