Ujumbe mzuri sana huu. Hapa ni njiapanda ya kwenda mjini Mugumu, makao makuu wa wilaya ya Serengeti. Ni katika kijiji cha Robanda kilichoko mwanzoni kabisa baada ya kumaliza Hifadhi ya Serengeti, ukiachilia mbali pale Fort Ikoma.
Nakumbuka zaidi ya miaka 15 iliyopita nilipita katika Kijiji cha Robanda nikiwa safarini kwenda Mwanza. Sikupita Mugumu, nilipitia upande wa kushoto wa kibao hiki katika maeneo ya Ikizu, Ushashi hadi nikatokea Bunda.
Wakati huo, tulipofika kijijini hapa njaa ilikuwa inauma sana. Fikiria mwendo mrefu wa kutoka Karatu kupitia Ngorongoro hadi Hifadhi ya Serengeti ambako hakuna hata kioski njiani, achilia mbali hata banda la mama ntilie.
Bahati nzuri hapa kijiji tuliwakuta mama ntilie ambao walikubali kutuandalia chakula maalum. Napenda sana kuzungumza na vijana wenzangu kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo, hivyo kati ya vijana watatu waliokuwa wanapata mlo hapo akatokea mmoja na kutamka bayana kwamba mimi ndiye ninayefaa kumuoa dada yake, Nyambura eti kwa sababu nilionekana nafahamu mambo mengi na kwamba walau dada yake angeweza kubadilika kuliko akiolewa na mtu wa kijijini kwao.
Anyway, mwanzoni nilidhani utani, ndiyo maana nikamkubalia kwamba nitafurahi akiwa shemeji yangu. Kumbe jamaa hakuwa anatania bwana, aliondoka hapo haraka wakati sisi tukisubiri 'special order' ya mama ntilie.
Dakika kumi baadaye yule kijana akarejea akiwa ameongozana na binti mmoja, ambaye nadhani alikuwa amemaliza shule ya msingi mwaka uliotangulia. "Huyu hapa, si unamuona?" akaniuliza akinionyeshea binti huyo ambaye alikuwa amebeba mfuko wa Rambo mkononi mwake. "Akikaa hapa ataolewa na hawa vijana ambao mawazo yao hayatofautiani na yangu. Kinyume chake baba atamuoza kwa wazee wenzake matajiri wa ng'ombe ambako atakuwa mke wa tatu au wa nne. Sasa wewe mchukue, si mna gari? Nenda naye, najua nitakavyomweleza baba..."
Nikiendelea kudhani ni utani, nikamwambia kwamba hakuna shida nitaondoka naye. Nilijua ni masikhara hivyo nikapata chakula pamoja na wenzangu na baada ya hapo tukaanza kuelekea kwenye gari. Yule binti bwana naye si akainuka na mfuko wake wa Rambo! "Sasa mbona unaniacha?" akauliza kwa lafudhi ya Kikurya. "Nakuacha kwenda wapi?" nikamuuliza kwa mshangao, maana yale mazungumzo nilijua ni utani kama utani mwingine.
"Sasa wewe jamaa, si tumeongea ndiyo maana nikaenda nyumbani kumwita dada muondoke naye?" yule kijana akaingilia kati.
Mshangao ukazidi, sikujua niende kwenye gari au nibaki nizungumze na hawa watu. Miguu ikafanya ganzi.
No comments:
Post a Comment