Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 13 December 2013

MBEGA MNYAMA ALIPOKUTANA NA MBEGA


 Mbega wakiruka mti hadi mti. Ni nadra sana kuwakuta wako ardhini hawa jamaa, halafu wana aibu sana.


Ndugu zangu,
Jumanne nilikuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha (zamani ikijulikana kama Ngurdoto au 'Engutoto' na baadaye Momela).
Alama ya hifadhi hii ni mnyama aitwaye Mbega - wale weusi na weupe - au kwa Kiingereza anaitwa Black and White Colobus (Colobus guereza). Ni wanyama wazuri ambao wameadimika kutokana na kuwindwa na majangili wanaotaka ngozi yao.
Umekwishawahi kusikia usemi kwamba 'Mbega aliponzwa na uzuri wake?'. Basi uzuri wa wanyama hao ni wa pekee. Manyoya yao yanapendeza mno, halafu zile nyusi zao za asili hakika hata mwanamke ajipambe na atinde nyusi kiasi gani katu hawezi kuwafikia. Habari ndiyo hiyo.
Ni hifadhi chache sana pamoja na misitu ambamo Mbega wanapatikana. Lakini ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha ndimo wanamopatikana kwa wingi mno.
Naam, jamaa zangu hupenda kuniita 'Mnyama' kwa sababu ya jina langu la Mbega. Hata tulipokuwa tunaelekea huko, jamaa zangu walikuwa wananitania: "Leo Mnyama unakwenda kukutana na ndugu zako!" Nami nikawaambia, hakuna shida.
Na kweli, wakati tukiwa tumetoka katika eneo linalojulikana kama 'Serengeti Ndogo', mwendo mfupi baada ya kutoka Geti Kuu la Ngongongare (neno linalotokana na neno la Kimasai la Engong Engare, yaani Eneo lenye maji), nikasikia dada mmoja akisema: "Mnyama, ndugu zako wale!"
Gari zima wakashangilia, nami nikafurahi pia kwa sababu nilikuwa natamani sana niwaone wanyama hao adimu na adhimu. Nikawapiga picha.

Kwa taarifa yako tu
Mbega weupe-na-weusi ni ndegere wa kale wanaotokea katika jenasi ya Colobus, wakiwa wanapatikana zaidi barani Afrika. Wana uhusiano wa karibu na mbega wekundu wanaotokea kwenye jenasi ya Piliocolobus. Mbega ni jamii ya wanyama wasiokula nyama (herbivorous), chakula chao kikuu ni majani, matunda, maua na kadhalika. Yaani hawa jamaa ni ma-vegetarian hasa.
Wanyama hawa wanaishi katika makundi ya wanyama 9, kutegemeana na dume mmoja katika kundi la majike wengi na watoto.
Mbega ni mhimu kwa usambazaji wa mbegu kutokana na tabia yao ya ulaji na mfumo wa mmeng'enyo. Ni asusa kwa wanyama wengi walao nyama (carnivorous), na wako hatarini kutokana na wawindaji wanaotaka nyamapori, lakini pia ukataji wa misitu ni hatari kwao kwa sababu unaondoa makazi yao.
Kuna aina tano ya spishi za kima hawa, huku kukiwa na spishi ndogo nane ambazo ni: Black colobus (C. satanas), Gabon black colobus (C. s. anthracinus), Bioko black colobus (C. s. satanas), Angola colobus (C. angolensis), Sclater’s Angola colobus (C. a. angolensis), Powell-Cotton’s Angola colobus (C. a. cottoni), Adolf Friedrichs’s Angola colobus au Ruwenzori black-and-white colobus (C. a. ruwenzorii), Cordier’s Angola colobus (C. a. cordieri), Prigogine's Angola colobus (C. a. prigoginei), Peters's Angola colobus au Tanzanian black-and-white colobus (C. a. palliatus), King colobus (C. polykomos), Ursine colobus (C. vellerosus) na Mantled guereza au Abyssinian black-and-white colobus (C. guereza(.
Wanatokea katika Himaya ya Animalia, Faila ya Chordata, Daraja ya Mammalia, Oda ya Primates, Familia ya Cercopithecidae na Familia ndogo ya Colobinae.

Ndugu yenu,
Daniel Mbega.

No comments:

Post a Comment