Na Daniel Mbega
BAADA ya ushindi wa
Lugalo, Chifu Mkwawa hakutulia, bali aliendelea kuimarisha himaya yake pamoja
na jeshi lake. Lakini pia kipindi hicho Wajerumani nao walikuwa wakipanga
mikakati ya namna ya kuisambaratisha himaya hiyo.
Kitendo cha kupigwa
kwa jeshi lao imara lenye silaha kali, tena na wapiganaji wenye mikuki na
mishale tu, kiliichanganya Berlin kwa sababu hakikuwahi kutokea hapo kabla.
Hivyo Gavana Julius Freiherr von Soden aliyekuwa anaongoza koloni hilo la
Afrika Mashariki alikuwa katika presha kubwa kutoka kwa wakubwa wake kuhusiana
na namna atakavyomshinda Mkwawa.
Gavana huyo alijitahidi kukabiliana na presha ya Wahehe waliokuwa wakkivamia misafara yake hadi miaka miwili baadaye alipoondoka nchini. Wajerumani walikuwa na mbinu ya kuidhoofisha himaya ya Wahehe kwa mazungumzo, siyo kwa vita, kwa sababu walitambua kwamba hiyo ingeweza kuwagharimu tena.
Gavana huyo alijitahidi kukabiliana na presha ya Wahehe waliokuwa wakkivamia misafara yake hadi miaka miwili baadaye alipoondoka nchini. Wajerumani walikuwa na mbinu ya kuidhoofisha himaya ya Wahehe kwa mazungumzo, siyo kwa vita, kwa sababu walitambua kwamba hiyo ingeweza kuwagharimu tena.
Historia inaeleza
kwamba, uamuzi wa Von Soden wa kutotumia jeshi kupambana na Mkwawa ulimfanya
aonekane gavana bomu kati ya magavana wote walioongoza koloni hilo, lakini hiyo
ilitokana na historia yake. Yeye ndiye alikuwa gavana pekee aliyetokea uraiani,
kwani aliyemtangulia von Wissmann na wafuasi wake wa baadaye walikuwa makamanda
wa jeshi.
Katika kipindi
hicho cha Von Soden, Mkwawa naye alifanya majaribio kadhaa ya mazungumzo na
Wajerumani akituma ujumbe wake Dar es Salaam. Mazungumzo hayo yalichukua muda
wa miezi kadhaa kupitia kwa wawakilishi wake, lakini hayakuwa na mafanikio kwa
sababu watawala wa Kijerumani walikuwa na mashaka na msimamo wa Mtawala huyo wa
Wahehe kwamba angeweza kuwabadilikia. Kwa kifupi, hawakumwamini.
Pamoja na Von Soden
kuwa na nia njema ya kufanya mapatano, maofisa wengine wa Kijerumani walikuwa
na mawazo kwamba hakukuwa na haja yoyote ya kufanya mazungumzo na mtawala wa
Kiafrika ambaye alikuwa ameidhalilisha Ujerumani kama alivyofanya Mkwawa.
Luteni Tom von
Prince (baadaye Kapteni baada ya kuiangusha Kalenga) aliwahi kusema: “Tangu
kuangushwa kwa kikosi cha Zelewski, hasa nikiwa askari wa jeshi lile la zamani,
haja yangu kubwa ilikuwa kulipa kisasi kwa kudhalilishwa kwa jeshi letu, na
tangu hapo nikaweka mkakati, sikuhitaji kuingia kwenye vita yoyote, sikufanya
chochote ambacho kingeweza kuingilia kati mpango huu.”
Wajerumani wakati
huo walikuwa na mashaka kwamba watawala wa Kiafrika, hususan Mkwawa walikuwa
wameanza kuonyesha upinzani wa wazi, hasa Mtemi Isike wa Tabora na Mbunga wa
Ungoni ambao himaya zao zilipakana na Uhehe. Chifu mmoja wa Usagara aliwahi
kutamka wazi, “Watu hawa (Wahehe) ndio pekee walioweza kuoga mchanga wa damu ya
Mzungu ambao ‘bomba zao za moto’ ziliwafanya wengi washindwe kujitetea. Na
kweli, vijiji vingi vilivyokuwa jirani na boma la Wajerumani viliendelea kutoa
msaada kwa Mkwawa na Himaya yote ya Uhehe mpaka pale Kalenga ilipoangushwa.
Sababu za Mkwawa
kutochukua uamuzi wa kuwafukuzia Wajerumani baada ya vita vya Lugalo zinatajwa
kuwa nyingi, ingawa kubwa zaidi, kwa mujibu wa waandishi wa zamani wa historia
Erick Mann, Alison Redmayne, na wengineo, ilikuwa ni kupoteza askari wake
wengi. Vikosi vya Mkwawa havikuwahi kuvamia eneo lililokuwa likikaliwa na
Wajerumani. Katika vita vya Lugalo, Mkwawa alipompoteza makamu kiongozi wa
Kalenga, Ngosi Ngosi Mwamugumba.
Pia inaonekana
kwamba, Mkwawa alitegemea mazungumzo ya amani dhidi ya Isike wa Wanyamwezi,
Chifu Songea wa Wangoni, na Mbunga wa Wandebele na wengineo yangeweza kuweka
umoja na kuwapiga Wazungu. Kwa maana nyingine, Mkwawa ndiye mtu pekee
aliyeanzisha umoja ambao leo hii tunajivunia na kama machifu wenzake
wangetambua azma hiyo, pengine Wajerumani wangeweza kuondolewa kwa nguvu hata
kabla ya jaribio la Vita vya Maji Maji vya mwaka 1905 hadi 1907. Kama mpango wa
Mkwawa ungefanikiwa, Wajerumani wangepigwa kuanzia Tabora hadi Songea, ambapo
ungeligawa koloni hilo katikati.
Mbali ya mkakati
huo mkubwa, Wahehe walilazimika kupambana na Wajerumani ambao walikuwa
amejitanua kutoka kaskazini hadi mashariki: kasi ya kuongezeka kwa Avadaliki
(kama Wajerumani walivyokuwa wakiitwa na Wahehe) ilimaanisha kwamba Wahehe
wangeweza kuzuiwa kwenye msafara wa wafanyabiashara kutoka Bagamoyo hadi
Tabora. Ili kudumisha fursa ya uchumi, na hatimaye heshima ya utawala, Wahehe
wakaendelea kuvamia misafara hiyo. Miongo kadhaa nyuma, juhudi zao za kuvamia
misafara hiyo zilikuwa zimelenga kuteka watumwa, fedha, silaha, na kudumisha
hadhi yao. Kwa ujumla, himaya hiyo kubwa ilikuwa imefanya uvamizi wa misafara kama
ndiyo njia yao kuu ya uchumi ambayo watawala wa kigeni walikuwa wakkiitegemea.
Taarifa zinasema
kwamba, Mkwawa pia alikuwa na hofu ya uasi ndani ya jeshi lake. Wakati ambapo
Vita vya Lugalo vilikuwa vimewafanya Wakinga, Wasagara, Wabena na makabila
mengine kuwa ‘watwana’ na kwamba Wahehe ndio waliokuwa na sauti zaidi, lakini
kwa kuangalia hali ya baadaye, kuendelea kuwepo kwa kambi za Wajerumani katika
maeneo ambayo awali yalitambuliwa kwamba ya Wahehe yaliwapa fursa makabila hayo
kuasi, japo siyo moja kwa moja, huku wakimwita Mkwawa ‘chinja chinja’.
Wajerumani sasa
walionekana wema kuliko Mkwawa, na Wasagara pamoja na makabila mengine ambayo
yalikuwa yakinyanyaswa na Wahehe waliona kwamba Wazungu hao ndiyo kimbilio lao
na wangeweza kuwatetea.
Tutaendelea..
No comments:
Post a Comment