JUDITH…JUDITH…!
INNOCENT
A. NDAYANSE (ZAGALLO)
0755
040 520 / 0653 593 546
PUUU! Mlango mkubwa wa nyumba ya mzee Ndayishimiye
ulitikisika kwa kishindo. Kisha ukimya ukarejea. Mzee Ndayishimiye ambaye
wakati huo alikuwa mezani na familia yake wakipata mlo wa usiku, walishtuka na
kubaki wameduwaa.
Kwa kipindi cha wiki tatu mfululizo, matukio ya
kutisha na kusikitisha yalishamiri jijini Kigali nchini Rwanda. Watu wengi
waliuawa kwa kuvunjwa shingo, kupondwa na nyundo vichwani, kuchomwa moto na
hata kwa risasi.
Yalikuwa ni mauaji yaliyoitikisa nchi nzima ya
Rwanda, ukanda wa Maziwa Makuu, nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki,
Afrika na hata dunia nzima. Mauaji hayo ya kimbari yalisababishwa na tatizo
sugu la ukabila lililokuwa likiitawala ‘meli’ ya Rwanda.
Mtutsi alijiona kuwa yeye ni yeye ndani ya Rwanda.
Nani mwingine anayetaka kuwa na sauti? Mhutu naye hakuwa amelala. Yeye pia
aliamini kuwa ni yeye ndiye mwenye haki na raia halali wa Rwanda, kwamba Mtutsi
ni mkimbizi tu!
Ni kutokuelewana huko ndiko kulikozua mzozo na
hatimaye mapigano yaliyosababisha uadui mkubwa baina ya makabila hayo mawili
makubwa nchini humo.
Usiku huu, saa 2.30, ndiyo kwanza Mzee Ndayishimiye
alikuwa amerejea huku akitweta kwa woga. Hakuwa katika hali ya kawaida. Amani
ilikosekana moyoni mwake. Tangu alipoingia humo ndani kwake, alitaka kumweleza
mkewe hayo aliyoyashuhudia huko alikotoka lakini alijikuta akisita. Aliona kuwa
ni mapema mno kulizungumzia hilo.
Fikra zake zilikuwa umbali wa nusu kilometa ambako
alishuhudia rafikiye mpenzi, mzee Shomvi Niyonzima akiuawa kikatili pamoja na
familia yake. Mzee Shomvi aliuawa kwa kufungiwa ndani ya nyumba kisha nyumba
hiyo kuchomwa moto. Lilikuwa ni tukio lililomtisha na kumsikitisha sana mzee
Ndayishimiye!
Alishuhudia nyumba hiyo ikiteketea huku sauti za
vilio vya mkewe Shomvi na wanae waliokuwa ndani humo zikisikika! Vilio hivyo
hivyo awali vilisikika kwa nguvu lakini hatimaye vilipungua taratibu na kuzidi
kutia simanzi kwa kuwa moto ule ulizidi kuwaka na paa likatumbukia ndani, hali
iliyotoa taswira ya kuwa hakuna kiumbe yeyote atakayenusurika.
Ilimuuma mzee Ndayishimiye!
Hali ya hewa ilikuwa imechafuka! Mzee Ndayishimiye
naye sasa akakiona kifo kikimchungulia. Akajenga imani ya zahama hiyo kufika
nyumbani kwake! Kwa mfadhaiko mkubwa kichwani mwake, akatembea kwa hatua ndefu
hadi kwake ambako aliwakuta wanafamilia wake wakiwa ndiyo kwanza wakijiandaa
kupata mlo wa usiku.
Bila ya kuwaambia chochote alijiunga nao mezani.
Lakini mwonekano wake ulimshangaza mkewe
ambaye hakusita kumuuliza, “Baba Judi vipi, za huko ulikotoka?”
Mzee Ndayishimiye hakujibu, badala yake alitwaa
tonge la ugali na kutowelea kwenye mboga kisha akalipeleka kinywani. Wala
hakumtazama hata mkewe, hali iliyozidi kuwashangaza mama Judi na Judith ambaye
ndiye aliyekuwa mtoto mwenye uwezo wa kupambanua mambo.
“Baba!”
Judith alimwita baada ya kumwona akiduwaa na tonge la pili mkononi bila
ya kulipeleka kinywani.
Ndiyo, Mzee Ndayishimiye hakuwa timamu. Sasa alitoa
macho pima, akawatazama mkewe na watoto wake kwa zamu huku kijasho chembamba
kikimtoka kwenye paji la uso.
“Baba kwani kuna nini?” Judith alimuuliza kwa
msisitizo, naye sasa akiacha kula na kumtazama kwa makini.
Mama Judith alipeleka mnofu wa nyama kinywani huku
akimtazama mumewe kwa jicho kali na la udadisi. Akamgeukia mwanaye, Judith kisha
akayarejesha tena kwa mumewe ambako alimkuta akimtazama Judith bila ya
kupepesa, jicho nyanya!
“Wamewamaliza!” hatimaye mzee Ndayishimiye alisema
kwa sauti ya chini, nzito na iliyojaa fadhaa.
Mara Judith akayarudisha macho kwa baba yake.
Akamtazama bila ya kutamka chochote. Walipokutanisha macho, mzee Ndayishimiye
akaamua kumgeukia mkewe ambaye naye bado alikuwa akimtazama.
“Nini?” mkewe alimuuliza, sauti yake ikionyesha
dhahiri jinsi alivyoipokea kauli ya mzee huyo kwa mshangao.
Kabla mzee Ndeayishimiye hajajibu, ndipo mlango wao
ukalia puu! Ukatikisika kwa nguvu! Akili na macho ya wote yakahamia hapo
mlangoni. Wakaduwaa! Macho yamewatoka pima! Kisha ukimya ukarejea!
Kisha tena, puu! kwa mara nyingine mlango ukagongwa
na kutikisika zaidi. Pigo la tatu liliulazamisha mlango ufunguke! Wanaume wanne
wenye silaha wakaivaa sebule hiyo.
Ndiyo, walikuwa ni wanaume wenye nyuso zilizotangaza
shari, mavazi yao ya kijeshi yakiwa ni ishara kuwa wako kazini.
Mzee Ndayishimiye na familia yake wakaendelea kuwa
katika hali ileile, wameduwaa, na zaidi, kila mmoja alikuwa katahayari!
Wale wanaume wakawasogelea wanafamilia hao bila ya
kutamka chochote. Kisha wakatulia. Wakatazamana. Mara mmoja wao akainua bunduki
na kumlenga mzee Ndayishimiye kifuani. Ilikuwa ni kama vile mchezo fulani wa
kuigiza. Askari huyo alitulia kwa sekunde chache na kumgeukia mwanzake ambaye
alionekana kama kiongozi wa msafara. Wakatikisa vichwa kwa pamoja kama ishara
ya kukubaliana.
Inaendelea kesho...
No comments:
Post a Comment