INNOCENT A. NDAYANSE
(ZAGALLO)
0755 040 520 / 0653 593
546
UTANGULIZI
Judith
amefanikiwa kutoroka mikononi mwa Makella wakati Makella akiwa anaoga. Na
Judith haondoki mikono mitupu, anachukua na kibunda cha Dola 2,000 ambazo
Makella alizipata katika harakati zake za kuwaua Wautsi. Makella anapotoka
bafuni na kukuta hayupo, anaanza kumwadhibu mhudumu wa gesti hiyo. Je, nini
kitaendelea? Ungana na msimulizi wako …
“Sema!
yule malaya yuko wapi?”
“Ametoka!”
binti yule alijibu.
Kofi la
pili!
“Jamani
utaniua bure!” mhudumu huyo alilalamika kwa sauti iliyoashiria kilio.
“Nitakuua
kweli!” Makella aliwaka. “Sema yuko wapi…sema…sema au nakuua!”
“Subiri
nikwambie!” mhudumu alisihi.
Makella
alimwachia. Akamtazama kwa macho makali huku akihema kwa nguvu. “Yuko wapi?”
akarusha swali kwa ukali uleule huku akiendelea kuhema kama mtu anayekaribia
kufa.
“Katoka!”
mhudumu alijibu kwa woga.
“Katoka?!”
Makella akamkodolea macho zaidi, pumzi zikapanda na kushuka kwa kasi. Pua
zikamcheza kama nguruwe-pori!
“Ndiyo!”
“Kaenda
wapi?”
“Kasema
eti anafika hapo mtaa wa pili!”
“Kaniibia!”
Makella aliropoka kwa nguvu.
“Nini?”
mhudumu alibaki kinywa wazi.
Hata hivyo
Makella hakuwa na muda wa kumsimulia mhudumu huyo hadithi nzima. Hakuuona
umuhimu wa kufanya hivyo. Hasira zikiwa zinazidi kuongezeka kichwani mwake,
alifoka, “Toka! Potea machoni kwangu kabla sijakisambaratisha kichwa chako mbwa
wee!”
Haikuwa
amri ambayo ilihitaji swali au mjadala wowote kwa wakati huo. Kwa kuuhofia
usalama wake, mhudumu huyo alitoka mkuku, ufunguo wa akiba wa chumba hicho
akiwa ameuacha kwenye kitasa cha mlango.
Makella
alizidi kuchanganyikiwa. Akaivua taulo na kuitupa kitandani . Kisha akavaa nguo
zake kwa kasi isiyokuwa ya kawaida. Dakika ya pili alikuwa akitoka chumbani
humo mithili ya chizi, akiteremka ngazi za ghorofa hiyo kwa kukimbia.
Aliikamata bunduki imara mkononi akionekana kuwa yuko tayari kuitumia muda
mfupi ujao dhidi ya yeyote atakayestahili.
Alipofika
nje ya geti akamfuata mlinzi aliyekuwa akirandaranda katika eneo hilo. “Kuna
mwanamke yeyote mrefu, kavaa fulana ya bluu na sketi nyeusi aliyepita hapa?”
Yule
mlinzi, kama ilivyokuwa awali kwa yule mhudumu naye alimtazama Makella kwa
mshangao.
“Nakuuliza
wewe!” Makella aliwaka.
Sasa yule
mlinzi aliituliza akili yake na kumuuliza Makella, “Umbo lake likoje?”
“Mrefu!
Mweusi!”
Yule
mlinzi aliitika kwa kutikisa kichwa kisha akasema, “Kapita hapa kama dakika
kumi zilizopita!”
“Ni
malaya! Kaniibia!”
“Kakuibia?”
Makella
hakujibu. Badala yake akarusha swali: “Kaelekea wapi?”
“Kaelekea
huko!” mlinzi akajibu huku akionyesha kwa kidole upande wa mashariki.
Makella
hakusubiri, kama kichaa alitoka mkuku, akaivaa Barabara ya 17/18. Akavuta hatua
ndefu, akilini mwake akiwa hana hakika ya kufanikiwa katika harakati alizozianzisha.
Lakini alijipa imani kuwa atafanikiwa.
Akazidi
kukaza mwendo. Mara akasonya kwa nguvu na kuinyanyua juu bunduki yake AK-47
yenye risasi ishirini. Kisha akajikuta akibwata kwa mnong’ono uliofurika tani
kadhaa za hasira, “Nitampata! Na ole wake nimpate, atajuta kuzaliwa Mtutsi!
Kwanza nachukua pesa zangu, halafu…” akaiacha sentensi hiyo ikielea.
**********
KITENDO cha dereva teksi kumwona mtu akiingia garini haraka vile, naye
akajitoa kwenye kundi la wenzake alikokuwa akiongea, akajitoma garini. Judith
alikuwa ameketi kiti cha mbele. Wakatazamana. Judith akashusha pumzi ndefu na
kumuuliza, “Una mafuta ya kutosha?”
“Yapo, dada. Kwani una safari ndefu?”
“Nakwenda mpakani.”
“Yanatosha. Kuna lita thelathini. Kwa mpakani yanatosha. Vipi, mbona safari
ya huko saa hizi? Kuna tatizo?”
Lilikuwa ni swali ambalo Judith hakulipenda na hakulitarajia. Kwa hali
hiyo hakuwa tayari pia kulijibu. Zaidi, alisema, “Twende.”
Dereva alimtazama kidogo na kugeukia mbele. Alishagundua kuwa abiria
wake hayuko katika hali ya kawaida. Akaling’oa gari taratibu na kuingia
barabara kubwa. Dakika tano baadaye, Judith alimwambia, “Kama unaweza,
tafadhali ongeza mwendo. Nina haraka.”
Kwa mara nyingine dereva alimtazama Judith na safari hii akauona uso
wake ukiwa umebadilika. Alionekana kuchangamka kidogo. Ndiyo, Judith aliamua
kuirejesha hali hiyo ili kumfanya dereva asiwe na wasiwasi naye na amchukulie
kama abiria wengine wa kawaida.
“Sawa, dada,” dereva alisema huku akibadili gia na kuongeza mwendo. Kwa
kiasi fulani Judith akajisikia afueni.
Kwa jumla alikuwa na hofu kuhusu Makella. Akili yake ilimwambia kuwa kwa
vyovyote vile, Makella atakapookolewa na wafanyakazi wa Hoteli ya Kiyovu,
kitakachofuata ni kumsaka. Na huenda akapata fununu zitakazomsaidia kumfikisha
huko mpakani. Na kama atafanikiwa kufika mpakani na akamwona, kitakachofuata ni
kumshindilia risasi zote zitakazokuwa kwenye bunduki yake.
Akawa akiomba Mungu kimoyomoyo, lisitokee hilo analolifikiria.
Nusu saa baadaye walikuwa wamefika mwisho wa safari yao. Lilikuwa ni
eneo lililochangamka sana. Magari mengi makubwa yalikuwa yameegeshwa huku
wahusika wake wakiwa wameketi kwenye baa zilizofurika katika eneo hilo.
Judith alipita katika makundi hayo na kwenda kwenye kijibanda
kilichokuwa sehemu yenye kijigiza ambako aliketi na kuagiza bia baridi. Aliamua
kukaa huko ili ajipange jinsi ya kuondoka eneo hilo na kwenda mbali zaidi
ambako aliamini kuwa huenda ndiko kwenye usalama. Na aliamua kuendelea kunywa
bia kwa kuwa aliona kuwa ndiyo nguzo pekee iliyomwondolea woga na kumwongezea
ujasiri.
Kama alitarajia kuwa angepata utulivu kwa kuketi peke yake basi haikuwa
hivyo. Muda mfupi baadaye wanaume wawili
walikuja katika kibanda hicho huku wakiwa na chupa za bia. Aliyetangulia
alikuwa ni Baraki, dereva wa gari kubwa lililokuwa na safari ya kuelekea
Tanzania. Mwenzake alikuwa ni Livingstone ambaye alikuwa ni utingo.
Wakamsalimia Judith na kuketi katika meza ya pili iliyokuwa na viti
vitatu. Lakini Baraki hakukaa muda mrefu mara akamgeukia Judith na kumuuliza, “Dada
yetu mbona umekaa peke yako? Karibu hapa tujumuike pamoja.”
“Asante,” Judith alijibu bila ya kuwafuata.
Itaendelea kesho…
No comments:
Post a Comment