Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 15 December 2013

NYAYO ZA CHIFU MKWAWA (13)


Mchoro wa Chifu Mkwawa

Na Daniel Mbega

Uhusiano baina ya Merere na na wamisionari ulikuwa mzuri. Mmisionari mkuu, Merensky, aliwaona Wahehe kama wakorofi na wakatili, lakini akamuona Merere kama ‘dikteta na dhalimu’ ambaye alikuwa katili kwa watu wake na kuwatumikisha kama watumwa. Lakini wamisionari wengi wa Berlin waliamini kwamba Merere angekuwa mshirika mzuri, Mtawala imara wa Kiafrika ambaye asingekuwa na subira ya kuanzisha vita na Wahehe.
Inaelezwa kwamba, Merere mwenyewe alimwandikia ujumbe Soden kumweleza kwamba alikuwa na hamu ya kuungana nao ili kuuvunja utawala wa Mkwawa, lakini ikiwa tu Wajerumani wataharakisha kumuomba msaada. Kwa ujumla, Wajerumani walinufaika na ushirika wao na Merere na mwanawe, ambao walimpatia msaada hadi Vita ya Wajerumani na Wahehe ilipomalizika, lakini ushirikiano huo wa Wasangu na Wajerumani ulikuwa zaidi ni mpango wa Merere na siyo wa Wajerumani. Merere alitambua kwamba Wamisionari wa Berlin walikuwa ni mawakala tu wa gavana wa Dar es Salaam, akifahamu fika kwamba wamisionari wa Moravian na Scotland waliokuwa jirani walimtazama yeye kama mtu mbaya zaidi kuliko Mkwawa.
Merere Towelamahamba na mwanawe, Merere Mugandilwa (Merere IV), wote waliwashawishi Wajerumani kuimarisha ushirika wao na kuanzisha vita dhidi ya Wahehe. Ushirika huo haukuzaa matunda hadi Tom von Prince alipokuwa kwenye msafara usio maarufu wa Kupinga Biashara ya Utumwa wa Wissmann mwaka 1893 na 1894.
Lakini Wajerumani walikwenda mbali zaidi, kwani waliamua, kwa kushirikiana na Wasangu, kuwapiga Wanyiha waliokuwa wakiongozwa na Kimaraunga na kuelekea Rukwa pamoja na Tabora, ambako walianzisha mapambano na Mtemi Isike wa Unyamwezi. Isike akaamua kuanzisha ushirika na Mkwawa ili wasaidiane kuwapiga Wajerumani.
Ilikuwa ni katika kipindi hiki ambapo ujumbe wa Mkwawa uliwasili kwa Isike, uliotumwa na utawala wa Wahehe kukamilisha mkataba wao wa urafiki na Wanyamwezi kwa nia ya kuwadhibiti Wajerumani waliokuwa wakiendelea kutanua himaya yao. Isike akawapatia wawakilishi wa Mkwawa dada yake, Ilagila, ili amuoe kama ishara kwamba amekubali ushirika huo ambao ungeweza kuwa hatari zaidi kwa Wajerumani kutokana na uimara wa jeshi la Mkwawa na warugaruga wa Isike, ambaye pia alikuwa amekubaliana na Wajerumani ili kuvuta muda kusubiri ushirika wake na Mkwawa uzae matunda. Hata hivyo, von Prince aliamua kuivamia ngome ya Isike mnamo Januari 10, 1893 akiwa na askari wa kawaida 66, wanamgambo 80 aliowachukua Tabora, Wangoni kadhaa aliowachukua Urambo na kikosi kikubwa ya askari wa Nyaso kutoka Rukwa kilichokuwa na bunduki 200 ambazo von Prince aliziteka kutoka kwenye msafara mmoja.
Wajerumani wakampiga Isike na kumuua, hivyo kufuta ndoto za kuwepo kwa umoja baina ya Wanyamwezi na Wahehe. Kwa hiyo, Wajerumani tayari wakawa wamejiimarisha kaskazini-magharibi mwa Himaya ya Uhehe na kuizunguka himaya hiyo maarufu, kwani tayari kwa upande wa mashariki walikuwa wamejiimarisha mpaka Kilombero hadi Mahenge.

 Tutaendelea...

No comments:

Post a Comment