Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday, 17 December 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (15)


Na Daniel Mbega


Kuanguka kwa ngome ya Lipuli
Kalenga ni mojawapo ya vijiji vya kihistoria mkoani Iringa, kinachukua nafasi kubwa katika historia ya Chifu Mkwawa kama ilivyo kwa vijiji vya Makambako, Lungemba, Lugalo, Image, Lupembe lwa Senga, Mbweni na Mlambalasi. Hapa Kalenga ndipo yalipokuwa makao makuu ya ngome ya Chifu Mkwawa, Lipuli.
Ngome ya Lipuli ilikuwa na urefu wa futi 12 na urefu wa mail inane (takriban kilometa 12). Ngome hiyo ilianza kujengwa mwaka 1887 baada ya Mkwawa kusikia habari za harakati za Wajerumani katika Pwani ya Afrika Mashariki. Chifu Mkwawa alikuwa amejifunza namna ya kujenga ngome hiyo baada ya kuona ngome nyingine za mawe huko Unyamwezi au ngome za Waarabu za Wazungu huko pwani.
Mahali ilipokuwa ngome hiyo, kwa sasa kuna makaburi ya mwanawe wa kwanza Chifu Sapi na Chifu Adam Sapi, mjukuu wa Mkwawa. Takriban meta 500 kutoka hapo kuna kaburi dogo lenye mnara ambapo alizikwa Kamanda wa Kijerumani Erich Maas ambaye alipigwa risasi na wapiganaji wa Kihehe wakati wa mapambano ya ana kwa ana Wajerumani walipokuwa wakiivunja ngome ya Lipuli.
Wajerumani, wakiongozwa na Kamanda Tom Von Prince walianza harakati za kuivamia Kalenga. Safari hii walichagua njia ya hatari zaidi kuelekea Kalenga, ambayo hata Chifu Mkwawa mwenyewe hakutarajia kama wangeweza kuifahamu. Walipitia Kisaki, Ulanga na baadaye wakapanda milima ya Udzungwa na wakaanza kuteremka kuelekea Kalenga.
Mpango wa kuishambulia Kalenga ulianza Oktoba 28, 1894 wakitokea Mlima Lugulu, ambao unaitazama Kalenga katika kilele cha meta 400 ambako walijenga mahema yao kwenye kichaka cha miiba. Wajerumani wakapambana na Wahehe kwa siku mbili wakiishambulia Kalenga kutoka Mlima Lugulu, Wahehe walijitahidi kupambana na Wajerumani.
Hadi kufikia Okotoba 30, 1894 Wajerumani wakawa wamefanikiwa kuingia kwenye ngome ya Lipuli huku wakiwachoma kwa singe. Baada ya kuona hali imekuwa ngumu Chifu Mkwawa akafanikiwa kutoroka wakati Kalenga ikianguka. Wajerumani wakawa wamefanikiwa kuiteka ngome, wakateketeza silaha zote na kutweka pembe za ndovu walizozikuta. Wajerumani waliamini kwamba, kuiangusha ngome ya Lipuli kungeweza kumfanya Chifu Mkwawa akaketi meza moja na kukubali masharti yao.
Baada ya kuanguka kwa Kalenga, mtoto wa Chifu Mkwawa, Mtwa Risasiyaukali, aliamua kujipiga risasi mwenyewe badala ya kudhalilishwa na Wajerumani. Alikuwa miongoni mwa mateka waliokamatwa na Wajerumani na kulazimishwa kubeba mizigo kupeleka Dar es Salaam. Baada ya kifo chake, watu wa Mbweni waliamua kuiweka maiti yake mahali ambako maiti ya baba yake mkubwa, Malangalila Gamoto, ilikuwa imewekwa.

Kwa maana nyingine, hata baadaye kifo cha Mkwawa kilikuwa mfululizo wa vifo vingine vya kuepuka kudhalishwa vilivyotokea kwenye ukoo huo.
Tutaendelea...

No comments:

Post a Comment