Vladimir Putin, Rais wa Russia
Rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema kuwa anatumai sana sana kwamba hatalazimika kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine.
Katika kipindi chake cha kila wiki, Putin
amekanusha madai kuwa Urusi ilihusika katika maandamano ambayo yanakumba
Ukraine lakini akakiri kwamba kwa mara ya kwanza wanajeshi wa Urusi walioenekana katika jimbo la Crimea.Mjini Geneva mashauriano yameanza kwa mara ya kwanza kati ya Marekani, Muungano wa Ulaya, Urusi na Ukraine katika juhudi za kupunguza uhasama Mashariki mwa Ukraine.
Mkutano huo, ambao ni wa kwanza kuhudhuriwa na makundi hayo manne kujadiliana hali ya Ukraine, unafanywa baada ya usiku wa mapigano makali.
Wizara ya mambo ya nje nchini Ukraine imesema watu watatu wanaounga mkono Urusi waliuawa walipojaribu kushambulia kambi moja ya jeshi katika mji wa Marioupol.
Wajumbe wanne wanaokutana Geneva wameafikiana kwa swala moja muhimu kwamba hali katika Ukraine Mashariki ni mbaya sana na lazima itulizwe.
Ili kutuliza hali hiyo, Marekani na Jumuiya ya Ulaya wametoa wito Urusi iwaondoe wanajeshi wake kutoka mipaka na Ukraine. Hadi kufikia sasa wameandaa vikwazo watakavyowekea Urusi iwapo haifanyi hivyo.
Kwa upande wake Urusi inasema watu wachache wanaoongea Kirusi Mashariki mwa Ukraine wanapaswa wanahitaji kupewa ulinzi. Huenda Urusi inachunguza ishara iwapo Ukraine iko tayari kutoa Uhuru kwa maeneo yaliyo Mashariki mwa taifa hilo.
Wakati huohuo Ukraine inataka hakikisho kuwa Crimea bado ni sehemu moja ya Ukraine. Mabalozi walio Geneva wana mengi ya kujadiliana ingawa mashauriano hayo ni ya masaa machache tu huku uhasama unaoendelea nchini Ukraine ukizidi kutokota.
CHANZO: BBC/SWAHILI
No comments:
Post a Comment