Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 18 April 2014

UKAWA: HATUTARUDI BUNGENI NG'O

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na Waziri wa Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Abubakar Khamis, akizungumza na wajumbe waliosusa Bunge.

UMOJA  wa Katiba ya Wananchi bungeni (Ukawa) umetangaza rasmi kwamba, wanakwenda kwa wananchi kuwashitaki wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa ni siku moja baada ya kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.

 Umoja huo ulitangaza msimamo huo jana katika mkutano wa waandishi wa habari na kusema hawatahudhuria vikao hadi hapo Rasimu ya Katiba yenye maoni ya wananchi itakapokubalika kujadiliwa bungeni.

Kufuatia msimamo huo, kuanzia kesho wajumbe wataanza kampeni ya kuzunguka nchi nzima kuwashitaka CCM kwa wananchi kuhusu kile kinachoendelea bungeni.

Pia kuueleza umma msimamo wao dhidi ya Bunge hilo walilodai limepuuza kile Watanzania walichopendekeza kwenye Tume ya Jaji Warioba.

Mjumbe wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alitangaza kuwa kesho kutakuwa na mkutano wa hadhara Zanzibar kuanzisha kampeni hiyo na baada ya hapo watakwenda katika mikoa mingine kusambaza yanayotokea bungeni na msimamo wao kuwa maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba yazingatiwe na siyo rasimu ya CCM.

Juzi wajumbe hao walitoka nje na kutangaza kuwa wanasusia vikao vya Bunge hilo.

Alisema wajumbe wa umoja huo ni karibu 190, lakini hakuwa na uhakika kuwa ni wangapi walitoka nje.

WAGOMEA MKUTANO KAMATI YA UONGOZI
Wakati hayo yakijiri, viongozi wa Ukawa waligomea mkutano wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, ambayo Mwenyekiti wake ni Samuel Sitta, uliotishwa kutafuta maridhiano.

Profesa Lipumba alisema wanaweza kuachana na mkutano huo kama wajumbe walio wengi wataendelea kudharau rasimu yenye maoni ya wananchi, ambayo kisheria ndiyo inayotakiwa kujadiliwa.

“Hata ikifika Agosti sisi hatutakuwa na shughuli mpaka hapo tutakapoanza kujadili rasimu ya maoni ya wananchi,” alisema.

Alisema wanasusia Bunge kwa sababu badala ya kujikita kwenye rasimu, kinachoendelea ni kutumia lugha za kibaguzi, vitisho kutukana bila kukemewa na viongozi wa serikali walioko bungeni.

“Kila kilicho ndani ya rasimu kinakataliwa. Hata mapendekezo ya kuwa waadilifu, wawazi, wawajibikaji yanakataliwa. Kwenye kamati wajumbe wote wa CCM na wanaowaunga mkono wameyatupa.Tunafanya nini?” alihoji.

KUITWA KWA MARIDHIANO
Profesa Lipumba alisema licha ya kuwapo madai kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Sitta amewaita ili kutafuta maridhiano, alijibu: “Mimi sina habari, hajanipigia simu wala kunitafuta.”

Awali, katika kikao cha asubuhi, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, aliwaeleza wajumbe kuwa aliitwa na Ofisi ya Bunge kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi kuandaa ratiba ya Bunge la Bajeti.

Alisema alipoingia ukumbini, alikuta kinachofanyika ni kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, ambacho alikataa kushiriki.Pia mjumbe wa Kamati ya Uongozi na mjumbe wa Ukawa, Abubakary Khamis Bakari, alieleza kuwa alialikwa, lakini alikataa.

NI HALALI KUSUSA?
Mbowe alipoulizwa kama ni mwafaka kususa, alisema ni sahihi, kwani kinachoendelea ni kubaguliwa, kutukanwa kwa wanaotoa maoni tofauti na CCM.

Alisema hakuna wajumbe wenye uhalali wa kutunga katiba peke yao, kwa vile inatakiwa  kuandikwa kwa maridhiano ili kuendeleza umoja wa taifa.

“Kuendelea kushiriki katika mchakato huo, ni kuwanyonya wananchi na hakuna tija. Hatutaweza kushiriki kwenye mjadala usio na maridhiano wa kutukanana, kubaguana na kudharauliana,” alisema.

Alisema kutoka nje ya kikao ni sahihi tena ni njia ya kutafuta haki, kwani haki inacheleweshwa, lakini haipotei.

Aliwalaumu viongozi kukaa kimya bila kukemea kauli za karaha, kejeli na matusi  zinazotolewa dhidi ya wajumbe walio na msimamo tofauti na wa CCM.

LUKUVI 
Katika kikao cha pamoja, wajumbe hao walikutana asubuhi na kuzungumzia hatma yao na pia walimjadili Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kufika bungeni ili kuyaweka rasmi maneno aliyozungumza kwenye Kanisa la Methodist, mjini Dodoma.

 Mjumbe Mustapha Akunay, akizungumzia Lukuvi, alisema Sitta alimuita Lukuvi ama kukanusha au kuthibitisha kauli yake kuwa kukiwa na serikali tatu, jeshi litachukua nchi.

“Lakini alichokifanya ni kukoleza maneno na kuongeza ugomvi,” alisema. Akichangia hoja ya Lukuvi, Mosses Machali, alihoji sababu za kumpa dakika 30 kwa kuvunja kanuni.

Walisema wana mkanda wa hotuba yake aliyoitoa kwenye kanisa hilo, ambayo pamoja na kusema jeshi litapindua nchi, aliingilia uhuru wa Waislamu wa kuabudu.

Wajumbe wote walikubaliana kuupeleka mkanda huo Zanzibar na kuusambaza ili watu wafahamu jinsi viongozi wanavyochochea chuki kuwa iwapo serikali tatu zitaruhusiwa, zitachochea udini Zanzibar.

Walidai Lukuvi atashitakiwa kwa Wazanzibari kuwa wakiruhusiwa wajitawale, watachochea udini na kurudisha Waarabu, ambao watazalisha siasa za itikadi kali.

LIPUMBA AWAKANA UAMSHO

 Akizungumzia madai ya Lukuvi kuihusisha CUF na Jumuiya ya Uamsho ya Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), maarufu kama Uamsho, Profesa Lipumba alisema, atachukuliwa hatua kwa kuihusisha na taasisi hiyo ya kidini kwa kuikashifu.

Alisema Uamsho si mshirika wa CUF na katika hotuba zao, wanaharakati hao  wanamshambulia Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad.
 
TANZANIA KWANZA WACHACHAMAA

Wakati huo huo, kundi la wajumbe wanaosimamia katiba wanaojiita Kwanza, wamewashambulia Ukawa kwa kususia vikao.

Wakizungumza na wanahabari jana, walikilaani kitendo cha Profesa Lipumba kuwaongoza wajumbe kutoka nje ya kikao cha Bunge hilo.

Mwenyekiti wa Tanzania Kwanza, Said Nkumba, alisema kitendo hicho ni usaliti dhidi ya wananchi wenye tumaini la kupata katiba na kuonya kuwa Ukawa haina nia wala dhamira ya kuwatetea wananchi, ndiyo maana wamekimbia nafasi hiyo.

“Walisema wanawatoa hofu wananchi kuwa mchakato wa kupata katiba iliyo bora unafanikiwa kama ilivyoelekezwa,” alisema Nkumba.

Awali, Nkumba alisema Ukawa wamekwamisha mijadala mingi bungeni, wakianzia kwenye kuandaa kanuni, hasa eneo la kupiga kura, kusoma ripoti za kamati 12 za wachache na kufafanua hoja zao.

“Ukawa badala ya kujadili hoja muhimu, wamekuwa wanakashifu waasisi wa taifa, kubishania na kudai Hati ya Muungano na kukataa kuanza majadiliano hadi watakapopata nakala halisi ya hati hiyo na sasa wanadai saini ya Karume iliyo kwenye Hati iliyowasilishwa bungeni imeghushiwa,” alisema.

 Waliwalaumu kwa kuwaita wanaounga maoni ya wengi Intarahamwe siyo sahihi na wanapaswa kuomba radhi, kwani ni matusi makubwa.

“Kuwaita Interahamwe, kuna tafsiri nyingi kuwa sisi tunaweza kuwaua,” alisema Nkumba, aliyefuatana na wajumbe kadhaa, akiwano Adam Malima, Asha Mtwangi na Paul Makonda.

MADAI YA LUKUVI DHIDI YA CUF
 Awali, Lukuvi aliishutumu CUF akidai kuwa ina uhusiano na Uamsho inayoendesha harakati zake visiwani Zanzibar.

 Lukuvi alitoa madai hayo bungeni jana, alipokuwa akitoa ufafanuzi ya kauli yake anayodaiwa kuitoa Jumamosi iliyopita mkoani Dodoma katika Kanisa la Methodist wakati wa sherehe za kumsimika Askofu Joseph Bundara wa Jimbo la Dodoma.

Katika sherehe hizo, Lukuvi anadaiwa kutoa kauli za ubaguzi na vitisho kanisani kwamba, Wazanzibari wanaotaka serikali tatu wanataka ijitenge ili iwe nchi ya Kiislamu.

Kauli hiyo ilisababisha wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge wakisema ina lengo la kuwatisha wananchi pamoja na ubaguzi.

Akitoa ufafanuzi juu ya kauli yake hiyo baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, Lukuvi alikiri kutoa kauli hiyo kwa kile alichoeleza kuwa alikuwa akielezea hofu yake juu ya uwezekano wa kutokea kwa uasi wa kijeshi endapo serikali ya Muungano inayopendekezwa katika Rasimu ya Katiba itashindwa kujiendesha na kugharimia vyombo vya dola, yakiwamo majeshi.

Lukuvi alisema alikwenda katika kanisa hilo kumwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alialikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kumsimika Askofu Bundara.

Alisema hofu nyingine aliyoieleza kwenye hotuba yake wakati wa sherehe hiyo, ni uwezekano wa kutokea kwa chuki za kidini kutokana na baadhi ya vyama kutumia taasisi za dini kueneza itikadi zake, akiihusisha CUF na Uamsho.

Alidai harakati zinazofanywa na Uamsho visiwani Zanzibar zinafanana na harakati za CUF, ambazo ni kudai serikali ya mkataba, hata kauli za viongozi wa taasisi hizo mbili katika masuala ya Muungano zinafanana. Uamsho umekuwa ukihusishwa na vurugu zinazotokea mara kwa mara Zanzibar, zinazohusishwa na vuguvugu la kudai mamlaka kamili ya Zanzibar.

Lukuvi alitoa mfano wa Mwenyekiti Sitta, alipotumwa Zanzibar kupeleka Rasimu ya Katiba, Rasimu hiyo ilichukuliwa na Uamsho na kuichanachana na kuisigina mbele yake.

“Sasa niwaulize humu ndani…Uamsho ni nani?” aliwauliza wajumbe waliobakia bungeni wengi wakiwa ni wa CCM na kujibiwa: “Ni CUF”.  Akauliza mara ya pili: “Uamusho ni nani? na kujibiwa: “Ni CUF”.

Aliongeza kusema: “Lakini kuna swali liliulizwa hapa bungeni kuhusu Uamsho CUF wakaja juu wakasema ni taasisi ya kidini…sasa unaniambiaje mimi nisiwe na hofu ya kidini wakati kuna chama cha siasa kinahusiana na Uamsho yenye ladha ya kidini?”

 “Na kwa kuwadhihirishia hivyo, kila mara CUF na Uamsho utakapomtaja Mwalimu Nyerere na kumtaja Karume wanakwambia alaaniwe. Lakini hizi ndiyo sera za hao mnaowasema.

Sasa tunakuwaje na chama cha siasa, ambacho tayari kinajipanga kutawala Zanzibar. Lakini kinaendeshwa na sera za Uamsho, kwa nini usiwe na wasiwasi na mihemko yote ile ya Uamsho mpaka na Bara tukatikishika? Kwa nini tusiwe na wasiwasi kwamba, CUF ikichukua nchi basi Uamsho ndiyo utatawala?” alisema na kuongeza:

 “Kwa nini tusiwe na hofu, yametokea na sisi tumeyaona, kwa nini wanajificha kwenye kivuli cha dini ili kufanya siasa?...na kwa nini dini imetumika vizuri sana kueneza sera za CUF, na kila wanachosema CUF ndicho wanachosema Uamsho.”

 “Na ukishaona chama kinajitayarisha kuchukua madaraka kama ilivyo kwa CUF, kinatumia taasisi hii yenye msimamo mkali kueneza sera zake ni hatari kwa mustakabali wetu, ni hatari kubwa,” alisema.

 Alisema kama kweli Uamsho ni taasisi ya kidini, lakini inatekeleza sera, ambazo zinatekelezwa na vyama vya siasa, ni lazima Watanzania wajiulize kuna nini.

Aidha, Lukuvi, alisema endapo muundo wa Muungano wa serikali tatu utakubaliwa, ipo hatari ya kutokea mivutano kati ya Watanganyika na Wazanzibari.

 Alisema kuna tishio la baadhi ya watu, ambao wameanza kufikiria kwamba, walio Wazanzibari wanafaidi sana wakiwa Tanzania Bara na kufikiria kuwafukuza na kunyang’anya mali zao na iwapo watafanikiwa kuwanyang’anya watawafukuza.

“Baada ya Wazanzibari kuondoka, tutaanza kuangalia hawa Wachina, hawa Wahindi na vinginevyo tutakuja hata kwenye dini, Wakristo wana mali zaidi kuliko Waislamu.”

 “Lakini kwa Zanzibar, ambayo ina dini kubwa moja…na tunajua hizi dini, kwa mfano, katika dini ya Ukristo kuna dini ndogo ndogo nyingi na ndani ya Ukristo kuna watu wenye siasa kali, lakini na ndani ya Uislamu kuna watu wenye siasa kali…kwa hiyo mimi nina hofu nyingine ya ubaguzi,” alisema na kuongeza:

 “Nasema kunaweza kukatokea ubaguzi wa kidini, inaweza ikatokea ubaguzi wa kieneo kwani inaweza kutokea hata Unguja akaenda mtu akasema Waunguja wote ondokeni hapa pamejaa…sasa hizi ni hofu zangu, mfumo huu wa serikali mbili umetuondolea hofu hizi hatuna hofu kabisa ya maisha haya, leo hatumfikirii Mpemba atoke au Muunguja atoke, Msukuma atoke hatufikirii.”

 Alisema alichofanya wakati akizungumza kwenye sherehe ya kumsimika Askofu Bundara, ni kueleza hofu yake juu ya muundo wa Muungano wa serikali tatu kwamba, hautaweza kumudu gharama za kuendesha serikali ya Muungano, hivyo italeta matatizo.

“Binadamu tumeumbwa na hofu, kila binadamu ameumbwa kuwa na hofu, sasa huwezi kusema hofu zangu nisiziseme…kama wewe huna hofu shauri yako, lakini ya kwanza hofu niliyonayo ni juu ya rasimu yenyewe, kwanza kwa sababu imejengwa katika misingi, ambayo mimi siamini, sababu zilizowafanya wale wazee wakachukia sana pale ni dhahiri mpaka wakasema tuachane na serikali mbili lazima iwe serikali tatu, mimi nyingine sikuziamini,” alisema na kuongeza:

 “Kwa mfano, wanasema kitu, ambacho kimewaudhi sana ni katiba ya 2010, mimi nimesoma ile katiba ya 2003 soma mle ndani sehemu nyingi imetajwa kwa Zanzibar ni nchi. Sasa nashangaa hili wanaliona leo…kwani Zanzibar kuwa nchi ndiyo tunakula?...wanasema eti Zanzibar ina bendera yake na rais anapigiwa mizinga, Marekani kila jimbo lake lina bendera…mimi siamini.”

 Alisema serikali ya Muungano inayopendekezwa katika rasimu haina vyanzo vya mapato hivyo, itashindwa kujiendesha, ikiwamo vyombo vya dola, kama vile jeshi, hivyo upo uwezekano ukatokea uasi.

“Sasa hapa kuna ubaya gani wa kueleza hofu yangu na hapa niseme tu, sitaacha kusema hofu hii, nitasema popote ilimradi nasema ukweli. Siogopi chochote,” alisema.

AMSIFU MREMA
Lukuvi alimsifu Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo, Augustino Mrema, kuwa katika mchango wake naye alieleza juu ya hofu hiyo.

Alisema Mrema ndiye mpinzani wa kweli na kwamba, wenzake wanamuogopa na kuongeza kuwa alikosa kura chache kuwa Rais mwaka 1995.

“Nashangaa Mrema alisema haya Jumatatu iliyopita, lakini hawajasema kitu, lakini mimi nimesema Jumamosi, watu wanasema…..nimeamini kweli Mrema wanakuogopa….naahidi nitafuatilia haki zako ili uweze kuzipata,” alisema Lukuvi.

Mrema aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, cheo ambacho hakipo kikatiba.

Mrema amekuwa akiendesha harakati za kulipwa mafao pamoja na kiinua mgongo kutokana na kushika wadhifa huo jambo, ambalo limekuwa gumu kutekelezwa.

Kabla ya shughuli za Bunge kuanza, Sitta alitangaza kusikitishwa na uamuzi wa Ukawa kususia Bunge na kusema  wamemrudisha Lukuvi kutoka  Uwanja wa Ndege Dodoma akiwa safarini kwenda India katika matibabu ili aeleze bungeni alichozungumza kanisani.

Imeandikwa na Theodatus Muchunguzi, Abdallah Bawazir na Jacqueline Massano, Dodoma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment