Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday, 18 December 2013

USHAFIKA KIKONGOMA? NDIPO MAHALI ALIPOZAMA MAMA YAKE MKWAWA

Ndugu zangu,
Wakati nikifanya upekenyuzi wangu wa kufuatilia Nyayo za Chifu Mkwawa, hatimaye nilifika hapa Kikongoma, takriban kilometa 12 kutoka Kalenga. Wenyeji wanapaita 'Daraja la Mungu' kutokana na ukweli kwamba, Mto Ruaha unapita chini katika kina cha zaidi ya futi 12 ukiwa umefunikwa na miamba mikubwa ya mawe kwa umbali wa takriban kilometa moja hivi.
Unaweza kukatisha juu kwenda upande wa pili kwa mguu bila shida yoyote. Hapa kuna sehemu ya miamba ambako kuna upenyo mwembamba, lakini unaoweza kupitisha mtu mzima na akazama.
Ni katika eneo hili ambapo inaelezwa kwamba mama yake Chifu Mkwawa, Sengimba, aliamua kujitumbukiza.
Simulizi ziko za aina mbili - Ya kwanza inaeleza kwamba Sengimba alijitumbukiza hapo baada ya kukamatwa na akina Mwambambe Mwalunyungu na Mpangile, mdogo wake Mkwawa (ikiwa unafuatilia simulizi zangu za 'Nyayo za Chifu Mkwawa' kwenye blog hii utakuwa umemwelewa). Wakati huo Mama Mkwawa na Chifu Mkwawa walikuwa wameelezwa na wazee kwamba wakimbilie Dodoma ili kumficha chifu asiuawe na Mwambambe.
Lakini kutokana na mama huyo kutokuwa na mbio, ilibidi ashindwe kukimbia, lakini akamtaka Mkwawa aendelee kukimbia akipitia Pawaga. Alipokamatwa na akina Mwambambe wakata awaelekeze 'dawa ya vita' iliyokuwa inatumiwa na Chifu Munyigumba, ndipo akawataka wamfuate mpaka hapo, ambapo alizunguka nyuma ya miamba kwa maelezo kwamba anakwenda kuwaletea. Kumbe akajitumbukiza.
Simulizi ya pili ambayo nilielezwa na Mwamuyinga ni kwamba, mama huyo alijiua baada ya kukamatwa na Wajerumani, ambao walitaka akawaonyeshe alipo mwanawe Mkwawa hasa baada ya ngome ya Lipuli kuangushwa. Kwamba aliwaambia wamfuate mpaka hapo ndipo alipo mwanawe na kuwataka wasubiri hasa baada ya kuvua nguo zake zote na kuziweka juu ya jiwe, halafu akazunguka upande wa pili na kutumbukia.
Kwa kuwa bado naendelea kufanya utafiti, ninawaomba wadau, mwenye kuuelewa ukweli kati ya simulizi hizo mbili tafadhali asisite kunieleza hata kwa barua-pepe.
Lakini kimsingi Mama Sengimba ndiye mtu wa kwanza katika kabila la Wahehe kujiua, siyo Chifu Mkwawa! Huu ni ujasiri mkubwa sana - yaani No Retreat No Surrender!

Pamoja nami, niliwachukua wanafunzi takriban 13 wa vyuo mbalimbali nchini wanaosomea Utalii na Historia, ambao niliwakuta pale Kalenga. Hapa hakuna usafiri wowote wa kuwapeleka katika maeneo mengine ya kujifunza historia, wanategemea tafiti zao wazifanyie hapo tu kwenye makumbusho ya Kalenga.
Kwa kuwa nilikuwa na nafasi ya kutosha kwenye gari (Pick-Up Double Cabin) na nilikuwa katika harakati za utafiti wangu, nikajitolea kuwachukua ambapo kwanza tulikwenda moja kwa moja mpaka Mlambalasi yapata kilometa 80 kutoka Iringa, mahali alipokuwa amejificha Chifu Mkwawa na ndipo alipojiulia. Kiwiliwili chake kimezikwa pale pamoja na mabaki ya mlinzi wake.
Tulipotoka huko ndipo tukachepuka kwenda Kikongoma. Eneo hili ni maarufu sana, kwani inaelezwa kwamba nyakati nyingine Wahehe, wakiongozwa na familia ya Chifu Mkwawa, huenda kutambika hapo.
Miamba iliyoufunika Mto Ruaha.

Mwaweza wasiliana nami kwa simu +255-715 070109 au barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com

No comments:

Post a Comment