Yangeyange mweupe.
Yangeyange fuata-ng'ombe.
Yange tumbo-kahawia.
Yangeyange Kulasitara.
Yangeyange njano.
Na Daniel Mbega (Mhifadhi Asilia)
SEKTA ya Utalii, hasa utalii wa
ndani ndiyo huchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Taifa katika sehemu nyingi
duniani, kwani ni sekta ambayo haihitaji mtaji mkubwa sana wa Serikali
kuiendesha.
Hii inatokana na ukweli kwamba,
mtaji uliopo ni wa asili kwani kuna vivutio vingi kama wanyama, ndege, mimea na
mbuga nzuri ambazo macho ya binadamu yeyote anayependa kubadilisha mtazamo wake
yangependa kuvinjari.
Hata hivyo, wananchi wengi wa
Tanzania wameonekana kutokuwa na utamaduni kwa kwenda kutembelea vivutio vyetu
vya asili vya utalii, badala yake wengi wao wako tayari kununua mikanda mingi
ya filamu za Kimagharibi na kupoteza muda mwingi kuangalia.
Hii ni mbaya kwa sababu siyo tu
tunawajengea utamaduni mbovu hata watoto wetu, bali tunaikosesha Tanzania
mapato ya ndani huku tukijenga hisia mbovu kwamba mbuga za wanyama ziko kwa
ajili ya Wazungu pekee, jambo ambalo siyo sahihi.
Kama hatukuepuka tabia hii, ipo
siku tutakuja kujikuta tuna kizazi ambacho hakiifahamu sura halisi ya Tembo,
zaidi ya kuendelea kuwatazama kwenye picha za kawaida tu, wakati nafasi ya
kwenda kuwaona ‘laivu’ tunayo na tunakuwa na shingo ngumu kubadilika.
Tanzania tunavyo vivutio vingi vya
utalii, lakini katika safu hii, ambayo inalenga zaidi kuwahamasisha Watanzania
kupenda utalii wa ndani, leo hii tutawazungumzia ndege jamii ya Yangeyange.
Yangeyange ni ndege wakubwa wa jenasi mbalimbali
katika familia
ya Ardeidae wenye miguu mirefu, shingo ndefu
na domo refu na jembamba. Hupinda shingo yao wakiruka angani. Ndege hawa ni
weupe au weusi au rangi hizi mbili (pengine kijani au buluu). Ndege hawa wana
majina mengine ya kienyeji (mwenye nayo naomba anitumie kwa jina la kabila yake
kwa ujumbe wa sms kupitia namba ya simu hapo chini tafadhali).
Spishi nyingine
huitwa ngojamalika, kulasitara au dandala. Yangeyange wengine hupenda kula
samaki, wengine hula wadudu na wanyama wadogo kama vyura na mijusi. Hujenga
matago yao kwa matawi juu ya miti, matete au mafunjo.
Yangeyange ama Egret au Heron wanatoka
katika Himaya (Kingdom) ya Wanyama (Animalia), Faila ya Chordata (Wanyama wenye
ugwe wa neva mgongoni), Ngeli ya Aves (Ndege), Oda ya Ciconiiformes (Ndege kama makorongo), Familia Ardeidae (Ndege walio na nasaba na koikoi), Jenasi ni
za (Bubulcus
Bonaparte, Butorides
Blyth, na Egretta
T. Forster).
Aina ama spishi zinazopatikana
Afrika ni Yangeyange au Yange
Fuatang’ombe (Cattle Egret), Ngojamalika
(Striated Heron),
Kulasitara
(Black Heron),
Yange-pwani (Dimorphic Egret),
Dandala
(Little Egret),
Yange Koo-jeupe (Western Reef Heron), Yange Domo-njano (Intermediate or Yellow-billed Egret), na Yange Mweusi (Slaty Egret).
Pamoja na kujua aina na jamii ya ndege
hawa, lakini hapa tutaangalia zaidi Yange Fuatang’ombe (Cattle Egret). Yange
Fuatang’ombe ni familia ya Heron wasiokula nyama, yaani cosmopolitan ambao wanapatikana katika
ukanda wa Tropiki na kanda za joto.
Ndege hawa wako katika jenasi ya
Bubulcus. Asili yao I sehemu za Bara Asia, Afrika na Ulaya, na wameweza
kusambaa sehemu mbalimbali duniani. Ukienda katika jamii za wafugaji utawaona
ndege hawa, mara nyingi wakiwa wanawafuata ng’ombe kwa ajili ya kula kupe.
Lakini zaidi wanapatikana katika
maeneo ya hifadhi kama Ziwa Manyara na kwingineko, na kwa hakika ni ndege
wazuri mno kuwaangalia.
Ndege hawa wana urefu wa kati ya
sentimeta 88–96 (Inchi 35–38) kwa kuzingatia upana wa mabawa yake kutoka ncha
moja hadi nyingine; urefu wao halisi ni kati ya sentimeta 46–56 (Inchi 18–22)
na wanaweza kuwa na uzani wa gramu kati ya 270–512 (wakia 9.5–18.1). Midomo yao
imechongoka sana, lakini huwa hawaleti madhara wanapodonoa kupe na inzi kwenye
ng’ombe.
Kwa ujumla, ndege hawa wana
uhusiano mzuri na binadamu na mifugo yao, na wanasaidia kuwashambulia wadudu
wenye madhara kwa mifugo hiyo, hasa kupe na inzi.
Mara nyingi malisho yao ni wadudu
kama panzi, inzi, buibui, vyura, na hata minyoo. Kwa nyakati nyingine wanaweza
kula matunda.
Ukiwa katika hifadhi za wanyama
mara nyingi utawaona ndege hawa wakiwa migongoni mwa wanyama kama pundamilia,
nyumbu na hata nyati, wakidonoa wadudu ambao huwashambulia wanyama hao.
Kwa kifupi, ndege hawa wana manufaa
makubwa kwa binadamu hasa wafugaji, kwani husaidia kupambana na wadudu wenye
madhara kwa mifugo, wadudu ambao wanaweza kusababisha magonjwa hatari ya mifugo
kama Ndigana.
Ni vyema Watanzania wakajenga
utamaduni wa kutembelea mbuga na hifadhi zetu na kushuhudia raslimali za asili
zilizopo badala ya kudhani mbuga hizi ni maalum kwa ajili ya wazungu.
* Mwenye maoni, au anayewajua ndege
hawa kwa majina ya kienyeji, anitumie kupitia namba 0715 070109, au e-mail: brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment