Waziri Mkuu Mizengo Pinda
HOTUBA YA WAZIRI MKUU MIZENGO P. PINDA, WAKATI WA
KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 14 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA 21, DESEMBA 2013
I:
UTANGULIZI
a)
Masuala
ya Jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu
mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo. Tumekuwepo hapa
Dodoma kwa takriban siku 15 za kazi ambapo tumeweza kutekeleza majukumu na kazi
za Mkutano wa 14 wa Bunge lako Tukufu ambapo tunahitimisha shughuli zilizopangwa
hivi leo.
Mheshimiwa Spika,
2. Nitumie nafasi hii ya mwanzo kabisa
kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Asha Rose Migiro, (Mb.) kwa kuteuliwa na
Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu. Wengi wetu tunafahamu
uwezo mkubwa wa Dkt. Asha Rose Migiro na bila shaka ndiyo sababu Mheshimiwa
Rais alifanya uamuzi wa kumteua kuwa Mbunge kwa kuzingatia sifa nzuri
alizonazo. Pamoja na kumpongeza napenda kumtakia kazi njema ndani na nje ya
Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika,
3. Tangu Mkutano wa 13 wa Bunge baadhi ya
Waheshimiwa Wabunge wamepotelewa na Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia
fursa hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Lakini katika Mkutano
huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili Azimio la Bunge kuhusu
kuungana na Nchi ya Afrika Kusini, katika kuombeleza kifo cha Muasisi, Mpinga
ubaguzi wa rangi, Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Madiba
Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba 2013. Wote tunakubaliana kwamba huu ni
msiba Mkubwa kwa Dunia nzima na hasa kwa wale wanaomfahamu Mzee Mandela na
historia yake.
4. Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kutuwakilisha vyema Watanzania wote katika msiba huu mkubwa wa Afrika na Dunia nzima.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa mazishi ya Hayati Nelson Mandela
tarehe 15 Desemba, 2013 pale Qunu ilitosha kabisa kuitangaza Tanzania Dunia
nzima katika ushiriki wake kwenye harakati za ukombozi Barani Afrika katika
Karne ya 20. Ninaamini kwamba hiyo ni Historia ambayo haitafutika vizazi vingi
vijavyo. Tutaendelea kumuenzi Mzee Mandela kwa kuiga na kufuata nyayo zake.
b) Maswali Mheshimiwa Spika,
5. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge waliweza kuuliza maswali ya msingi 170 na ya nyongeza 458 ambayo yote
yalijibiwa na Serikali. Aidha, maswali 17 ya msingi na 15 ya nyongeza
yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza maswali mazuri na Waheshimiwa
Mawaziri kutoa majibu ya maswali hayo kwa umahiri mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
6.
Pamoja
na shughuli hizo za kawaida, Bunge lako lilikamilisha kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Bunge lilijadili na kukamilisha Muswada wa
Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013. [The Referendum Bill, 2013];
Pili:
|
Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za
Bunge za Sekta
|
Mtambuka.
|
|
Tatu:
|
Kujadili Taarifa Mbili (2) za Kamati za Kudumu za
Bunge
|
zinazosimamia Fedha za Umma; na
|
|
Nne:
|
Kujadili Taarifa Tisa (9) za Kamati za Bunge za
Kisekta.
|
7. Aidha, Bunge lako Tukufu lilijadili
kwa utaratibu wa Hati ya Dharura Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya
Ushuru wa Bidhaa wa Mwaka 2013 [The Excise (Management and Tariff) (Amendment)
Bill, 2013]. Mwisho Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa
mwaka 2013 ulisomwa kwa mara ya kwanza.
8. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kujadili Taarifa hizo na kutoa maoni na ushauri kwa uwazi
mkubwa na kwa kina.
Mapendekezo na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa
Wabunge umepokelewa na Serikali na utazingatiwa kwa uzito unaostahili.
II:
KILIMO
a) Hali ya chakula Nchini Mheshimiwa Spika,
9. Kama
nilivyoeleza katika Mkutano wa Bunge wa 13, hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini
kwa ujumla imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia mavuno
mazuri ya msimu wa Kilimo wa 2012/2013 katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.
Tathmini ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2013 katika
maeneo yenye matatizo ya usalama wa chakula na lishe inaonesha kuwa jumla ya
Watu 828,063 wanakabiliwa na upungufu wa chakula na watahitaji msaada wa
chakula wa Tani 23,312 hadi ifikapo mwezi Februari 2014. Aidha, kati ya mwezi
Julai na Novemba 2013, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulitenga
jumla ya Tani 16,119 za chakula cha mgao kwa Halmashauri zenye mahitaji ya
chakula cha msaada. Hadi kufikia tarehe 16 Disemba 2013, jumla ya Tani 13,716
zilikwishachukuliwa na Halmashauri husika. Tani 2,402 zilikuwa hazijachukuliwa
na Halmashauri za Mwanga, Babati, Igunga, Mpwapwa na Manyoni.
10. Ninawaagiza
Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ambazo hazijachukua chakula hicho kufanya
hivyo kabla ya tarehe 15 Januari 2014. Ambao hawatatekeleza
maagizo haya watachukuliwa hatua za kisheria. Nitumie nafasi hii kuwahakikishia
Wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa chakula katika
Halmashauri zenye hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu
wenye uhaba wa chakula.
b) Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
11. Kutokana na miezi hii kuwa katika
kipindi cha mwisho wa msimu wa ununuzi wa mazao, kiasi cha mazao yanayoingia
sokoni kimeanza kupungua. Hali hii imesababisha bei za wastani za vyakula hasa
mahindi na mchele katika soko hapa Nchini kuanza kupanda ingawaje si kwa kiasi
kikubwa. Kwa mfano, bei ya mahindi Kitaifa imepanda kutoka Shilingi 536.86 kwa
kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi kufikia Shilingi 538.26 kwa kilo mwezi Novemba,
2013. Kwa upande wa Mchele, bei ya wastani wa Kitaifa imepanda kutoka Shilingi
1,188.60 kwa kilo mwezi Oktoba, 2013 hadi Shilingi 1,191.10 kwa kilo mwezi
Novemba, 2013.
12. Pamoja na kuwepo kwa hali ya kupanda
kwa bei, bado bei za sasa kwa baadhi ya mazao mfano mahindi, mchele, maharage
na viazi ziko chini ikilinganishwa na zile za kipindi kama hiki mwaka jana.
Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa yenye mavuno mazuri kuendelea kuwahamasisha
wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao na kuuza ziada
katika Soko ili kusaidia kupunguza bei ya vyakula katika miji yetu. Halmashauri
zihakikishe kuwa zinathibiti ununuzi holela wa chakula kutoka mashambani na
majumbani mwa Wakulima kwa lengo la kujihakikishia upatikanaji wa chakula cha
kutosha.
c) Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa Spika,
13. Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula ilipanga kununua Tani 250,000 za nafaka. Wakala umeendelea
na kazi hiyo na hadi kufikia tarehe 11 Desemba, 2013, Wakala ulikuwa
umekwishanunua kiasi cha Tani 218,499 za nafaka sawa na Asilimia 87.4 ya kiasi
kilichopangwa kununuliwa. Aidha, hadi kufikia tarehe 16 Desemba, 2013, Maghala
ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na akiba ya jumla ya Tani
233,808 za nafaka. Kati ya hizo, Tani 233,315 ni za Mahindi na Tani 493 ni za
Mtama.
14. Wakati huo huo, Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula unaendelea kuhamisha chakula kutoka katika maghala yake
yaliyoko katika Mikoa iliyozalisha ziada kwenda kwenye maghala yaliyoko kwenye
Mikoa yenye upungufu wa chakula ili kukabiliana na mahitaji ya chakula cha
msaada kitakachohitajika kusambazwa kwa walengwa. Hadi kufikia tarehe 9
Desemba, 2013, jumla ya Tani 44,129 za Mahindi zimekwishahamishwa. Serikali
inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara kununua chakula katika Mikoa yenye ziada
ya chakula na kukipeleka katika Mikoa yenye upungufu wa chakula.
Mheshimiwa Spika,
15. Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa
13 wa Bunge, Serikali ilichapisha jumla ya vocha 2,796,300, kwa ajili ya
pembejeo za Kilimo kwa msimu wa Kilimo wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 12
Desemba, 2013, Tani 74,925 sawa na Asilimia 96 za mbolea ya kupandia na Tani
42,295 sawa na Asilimia 91 ya mbolea ya kukuzia zilikuwa zimekwishafikishwa
katika Mikoa husika kulingana na aina ya mazao yanayohitaji mbolea hizo. Aidha,
Maghala ya Wakala wa Mbolea Jijini Dar es Salaam yana akiba ya kutosha ya
mbolea hiyo. Nirejee kutoa wito kwa Wakuu wote wa Mikoa kuhakikisha kuwa vocha
zote zinatolewa kwa walengwa kwa wakati sambamba na aina ya pembejeo
inayomlenga Mkulima husika kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.
e) Malipo ya Madeni ya Wakulima ya Mahindi.
Mheshimiwa Spika,
16. Katika mwaka wa 2013/2014, Serikali
ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni 109.6 kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) kwa ajili ya kununua Tani 250,000 za nafaka. Hadi kufikia tarehe 19
Desemba, 2013 NFRA ilikuwa imenunua jumla ya Tani 218,499 zenye thamani ya
Shilingi Bilioni 109.25 na kwa ajili hiyo. Kutokana na Serikali kutoa bei nzuri
ya wastani wa Shilingi 500/= kwa kilo ya mahindi, zoezi hilo lilikuwa na
matokeo mazuri katika msimu huu kulinganisha na miaka iliyopita na liliwavuta
Wananchi wengi kupeleka nafaka katika Vituo vya kununulia nafaka. Hadi sasa
Serikali imeshatoa Shilingi Bilioni 100.6 kwa ajili ya zoezi hilo na
imehakikisha kuwa wananchi wote waliouza nafaka zao kwa NFRA wamelipwa fedha
zao. Aidha, natambua kuwa NFRA ilitumia baadhi ya Wakala kukusanya nafaka hiyo
kutoka kwa Wakulima na kama nilivyosema katika Mkutano wa 13 wa Bunge, Serikali
inatambua kuwa Wakala hao kutoka Mikoa ya Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga,
Ruvuma, Rukwa na Tanga wanaidai Serikali jumla ya Shilingi Bilioni 8.65
Niwaombe Wakala wote wanaoidai Serikali kuendelea kuwa na subira wakati
Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa deni hilo kwa vile kiasi cha deni
lao lipo ndani ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ununuzi wa nafaka katika mwaka
wa fedha wa 2013/2014.
III:
MPANGO
WA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA
Mheshimiwa Spika,
17. Tarehe 12 Desemba, 2013 Serikali ilizindua
Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha (yaani National Financial
Inclusion Framework). Uzinduzi wa Mpango huu ulifanywa na Malkia wa
Uholanzi Mheshimiwa Máxima Zorreguieta
Cerruti
ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika
Mpango wa Huduma Jumuishi za Kifedha na kushuhudiwa na Makamu wa Rais,
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Wawakilishi wa Taasisi za Umoja wa
Mataifa.
Mheshimiwa Spika,
18. Lengo la Mpango huo ni kusimamia
ukuzaji wa huduma za kifedha kwa jamii Nchini na kutafuta ufumbuzi wa
changamoto zinazoikabili Sekta ya Fedha. Vilevile, Mpango unalenga kusogeza
huduma karibu kwa jamii pana zaidi ya Watanzania kwa kutumia mifumo ya
Teknolojia mbalimbali katika kufikisha huduma za kifedha kwa Wananchi na hasa
Wakulima, Wafugaji na Wavuvi waliopo Vijijini ambao wengi wao wako nje ya mfumo
rasmi wa kifedha. Teknolojia hizo ni pamoja na:
(a)
Huduma
za Kibenki za moja kwa moja na kupitia Wakala (Agent Banking);
(b)
Huduma
za kifedha kupitia Mitandao mbalimbali kama vile M-PESA, TIGO PESA, AIRTEL
MONEY na Easy PESA.
(c)
Vituo
vya malipo kwa kutumia Wakala (Point of Sales – POS).
19. Aidha,
Mpango huu utaweka mazingira linganifu na yaliyo bora kwa kutumia Sayansi na
Teknolojia kutekeleza Sera ya Fedha kwa ufanisi, kuimarisha Sekta ya
Fedha katika Pato la Taifa na Kukuza Uchumi kwa
ujumla. Mpango huu pia utawezesha kuongeza kasi ya upatikanaji wa Chakula,
masuala ya Lishe na Maendeleo Vijijini kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
20. Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia
katika Nchi mbalimbali Barani Afrika unaonesha kuwa Watu wanaonufaika na Mfumo
rasmi wa Taasisi za Kifedha ni Asilimia 24 tu. Kwa upande wa Tanzania, Wananchi
waliopo kwenye Mfumo rasmi wa Asasi za Kifedha ikijumuisha wale waliojiunga na
Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOs) ni Asilimia 22. Asilimia 78 ya
Watanzania wapo nje ya Mfumo wa Kifedha na wengi wao ni kutoka Vijijini hasa
Wakulima wadogo. Mpango huu wa Huduma Jumuishi za Kifedha unalenga kufikia
Asilimia 50 ya Watu wazima wanaotumia huduma rasmi za kifedha ifikapo mwaka
2016.
Mheshimiwa Spika,
21.
Kiwango
hiki kidogo cha Wananchi walio katika Mfumo rasmi wa huduma za kifedha
unatokana na changamoto zifuatazo:
Moja: Miundombinu ya kuanzisha huduma za Kifedha
Vijijini ni hafifu hususan barabara, mawasiliano, makazi na huduma za
kiusalama;
Mbili:
Wananchi
wengi wa Vijijini bado hawajahamasishwa kutambua umuhimu na faida ya
huduma za kifedha. Aidha, utamaduni wa kujiwekea akiba na kukopa
ni mdogo; na.
Tatu: Taasisi
nyingi za kifedha zinaogopa kwamba Wananchi wengi wa Vijijini ambao
ni Wakulima hawana fedha za kutosha kuweza kuweka akiba katika
Taasisi hizo na uwezo wao wa kukopa mikopo ni mdogo, hivyo wakipeleka
huduma zao huko hawatapata faida.
Mheshimiwa Spika,
22. Zipo faida nyingi za kueneza Huduma Jumuishi za
Kifedha kwa Wananchi wengi wa Vijijini hasa Wakulima. Miongoni mwa faida hizo
ni pamoja na:
Moja:
|
Kuwezesha Wananchi kujiwekea Akiba na pia kupata
mikopo ya
|
kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo na
shughuli nyingine za kijamii hivyo kujiongezea kipato na kuondoa umaskini;
|
|
Mbili:
|
Huduma za Kifedha Vijijini zinawawezesha Wananchi
wengi hasa
|
Wakulima kupata mikopo ya pembejeo na mikopo ya
ununuzi wa
|
|
mazao;
|
|
Tatu:
|
Huduma za Kifedha Vijijini ni Mkombozi wa Makundi
maalum kama vile Vijana, Wanawake, Wazee, na Walemavu. Aidha, zinasaidia
Wananchi kujiongezea kipato, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya Kilimo
na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki; na
|
Nne:
|
Kuwepo kwa Huduma za Kifedha Vijijini kunaongeza
Usalama wa Chakula, kulinda mazingira na kufanya Vijiji kuwa ni sehemu nzuri
ya kuishi.
|
Mheshimiwa Spika,
23. Serikali imeonesha juhudi kubwa
katika kuanzisha Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini kwa mfano tumeweza kuanzisha
Benki nyingi Nchini. Tayari tunazo Benki takriban 52 zenye matawi zaidi ya 609
kote Nchini. Lakini pia tunazo huduma za Bima kwa Makampuni Binafsi zaidi ya 27
na Mawakala wa Bima takriban 600. Ipo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Umma 5,
Masoko ya Mitaji na Vikundi na Taasisi ndogondogo za Fedha (SACCOS) takriban
5,600.
24. Aidha tunazo huduma za Kifedha kwa
kutumia Huduma za Kifedha kupitia mtandao (PESA – MTANDAO) na Vituo vya malipo
kwa kutumia Wakala (POINTS OF SALES – POS). Inakadiriwa kuna Mawakala na Vituo
zaidi ya 55,000 ambapo Waajiriwa wa moja kwa Moja (Direct Employment)
wanakadiriwa kufika takriban 100,000.
25. Maisha bora kwa kila Mtanzania ni
pamoja na kutumia Teknolojia na kurahisisha maisha. Kwa mfano, huduma za M-PESA
peke yake zinawezesha malipo kwenye biashara mbalimbali zaidi ya aina 300
ikiwemo manunuzi kwenye Supermarket na maduka ya kawaida. Huduma hizo ambazo
zinatolewa pia kwa njia ya TIGOPESA, AIRTEL MONEY, EASY PESA zinaweza kulipia
Luku, Ada za shule na Vyuo, Tiketi za ndege, kufanya marejesho Bodi ya Mikopo
ya Elimu ya Juu, n.k. Aidha, baadhi ya Makampuni haya yameunganisha huduma zao
na Benki zaidi ya 20 ikiwemo CRDB, NMB, Benki ya Posta, Standard Chartered,
Amana Bank na Diamond Trust Bank (DTB). Vilevile, kwa kutumia huduma za
jumuishi za kifedha mteja anaweza kuhamisha fedha kutoka Akaunti ya Benki
kwenda M- PESA, TIGO PESA n.k. halafu akazitoa kupitia Wakala. Kwa sasa
Watumishi walio Vijijini hawana tena sababu ya kufunga Ofisi kufuata mishahara
Benki bali kupitia huduma hizi za Kifedha na
wanaweza kutoa pesa kupitia Wakala, na kwa kufanya hivyo ufanisi na tija kwa
Watumishi unaongezaka.
Mheshimiwa Spika,
26. Ni kweli kwamba tunayo kazi kubwa ya
kutekeleza Dhana ya Huduma Jumuishi za Kifedha Nchini. Lakini ni ukweli kuwa
Uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha una manufaa makubwa
na mengi ikiwemo kuongeza kasi ya Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini kwa
kupeleka maendeleo Vijijini, kuongeza Akiba ya Chakula na pia kufikia malengo
ya Milenia. Ni matumaini yangu kwamba uzinduzi wa Mpango huu utatuwezesha
kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi. Natoa wito kwa Mabenki, Taasisi za Kifedha
na Vituo vya Kifedha kupitia mitandao (PESA MTANDAO) na Vituo vya malipo kwa
kutumia Wakala kuongeza jitihada katika kusambaza huduma za Kifedha Vijijini
ambako ndiko kwenye kundi kubwa la Wananchi wanaohitaji huduma hiyo.
IV: NISHATI
NA MADINI
a) Mradi
wa Gesi
Mheshimiwa Spika,
27. Kama ambavyo Wananchi wengi
wanafahamu, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa mitambo ya kusafishia Gesi Asilia
katika maeneo ya Madimba, Mtwara Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa. Pia ujenzi
wa Bomba la kusafirishia Gesi hiyo kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es
Salaam unaendelea vizuri. Mradi huu utakapokamilika utaunganisha maeneo
yanayozalisha Gesi Asilia hususan Mnazi Bay-Mtwara, Songo Songo, Kisiwani,
Mkuranga, Ntorya na maeneo yaliyogunduliwa Gesi katika eneo la bahari ya kina
kirefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Gesi Asilia mbali na matumizi
mengine, inatumika katika kuzalisha umeme ambao kwa sasa Asilimia kubwa
unazalishwa kwa kutumia nishati ya mafuta yanayoingizwa kutoka Nchi za nje na
hivyo kuligharimu Taifa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.
28.
Katika
utekelezaji wa mradi huu, Kazi zifuatazo zimekamilika hadi kufikia tarehe 30
Novemba, 2013:
Moja:
|
Kukamilika kwa upakuaji wa Shehena ya Sita (6) ya
Mabomba ya Mradi yapatayo 4,444 ya umbali wa Kilomita 51.169 katika Bandari
ya Mtwara. Jumla ya mabomba yaliyowasili Nchini hadi Novemba, 2013 ni 24,935
ya umbali wa kilomita 295.5;
|
|
Pili:
|
Kusafisha Mkuza wa Mabomba, tayari Kilomita 498.5
zimekamilika;
|
|
Tatu:
|
Usafirishaji wa mabomba kutoka kwenye yadi za
kuhifadhia na kuyasambaza kwenye Mkuza tayari kwa kuyaunganisha kwa kuchomelea.
Hadi sasa mabomba ya Kilomita 186.9 yamekwishasafirishwa;
|
|
Nne:
|
Uchimbaji wa njia ya kuweka bomba, yenye umbali wa
Kilomita 27.0 umekamilika;
|
|
Tano:
|
Uwekaji wa mabomba kwenye njia yake sambamba na
kuweka Mkongo wa Mawasiliano (Fiber Optic Cable) umekamilika Kilomita
21.1;
|
|
Sita:
|
Kufukia bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano.
Tayari Kilomita 7.30 za Bomba pamoja na Mkongo wa Mawasiliano
zimefukiwa; na
|
|
Saba:
|
Utafiti wa njia ya Bomba la Baharini nao
umekamilika.
|
|
Hayo ni maeneo machache ambayo nimeona niyataje.
Mheshimiwa Spika,
29. Ni kweli kwamba kazi za mradi huu ni
kubwa lakini kwa ujumla zinaendelea vizuri na kwa kasi. Moja ya faida za mwanzo
za mradi huu ambazo tumeziona ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa Wafanyakazi
wa Mradi ambao sehemu kubwa ya ajira ni ushirikishwaji wa wazawa katika Mradi
wa Gesi na Mafuta. Kwa kuwa kazi za ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi ni za
kitaalamu sana, malengo ya Shirika la Petroli Nchini (TPDC) ni kuajiri
wafanyakazi Wakiwemo Wazawa mapema ili waweze kushiriki na kujifunza kwa
vitendo shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mitambo na Bomba la Gesi hatua
kwa hatua, tangu mwanzo hadi mwisho wa ujenzi. Utaratibu huu utasaidia kupata
wataalamu wazuri na wazoefu wa Kitanzania watakaoendesha (operations) na
kufanya matengenezo (Maintenance) ya mitambo na Bomba la Gesi kwa
kipindi chote cha matumizi.
30. Vilevile moja ya makubaliano katika
Mkataba wa utekelezaji wa Mradi huu, Mkandarasi anawajibika kuwapeleka
Wafanyakazi kwenye mitambo na mabomba yanayofanya kazi kwa sasa kwa kipindi
kisichopungua mwezi mmoja ili wajifunze pia kwa vitendo na kwa nadharia shughuli
zote za kuendesha mitambo ya kusafisha Gesi Asilia na Bomba la Gesi. Malengo ya
TPDC ni kuwapeleka wafanyakazi husika kwa awamu tofauti tofauti wakati wa
kipindi cha ujenzi ili ikifika kipindi cha kukabidhi mradi Wafanyakazi wote
wawe wamekwishapata uzoefu wa kutosha.
Mheshimiwa Spika,
31. Kampuni nyingi zilizopo Mtwara
zinazojishughulisha na mambo ya utafiti na uzalishaji wa Gesi na Viwanda
vinavyohusiana na matumizi ya Gesi, zimekuwa zikisomesha na pia kuajiri wazawa.
Kwa mfano, Mpango wa kujenga mitambo ya kutengeneza Gesi kuwa kimiminika (LNG)
wa Kampuni ya British Gas Tanzania utakuwa na utengenezaji wa ajira
nyingi za kiwango kuanzia Kada ya Chini na Kada ya Kati ambayo itasomesha
Watanzania kupitia VETA katika fani mbalimbali. Wako watakaosomeshwa katika
fani ya Vyuma, wengine ujenzi, uhandisi wa miundombinu na ufundi wa vyuma na
umeme.
32. Katika Kada ya Kati, Kampuni ya Gesi
Tanzania wanatarajiwa kusomesha wataalamu 16,756 waliofaulu vizuri masomo ya
Kidato cha Nne. Takwimu zinaonesha kuwa kwa Mtwara tu, kumekuwapo ajira mpya
400, na Watanzania wanaotoa huduma mbalimbali kwenye Kampuni za Gesi na Mafuta
ni sawa na Asilimia 70 ya watoa huduma hiyo Nchini. Asilimia 30 iliyobaki ya
watoa huduma inatolewa na Wageni.
33. Katika Kada za Juu, Kampuni
itasomesha na kuajiri Wataalamu wa Jiolojia, Uhandisi, Kemia na Sayansi husika
kwenye Gesi na Mafuta. Matokeo yameanza kuonekana ambapo jumla ya Wanafunzi wa
VETA 370 wamesomeshwa kuhusu Gesi na Mafuta kwa kiwango cha cheti cha Kimataifa
na Wanafunzi 12 wa Kada za Juu wamepata ufadhili na wanasomea fani za Gesi na
Mafuta ndani na nje ya Nchi.
Mheshimiwa Spika,
34. Napenda kulijulisha Bunge lako
Tukufu kwamba Kampuni ya British Gas Tanzania wamegundua gesi kiasi cha Futi za
Ujazo Trilioni 13. Katika kuandaa na kuendesha mradi wa uzalishaji Gesi nyingi
kiasi hicho ni dhahiri kwamba ajira zitapatikana kwa maelfu ya Watanzania.
Katika hatua ya ujenzi, mradi utatoa ajira kwa maelfu; na katika uzalishaji (operations)
ajira nyingine zaidi kwa maelfu zitapatikana hapa Nchini, na katika mnyororo wa
usambazaji ajira nyingi pia zitajitokeza. Nitumie fursa hii kuwapa Watanzania
matumaini, kwamba Mradi wa Gesi Nchini una manufaa mengi sana, kuanzia
upatikanaji wa Gesi na Ajira kwa Wazawa. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee
kuwaelimisha Wananchi wetu
kuhusu manufaa ya mradi huu katika Nchi yetu. Ni fursa ya kipekee ambayo
Wananchi wetu wanatakiwa wafaidike nayo katika kuwaletea maisha bora.
V:
MATUMIZI
YA MASHINE ZA KIELEKTRONIKI (EFDs)
Mheshimiwa Spika,
35. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014,
Serikali ililiarifu Bunge lako Tukufu kuhusu mikakati mbalimbali
itakayotekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuimarisha
ukusanyaji wa Mapato ya Ndani. Moja ya hatua hizo muhimu ni kuendelea
kuimarisha matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutoa Risiti (Electronic
Fiscal Devices- EFDs). Mashine hizi zimeunganishwa kwa Mtandao wa Kompyuta
moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa lengo la kuwezesha Serikali
kupata mapato stahiki bila udanganyifu. Aidha, Mashine hizi zinasimamiwa
kupitia Mtandao wa Kielektroniki ambapo hupeleka taarifa moja kwa moja kwenye
Hifadhi Kuu ya Kumbukumbu za Mamlaka ya Mapato Tanzania kila siku.
Mheshimiwa Spika,
36. Katika
utekelezaji wa zoezi hili kwa mwaka huu, Serikali imelenga kuingiza Walipa Kodi
200,000 kati ya 1,500,000 ili waweze kutumia Mashine za Kielektroniki. Walengwa
wa utaratibu huu ni Wafanyabiashara wenye biashara kubwa zenye Mtaji wa kati ya
Shilingi Milioni 14 na Shilingi Milioni 40. Katika zoezi hili, Wafanyabiashara
Wadogo wanaoendesha biashara zisizo rasmi kama vile Wamachinga na wale
wanaotembeza bidhaa barabarani na Mama Lishe hawahusiki na utaratibu huu hata
kidogo.
Mheshimiwa Spika,
37. Katika utekelezaji wa zoezi hili
kumejitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wafanyabiashara Nchini hususan wa
Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Lindi na Dar es Salaam (Kariakoo) kuhusiana na bei na
matumizi ya Mashine hizi. Malalamiko makubwa ya Wafanyabiashara hao ni kuhusu:
Bei kubwa ya ununuzi wa Mashine za Kielektroniki; Bei kubwa ya Karatasi za
kutolea Risiti; Mchakato uliotumika kununua Mashine za Kielektroniki; Walengwa
wa kutumia Mashine hizo; na Gharama za matengenezo.
Mheshimiwa Spika,
38. Kwa kuzingatia maendeleo ya Sayansi
na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kisasa (ICT); Wataalam wanathibitisha kwamba,
Mashine za Kielektroniki zinafanya kazi zifuatazo:
Moja: Zinatoa Risiti na Ankara za Kodi kwa urahisi
na Mfanyabiashara huondokana na adha ya kuchapisha au kununua vitabu vingi vya kuandikia
risiti ambavyo utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu;
Pili:
Zina
uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali
ya biashara (stock) bila kufutika kwa muda usiopungua
miaka mitano;
Mtumiaji anaweza kutoa kwa urahisi taarifa za
mauzo yake kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi, kwa mwaka na kwa wakati wowote kwa
kipindi kisichopungua miaka mitano;
|
|
Nne:
|
Humwezesha Mfanyabiashara kutuma taarifa zake za
mauzo moja kwa moja kwenda Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka
nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo, kama vile Taasisi ya Taifa ya
Takwimu, Benki Kuu, EWURA, na SUMATRA;
|
Tano:
|
Mashine zinaweza kupokea maelekezo moja kwa moja
kutoka
|
kwenye Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, na
kumtaarifu
|
|
Mfanyabiashara taarifa yoyote ya Kodi inayomhusu;
|
|
Sita:
|
Kutuma na kupokea fedha kwa njia ya “Mobile
Money”. Utaratibu huu unamwezesha Mtumiaji kutumia Mashine hizi kulipia
kodi na huduma nyingine moja kwa moja kama vile, Ankara za Umeme, Maji, Simu,
n.k;
|
Nane:
|
Mashine za Kielektroniki zinatumia lugha ya
Kiswahili na Kiingereza inayoeleweka kwa Wananchi wengi;
|
Tisa:
|
Mashine za Kielektroniki zinaiwezesha Mamlaka ya
Mapato Tanzania kutambua mauzo sahihi ya Mfanyabishara na hivyo kuweza kutoza
Kodi halali.
|
Mheshimiwa Spika,
39. Msingi wa bei ya kununulia Mashine
hizi za Kielektroniki umezingatia pamoja na mambo mengine, manufaa na faida
nyingi nilizozitaja kwa mtumiaji na ubora wa mashine zenyewe. Aidha, kwa mujibu
wa utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Nchi mbalimbali
Duniani unaonesha kuwa mashine zenye ubora unaokidhi mahitaji niliyoyataja hapo
juu zinauzwa na wasambazaji kwa kati ya Shilingi 600,000/= (Dola 375) hadi
Shilingi 778,377/= (Dola 486) ikilinganishwa na bei za Mashine za Kielektroniki
za Nchi nyingine zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania ambazo zinauzwa
bei kubwa za kati ya Dola za Kimarekani 360 hadi 870. Pamoja na bei hizo,
Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kujadiliana na Wasambazaji wa Mashine
hizo ili kuona uwezekano wa kushusha bei hizo.
Mheshimiwa Spika,
40. Kuhusu bei za karatasi za kutolea
Risiti uchunguzi unaonesha kuwa karatasi hizo zinauzwa kati ya Shilingi 2,200/=
hadi Shilingi 4,500/= kuzingatia ubora na ukubwa mbalimbali wa Risiti hizo.
Karatasi hizo zina uwezo wa kutoa wastani wa risiti kati ya Risiti 200 hadi
1,000 kulingana na urefu wa “Paper Roll”! au Bunda. Bei ya Karatasi hizi
zinazojulikana kama “Thermal Paper” umezingatia kwamba ni za kisasa na
hazifutiki kwa urahisi na zina Alama za Siri ndani yake kwa ajili ya kuongeza
usalama.
41. Kuhusu utaratibu uliotumika kuwapata
Watengenezaji na Wasambazaji wa Mashine hizi za Kielektoniki na Wasambazaji wa
karatasi, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa ulikuwa wa wazi na wa
ushindani wa Kimataifa na haukuwa na dosari yoyote.
Mheshimiwa Spika,
42. Katika kutafuta Watengenezaji na
Wasambazaji, kwenye Awamu ya Kwanza Watengenezaji Wanne (4) na Wasambazaji Sita
(6) walipatikana kwa kutumia Zabuni ya wazi ya Kimataifa (International
Competitive Tendering) kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma
ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005. Kuanzia Mwezi Desemba Mwaka 2009
mpaka Mei 2010 makubaliano yaliingiwa kati ya kila Mtengenezaji na Msambazaji
aliyechaguliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya “Memorandum of
Understanding (MOU).
43. Kwenye Awamu ya Pili ya utekelezaji
wa utaratibu huohuo wa Zabuni ya Watengenezaji ilitangazwa kwenye gazeti la
Daily News, The African, Tovuti ya TRA na Tovuti ya PPRA. Jumla ya Wazabuni
Kumi na Nne (14) walituma maombi ambayo yalifunguliwa mara moja baada ya saa
Nne asubuhi tarehe 27 Septemba 2012. Watengenezaji wa Mashine Wanne (4)
walichaguliwa kati ya Kumi na Nne (14) waliokuwa wameomba na Wasambazaji Watano
(5) walipatikana kati ya Tisa waliotuma maombi yao ndani ya muda. Kwa kifupi,
huo ndio utaratibu uliotumika ambao ulikuwa wa wazi na ushindani.
Mheshimiwa Spika,
44. Ili kuhakikisha ubora wa Mashine
hizi za Kielektroniki, Watengenezaji wametoa “Guarantee” ya muda wa
miaka mitatu kwamba Mashine inayoharibika bila kukusudia na watawajibika kutoa
mashine nyingine na pia kutoa elimu ya matumizi ya mashine hizo. Vilevile, kwa
mujibu wa Mkataba ulioingiwa kati ya Wasambazaji na TRA, Wasambazaji
wanawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo kila zinapoharibika ili
kuondoa usumbufu kwa watumiaji kutafuta watengenezaji wao wenyewe. Napenda
kuwahakikishia Wafanyabiashara na Wananchi wote kwamba, utaratibu wa kutumia
Mashine za Kielektroniki haukuwekwa kwa nia mbaya, bali unalenga kumrahisishia
Mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za kila siku za biashara na kuwawezesha
kulipa kodi stahiki Serikalini.
Mheshimiwa Spika,
45. Kwa kutambua umuhimu
wa mashine hizi katika kuongeza Mapato ya Ndani; na ili kuyashughulikia
malalamiko ya baadhi ya Wafanyabiashara yaliyojitokeza, Serikali imesogeza
mbele muda wa mwisho wa kununua Mashine za Kielektroniki hadi tarehe 31
Desemba, 2013. Lengo ni kuwawezesha Walengwa kupata nafasi zaidi ya kujiandaa
kununua mashine hizi na kujifunza namna ya kuzitumia. Aidha, Serikali kwa
kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Sekta Binafsi inaendelea kutoa elimu
kuhusu matumizi endelevu na faida za Mashine za Kielektroniki kwa Wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa na
huduma. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa ngazi zote
kushirikiana na Serikali kuwaelimisha Wananchi na Wafanyabiashara kuhusu
manufaa ya Mfumo huu wa Mashine za Kielektroniki ili kwa pamoja tushirikiane
kujenga Nchi yetu na kuleta maendeleo endelevu kwa kulipa Kodi stahiki.
VI: USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
46. Tarehe 16 – 25 Oktoba 2013 nilifanya ziara ya
kikazi Nchini China kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China
Mheshimiwa Li Keqiang.
Katika ziara hiyo, nilifuatana na Viongozi wa
Serikali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge,
Viongozi wa Asasi za Sekta Binafsi Tanzania na Watendaji Wakuu wa Serikali na
Mashirika ya Umma ambao walishiriki kwenye mazungumzo na Wabia wetu kwa upande
wa Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa Spika,
47. Dhamira kubwa ya ziara hiyo kimsingi
ilihusu; kukuza mashirikiano ya kibiashara na utalii Nchini, kufanya mazungumzo
na vyombo vya fedha ili kupata mikopo, kuendeleza uhusiano wa Nchi hizi mbili
marafiki, kuona Sekta Binafsi ya Tanzania inavyoweza kushirikiana na wenzetu wa
China na mwisho kutoa shukrani kwa misaada na mikopo ambayo Nchi yetu imepokea
kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa Spika,
48. Kama mnavyojua Taifa la Jamhuri ya
Watu wa China ni miongoni mwa Nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa sana na
limepiga hatua kubwa sana katika maendeleo yake. Kutokana na maendeleo makubwa
yanayotokea katika Taifa la China, nilitoa mwaliko wa kuwakaribisha ili kushirikiana
na Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wake katika Nyanja za kiuchumi,
utamaduni na kisiasa. Yapo maeneo mengi ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na soko
kubwa la bidhaa za China na uwekezaji.
Mheshimiwa Spika,
49. Katika ziara hiyo nilipata fursa ya
kutembelea Miji ya Beijing, Shenzhen, Chengdu na Guangzhou ambapo nilipata
nafasi ya kukutana na Viongozi wa Makampuni mbalimbali ya China. Kutokana na
Mikutano hiyo, baadhi ya Makampuni na Taasisi za Umma wameanza kuja Nchini kwa
ajili ya kuendeleza mazungumzo na Serikali pamoja na Sekta Binafsi ili
kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi.
50. Kwa ujumla ziara hii ilikuwa na
mafanikio makubwa. Kwa mfano, pamoja na kuendeleza na kudumisha ushirikiano
ambao umeanzishwa na Viongozi waasisi wa Nchi hizi mbili yaani Hayati Mwalimu
Julius Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong wa Jamhuri ya Watu wa China,
kwenye ziara hiyo, niliweza kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Bwana Li
Keqiang, pamoja na Viongozi wa Makampuni yapatayo 30 ya China. Ninaamini
tukijipanga vizuri tutaweza kufanya mengi kati ya Tanzania na China.
Mheshimiwa Spika,
51. Ziara yangu pia ilifanikisha kutiwa
saini kwa Mikataba ya ushirikiano wa Tanzania na China katika eneo la Sayansi
na Teknolojia na katika Utalii. Mikataba mingine iliyotiwa saini ni kuhusu
uuzaji wa bidhaa za baharini za Tanzania Nchini China na kuanzisha Ukanda wa
Kisasa wa Viwanda vya Nguo pamoja na kukuza zao la Pamba Nchini. Aidha,
Mikataba ya Maelewano inayohusu Sekta za Nishati, Nyumba na Makazi baina ya
Makampuni ya China na ya Mashirika yetu ya Umma yakiwepo Kampuni ya Umeme –
TANESCO, Shirika la Taifa la Maendeleo – NDC na Shirika la Taifa la Nyumba –
NHC ilisainiwa.
Mheshimiwa Spika,
52. Mafanikio mengine ya ziara hiyo ni
pamoja na kuyashawishi Makampuni makubwa ya usafiri wa anga na Mawakala wa
safari za kitalii kuwekeza Tanzania. Katika jitihada hizo nilikutana na
Makampuni ya China Hainan, China Southern Air Line Holding Company na
China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited.
53. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa kwa
kiasi kikubwa Makampuni haya ya Usafiri wa Anga ya Nchini China yameonesha
utayari wao wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na
China. Aidha, Kampuni ya
China Travel Service (Holdings) Hong Kong Limited ambayo
inafanya biashara ya kusafirisha Watalii katika Nchi mbalimbali duniani
wameonesha nia ya kuja kuwekeza hapa Nchini katika Sekta ya Hoteli kubwa za
Kitalii. Kampuni ya China Merchants Holdings International Limited ambayo
imehusika katika ujenzi wa Bandari kubwa na Mji wa Shenzhen katika Jimbo
la Guangdong, kwa upande wake imekubali kuingia ubia na Serikali yetu katika
ujenzi na kuendeleza Bandari mpya ya Bagamoyo na Mji wa Bagamoyo unaotarajiwa
kuwa “Trade Hub” ya Afrika.
Mheshimiwa Spika,
54. Tanzania imedhamiria kuendeleza
uchumi wake kwa lengo la kufikisha Tanzania kuwa Nchi ya Uchumi wa Kati kabla
au ifikapo mwaka 2025. Viashiria vyote vinaonesha hivyo, na ndio sababu
Makampuni yote niliyozungumza nayo wakati wa ziara hiyo yameonesha shauku kubwa
ya kuja kuwekeza Tanzania katika Sekta mbalimbali na mengine tayari yapo Nchini
kutekeleza miradi mbalimbali. Napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa Serikali
kwa upande wake tutajitahidi
kupokea Uwekezaji huo na hivyo kunufaika na matokeo tunayotarajia. Aidha,
tutaendelea kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na uwekezaji ili kuweza
kuvutia Mitaji na Wawekezaji wengi zaidi pamoja na Watalii kutoka China na
maeneo mengine duniani.
VII: JUMUIYA
YA AFRIKA MASHARIKI
Mheshimiwa Spika,
55. Mtakumbuka tarehe 7 Novemba, 2013
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alihutubia Bunge ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la Jumuiya
ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya hiyo. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Wakuu wa Nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2013 Kampala
Nchini Uganda, Wakuu wa Nchi hizo akiwemo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete walikutana na waliidhinisha na kuweka Saini Itifaki ya Umoja wa
Fedha wa Afrika Mashariki. Aidha, Viongozi hao walizitaka Nchi Wanachama
kukamilisha taratibu za kuridhia Itifaki hiyo ifikapo mwezi Julai, 2014.
Mheshimiwa Spika,
56. Manufaa ya Umoja wa Fedha ni pamoja
na: kupunguza gharama ya kufanya biashara katika Nchi Wanachama; kuwezesha Nchi
Wanachama kuwa na kiwango kidogo na tulivu cha Mfumuko wa Bei; kuwa na viwango
vidogo vya riba ya kukopa; na kuepusha athari za ubadilishaji wa fedha ndani ya
Jumuiya kwa kuwa na Sarafu Moja. Matarajio ni kujenga ukanda tulivu wa kifedha
(Monetary and Financial Stability Zone) utakaorahisisha na
kusaidia ukuaji wa biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Jumuiya.
Mheshimiwa Spika,
57. Katika Mkutano huo wa Kampala Wakuu
wa Nchi pia waliridhia Mfumo wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kuagiza kuwa ifikapo mwezi Januari 2014, Nchi Wanachama
ziwe zimeanza utekelezaji wake na kuukamilisha ifikapo au kabla ya mwezi Juni
2014. Aidha, Wakuu wa Nchi walipokea Taarifa kuhusu maendeleo ya Mpango Kazi wa
kuelekea kuanzisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Walitumia muda wa
Mkutano huo kujadili hali ya usalama iliyopo katika Nchi hizi na waliona kuna
umuhimu wa kuongeza juhudi katika kukabiliana na Ugaidi.
Mheshimiwa Spika,
58. Kwa ujumla Mkutano huo ulikuwa na
mafanikio sana hasa katika kuimarisha Umoja wa Jumuiya. Aidha Wakuu wa Nchi
wote kwa pamoja walitumia muda huo kubadilishana mawazo kuhusu kuhakikisha
kwamba mahusiano yetu kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanadumu na
tunaendelea kuijenga Jumuiya na kuiimarisha kwa nguvu zetu zote.
Mheshimiwa Spika,
59. Wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 12
wa Bunge, nilieleza kuhusu Programu ya Kuboresha Miji Nchini (Urban Local
Government Strengthening Programme-ULGSP) ya miaka mitano (5)
kuanzia mwaka 2013 hadi 2018. Huu ni mwendelezo wa Programu ya
Uendelezaji na Uboreshaji Miji Nchini (Tanzania Strategic Cities
Programme -TSCP); ambao kwa sasa unakaribia kumalizika utekelezaji
wake. Programu hii ya ULGSP kwa sasa inahusisha Manispaa 11 na Miji 7. Manispaa
hizo ni Tabora, Morogoro, Shinyanga, Lindi, Sumbawanga, Musoma, Songea,
Singida, Iringa, Bukoba na Moshi. Miji mingine inayohusika ni Kibaha, Geita,
Babati, Korogwe, Mpanda, Njombe na Bariadi. Halmashauri hizi zinazojumuisha
Manispaa na Miji 18 ziko tayari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, ambavyo
ni pamoja na:
i.
Kuongeza
Bajeti ya mapato kila mwaka;
ii.
Kutokuwa
na Hati Chafu za Hesabu za Halmashauri,
iii.
Kuunda
Kamati za kushughulikia matatizo yanayotokana na Programu kwenye ngazi ya
Halmashauri, ngazi ya Kata na Mitaa;
iv.
Kuhakikisha
Programu hiyo imetangazwa na kueleweka na wakazi wa Halmashauri za Manispaa na
Miji;
v.
Kuhakikisha
kuna Wakuu wa Idara wa kutosha;
vi.
Kuhakikisha
Sheria za Manunuzi zinafuatwa;
vii.
Kuhakikisha
Watu watakaohamishwa na Programu na kulipwa fidia hawazidi nyumba 20;
viii.
Kuhakikisha
miradi iliyotekelezwa inalingana na thamani ya fedha
iliyotumika;
ix.
Kutekeleza
miradi ya miundombinu iliyoko kwenye menu;
x.
Kupeleka
taarifa za kila robo mwaka za miradi kwa muda unaotakiwa;
xi.
Kuhakikisha
kuna Master Plan ya Mji;
xii.
Kuhakikisha
ukusanyaji wa kodi ya majengo unaongezeka kati ya Asilimia 5 hadi 30; na
xiii.
Kuhakikisha
taarifa za Mkaguzi wa Ndani zinaenda kwenye vikao vya Halmashauri kila robo
mwaka.
Ukikosa hapa fedha hizo hazipatikani.
Mheshimiwa Spika,
60.
Nimetaja baadhi ya Vigezo kwani viko zaidi ya 200 na vinagusa kila Sekta ya
Halmashauri. Upimaji wa vigezo vyote vitafanyika mara 2 kwa mwaka; na
Halmashauri zitakazoshindwa kufikia Alama (Marks) 60 na kuendelea,
watapunguziwa fedha za miradi yao. Hivyo, Mikoa na Mabaraza ya Madiwani lazima
yahakikishe kuwa vigezo vyote vinasimamiwa na kutekelezwa kikamilifu. Aidha,
TAMISEMI wawachukulie hatua za kisheria wale wote watakaozembea katika kutimiza
vigezo hivi na kuathiri maendeleo ya Wananchi.
Mheshimiwa Spika,
61. Programu hii ambayo ni ya kwanza
Afrika itatumia Dola za Kimarekani 255, fedha ambazo zilikuwa zitolewe mwezi Julai
mwaka huu, lakini kutokana na matatizo ya ubadhirifu yaliyojitokeza kwa
Wasimamiaji wa fedha zilichelewa kutolewa. Hata hivyo, baada ya kuwapeleka
wahusika wa ubadhirifu kwenye Vyombo vya Sheria, Wafadhili waliridhika na hatua
zilizochukuliwa, hivyo tarehe 27 Novemba, 2013 Wafadhili walitoa fedha za Awamu
ya Kwanza, ambazo zilitumwa kwenye Halmashauri hizo 18. Miradi iliyopo kwenye
Programu ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa barabara na mifereji ya mvua,
uwekaji taa barabarani, ujenzi wa Stendi za Mabasi, upimaji viwanja,
utengenezaji wa madampo, kuweka miundombinu ya majitaka na uboreshaji wa
makazi. Hii ni baadhi ya Miradi ya Miji iliyoibuliwa na Halmashauri zenyewe
kufuatana na matatizo ya Miji hiyo. Hivyo, ninawaomba TAMISEMI – wasimamie
Programu hii vizuri ili Miradi husika iweze kutatua matatizo ya Wananchi katika
maeneo yao na kuhakikisha Mapato ya Halmashauri yanaongezeka. Lengo ni
kuwezesha Halmashauri hizo kujitegemea baada ya Miradi hiyo kukamilika.
XI: USIMAMIZI NA UDHIBITI WA FEDHA KATIKA MAMLAKA ZA
SERIKALI ZA MITAA
Mheshimiwa Spika,
62. Kama ambavyo itakumbukwa, wakati wa majadiliano
ya Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu
zilizokaguliwa za Serikali za Mitaa, kwa mwaka 2011/2012, Waheshimiwa Wabunge
walionesha masikitiko yao kwa vitendo vya ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na
baadhi ya Halmashauri Nchini.
Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia
mjadala huo walidai kuwa Serikali imekuwa haichukui hatua dhidi ya Watumishi
wanaofanya makosa katika Halmashauri. Napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge
kwamba pamoja na matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha za Umma, Serikali
imejitahidi kuimarisha usimamizi na utendaji katika eneo hili. Jitihada hizi
zimedhihirishwa na Matokeo ya Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ambayo yanaonesha kuongezeka kwa ubora wa Hati za Ukaguzi zinazotolewa
kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa hususan kuanzia mwaka 2000 hadi sasa. Kwa mfano,
mwaka 2000/2001 Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifanywa na Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali unaonesha kuwa Halmashauri zilizopata Hati safi zilikuwa 16 sawa na
Asilimia 14 ya Halmashauri zote. Aidha, Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati
zenye Shaka zilikuwa 23, sawa na Asilimia 20 na Halmashauri zilizopata Hati
Chafu zilikuwa 75 sawa na Asilimia 65 ya Halmashauri zote.
Mwaka 2005/2006 Idadi ya Halmashauri zilizopata Hati
Safi iliongezeka hadi kufikia 53, sawa na Asilimia 43 na Halmashauri zilizopata
Hati zenye Shaka zilikuwa 67, sawa na Asilimia 54 na Halmashauri zenye Hati
Chafu zilikuwa Nne (4), sawa na Asilimia Tatu (3).
Mwaka 2011/2012 taarifa za Ukaguzi ziliimarika zaidi
ambapo Halmashauri zilizopata Hati Safi ziliongezeka maradufu hadi kufikia 104,
sawa na Asilimia 78 na zilizopata Hati zenye Shaka zilikuwa 29, sawa na
Asilimia 21 na hakukuwa na Halmashauri iliyopata Hati Chafu.
Mheshimiwa Spika,
63. Jitihada hizi ni kubwa. Hivyo,
Serikali itaendelea kuimarisha Usimamizi na Udhibiti na Mapato na Matumizi ya
Serikali katika Sekta zote na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuongeza ufanisi
na tija katika utendaji na kudhibiti ubadhirifu wa fedha na mali za Umma. Lengo
ni kuongeza kasi ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu na Kukuza Uchumi
kwa haraka.
Mheshimiwa Spika,
64. Pamoja na jitihada hizo za Serikali
zinazoonekana, napenda kuwahakikishia kwamba Watumishi waliohusika na
ubadhirifu wa mali na fedha za Umma wamechukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo
kusimamishwa kazi, kushushwa vyeo, na kufikishwa mahakamani. Aidha, kesi za
Watumishi hao ziko katika Mahakamani na katika Vyombo vya nidhamu vya
Halmashauri na Tume ya Utumishi wa Umma kulingana na makosa yao kuhakikisha
kwamba tunajenga nidhamu. Kutokana na hatua hizo kati ya mwaka 2011/2012 hadi
Septemba, 2013 jumla ya Wakurugenzi 52, Wakuu wa Idara 65 na Watumishi wengine
749 wamechukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kwa ubadhirifu wa fedha katika
Halmashauri mbalimbali Nchini. Hatua hizo za kinidhamu ni kama ifuatavyo:
i)
Waliofukuzwa
kazi ni 232,
ii)
Waliosimamishwa
kazi ni 186,
iii)
Waliovuliwa
Madaraka ni 33,
iv)
Waliopunguziwa
Mshahara ni 1,
v)
Walioshushwa
Cheo ni 32,
vi)
Walipewa
ONYO ni 113,
vii)
Waliofikishwa
Mahakamani ni 233,
viii) Waliofikishwa
Polisi na TAKUKURU ni 36.
Serikali itaendelea kusimamie eneo hili kuhakikisha
fedha za Umma zinatumika vizuri.
Mheshimiwa Spika,
65.
Pamoja na hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa Watumishi hao mmoja mmoja,
Serikali imeendelea kuchukua hatua nyingine mbalimbali kukabiliana na tatizo la
ubadhirifu wa mali za Umma katika Halmashauri. Juhudi hizo ni pamoja na
kuongeza uwezo kwa kuajiri Wahasibu wa kutosha katika Halmashauri zetu;
kuanzisha Kamati za Mapato na Matumizi katika ngazi zote za Halmashauri na
kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Kamati za Mapato na Matumizi za Halmashauri
zote. Mbinu nyingine zinazotumika ni kufanya Ukaguzi Maalum kubaini ufisadi na
ubadhirifu wowote uliojitokeza. Kwa mfano, Katika mwaka wa fedha 2011/12
kumefanyika Kaguzi maalumu kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kumi na nne
(14), ambazo ni Kilindi, Kiteto, Muheza, Ruangwa, Musoma, Kilwa, Temeke,
Singida, Arusha, Mvomero, Morogoro, Dodoma, Mbarali na Bunda. Kaguzi hizo
zimesaidia sana katika kujenga nidhamu ya Watumishi katika Halmashauri hizo.
Mheshimiwa Spika,
66. Serikali pia imeweza kubadili na
kuweka Mfumo wa ‘Lawson’ katika kila Halmashauri ili kumaliza tatizo la
Mishahara kwa Watumishi waliofariki, walioacha kazi, wastaafu, n.k. Vilevile
kuna Mfumo wa Epicor 9.05 ambao zinasaidia kudhibiti Bajeti za Mapato na
Matumizi katika Halmashauri Nchini. Mafunzo kuhusu matumizi ya Mifumo hii mipya
yanaendelea kutolewa ili kuweza kutumia mifumo hii kwa ufanisi. Vilevile, Wakuu
wa Mikoa walikwishaagizwa kuhudhuria Vikao vya Baraza za Halmashauri; katika
kujadili Hoja za Ukaguzi ili Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
aweze kufuta zile zilizojibiwa kikamilifu. Hoja ambazo hazikupata majibu
kikamilifu, Sheria zifuatwe na wenye kuhusika na ubadhirifu wowote wachukuliwe
hatua zinazostahili. Aidha, Maafisa Masuuli (Wakurugenzi) wanaohusika na Hoja
mbalimbali za Ukaguzi wanapaswa kuitwa kwenye Halmashauri walizotoka ili kujibu
hoja zinazowahusu bila kujali wamehamishiwa wapi.
XI: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
67. Tumekuwa na muda mzuri wa kujadili
masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Nchi yetu hapa Bungeni kwa kipindi chetu
tulichokuwa katika Mkutano huu. Napenda niwashukuru wote waliosaidia
kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na
Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi
nzuri ya kuongoza Vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena
Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu
wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi
zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma
mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa
kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi
mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa kazi
nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote
walioshiriki katika Mkutano huu.
68. Niwashukuru Wabunge wote kwa
kujadili vizuri hoja za zilizojitokeza hapa Bungeni. Lakini kipekee niwashukuru
Waheshimiwa Mawaziri Wanne waliokubali kubeba jukumu ka kuwajibika kwa yote
yaliyotokea. Tunawashukuru kwa uzalendo wao kwa Nchi yetu na tunawatakia kila
la kheri katika maisha yao. Mheshimiwa Spika,
69. Tunahitimisha shughuli za Bunge hili
tukiwa tumebakiza siku chache kabla ya kufika Mwisho wa Mwaka huu 2013.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema atujalie katika siku hizi
chache tuweze kusherehekea Sikukuu njema ya Krismas na tuvuke salama mwisho wa
mwaka na kuingia Mwaka Mpya 2014 kwa Amani na Furaha!
Mheshimiwa Spika,
70. Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge
wote tunavyofahamu, tutakuwa na Bunge la Katiba litakalofanyika mapema mwakani
na kwa tarehe itakavyopangwa. Kutokana na utaratibu huo ni dhahiri kwamba wengi
wetu tutakutana wakati wa Bunge la Katiba. Nitumie fursa hii kuwatakia safari
njema mnaporejea kwenye maeneo yenu na wengi wenu niwatakie mapumziko mema ya
Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya hadi tutakapokutana wakati wa Bunge la Katiba.
Mheshimiwa Spika,
71. Baada ya kusema hayo, naomba sasa
Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi litakapokutana kwa Mkutano maalum wa Kumi na
Tano wa Bunge la Bajeti tarehe 06 Mei, 2014 saa 3:00 Asubuhi katika Ukumbi huu
hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
72.
Naomba
kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment