Dk. Willibrod Slaa
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibroad Slaa amehitimisha ziara yake ya siku 22 ya kuimarisha na kukagua uhai wa chama katika majimbo 19 mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Singida, akiitaka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukomesha manyanyaso na ukatili wanaofanyiwa wananchi.
Amesema
kuwa baada ya kuzungumza na wananchi hususan maeneo ya vijijini ambako
alijikita kwa siku hizo 22, ameendelea kuthibitisha kuwa sehemu kubwa ya
kero zinazowakabili Watanzania, hazihitaji gharama yoyote kuzimaliza
ili wananchi waishi kwa amani katika nchi yao, akitolea mfano wa kero ya
manyanyaso mbalimbali, hususan kutoka kwa vyombo vya dola.
Amesisitiza
kuwa kama Serikali ya Rais Kikwete inataka kupata uhalali mbele ya
Watanzania na iwapo Rais mwenyewe anataka kumaliza muda wake na kuacha
kumbukumbu kwa wananchi, inatakiwa kukomesha mara moja manyanyaso
wanayofanyiwa wananchi, kwani kufanya hivyo ni wajibu wa serikali na
hakuna gharama yoyote.
Akitolea
mifano ya matukio ya kikatili na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu
unaofanywa vyombo vya serikali kupitia matukio mbalimbali zikiwemo
operesheni mbili za hivi karibuni, Tokomeza Ujangili na Kimbunga, Katibu
Mkuu amesema kwa namna ambavyo serikali iliyoko madarakani inawatenda
raia wake, Tanzania inavunja rekodi hata ya Afrika Kusini ya enzi za
Makaburu.
“Tunamtaka
Rais Kikwete kuacha kufanya kama afanyavyo baba asiyejali au baba wa
kambo anayechukia watoto…JK ukitaka ubaki na heshima baada ya kuondoka
madarakani, fanyia kazi orodha ya manyanyaso wanayofanyiwa wananchi.
Tena mengi yanafanywa na polisi, jeshi na wakuu wa wilaya, watendaji wa
vijiji na watendaji wa kata na madiwani.
“Yapo
mengine ya kubambikia kesi watu, kunyang’anywa ardhi, kunyimwa haki kwa
nuguvu tu, kuchangishwa michango haramu inayoambatana na vipigo na
kunyang’anya watu mali zao, huku mapato na matumizi hayasomwi na kero
nyingine kubwa ni migogoro ya ardhi. Kuachia manyanyaso haya dhidi ya
wananchi ni kuonesha udhaifu mkubwa wa kiuongozi. Labda watuambie kuwa
serikali hii ya CCM sasa imeshaamua kuwageuka raia wake.
“Hauhitaji
hata senti moja kuondoa manyanyaso ya serikali kupitia vyombo vya dola
wanayofanyiwa wananchi. Mnapomtesa Mtanzania namna hii…watu wanateswa
sana na kubambikiwa kesi, wanapigiliwa spoke sehemu za siri, wanawekewa
chupa na kubakwa, mnataka aende kuishi wapi.
“Hayo
maendeleo mnayoyazungumza ni kwa ajili ya nani kama wananchi wanapigwa,
kuteswa na kuuwawa bila hatia. Tumefikia mahali serikali inawatenda
raia wake kuliko hata Makaburu walivyomtesa Mzee wetu Hayati Mandela
alipokuwa gerezani.
“Mwalimu
Nyerere alisema ukaburu si rangi. Huu unaofanyika ni ukaburu ambao
wakati ule wa ubaguzi wa rangi tuliimba sana shuleni na majeshini
kupinga ukatili wa makaburu wa Afrika Kusini dhidi ya weusi waliokuwa
wengi. Leo Serikali hii inafanyia raia wake matendo zaidi ya yale.
Tunakwenda wapi. Kikwete chukua hatua.”
“Kila
nilikopita ni vilio vya manyanyaso, kuanzia Kakonko kule Wilaya ya
Buyungu, kote huko Kasulu Vijijini viongozi wangu wote wa serikali nzima
ya kijiji wamebambikwa kesi ya mauaji, wote kabisa. Hapo Nzega
nimeshuhudia kwa macho yangu mateso wanayoyapata wachimbaji wadogo
wadogo, wengine wamepigwa vibaya na askari polisi, tena machimbo yao
yametekwa na viongozi wa wilaya na kuyageuza mali zao na sasa wanachuma
pesa kwa kupiga raia.”
Katibu
Mkuu Dkt. Slaa ambaye alianza ziara yake Desemba 4, mwaka huu kwa
kufanya mkutano wa hadhara na kikao cha ndani Jimbo la Kahama, mkoani
Shinyanga, amehitimisha ziara yake Desemba 23, kwa kuhutubia wananchi wa
Vijiji vya Shelui na Nyengege, Jimbo la Iramba Magharibi.
Amewataka
wanaCHADEMA kuuchukulia mchakato na mjadala wa Katiba Mpya ya
Watanzania kuwa agenda ya muhimu, ya kudumu na lazima katika mikutano
yao yote, ikiwemo ya ndani ya chama, hadhara au ‘vijiweni’, lengo la
msingi liwe kuwataarifu wanachama na wananchi kwa ujumla, tulikotoka,
tulipo na tunakokwenda.
Ametumia
ziara hiyo kuwasisitiza viongozi na wanachama wa CHADEMA nchi nzima
kuhakikisha wanatekeleza maagizo mbalimbali ya vikao ya chama, hususan
kwa sasa wasimamie kikamilifu maelekezo ya Waraka Katibu Mkuu Namba 6 wa
mwaka 2013.
Waraka
huo ambao unahusu mkakati wa kusukuma ujenzi wa misingi/matawi na
uchaguzi wa ndani ya chama 2013/2014, umeelekeza viongozi nchi nzima
namna ya kuendesha programu ya ‘M4C-CHADEMA ni Msingi’ inayoendelea nchi
nzima, ikisimamiwa na kanda 10 za chama ambapo moja ya malengo mahsusi
ni kusimika na kuimarisha chama kwenye vitongoji na mitaa.
“Ni
lazima kila mwanaCHADEMA, wapenzi wa chama hiki, wananchi wenye mapenzi
mema na ukombozi wa pili wa taifa lao, tuungane, tushikamane pamoja
kusukuma jitihada hizi za kusimika chama chenu, ambacho ndiyo tumaini
jipya la Watanzania katika ngazi ya chini kabisa ya uongozi katika nchi
yetu.
“Viongozi
wote wenye mapenzi mema na CHADEMA, kuanzia ngazi ya taifa hadi chini
kabisa lazima wahakikishe CHADEMA ni msingi inakamilika kama
ilivyokusudiwa,” amesisitiza Katibu Mkuu Dkt. Slaa katika ziara hiyo.
Katika kuwakumbusha juu ya waraka huo, Katibu Mkuu Dkt. Slaa amewasisitiza wanachama na viongozi umuhimu wa kuzingatia;
1. Kupata viongozi imara wa chama kuanzia ngazi ya chini kabisa ya msingi
2. Ratiba ya utekelezaji wa mkakati wa CHADEMA ni Msingi.
3. Ratiba
ya uchaguzi wa ndani ya chama ngazi ya jimbo hadi taifa (pamoja na
mabaraza ya chama), baada ya ngazi za chini kumalizika.
4. Kuzingatia taratibu za kikatiba za uchaguzi, kwani uchaguzi wa ‘mezani’ hautakubalika ndani ya CHADEMA.
5. Rushwa na kampeni chafu (katika uchaguzi kwa ngazi yoyote ile) hazitavumiliwa hata kidogo.
6. Maadili ya chama yasimamiwe kwa kila ngazi ya uchaguzi.
7. Ulinzi wa chama/ viongozi na wanachama ngazi zote, ambapo Red Brigade na BAVICHA ndiyo
nguzo ya ulinzi.
Ukombozi wa kweli kwa mwananchi uanzie serikali za mitaa
Katibu
Mkuu amewataka Watanzania kuelewa kuwa ukombozi wa kweli wa mwananchi
utapatikana iwapo watu wataweza kuchagua viongozi imara, makini,
waadilifu na wapenda watu kuanzia ngazi ya kitongoji, mtaa na kijiji na
hatimaye madiwani ambao huunda halmashauri ya wilaya, mji, manispaa au
jiji.
“Ikulu
ya kwanza ya mwananchi ni hapa ulipo, hapa kijijini au mtaani kwako.
Ikulu ya pili ni halmashauri yenu ya wilaya. Hizi ni sehemu muhimu sana
katika kuhakikisha watu wetu wanapata matumaini, haki na hatimaye ustawi
wa maendeleo ndani ya nchi yao. Hakuna maana yoyote kuichagua CHADEMA
iende Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam halafu huku mnaweka watu wabovu.
Itakuwa sawa na kazi bure,”amesisitiza Katibu Mkuu Dkt. Slaa.
Amesema
kuwa hasa wakati huu ambapo Taifa linajiandaa kwenda kufanya uchaguzi
wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, Watanzania wanapaswa kutambua umuhimu
wa halmashauri za serikali za mitaa katika kusukuma maendeleo ya watu
katika maeneo yao wanayoishi.
Amesisitiza
kuwa katika ngazi hiyo ya uongozi, si kazi ngumu kumtambua mtu ambaye
anaweza kuwa kiongozi mwadilifu, makini mwenye uwezo na mpenda watu, kwa
sababu watu wote wanafahamiana kutokana na kuishi pamoja.
Pinda kubanwa chaguzi serikali za mitaa
“Katika
ziara yangu hii ya siku 22, nimebaini kuwa kuna maeneo mengi sana ya
vijiji ama hayana serikali kabisa, sehemu nyingine mwenyekiti hayupo au
wajumbe, lakini Serikali ya CCM kupitia kwa wakurugenzi inaogopa
kuitisha uchaguzi, kisa wanaogopa wakiitisha uchaguzi CHADEMA itashinda.
“Sasa
napenda kutumia mkutano wangu huu wa kuhitimisha ziara hii, kutoa
maagizo kwa viongozi wa chama wilaya na majimbo, kutuandikia taarifa ya
kina Makao Makuu, ikieleza maeneo yote ya serikali za mitaa ambayo yako
wazi na wakurugenzi hawajatangaza au hawataki kutangaza ndani ya muda
unaotakiwa kisheria uchaguzi wa kuziba nafasi kufanyika.
“Tunataka
taarifa za kina ambazo tutazitumia kumbana Mizengo Pinda maana yeye
ndiye anahusika kusimamia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
au TAMISEMI. Hatuwezi kukubali kuona wananchi wanakosa haki yao ya
uwakilishi kwa sababu tu CCM wanaogopa ukiitishwa uchaguzi CHADEMA
tutashinda. Katika hili pia tutakufa na Pinda,” amesema Katibu Mkuu.
Katibu
Mkuu Dkt. Slaa ametembelea jumla ya majimbo 19 ambayo ni; Kahama
(Shinyanga), Kakonko, Muhambwe, Kasulu Vijijini, Kasulu Mjini, Buhigwe,
Kigoma Kaskazini, Kigoma Mjini, Kigoma Kusini; mkoani Kigoma. Mengine
ni;
Kaliua,
Urambo, Tabora Kaskazini, Tabora mjini, Sikonge, Igalula, Bukene,
Nzega, Igunga (Tabora) na Iramba Magharibi mkoani Singida.
Katika
maeneo yote aliyotembelea, Katibu Mkuu Dkt. Slaa amepokea kero na
ushauri wa wanachama na Watanzania kwa ujumla, kuhusu masuala mbalimbali
ya chama na nchi, ya kitaifa na mengine yanayohusu maeneo husika (local
politics), kwa njia kadhaa ikiwemo taarifa za viongozi kuhusu utendaji
wa chama, kupitia maswali na maoni katika mikutano pamoja na kufika
mwenyewe kujionea hali halisi ya baadhi ya masuala aliyoambiwa.
Imetolewa Desemba 23, 2013 na;
Tumaini Makene Ofisa Mwandamizi wa Habari-CHADEMA
Hivi ndivyo ilivyokuwa...
Kahama
No comments:
Post a Comment