Wakati timu yake leo ikikabiliwa na pambano gumu la watani wa jadi Simba la kilele cha ligi kuu ya Bara kwenye Uwanja wa Taifa, kiungo wao wa kimataifa Haruna Niyonzima 'Fabregas' amesema hataki kuulizwa chochote kuhusu timu yake ya Yanga.
Aidha, Niyonzima, nahodha wa timu ya taifa yaRwanda (Amavubi), ambaye hayuko kambini na kikosi cha Mholanzi Hans van der Pluijm, amesema akili zake kwa sasa amezielekeza kwa familia yake tu.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam juzi, Niyonzima alisema: "Kwa sasa niko bize na familia yangu, sitaki kuzungumza chochote kuhusu Yanga na mpira wa Tanzania."
Niyonzima ambaye ameitelekeza timu yake, alikuwa akisugua benchi baada ya kuporwa namba katika kikosi cha kwanza cha Yanga na kiungo mzawa Hassan Dilunga aliyesajiliwa katika dirisha dogo la Desemba mwaka jana kutoka Ruvu Shooting.
Dilunga, aliyehamia Yanga pamoja na aliyekuwa kocha wake Ruvu Shooting, Mkwasa, amekuwa na kiwango cha juu katika kikosi cha Yanga na amehalalisha kupora namba ya Niyonzima.
Alipotafutwa na NIPASHE, Baraka Kizuguto, Kaimu Ofisa Habari wa Yanga, alisema Niyonzima hatocheza mechi ya leo, ambayo Yanga itakuwa inajaribu kulipa deni la karibuni la kipigo cha 3-1 cha mechi ya 'Nani Mtani Jembe'. Alisema wachezaji ambao hawako kambini, Niyonzima akiwemo, hawatakuwa kwenye kikosi cha leo lakini hakuwa tayari kueleza sababu za nyota huyo na wengine wanne kutokuwapo kambini.
Wachezaji wengine wa Yanga ambao hawatacheza leo kutokana na kutoshiriki maandalizi yake ni kipa mzoefu Juma Kaseja, Emmanuel Okwi, Athumani Iddi na Said Bahanuzi.
Mabingwa wa mwaka jana Yanga (55) waliojihakikishia nafasi ya pili, wameshavuliwa taji hilo na Azam yenye pointi 59 na ambayo itakabidhiwa kombe la ligi kuu ya Bara baada ya mchezo dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Simba, iliyo katika nafasi ya nne kwa tofauti ya pointi 22c chini ya Azam itabaki katika nafasi hiyo hata kama itaendelea kuwa na msimu mbovu kuliko yote katika histoa yake ya ligi kuu ya Bara, baada ya kubadilika kutoka kuwa ligi daraja la kwanza.
Hali hiyo inafanya mchezo wa leo baina ya watani wa jadi hao kuwa wa kulinda heshima ya klabu hizo mbili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment