Chumba kimoja madarasa mawili.
Hakuna kupiga kelele, si wanajifunza?
Mchaka mchaka...chinja. Idi Amin akifa, mimi siwezi kulia, nitamtupa Kagera, awe chakula cha mamba.
ELIMU YA
KUJITEGEMEA
1. Tumeizika elimu, elimu
ya kizamani,
Elimu ile haramu, maana ya kikoloni,
Imetuishia hamu, kuiga ya ugenini,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
2. Yafaa kwa wote umma,
elimu yetu ya sasa,
Imeondoa dhuluma, ubaguzi na mikasa,
Wenye baba na yatima, wote ni sawa kabisa,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
3. Imeondoa ubwana, elimu
ya Tanzania,
Watu kuitwa watwana, aibu gani kisia,
Tuko sawa wote wana, si Zuberi si Rukia,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
4. Yatayarisha vijana,
taifa kutumikia,
Na bila kubaguana, umoja twazingatia,
Na mtu mwenye hiana, mbali tutamtupia,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
5. Inaendeleza mila,
zilizodharauliwa,
Na ngoma za makabila, hazikusahauliwa,
Nyimbo za kila mahala, siku hizi twaimbiwa,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
6. Zimeanzishwa sanaa,
shule na vyuoni pia,
Vijana wengi kadhaa, jembe wameshikilia,
Na vijana mashujaa, sasa wajitegemea,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
7. Chako ni chako jamani,
usikionee haya,
Sina nia kulaani, elimu toka Ulaya,
Bali natoa maoni, na tena bila ubaya,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
8. Wakoloni walifika, huku
na dharau zao,
Kudharau Afrika, kutukuza nchi yao,
Sasa wanaaibika, hawana tena kikao,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
9. Uhuru tulipopata, mambo
haya tuliona,
Na wala hatukusita, kuiondoa laana,
Ya zamani tukafuta, tukaweka ya maana,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
10.
Elimu
yatuletea, maisha yenye kufaa,
Elimu yakazania, kuukuza Ujamaa,
Pia kujitegemea, bila kukata tamaa,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
11. Elimu yetu ya leo,
inafaa vijijini,
Yawafaa wenye vyeo, yawafaa maskini,
Yaleta maendeleo, kupendana na amani,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
12.Elimu ya kizamani,
iliwajaza makupe,
Wakatunyonya jamani, tukabakia weupe,
Sasa tusiithamini, mashimoni tuitupe,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
13.Elimu ya kizamani,
ilijaa ubaguzi,
Rangi waliithamini, wakadharau ujuzi,
Sasa hayo hatuoni, tumetoa uchafuzi,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
14.Twamshukuru Mwalimu, Baba
wa Taifa letu,
Katupatia fahamu, za kukuza nchi yetu,
Sasa tumejaa hamu, ya kukuza mila zetu,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
15. Siku hizi tunaweza,
kushiriki uamuzi,
Ngoma zetu tunacheza, tukisha kufanya kazi,
Kila zana twatengeza, na kujifunza ulinzi,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
16.Hapa mwisho wa shairi,
mbele sitaendelea,
Yote nimeyakariri, nanyi mmeyasikia,
Na bila shaka twakiri, yajengeka Tanzania,
Elimu yetu ya sasa, yawafaa wananchi.
No comments:
Post a Comment