Dk. Willibrod Slaa
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
‘SERIKALI YA KIKWETE IKOMESHE ‘UKABURU’
DHIDI YA WATANZANIA’
KATIBU Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibroad Slaa
amehitimisha ziara yake ya siku 22 ya kuimarisha na kukagua uhai wa chama
katika majimbo 19 mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Singida, akiitaka
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukomesha manyanyaso na ukatili wanaofanyiwa wananchi.
Amesema kuwa baada ya kuzungumza na wananchi hususan maeneo ya vijijini ambako alijikita kwa siku hizo 22, ameendelea kuthibitisha kuwa sehemu kubwa ya kero zinazowakabili Watanzania, hazihitaji gharama yoyote kuzimaliza ili wananchi waishi kwa amani katika nchi yao, akitolea mfano wa kero ya manyanyaso mbalimbali, hususan kutoka kwa vyombo vya dola.
Amesema kuwa baada ya kuzungumza na wananchi hususan maeneo ya vijijini ambako alijikita kwa siku hizo 22, ameendelea kuthibitisha kuwa sehemu kubwa ya kero zinazowakabili Watanzania, hazihitaji gharama yoyote kuzimaliza ili wananchi waishi kwa amani katika nchi yao, akitolea mfano wa kero ya manyanyaso mbalimbali, hususan kutoka kwa vyombo vya dola.
Amesisitiza
kuwa kama Serikali ya Rais Kikwete inataka kupata uhalali mbele ya Watanzania
na iwapo Rais mwenyewe anataka kumaliza muda wake na kuacha kumbukumbu kwa
wananchi, inatakiwa kukomesha mara moja manyanyaso wanayofanyiwa wananchi,
kwani kufanya hivyo ni wajibu wa serikali na hakuna gharama yoyote.
Akitolea
mifano ya matukio ya kikatili na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu
unaofanywa vyombo vya serikali kupitia matukio mbalimbali zikiwemo operesheni
mbili za hivi karibuni, Tokomeza Ujangili na Kimbunga, Katibu Mkuu amesema kwa
namna ambavyo serikali iliyoko madarakani inawatenda raia wake, Tanzania
inavunja rekodi hata ya Afrika Kusini ya enzi za Makaburu.
“Tunatamtaka
Rais Kikwete kuacha kufanya kama afanyavyo baba asiyejali au baba wa kambo
anayechukia watoto…JK ukitaka ubaki na heshima baada ya kuondoka madarakani,
fanyia kazi orodha ya manyanyaso wanayofanyiwa wananchi. Tena mengi yanafanywa
na polisi, jeshi na wakuu wa wilaya, watendaji wa vijiji na watendaji wa kata
na madiwani.
“Yapo
mengine ya kubambikia kesi watu, kunyang’anywa ardhi, kunyimwa haki kwa nuguvu
tu, kuchangishwa michango haramu inayoambatana na vipigo na kunyang’anya watu
mali zao, huku mapato na matumizi hayasomwi na nyingine kero kubwa kabisa ya
migogoro ya ardhi. Kuachia manyanyaso haya dhidi ya wananchi nji kuonesha
udhaifu mkubwa wa kiuongozi. Labda watuambie kuwa serikali hii ya CCM sasa
imeshaamua kuwatenda raia wake.
“Hauhitaji
hata senti moja kuondoa manyanyaso ya serikali kupitia vyombo vya dola
wanavyofanyiwa wananchi. Mnapomtesa Mtanzania namna hii…watu wanateswa sana na
kubambikiwa kesi, wanapigiliwa spoke sehemu za siri, wanawekewa chupa na
kubakwa, mnataka aende kuishi wapi.
“Hayo
maendeleo mnayoyazungumza ni kwa ajili ya nani kama wananchi wanapigwa, kuteswa
na kuuwawa bila hata hatia. Tumefikia mahali serikali inawatenda raia wake
kuliko hata Makaburu walivyomtesa Mzee wetu Hayati Mandela alipokuwa gerezani.
“Mwalimu
Nyerere alisema ukaburu si rangi. Huu unaofanyika ni ukaburu ambao wakati ule
wa ubaguzi wa rangi tuliimba sana shuleni na majeshini kupinga ukatiliwa
makaburu wa Afrika Kusini dhidi ya weusi waliokuwa wengi. Leo Serikali hii
inafanyia raia wake matendo zaidi ya yale. Tunakwenda wapi. Kikwete chukua
hatua.”
“Kila
nilikopita ni vilio vya manyanyaso, kuanzia Kakonko kule Wilaya ya Buyungu,
kote huko Kasulu Vijijini viongozi wangu wote wa serikali znima ya kijiji
wamebambikwa kesi ya mauaji, wote kabisa. Hapo Nzega nimeshuhudia kwa macho
yangu mateso wanayoyapata wachimbaji wadogo wadogo, wengine wamepigwa vibaya na
askari polisi, tena machimbo yao yametekwa na viongozi wa wilaya na kuyageuza mali
zao na sasa wanachuma pesa kwa kupiga raia.”
Katibu Mkuu Dkt.
Slaa ambaye alianza ziara yake Desemba 4, mwaka huu kwa kufanya mkutano wa
hadhara na kikao cha ndani Jimbo la Kahama, mkoani Shinyanga, amehitimisha
ziara yake Desemba 23, kwa kuhutubia wananchi wa Vijiji vya Shelui na Nyengege,
Jimbo la Iramba Magharibi.
Amewataka
wanaCHADEMA kuuchukulia mchakato na mjadala wa Katiba Mpya ya Watanzania kuwa
agenda ya muhimu, ya kudumu na lazima katika mikutano yao yote, ikiwemo ya
ndani ya chama, hadhara au ‘vijiweni’, lengo la msingi liwe kuwataarifu
wanachama na wananchi kwa ujumla, tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.
Ametumia
ziara hiyo kuwasisitiza viongozi na wanachama wa CHADEMA nchi nzima kuhakikisha
wanatekeleza maagizo mbalimbali ya vikao ya chama, hususan kwa sasa wasimamie
kikamilifu maelekezo ya Waraka Katibu Mkuu Namba 6 wa mwaka 2013.
Waraka huo
ambao unahusu mkakati wa kusukuma ujenzi wa misingi/matawi na uchaguzi wa ndani
ya chama 2013/2014, umeelekeza viongozi nchi nzima namna ya kuendesha programu
ya ‘M4C-CHADEMA ni Msingi’ inayoendelea nchi nzima, ikisimamiwa na kanda 10 za
chama ambapo moja ya malengo mahsusi ni kusimika na kuimarisha chama kwenye
vitongji na mitaa.
“Ni lazima
kila mwanaCHADEMA, wapenzi wa chama hiki, wananchi wenye mapenzi mema na
ukombozi wa pili wa taifa lao, tuungane, tushikamane pamoja kusukuma jitihada
hizi za kusimika chama chenu, ambacho ndiyo tumaini jipya la Watanzania katika
ngazi ya chini kabisa ya uongozi katika nchi yetu.
“Viongozi
wote wenye mapenzi mema na CHADEMA, kuanzia ngazi ya taifa hadi chini kabisa
lazima wahakikishe CHADEMA ni msingi inakamilika kama ilivyokusudiwa,”
amesisitiza Katibu Mkuu Dkt. Slaa katika ziara hiyo.
Katika
kuwakumbusha juu ya waraka huo, Katibu Mkuu Dkt. Slaa amewasisitiza wanachama
na viongozi umuhimu wa kuzingatia;
1. Kupata viongozi imara wa chama
kuanzia ngazi ya chini kabisa ya msingi2. Ratiba ya utekelezaji wa mkakati wa CHADEMA ni Msingi
3. Ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama ngazi ya jimbo hadi taifa (pamoja na mabaraza ya chama), baada ya ngazi za chini kumalizika
4. Kuzingatia taratibu za kikatiba za uchaguzi, kwani uchaguzi wa ‘mezani’ hautakubalika ndani ya CHADEMA.
5. Rushwa na kampeni chafu (katika uchaguzi kwa ngazi yoyote ile) hazitavumiliwa hata kidogo.
6. Maadili ya chama yasimamiwe kwa kila ngazi ya uchaguzi
7. Ulinzi wa chama/ viongozi na wanachama ngazi zote, ambapo Red Brigade na BAVICHA ni nguzo ya ulinzi.
Ukombozi wa kweli uanzie serikali za
mitaa, vijiji na halmashauri
Katibu Mkuu
amewataka Watanzania kuelewa kuwa ukombozi wa kweli wa mwananchi utapatikana
iwapo watu wataweza kuchagua viongozi imara, makini, waadilifu na wapenda watu
kuanzia ngazi ya kitongoji, mtaa na kijiji na hatimaye madiwani ambao huunda
halmashauri ya wilaya, mji, manispaa au jiji.
“Ikulu ya
kwanza ya mwananchi ni hapa ulipo, hapa kijijini kwako. Ikulu ya pili ni
halmashauri yenu ya wilaya. Hizi ni sehemu muhimu sana katika kuhakikisha watu
wetu wanapata matumaini, haki na hatimaye ustawi wa maendeleo ndani ya nchi
yao. Hakuna maana yoyote kuichagua CHADEMA iende Ikulu ya Magogoni, Dar es
Salaam halafu huku mnaweka watu wabovu. Itakuwa sawa na kazi bure,”amesisitiza
Katibu Mkuu Dkt. Slaa.
Amesema kuwa
hasa wakati huu ambapo Taifa linajiandaa kwenda kufanya uchaguzi wa Serikali za
Mitaa mwaka 2014, Watanzania wanapaswa kutambua umuhimu wa halmashauri za
serikali za mitaa katika kusukuma maendeleo ya watu katika maeneo yao
wanayoishi.
Amesisitiza
kuwa katika ngazi hiyo ya uongozi, si kazi ngumu kumtambua mtu ambaye anaweza kuwa
kiongozi mwadilifu, makini mwenye uwezo na mpenda watu, kwa sababu watu wote
wanafahamiana kutokna na kuishi pamoja.
Pinda kubanwa chaguzi serikali za
mitaa
“Katika
ziara yangu hii ya siku 22, nimebaini kuwa kuna maeneo mengi sana ya vijiji ama
hayana serikali kabisa, sehemu nyingine mwenyekiti hayupo au wajumbe, lakini
Serikali ya CCM kupitia kwa wakurugenzi inaogopa kuitisha uchaguzi, kisa
wanaogopa wakiitisha uchaguzi CHADEMA itashinda.
“Sasa
napenda kutumia mkutano wangu huu wa kuhitimisha ziara hii, kutoa maagizo kwa
viongozi wa chama wilaya na majimbo, kutuandikia taarifa ya kina Makao Makuu,
ikieleza maeneo yote ya serikali za mitaa ambayo yako wazi na wakurugenzi
hawajatangaza au hawataki kutangaza ndani ya muda unaotakiwa kisheria uchaguzi
wa kuziba nafasi kufanyika.
“Tunataka
taarifa za kina ambazo tutazitumia kumbana Mizengo Pinda maana yeye ndiye
anahusika kusimamia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa au TAMISEMI.
Hatuwezi kukubali kuona wananchi wanakosa haki yao ya uwakilishi kwa sababu tu
CCM wanaogopa ukiitishwa uchaguzi CHADEMA tutashinda. Katika hili pia tutakufa
na Pinda,” amesema Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu
Dkt. Slaa ametembelea jumla ya majimbo 19 ambayo ni; Kahama (Shinyanga),
Kakonko, Muhambwe, Kasulu Vijijini, Kasulu Mjini, Buhigwe, Kigoma Kaskazini,
Kigoma Mjini, Kigoma Kusini ambayo yako mkoani Kigoma. Mengine ni;
Kaliua,
Urambo, Tabora Kaskazini, Tabora mjini, Sikonge, Igalula, Bukene, Nzega, Igunga
(Tabora) na Iramba Magharibi mkoani Singida.
Katika
maeneo yote aliyotembelea, Katibu Mkuu Dkt. Slaa amepokea kero na ushauri wa
wanachama na wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya chama na nchi, ya kitaifa na
mengine yanayohusu maeneo husika, kwa njia mbalimbali ikiwemo taarifa za
viongozi kuhusu utendaji wa chama, kutoa fursa za maswali na maoni katika
mikutano pamoja na kufika mwenyewe kujionea hali halisi ya baadhi ya masuala aliyoambiwa.
Imetolewa leo Desemba 23, 2013 na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari-CHADEMA
No comments:
Post a Comment