Kigong'ota madoa-meupe mkubwa.
Kigong'ota mkia-dhahabu.
Kigong'ota paji-jekundu.
Na Daniel Mbega (Mhifadhi Asilia)
UKO kwenye mbuga ya wanyama –
haijalishi kama ni Serengeti, Ngorongoro, Mikumi, Manyara au Selous - mazingira
yote yametulia ukifurahia mandhari ya asili na upepo mwanana uliosheheni harufu
nzuri.
Waweza kuwa peke yako, wawili au
hata wengi, lakini pengine lengo lenu ni kuyasawiri mazingira hayo
tuliyojaaliwa na Muumba wetu ambayo hatuyalipii hata ushuru ili yaendelee
kushamiri zaidi ya kuhitaji matunzo ya asili kwa kuacha kuchoma moto misitu,
kuwinda ovyo bila vibali (ujangili) na kadhalika.
Basi, katika pitapita yako,
ukiamini kwamba hakuna mtu mwingine ndani ya msitu huo isipokuwa ninyi pekee,
ghafla unasikia sauti ndani ya msitu, katika miti mikubwa, kama mtu anatoboa
miti kwa tindo.
Unashtuka na kustaajabu. Kama una
silaha utaikamata barabara na kuanza kunyata kuelekea kule ulikoisikia sauti
hiyo. Unaweza kuhisi ni jangili anayewinda wanyama ama anakata miti.
Sauti hii inasikika na kukoma, kama
vile mtu anayesikilizia, halafu inaendelea tena. Unapoufikia mti ambao unadhani
umeisikia sauti hiyo, ghafla sauti inakoma. Hili linakufadhaisha na unajiandaa
ili uweze kumkabili huyo aliye juu ya mti.
Unapoangaza vizuri juu ya mti baada
ya sauti kuanza kusikika tena, mara unamwona ndege mmoja mdogo mwenye mdomo
uliochongoka ambaye anaendelea kutoboa mti bila hofu yoyote.
Nguvu zote zinakuishia na unabaki
kumkodolea macho ndege huyu ambaye ama anaweza kuwa wa kijivu, mwenye madoa
meupe na mkia wa njano, huku mdomo wake ukiwa mwekundu.
Ndege huyu anaitwa kigong'ota, au kwa majina mengine gongonola, gogota, vigotagota au ving'ota na katika sehemu nyingine huko Tanganyika (vijijini zaidi), wanaitwa Nyamkonghona. Ni ndege wa nusu-familia ya Picinae katika familia ya Picidae, ambaye kwa Kiingereza anaitwa Woodpecker.
Ndege huyu anaitwa kigong'ota, au kwa majina mengine gongonola, gogota, vigotagota au ving'ota na katika sehemu nyingine huko Tanganyika (vijijini zaidi), wanaitwa Nyamkonghona. Ni ndege wa nusu-familia ya Picinae katika familia ya Picidae, ambaye kwa Kiingereza anaitwa Woodpecker.
Vigong'ota vinatokea misituni na
maeneo mengine yenye miti kila mahali pa dunia isipokuwa Madagaska, Australia,
New Zealand na kanda za Aktiki na Antaktiki.
Spishi nyingi ni nyeusi mgongoni
kwenye madoa na/au mabaka meupe au njano. Spishi nyingine zina rangi ya majani
au kahawa. Miguu yao ina vidole viwili vikabilivyo mbele na viwili vikabilivyo
nyuma.
Mkia una manyoya shupavu na
kumsaidia ndege kutembea wima mashinani kwa miti. Ndege hawa wana domo lenye
nguvu ambalo hutumia kugogota miti na kutafuta wadudu katika nyufa za miti.
Ulimi wao mrefu wa kunata na wenye
nywele huwasaidia kuwatoa wadudu. Zaidi ya wadudu vigong'ota hula matunda na
makokwa; spishi nyingine hula hata utomvu wa miti. Dume huchimba tundu katika
mti na pengine jike humsaidia. Huyu huyataga mayai 2-6 ndani ya tundu.
Kigong’ota wapo wa aina nyingi kwa
spishi za Afrika kama Kigong'ota Mkia-njano (Campethera abingoni), Kigong'ota
Sharubu-jekundu (Campethera bennettii), Kigong'ota Madoa (Campethera
cailliautii), Kigong'ota Masikio-kahawia (Campethera caroli), Kigong'ota
Mgongo-kijani (Campethera maculosa), Kigong'ota wa Mombasa (Campethera
mombassica), Kigong'ota Kisogo-chekundu (Campethera nivosa), Kigong'ota Kusi
(Campethera notata), Kigong'ota Nubi (Campethera nubica), Kigong'ota
Madoa-madogo (Campethera punctuligera), Kigong'ota Kipaku (Campethera
scriptoricauda), Kigong'ota Miraba (Campethera tullbergi), na wengineo.
Ndege hawa wanapatikana katika
mbuga na hifadhi zetu nyingi zilizosheheni na mojawapo ya utajiri wetu wa asili
ambao tunastahili kujivunia.
Jamani ndugu zangu, utajiri huu ni
wetu na tunapaswa tuusawiri. Mbunga za wanyama zipo kwa ajili yetu, twendeni
tukatembelee na kujionea vivutio hivi adhimu. Tukienda sisi tutawajengea watoto
wetu utamaduni wa kuthamini vyao, badala ya kuwawekea mikanda ya akina Jet Li,
Aki na Ukwa na mingine ambayo haiwapi mafunzo yoyote ya maana.
* Mwenye maoni, au anayewajua ndege
hawa kwa majina ya kienyeji, anitumie kupitia namba 0715 070109, au e-mail: brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment