WANANCHI wa Kijiji cha Jojo, Kata ya Santilya, Wilaya ya Mbeya Vijijini, wamelaani kitendo cha Katibu Mtendaji wao, Anderson Yamaliha, kuwakamata wanaume watano, mwanamke mmoja na kuwafungia chumba kimoja, akidai waligoma kufanya kazi za maendeleo kijijini hapo.
Kutokana na kitendo hicho, Tanzania Daima ilimtafuta mtendaji huyo kwenye simu yake ya kiganjani lakini iliita tu bila kupokewa, hivyo kutafutwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Nelson Mwasile, ili kutoa ufafanuzi.
Katika ufafanuzi huo, Mwasile alikiri kutokea kwa tukio hilo, lililofanywa na mtendaji wake wa kijiji.
“Ni kweli vijana hao walikamatwa na mtendaji na kuwekwa kwenye chumba kimoja cha sebuleni kutokana na ukaidi wao wa kufanya shuguli za maendeleo, lakini hata mimi mwenyewe sikuwa mbali, nilikuwepo,” alisema Mwasile.
Vijana hao waliokamatwa walitetewa na wanaharakati na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakimtahadharisha Mtendaji Yamalila kwamba, sheria za nchi na haki za binadamu, haziruhusu jinsia hizo tofauti kufungwa chumba kimoja.
Kutokana na ubabe wa ukiukwaji huo, imedaiwa Mtendaji Yamalila aliamuru askari mgambo kuwapiga vijana hao huku akiahidi kula sahani moja na viongozi wa CHADEMA, akiahidi kuwabambikiza kesi hadi awafunge, kwa kuwa wanamkosesha usingizi na kukiharibu Chama tawala (CCM).
CHANZO: TANZANIA DAIMA
CHANZO: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment