Kaburi walimozikwa makamanda wa jeshi la Wajerumani waliouawa na Chifu Mkwawa pale Lugalo.
Na Daniel Mbega
KAMA tulivyoona huko nyuma, Wajerumani walionekana wema kuliko Mkwawa,
ambapo makabila mengi yaliyoizunguka Himaya ya Uhehe yaliyokuwa yakinyanyaswa
hapo kabla yaliona kwamba Wazungu hao ndiyo kimbilio lao na wangeweza kuwatetea
dhidi ya Mkwawa.
Wazungu kwa kiasi
kikubwa wanaipotosha historia katika kuhalalisha kile wanachodhani Waafrika
watakiona ndicho bora zaidi. Katika historia ya Mkwawa, wanadai kwamba, utajiri
ambao Chifu Mkwawa aliurithi kutoka kwa baba yake Munyigumba ulikuwa ni wa
dhulma, kwamba waliupata kwa kupora misafara, kama walivyofanya Wangoni na
Wasangu.
Na itakumbukwa kwamba,
Mkwawa aliendelea kuivamia misafara ya Wajerumani katika Njia ya Kati kadiri
alivyoweza, hali ambayo baadaye ikasababisha mapigano mengine katika Kijiji cha
Munisagara Desemba 7, 1892 ambapo pamoja na Wahehe kushindwa, lakini
walifanikiwa kukiteketeza Kijiji cha Kondoa kwenye Bonde la Mukondoa karibu na
ngome ya Wajerumani ya Kisaki.
Lakini siyo siri kwamba, ushindi wa Wahehe dhidi ya Wajerumani Agosti
1891 ulisikika kila pembe ya Afrika Mashariki ambapo Waafrika waliuzungumzia
sana. Lakini mwishoni mwa mwaka 1892 na mwanzoni mwa 1893 kulikuwa na kila
dalilia kwamba Wajerumani wangeweza kutawala kwa sababu nguvu zao dhidi ya
Wahehe zilikuwa zimeimarika na kutanua mpaka wao.
Wasagara, ambao awali walikuwa wameishi kwa hofu ya Mkwawa na kumpelekea
zawadi kila wakati ili asiwapige, sasa waliishi jirani na kambi za Wajerumani
na wakaanza kuubeza uwezo wa Wahehe waziwazi.
Wasangu nao, ambao waliwahi kuwa tishio kwa Wahehe, Wabena na makabila
mengi katika miaka ya 1850 na 1860, walinyanyaswa mno tangu enzi na Munyigumba na
Mkwawa baada ya Wahehe kuimarika na kuwageuzia kibao katika miaka ya 1870 na
1880. Kutoka na Wajerumani kupenya upande wa kaskazini na mashariki mwa Uhehe,
inaelezwa kwamba Chifu Merere Towelamahamba (Merere III) wa Usangu waligeuka
kuwa washirika wakubwa wa Wajerumani upande wa kusini ambapo waliweza
kuwaelekeza Wajerumani mahali gani na wakati gani wa kumshambulia Mkwawa.
Hata Wakinga na Wabena
ambao awali walionekana wanyonge wakaanza kugomea amri za Wahehe kwa matarajio
kwamba Wajerumani na Wahehe wangeweza kupigana na kuuana wenyewe. Wakati wa
Vita vya Lugalo, Wabena walikuwa wamewatoa wanamgambo zaidi ya 1,000; lakini
sasa miaka miwili baadaye walikuwa wameanza kukataa hata kupeleka chakula.
Kibaya zaidi kwa Mkwawa
ni kwamba, mgawanyiko ulitokea katika utawala wake chini ya kaka yake Mpangile
(ambaye baadaye ndiye aliyechukua nafasi ya Mkwawa kama ‘Chifu wa Wahehe’.
Kuzungukwa
na Wajerumani pamoja na usaliti wa watawala wengine kama Wasangu, Wabena na
Wasagara kuliifanya Himaya ya Uhehe iyumbe na kupunguza uimara wa Mkwawa, hali
hiyo ikawahamasisha Mpangile na wenzake kutumia madaraka yao na kuweka maazimio
kadhaa ya kisiasa ya kula njama na Wajerumani ili kumsaliti Mkwawa.
Wakati
ambapo matukio ya miaka ya 1892 na 1893 yalionekana taratibu yanamgeuzia kibao
Mkwawa, Chifu Merere Towelamahamba wa Usangu, kwa upande mwingine, aliiona
fursa ya kuingia kwa Wajerumani na vita yao dhidi ya Himaya ya Uhehe. Wasangu,
ambao Mkwawa hakuwahi hata kuingia nao maridhiano yoyote, walikuwa wameshikwa
na mshangao – wakaona fursa kubwa ya kutumia uvamizi wa Wajerumani kwa faida
yao. Jamie Monson aliwahi kuandika katika kitabu chake, “Wajerumani walionekana
kama washirika muhimu wenye nguvu na walinzi kwa jamii nyingi katika kanda ya
kusini. Wakafanya ushirika na watawala wa jadi kwa kuungana kidiplomasia.”
Merere
alikuwa mmoja wa watawala werevu sana kati ya ‘washirika’ wa Wajerumani. Tom
von Prince alikutana naye zaidi ya mara moja kwa amri kutoka makao makuu Dar es
Salaam kukamilisha baadhi ya makubaliano na Wasangu, ambao walionekana kuwa
washirika wazuri kutokana na mahali walikokuwa wakiishi magharibi mwa Uhehe
pamoja na uhasama wao wa muda mrefu uliokuwepo dhidi ya Mkwawa na watu wake.
Gavana von Soden pia akatumia fursa ya kuingia kwa Wamisionari wa Jumuiya ya
Wainjilisti ya Berlin (Berlin Evangelical Mission Society), kufungua mazungumzo
na Merere na kudumisha uhusiano wa ‘kirafiki wa kiserikali’.
Tutaendelea...
No comments:
Post a Comment