Na Daniel
Mbega, Serengeti
HAWANA
vyeti vya kuzaliwa, wala hawajulikani hata mahali gani wanapotupa makondo yao
ingawa ukifuatilia unaweza kuyaona, lakini Nyumbu (Wildebeest) wanaopatikana
katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni raia halali wa Tanzania.
Kwamba wanapatikana pia katika hifadhi ya Maasai Mara katika nchi jirani ya Kenya, katu hiyo haiwezi kuhalalisha uraia wao kwamba wanatokea huko.
Kwamba wanapatikana pia katika hifadhi ya Maasai Mara katika nchi jirani ya Kenya, katu hiyo haiwezi kuhalalisha uraia wao kwamba wanatokea huko.
Ni bahati
mbaya tu kwamba wanyama hawana paspoti kama ambavyo hawana vyeti vya kuzaliwa,
vingenevyo ushoroba (corridor) wanaoutumia ungewekwa kizuizi kama kile cha
Sirari, Namanga, Tarakea, Holili na kwingineko hakika hati hizo zingethibitisha
kwamba wanyama hawa huwa wanakwenda Kenya kutalii tu na kurejea tena nchini mwao
Tanzania.
Kuweka
mambo sawa ni kwamba, wanyama hawa wanapokwenda kwenye Hifadhi ya Maasai Mara,
huwa wanakwenda kwenye 'fungate' kwa muda usiozidi miezi miwili na kisha
kurejea kwao Tanzania kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Maelezo
haya yanathibitishwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, William
Mwakilema, ambaye anasisitiza kwamba kauli zinazotolewa na wenzao wa Kenya
kwamba wanyama hao wanapatikana nchini mwao na ni mali yao ni za upotoshaji
mkubwa kimataifa.
"Achana
na propaganda za Serikali ya Kenya inayojinasibu kwamba eti wanyama aina ya
Nyumbu ni wa kwao kwa sababu wanapatikana kwenye Hifadhi ya Masai Mara. Huu ni
uzushi mkubwa na unapotosha," anaeleza Mwakilema.
Mwakilema
anasema, Nyumbu hao wanaosafiri kwa makundi makubwa kila mwaka ni 'raia' halali
wa Tanzania kwa kuzaliwa na kwa nasaba.
Mhifadhi
huyo anabainisha kwamba, wanyama hao, ambao ndiyo alama na nembo ya Serengeti,
huzaliana kwenye hifadhi hiyo na kwamba wanatumia muda mrefu zaidi wakiwa
Tanzania kuliko wanavyokuwa Kenya.
"Hivi
tunavyozungumza ni kwamba wanyama hawa wamerejea Serengeti tangu mwezi Septemba
mahsusi kwa ajili ya kuzaliana. Wanapatikana nchini Tanzania kwa kipindi kirefu
cha mwaka kuanzia Septemba hadi mwanzoni mwa Julai ambapo huelekea Maasai Mara
kwa kipindi kifupi tu," anafafanua Mwakilema.
Aidha,
Mwakilema anasema, Nyumbu huelekea Maasai Mara kwa ajili ya kutafuta chakula tu
kwa muda mfupi na kurejea, kwani wanayafahamu vyema makazi yao ya asili.
Uhamaji wa Nyumbu
Hakuna
mahali popote duniani ambako kuna uhamaji wa Nyumbu kama wa Serengeti kuelekea
Maasai Mara ambao umekuwa miongoni mwa Maajabu Saba ya Dunia na hakika ndio
umeifanya Serengeti kushika nafasi ya kwanza katika Maajabu Saba ya Asili ya
Afrika mwezi Machi 2013.
Zaidi ya
nyumbu milioni 2 huhama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania
kuelekea Hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya kutafuta malisho kati ya kipindi
cha Julai na Oktoba.
Wanapohama
ni lazima wakatize kwenye Mto Mara ambako hukumbana na mamba ingawa wengi
hunusurika.
Mwakilema
anasema, wanyama hao wanapatikana katika Mfumo-asili wa Serengeti (The
Serengeti Ecosystem), unaochukua eneo la kilometa za mraba 40,000 huku wengi wa
nyumbu hao wakiwa wale wenye manyoya meupe (Connochaetes tuarinus mearnsi)
ambao wanapatikana pia katika sehemu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa
upande wa kusini; Hifadhi ya Serengeti na Maswa Game Reserve pamoja na Hifadhi
za Jamii zinazopakana.
Mwanzo wa
safari hizi za uhamaji ni kuzaliwa kwao, kama anavyosema Jonathan Scott,
mwandishi na mpigapicha wa Afrika Mashariki, ambaye ametumia miaka 30
akizunguka Serengeti na Maasai Mara. Na mwisho wao pekee ni kifo, bila kujali
wamefia Tanzania au Kenya.
Nyumbu
wanazaa kati ya Januari na Machi katika uwanda mpana wa Serengeti ambapo
kipindi hicho huwa kunakuwa na chakula na maji ya kutosha. Ikitokea hali ikawa
ni ngumu, nyumbu anaweza 'kuahirisha kuzaa' mpaka chakula na maji vipatikane.
Kwanini
wanazalia Tanzania? Mbali ya kuwa Serengeti ndiyo makazi yao ya asili, lakini
wanyama hao, na wengine wengi, hupenda kuzalia huko kwa kuwa ardhi ina madini
ya kutosha ya fosforasi ambayo ni virutubisho muhimu kwa majani, hivyo
kuwafanya ndama wanaozaliwa kupata nguvu muda mfupi baada ya kula majani hayo.
Mwakilema
anasema, katika kipindi cha uzazi, Nyumbu wanaweza kuzaa ndama 8,000 kila siku,
hivyo kuonyesha ni kwa nini hifadhi hiyo inao wanyama hao wengi zaidi.
Kutokana
na tabia yao ya uhamaji, nyumbu huwa hawana uhusiano wa kudumu. Majira ya
nyumbu kupandana ni wakati nyumbu madume wanapotengeneza himaya na kuwavutia
majike.
Himaya
hizi ndogo huwa zinaanzia meta za mraba 3,000, ambapo ndani ya kilometa moja ya
mraba kunaweza kuwepo himaya 300. Madume yanalinda himaya zao zisiingiliwe na
wengine na kuwaita majike.
Kwa
kawaida nyumbu huzaa mwishoni mwa kipindi cha masika, na ikitokea muda wa kuzaa
umefika huku mvua zikiendelea kunyesha, basi wanaweza kuahirisha kwa muda mpaka
mvua ziishe.
"Mimba
hutungwa kati ya mwezi Mei na Julai, kwa hivyo utaona kabisa kwamba hata wakati
wanapokwenda Maasai Mara huwa tayari majike wana mimba. Sasa unawezaje kusema
kwamba hawa ni nyumbu wa Kenya?" anahoji Mwakilema na kuongeza kwamba
wanyama hao wanabeba mimba kwa muda wa miezi nane na tisa.
Uainishaji wa kisayansi
Nyumbu
wanatokea katika Himaya ya Wanyama (Animalia); Faila (Phylum) ya Chordata na
Faila ndogo ya Vertebrata (Wanyama wenye ugwe wa uti wa mgongo); Ngeli ya
Mammalia; Oda ya Artiodactyla; Familia ya Bodivae na Familia ndogo ya
Alcelaphinae; Jenasi ya Connochaetes Lichtenstein, 1812.
Spishi
zake ni kama nyumbu weusi (Connochaetes gnou) wanaopatikana Afrika Mashariki,
hasa Tanzania na nyumbu wa bluu (Connochaetes taurinus) wanaopatikana Afrika
Kusini.
Connochaetes
ni neno la Kigiriki, yaani konnos, ambalo maana yake ni 'ndevu', na khaite ni
'nywele zinazoning'inia'.
Nyumbu
mkubwa kabisa ana urefu wa meta 1.27–1.47 (futi 4.17–4.82) kuanzia begani na
anakuwa na uzito wa kati ya kilogramu 120–270.
Uongo wa Wakenya
Taarifa
mbalimbali zinadaiwa kusambazwa na Wakenya kwamba nyumbu walioko Serengeti
wanatokea Kenya, propaganda ambazo zinalenga kuwahadaa watalii ili waone kwamba
hawana haja ya kuja Serengeti, eneo ambalo Januari 2013 limetangazwa na UNESCO
kuwa la Urithi wa Dunia.
Kama
walivyowahi kudanganya watalii kwamba Mlima Kilimanjaro uko Kenya, lakini
wakashindwa kuwapandisha kileleni kwa kuwa mlima huo hauko kwao, sasa wameanza
propaganda nyingine ya kutaka kuwadanganya walimwengu kuhusu nyumbu wa
Serengeti.
"Napenda
kuwaambia walimwengu kwamba, huu ni uongo, nyumbu hawa kwao Tanzania na siyo
Kenya. Watalii waachane na propaganda hizi, waje Serengeti wataona makundi
makubwa ya wanyama hawa," anasisitiza Mwakilema.
Huko nyuma
Wakenya pia walikuwa wakiwahadaa watu kwamba madini ya Tanzanite, ambayo
ulimwenguni kote yanapatikana Tanzania tu, kwamba yanatoka Kenya.
Hii ni
baada ya kuwa wananunua madini hayo na kwenda kuyapaki Kenya kabla ya
kuyasafirisha Ulaya, kama walivyokuwa wanafanya kwa kahawa inayolimwa Arusha na
Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment