Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 18 December 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (16)

Mwandishi wa makala haya Bw. Daniel Mbega (aliyeinama mwenye koti) akiwaongoza baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu mahali ambako mama yake Chifu Mkwawa, Sengimba, alitumbukia.

Na Daniel Mbega

KUANGUKA kwa Kalenga kulikuwa ni hatua ambayo haikutegemewa na wengi kwani ilionyesha dhahiri kuanguka kwa Himaya ya Uhehe. Lakini pamoja na kushindwa katika Vita ya Kalenga, Chifu Mkwawa na askari wake walianzisha sera ya namna mbili.
Kwanza, badala ya kukabiliana ana kwa ana na Wajerumani katika vita kama walivyofanya katika mapambano ya Image, vikosi vya Wahehe vikaanzisha vita ya msituni. Chifu Mkwawa aliwaonya wapiganaji wake kuepuka mapambano ya ana kwa ana, wakaendelea kuvamia misafara ya Wajerumani na kupora mali, kuvamia vikosi vya Wajerumani kwa kushtukiza, kuvamia maboma yao na kadhalika.
Pili, Chifu Mkwawa aliendelea na jitihada zake za kutaka suluhu na Wajerumani. Wakati kuanguka kwa Kalenga kulionyesha kwamba Wahehe na jirani zao ambao walikuwa wamewaunga mkono Wajerumani kitambo, ukweli kwamba jeshi la Wahehe lilikuwa limekimbia na Mkwawa na vikosi vyake walikuwa wanajipanga kutaka kuitwaa Kalenga kukampa imani Mkwawa kwamba Wajerumani wangeweza kukubali kuketi mezani.
Wahehe walirejea tena Kalenga na kuanza kuijenga upya ngome ya Lipuli, japokuwa siyo katika kiwango kile kama cha kabla ya kuanguka kwake Oktoba 1894. Chifu Mkwawa akawa na wakati mgumu wa kuimarisha himaya yake.
Tayari usaliti ulikuwa umeingia kwa Wahehe baada ya kuanguka kwa Kalenga, kwani hata wale machifu wadogo walianza kuipokea bendera ya Wajerumani, ambao hatimaye walijenga ngome yao Iringa mwaka 1896.
Kama ambavyo Wabena na Wasangu walikuwa wamemsaliti Mkwawa kwa kuwakubali Wajerumani, watu wake pia walianza kushirikiana na Wajerumani, ingawa wengi wao waliendelea kumuunga mkono, kumficha na hata kumpa msaada wa chakula na taarifa. Pamoja na hayo, Mkwawa aliendelea kuimarisha jeshi lake lililoundwa na vijana wa Kihehe.
Tatizo kubwa lililoibuka baada ya kuanguka kwa Kalenga lilikuwa ni kwa mdogo wake Chifu Mkwawa, Mpangile, ambaye ndiye aliyemfuata kwa kuzaliwa. Mpangile aliona hiyo ndiyo ilikuwa fursa kwake kuchukua nafasi ya kaka yake, akaanza kumlaumu Mkwawa kwamba ndiye aliyesababisha majanga yote yaliyotokea na kuanguka kwa Himaya ya Uhehe mwaka 1894.

Kikongoma
Japokuwa hakuna kitu kilichotajwa kama ‘uhaini’ kutokana na hatua hiyo ya Mpangile, mwaka mmoja na nusu baadaye baada ya Kepteni Tom von Prince kurejea Uhehe kuitazama ‘Iringa Mpya’, akamteua Mpangile kuwa ndiye ‘Chifu’ wa Wahehe.
Ignas Pangiligosi Muyinga, almaarufu kama Malugila Mwamuyinga, anasema tamaa ya madaraka ilimfanya Mpangile akubaliane na mpango wa Wajerumani wa kumsaka Chifu Mkwawa ili wamkamate. Kwa hiyo basi, Wajerumani walipoona Mkwawa anawapiga chenga na Wahehe wanafanya kila jitihada kumficha, njia pekee waliyoona kuwa ni bora ikawa kumkamata mama yake Mkwawa, Sengimba, ambaye ndiye mama mzazi wa Mpangile.
Lengo kubwa la kumkamata Sengimba lilikuwa kumlazimisha akawaonyeshe mahali alipo Chifu Mkwawa, maana walisema lazima atakuwa anajua. Wakati huo Chifu Mkwawa alikuwa amejificha Mlambalasi mlimani katikati kabisa ya msitu.
Baada ya kumakatwa, Sengimba akawaongoza Wajerumani, wakiwa pamoja na Mpangile, hadi kwenye ‘Daraja la Mungu’ la Kikongoma katika Mto Ruaha wilayani Iringa, takriban kilometa 35 kutoka Iringa mjini.
Kweli pale ni Daraja la Mungu, kwani katika umbali wa takriban kilometa moja hivi Mto Ruaha umezama chini kwa chini huku juu kukiwa na mawe yaliyotandikwa na ‘Mungu’ kufanya daraja ambalo mpaka leo hii watu wanapita kwa miguu bila shida.
“Hapa ndipo baadhi ya watu, wakiwemo Wazungu, wanapoipotosha historia halisi. Wao wanasema waliomkamata Sengimba walikuwa Mwamubambe Mwalunyungu aliyeupindua utawala baada ya kifo cha Munyigumba, ambaye aliongozana na Mhalwike hadi hapo Kikongoma ili Mama Sengimba awaonyeshe dawa ya vita aliyokuwa akiitumia Mkwawa.
“Maelezo haya siyo sahihi kabisa. Kwa sababu, Mwamubambe alimchinja Mhalwike ambaye alidhaniwa kwamba ndiye angeweza kurithi utawala huo, Chifu Mkwawa naye akakimbizwa Dodoma kwenda kufichwa. Hata aliporejea, Mwamubambe alikuwa na nguvu kubwa na aliwaua askari wengi wa Mkwawa. Kama Mkwawa alikuwa na dawa ya ushindi kwenye vita, hivi kweli angeweza kushindwa?” anahoji Mwamuyinga na kusisitiza kwamba, Sengimba aliwaongoza Wajerumani hadi Kikongoma, siyo Mwamubambe na Mhalwike kama wengi wanavyoeleza.
Mwamuyinga, katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala haya, anasema Sengimba aliwapeka Wajerumani hao hadi Kikongoma, mahali ambapo pana jiwe kubwa na kwa upande wa nyuma kuna upenyo mwembamba kuelekea chini ambako Mto Ruaha unapita kwa kasi.
“Alipofika pale kwenye jiwe, Mama Sengimba akavua nguo zake zote na kuzirundika kwenye jiwe hilo huku akiwatukana Wajerumani akisema; “Niwalagile ilihomelo la muswamu wangu nyo wakeng’e nyenye!” (akimaanisha – ‘Niwaonyeshe alipojificha mwanangu mpenzi, nyinyi wajinga sana!’). Wajerumani walikuwa wakkimshuhudia mama akivua nguo zake na hawakkujua anataka kufanya nini. Hata maneno aliyoyasema hawakuelewa maana yake. Wakamtazama hata alipolizunguka jiwe hilo, akaenda upande wa pili na kujitumbukiza kwenye mto uendao kasi kupitia upenyo ule. Wajerumani walipotaharuki wakakuta tayari amekwishachukuliwa na maji,” anasimulia Mwamuyinga.
Anaongeza kwamba, mahali hapo pana mazingara na kwamba kila anayepita ni lazima atupe vijiwe mahali alipoweka nguo zake. “Ni imani tu, lakini ukweli ni kwamba, usipofanya hivyo unaweza kupotea huko uendako.”
Pamoja na ukweli kwamba Wahehe wamekuwa wakifanya matambiko katika nyakati fulani, lakini kwa namna eneo hilo lilivyo, pamoja na tukio lililotokea enzi hizo, kuna kila sababu kwa mamlaka husika kuweka walau kumbukumbu yoyote mahali hapo ikiwa ni pamoja na kulitenga eneo hilo kama la makumbusho.

Ni eneo zuri linalofaa kwa utalii, uwe wa ndani au wa kimataifa, na kwa hakika linafaa hata kufundishia historia kwa vizazi vyetu – vya sasa na vijavyo.
Tutaendelea...

No comments:

Post a Comment