Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji JosephWarioba amesema wanasiasa wanaomtuhumu kwa
kumsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Muungano, ndiyo wasaliti
kwa kuwa waliingiza kwenye Katiba, mambo yanayokinzana na makubaliano ya
Muungano huo.
Jaji Warioba amesema usaliti huo ni pamoja na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kuondoa mamlaka ya Bunge la Muungano katika utungaji wa
sheria, kuitambua Zanzibar kuwa nchi inayojitegemea na kuongeza mambo ya
Muungano bila kufuata Katiba.
Ametoa kauli hiyo kujibu mwendelezo wa lugha za kejeli na matusi
anazorushiwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wengi kutoka CCM
na baadhi ya viongozi wa Serikali baada ya Tume aliyoiongoza kupendekeza muundo
wa serikali tatu.
Akizungumza juzi usiku katika kipindi cha Dakika 45
kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Jaji Warioba alisema viongozi
wa pande mbili za Muungano wanaomtuhumu, ndiyo waliouvuruga Muungano huo
“Mwalimu aliacha Bunge likiwa na mamlaka kamili, aliacha nchi ni
moja, aliacha mambo ya Muungano 11 sasa yamekuwa ni 22, kwa bahati nzuri Rais
Jakaya Kikwete alieleza bungeni hilo kwamba mambo hayo yaliongezekaje,” alisema
na kuongeza:
“Katika kubaini kuongezeka kwa mambo ya Muungano ndivyo ilikuwa
inapunguza mamlaka kwa Zanzibar, mambo 11 yaliyoachwa na mwalimu yaliingizwa
kikatiba lakini haya yaliyoongezeka yalipatikana kienyeji.”
Jaji Warioba alisema enzi za uhai wake, Mwalimu Nyerere
aliheshimu na kuilinda Katiba hivyo, walioivunja ndiyo wasaliti wa Muungano.
“Sasa kati ya mimi na wao ni nani msaliti kwa Mwalimu,
angekuwapo (Mwalimu) ni yupi angeonekana msaliti wa Serikali ya Muungano? Wao
ndiyo wameuvuruga, alichokiacha Mwalimu ni tofauti na kinachoonekana kwa sasa,”
alisema Jaji Warioba.
Kuhusu Bunge
Jaji Warioba alisema mipango mingi ya maendeleo inayopangwa
ndani ya Bunge la Muungano inatekelezwa upande wa Bara pekee.
“Si hivyo tu, Bunge hilo linajadili mambo ya Bara tu na
halihusishi upande wa Zanzibar. Zanzibar nayo inajadili mambo yake na
kujiamulia lakini jina la Bunge hilo ni Muungano,” alisema Jaji Warioba.
Kutokana na mazingira hayo, Jaji Warioba alisema Zanzibar
iliamua kuondoa mamlaka ya Bunge hilo katika utungaji wa sheria kupitia Baraza
la Wawakilishi Zanzibar.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema sheria zinazotungwa
katika Bunge hilo zitatumika ndani ya pande zote za Muungano, lakini Zanzibar
wakabadilisha hilo kupitia Katiba yao wakasema sheria zote zitakazotungwa ndani
ya Bunge hilo, lazima zipitiwe tena na Baraza la Wawakilishi,” na kuongeza:
“(Zanzibar) Hawakuishia hapo, wakafanya mabadiliko ya Katiba mwaka 2010
iliyovunja Katiba ikiitambua Zanzibar kama nchi kamili, ikaondoa mamlaka ya
Rais wa Jamhuri kugawa wilaya na mikoa kwa Zanzibar tofauti na Katiba ya
Muungano, kwa maana hiyo Zanzibar ikavunja nguvu ya Bunge la Muungano.”
Aidha, alisema hatua hiyo ilionekana kuuvunja Muungano kwa
vitendo baada ya kuvunja mamlaka ya Rais na kutambua marais kamili katika nchi
mbili tofauti.
“Kwa kawaida nchi inakuwa na amri jeshi mkuu mmoja ambaye
anapigiwa mizinga 21, Jeshi la Muungano linapiga mizinga kwa marais wawili kitu
ambacho hakiwezekani,” alisema.
Malalamiko ya Watanganyika
Jaji Warioba alisema Kwa upande wa Tanzania Bara, walibaini
malalamiko ya Watanganyika kuwa ni pamoja na kukosa fursa mbalimbali ndani ya
Zanzibar. “Watu wa bara nao wanasema Zanzibar inashiriki Bunge la Muungano,
inakagua miradi ya bara na kuihoji lakini wao hawana nguvu ya kushiriki mambo
hayo kwa upande wa Zanzibar,” alisema.
Aliongeza: “Mbaya zaidi wanasema Wazanzibari wanaweza kumiliki
ardhi na kupata uraia kwa upande wa bara lakini haki hizo haziwezi kupatikana
kwa Mtanganyika, njia pekee tukaona ni vyema Zanzibar nayo ilete mambo yake
ndani ya Muungano lakini ikashindikana.”
Hoja ya takwimu
Jaji Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge wasihangaike na takwimu
badala yake wajibu maswali yaliyojitokeza kutoka kwa washirika wa Muungano.
“Takwimu siyo tatizo, sisi hatukufanya jambo jipya, ila ilikuwa
ni kama marudio tu ya Tume ya Nyalali, wanahoji takwimu hizo je, hawakuona
dosari kwa takwimu za maoni ya asilimia 20 kwa jaji Nyalali?
Alisema Tume yake ilizunguka nchi nzima ikiwa na waandishi
waliorekodi kwa tepu, video na maandishi kwa ajili ya kuweka kumbukumbu katika
mtandao wa Tume.
CHANZO, MWANANCHI