MVUTANO wa muundo wa serikali mbili au tatu uliogubika Bunge Maalumu, umelifanya Baraza la Mahusiano ya Dini mbalimbali kwa Amani Tanzania (IRCPT), kutaka kura ya maoni ifanyike ili wananchi waamue muundo wa muungano.
Baraza hilo limebainisha kuwa viongozi wa dini watakubali kupiga kuraya maoni kuhusu mapendekezo ya Katiba ambayo yamezingatia maoni yaliyotolewa na wananchi.
Msimamo wa baraza hilo umo ndani ya kitabu cha mapendekezo kwa wajumbe wa Bunge Maalumu kuhusu rasimu ya Katiba, walichokisambaza juzi kwa wajumbe wa Bunge Maalumu.
Mratibu wa baraza hilo, Thomas Goda, alisema miongoni mwa taasisi zinazounda baraza hilo ni Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Kikistro Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekosti Tanzania (BMKT), Tanzania Asian Development Association (TADA) na Tanzania Episcopal Conference (TEC).
Goda, alisema kuwa wajumbe wa baraza lao walikutana Machi 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam ambapo waliijadili na kuichambua rasimu ya Katiba inayojadaliwa hivi sasa na wajumbe wa Bunge Maalumu.
Alisema baada ya kujadili na kuchambua rasimu hiyo wamebaini giliba za kisiasa, malumbano, jazba, tofauti za kiitikadi na kutozingatia kanuni ndizo zimetawala majadiliano ya Bunge Maalumu hivyo kutia doa safari ya kupatikana Katiba yenye kujumuisha makundi mengi.
Alibainisha kuwa wameandika kitabu chenye kurasa 12 kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza zilizo na mapendekezo 14.
Tanzania Daima Jumapili, imepata nakala ya kitabu hicho ambacho katika ukurasa wa sita pendekezo namba moja linawataka wajumbe waheshimu rasimu ya Katiba iliyobeba maoni ya wananchi na kuifanyia kazi kwa lengo la kuiboresha.
Pendekezo jingine ni kuwataka wajumbe wajadiliane kwa upendo, kuheshimiana na kuthaminiana bila kuathiriwa na mawazo pandikizi, masilahi binafsi, vyama, kabila au eneo la mjumbe.
Katika ukurasa wa nane wa kitabu hicho, 3.1, baraza hilo linataka wananchi waachiwe waamue kwa kupitia kura ya maoni juu ya muundo wa serikali.
Mapendekezo hayo pia yanataka Katiba itatambue uwepo wa mamlaka ya Mungu, sifa za rais awe mwana ndoa, ndoa ni kati ya mume na mke, itoe mwongozo wa matumizi ya rasilimali za taifa na ukusanyaji kodi, rais anayemaliza muda wake aondolewe kinga kama sehemu ya kujenga uadilifu na uwajibikaji.
Katika ukurasa wa 11 kitabu hicho kinataka kiongozi aliyefukuzwa au kujiuzulu kwa kukiuka miiko na maadili ya uongozi asigombee na asiteuliwe tena katika nafasi yoyote ya uongozi.
Mengine ni katiba itenganishe kuingiliana kwa mihimili mikuu mitatu ya dola; Serikali, Bunge na Mahakama (uteuzi wa wabunge watano usifanywe na rais, mawaziri wasiwe wabunge).
Katiba itambue kwa makusudi kuwepo uwakilishi wa baraza la viongozi wa dini na wazee wenye busara kuishauri serikali mambo ya kisheria na mambo yote nyeti ya kitaifa.
Viongozi wote wanaoteuliwa au kuchaguliwa nafasi ya uongozi, uadilifu wao lazima uthibitishwe na Tume ya Maadili kabla ya kuteuliwa au kuchaguliwa.
Naye mjumbe wa baraza hilo, Ali Mose, alisema wameingiwa na wasiwasi mkubwa kama Katiba iliyotarajiwa itapatikana, kwakuwa watu wameweka mizizi ya kiitikadi ambayo inakwamisha wajumbe kusikiliza hoja za upande mwingine.
Alisema kuna hatari ya kupatikana kwa Katiba isiyoyaunganisha makundi yote, jambo ambalo ni hatari na doa, kwa kuwa Katiba inajengwa katika misingi ya maridhiano.
‘Viongozi wa dini tuna jukumu la kuwaunganisha wajumbe ili maridhiano yafikiwe na taifa lipate Katiba nzuri itakayowafurahisha Watanzania wote,” alisema.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment