Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 13 December 2013

BABA GASTON ILUNGA WA ILUNGA AENDELEA KUTAMBA NA KAKOELE VIVA CHRISTMAS TANGU MIAKA YA 1970

 
Na Daniel Mbega

KILA mwaka katika kipindi kama hiki cha Majirio, yaani kuelekea siku ya kuzaliwa Kristo Masihi, Yesu Kristo (Krismas), kote duniani huwa kuna furaha kubwa mitaani na makanisani, majumba yakiwa yamepambwa kwa miti ya Krismas inayonukia, maua na vikorombwezo anuai kuikaribisha siku hiyo muhimu kwa wanadamu wote.
Zawadi mbalimbali huandaliwa kwa ajili ya kuwapatia ndugu na jamaa, Father Christmas naye akiwaandalia watoto zawadi, huku muziki mwororo ukitawala anga zote kupitia kwenye redio au televisheni.
Ni wakati huu ambapo muziki unaotawala huwa ni wa yule mkongwe wa muziki laini, marehemu Jim Reeves wa Marekani, ambaye vibao vyake 12 kikiwemo cha Jingle Bells pamoja na kundi la Boney M vibao vyao vinatamba duniani kote ikiwa ni pamoja na hapa Tanzania, ambako pia hukolezwa na kibao cha Komandoo Hamza Kalala kisemacho Noel-Krimas.
Lakini mbali na vibao hivyo, kwa ukanda mzima wa Afrika kibao ambacho hutamba zaidi na kuchukua chati ya juu ni kile kinachojulikana kama Kakoele, ama Viva Christmas au Noel Krismas, kwa vyovyote utakavyokiita.
Nasi kwa kuwatakia heri na baraka za kusherehekea sikukuu hiyo ya Krismas pamoja na Mwaka Mpya, kwa nia njema kabisa, leo tumeamua kuwaletea kibao hicho ambacho kimeimbwa kwa lugha ya Kilingala.
Wimbo huo umetungwa na kuimbwa na marehemu Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda Gaston Omer maarufu Baba Gaston Ilunga wa Ilunga, mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani ikiitwa Zaire) ambaye alikuwa maarufu katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Kibao hicho kilichomo kwenye albam yake ijulikanayo kwa majina niliyoyasema hapo juu kilifyatuliwa takribani miaka 35 iliyopita nchini Kenya, lakini bado kinaendelea kutamba na kitaendelea kutamba kwa mashabiki na wafuasi wote wa dini ya Kikristo kutokana na ujumbe uliomo ndani.
Wimbo huo unaosikika kila ikaribiapo sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya uliweza kumjengea jina na sifa kubwa mkongwe huyo ingawa hakuwa mashuhuri kama walivyokuwa akina Joseph Kabasele 'Le Grand Kalle', Dk. Nico Kassanda ‘Kassanda Nicalay’, L’Okanga La Ndju Pene Luambo Luanzo Makiadi (Francis Makiadi) ama Franco na wengineo kutoka Zaire.
Aliifyatua albam hiyo kwa ajili ya nyimbo za Krismas tu kama alivyofanya Jimmy Reeves, ambapo ina jumla ya nyimbo tano ukiwemo huo wa Kakoele au Krismas. Nyingine ni Nakumbuka Krismas, Bewela Krismas, Super Krismas na Topele Krismas.
Kakoele anayeimbwa na Baba Gaston ni msichana wa kileo, yaani 'Sister Duu', mkorofi na mchoyo wa mapenzi, lakini ni mzuri ajabu. Baba Gaston kwa kuwa anafahamu Krismas ni siku ya kuzaliwa Masihi aliyekuja kufundisha pendo la kweli kwa wanadamu wote, anamwendea Kakoele siku hiyo hiyo kumkumbusha kwamba Krismas ni siku ya 'Mfalme wa Pendo' (Yesu Kristo).
Kwa hiyo anamtaka ajaribu kujivua uchoyo wake na kuwa mkarimu siku hiyo kisha amwonyeshe angalau pendo linalotakiwa kwa binadamu badala ya lile la 'Chuna Buzi'.
Hali kadhalika, katika ushauri huo kwa Kakoele, anatukumbusha wanadamu wote kuwa tunawajibika wakati huu kushinda udhaifu wetu na kudhihirisha pendo la kweli ambalo limeletwa na Bwana Yesu Kristo.
Ni kibao kilichopambwa na maneno ya kumweleza muhibu wako, lakini kikiwa kimelenga hasa kuwataka wanadamu wote wapendane kama lilivyokuwa kusudi la Bwana Yesu, ambaye wanadamu wote tunaamini kwamba hata wakati anapaa aliwaambia wanafunzi wake kuwa, Wapendane, kama Mungu alivyowapenda wanadamu na kumtuma Yeye ili auokoe ulimwengu na vilivyomo!
Baba Gaston alizaliwa Julai 5, 1936 mjini Lubumbashi kusini-mashariki mwa Zaire na kujipatia elimu yake ya msingi katika shule ya St. Gabriel, Kapolowe katika Jimbo la Shaba na baadaye akafanikiwa kuendelea na masomo ya juu katika shule ya Benedict Catholic Fathers ya mjini Likasi.
Alijitosa katika ulimwengu wa muziki akiwa na miaka 20 katika Jiji la Kinshasa kwa kuanza kuimba kwaya kanisani kabla ya kuingia kwenye muziki wa Jazz akiwa na bendi yake mpya ya Orchestra Baba Nationale na wimbo wake wa kwanza ukiwa ‘Barua kwa Mpenzi Gaston’.
Mwaka 1972 gwiji huyo aliamua kuja Tanzania ambapo onyesho lake la kwanza lilikuwa katika ukumbi maarufu wakati huo wa White House, Kimara jijini Dar es Salaam, ambako pia ndiko kulikuwa maskani ya bendi ya Marquiz du Zaire (OMACO), bendi ambayo sasa ni marehemu!
Miaka mitatu baadaye mwanamuziki huyo akiwa na mkewe na watoto wake kadhaa aliamua kuchanja mbuga na kwenda Kenya ambako aliendelea kuimba kabla ya kwenda Arusha alikozindua kibao chake kingine maarufu cha Talaka Mpakani Yanitoa Jasho na kuongeza raha pale alipozingua na kibao kingine cha Mapendo Kizunguzungu.
Baadaye mwaka 1994 akiwa na familia yake alihamishia maskani yake mjini Arusha akitokea Nairobi, Kenya, ambapo alikuwa ameachana na muziki na alitegemea zaidi biashara zake za duka la kuuza vyakula mbalimbali katika eneo la Majengo katika barabara ya Sokoine.
Nyimbo zake nyingi aliimba kwa Kiswahili na wimbo maarufu ni ule wa "Kakolele Viva Christmas" ambao sauti inayoongoza iliimbwa na Kasongo Wakanema ambaye baadaye alijiunga na Super Mazembe. Wimbo huu uliuza nakala 60,000 chini ya Polygram. 
Baba Gaston anatajwa kwamba alipata kuimba na wanamuziki zaidi ya 700 na kwamba bendi yake ilikuwa 'chuo cha muziki'.
Pigo kubwa alilipata Julai 176 wakati wanamuziki wengi wakiwemo  Bwami Walumona, Kasongo Wakanema, Evani Kabila Kabanze (mwimbaji na mtunzi), Kalenga Nzaazi Vivi (mwimbaji na mtunzi), Lutulu Kaniki Macky, na Twikale wa Twikale walipoihama Baba Nationale na uanzisha bendi ya Orchestra Les Mangelepa. Wanamuziki wengine walijiunga na bendi za Bwambe Bwambe, Pepelepe, na Viva Makale.
Majina ya wanamuziki waliopata umaarufu wakiwa na Baba Gaston ni pamoja na Starzo ya Esta (muhimili mkubwa wa bendi ya Festival du Zaire), BadiBanga wa Tshilumba Kaikai (mwimbaji na mtunzi, ambaye baadaye alijiunga na Les Mangelepa), Mukala Kanyinda Coco (a.k.a. Mukala wa Mulumba Bebe, kutoka Orchestra Mbuta Mbuta, pamoja na mpiga bass Manitcho, na baadaye mpiga drum wa Mangelepa, ambaye kwa sasa yuko jijini London), Jimmy Kanyinda, Aloni Vangu, Zainabu (baadaye alijiunga na Orchestra Shika Shika), Pepe Mato, Yassa Bijouley (aliyezamia Mombasa, Kenya), Lisasi Ebale Mozindo, Zengele Saida (wa Bana Moja/Bana Ngenge), William Tambwe Lokassa, Kasongo Fundi (mpiga drum na bass, pia alikwenda Mangelepa ), Kazadi Mbiya Saleh wa Bambu, Medico Bwala, Lukangika Maindusa Moustang (baadaye akawa mpiga solo wa Mangelepa), Lumwamga Mayombo Ambassedeur (alikuwa mpiga rhythm wa Mangelepa), na Tshimanga Zadios (mpiga sax wa Mangelepa).
Mwimbaji wa kike aliyewahi kuimba na Baba Gaston alikuwa Nana Akumu wa Kudu. Anakumbukwa vyema kwa uimbaji wake akiwa na bendi ya Pepelepe jijini Nairobi kabla ya kujiunga na Franco katika bendi ya OK Jazz hasa kwenye wimbo wa "Mamou" ambao anapokezana na Franco mwenyewe kwenye mazungumzo ya simu. Huyu inasadikika bado anaimba akiwa jijini Brussels, Ubelgiji akisaidiana na mumewe Djo Mali na Dieudos, mpiga solo wa zamani wa Les Noirs.
Wanamuziki wengine waliopata kukaa muda mfupi kwa Baba Gaston, ambao sasa ni marehemu, ni pamoja na Mtanzania John Ngereza (ambaye baadaye aliongoza bendi ya Les Wanyika hadi alipofariki Februari 2000), Shoushou (Tchou Tchou), Lutulu Kaniki Macky (mwimbaji na mtunzi), Bosho Kayembe Nyonga (aliyeongoza bendi ya Festival Libaku jijini Nairobi kabla ya kufariki), Tabu Nkotela Kiombwe (aliyefariki mjini Mombasa, Kenya, wakati akiwa gerezani kutokana na kosa la wizi).
Mwanamuziki huyo alifariki dunai Jumamosi Machi 18, 1997 katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Alifariki akiwa anakaribia kabisa kufikisha miaka 61. Akaenda kuzikwa katika makaburi ya Lang’ata jijini Nairobi.
Katika kibao hicho Baba Gaston amemwita Kakoele huku akitoa ushauri wake hivi:
1. Kako yeye ngai nakoloba likamboo
(Kakoele neno nitakalokwambia)
Yo bomba na motema nayo
(lihifadhi moyoni mwako)
Ezalaka makasi kokotana pamba boyee mama
(Ni vigumu kukutana hivi kwa matatizo mama)
Bongo sima nagoo bolingana aa
(Halafu baadaye waishi kwa upendo)
Mama lele bolingo motema pasii x2
(Mama ee pendo linaumiza moyo x2)

2. Lokola ngai nayebanisee, Kako ee mama
(Kwa kuwa mimi nafahamika sana, Kako ee mama)
Na basemeki na ngai
(Na mashemeji zangu)
Ebingi tolingana
(Tunapaswa tupendane)
Ezalaka makasi tokutana pamba boyee
(Ni vigumu tukutane (maishani) hivi kwa matatizo)
Bongo sima nagoo tolingana aa
(Halafu baadaye tuishi kwa upendo)
Mama lele bolingo motema pasii x2
(Mama ee pendo linaumiza moyo x2)

Kiitikio:
Kakoele mama Kakoele x2
(Kakoele mama Kakoele x2)
Kakoele mama Kakoele, Papy akolela
(Kakoele mama Kakoele, Papy analia)
Mama yoka kooo
(Mama hebu sikia)
Kakoele mama elingi yaye
(Kakoele mama anataka pendo lako)
Papy akolela, yoka mama
(Papy analia, sikia mama)
Kakoele mama Kakoele
Viva Krismas x2
(Kakoele mama Kakoele,
Idumu Krismas x2)
Noeli mama Yesu abotami - tolingana
(Ni Krismas mama, Yesu amezaliwa - nasi tupendane)
Viva Krismas x2 Yesu abotami
(Idumu Krismas x2 Yesu amezaliwa)
Kakoele mama Kakoele x3
Yoka ko! Yoka ko!
(Kakoele mama Kakoele x3
Sikiliza! Hebu sikia!).


No comments:

Post a Comment