Mto Ruaha uliokauka, siyo mbali na eneo la vita Lugalo.
Na Daniel Mbega
KUANGUKA
kwa ngome ya Mtemi Isike huko Tabora kulizidi kuidhoofisha Himaya ya Wahehe kwa
sababu Chifu Mkwawa hakuwa na mshirika yeyote kati ya watawala wa jadi
waliomzunguka.
Baada ya
kumuua Mtemi Isike, Wajerumani walifanikiwa kuwateka askari wa Kinyamwezi
(walugaluga) na kuwaingiza kwenye jeshi lao ambalo sasa lilikuwa limejiimarisha
zaidi.
Mwaka 1893 Gavana von Soden, ofisa pekee wa kiraia
katika historia ya utawala wa Ujerumani katika Koloni la Afrika Mashariki,
aliondoka kurejea Berlin baada ya miaka kadhaa ya kupingana na wasaidizi wake
wa kijeshi pamoja na wakubwa wake kule Ujerumani. Nafasi yake ikachukuliwa na
Friedrich Radbod Freiherr von Schele.
Maagizo aliyopewa ni kuhakikisha anakomesha uvamizi wa misafara na kumwadabisha Chifu Mkwawa huku wakiwa na mkakati wa kuanzisha mapambano makali dhidi ya Wahehe na kuitwaa ardhi yao yenye rutuba. Lakini alitambua kwamba, wenyeji wote wa maeneo ya jirani walikuwa wanaendelea kuwahofia Wahehe.
Maagizo aliyopewa ni kuhakikisha anakomesha uvamizi wa misafara na kumwadabisha Chifu Mkwawa huku wakiwa na mkakati wa kuanzisha mapambano makali dhidi ya Wahehe na kuitwaa ardhi yao yenye rutuba. Lakini alitambua kwamba, wenyeji wote wa maeneo ya jirani walikuwa wanaendelea kuwahofia Wahehe.
Mashushushu wa Kijerumani wakati huo walikuwa wameanza
kuondoka katika ngome yao iliyokuwa katika Koloni la Waingereza na Wamisri
(Sudan ya sasa) na Koloni la Ureno Afrika Mashariki (Msumbiji) kwa sababu
maeneo hayo yalikuwa yameanzisha ushirikiano na Waingereza na wareno.
Katika kulipa kisasi cha mwaka 1891 na kampeni
zilizofuatia, serikali ya Ujerumani mjini Dar es Salaam ikawatuma majasusi wake
huko Aden, Cairo, Massawa, na Zanzibar, ambao waliwasiliana na vyanzo vyao huko
‘Msumbiji’, ‘Sudan’, na kwenye Himaya ya Ottoman wakitaka msaada wa namna ya
kufidia hasara waliyoipata. Baada ya majadiliano Waingereza walituma askari wa
Misri kufidia askari wa Kisudani waliokufa kule Lugalo na mahali pengine na
Wataliano wakawaruhusu Wajerumani kuwaandaa wapiganaji huko Massawa, bandari
maarufu kwenye Koloni la Wataliano Afrika Mashariki (Eritrea ya sasa).
Lakini baadaye wakaanzisha harakati za kuwatumia watu
wa pwani waliokuwa wakiishi jirani na Koloni la Ujerumani Afrika Mashariki.
Wengi kati ya hawa walikuwa Waislamu, ambao walitumia Kiswahili kama lugha ya
mawasiliano jeshini, ambayo waliona ni silaha ya kusambaza dini ya Uislamu.
Wajerumani pia, kama ilivyoelezwa hapo awali, wakawatumia wapiganaji wa jadi
kama Wanyamwezi wa Tabora, ambao walionekana kuwa hazina kubwa ya wapiganaji.
Wanyamwezi, ambao ndio walikuwa wapiganaji wa jadi
wengi zaidi kwenye jeshi la Mjerumani, walikuwa wameendeleza tu ushiriki wao wa
awali kwani ndio waliokuwa wanaongoza kwa upagazi, ambapo kote walikuwa
akifanya kazi kwa ujira. Ndiyo maana haikushangaza hata baada ya ujenzi wa Reli
ya Kati mwaka 1910 iliyochukua nafasi ya wapagazi, Wanyamwezi wengi wakajiunga
na jeshi la Mjerumani.
Hadi mapema
mwaka 1894, Jeshi la Mjerumani lilikuwa na wapiganaji karibu 2,000, likiwa
limefidia mara mbili zaidi ya askari waliopotea Lugalo, na Schele alikuwa na
uhakika kwamba alikuwa na jeshi ambalo lingeweza kuibomoa Himaya ya Uhehe.
Jaribio la kwanza la Wajerumani
kuibomoa Himaya ya Uhehe lilifanyika mapema mwaka 1894 huko Image wakiwa na
hadhari yasitokee kama yale ya kule Lugalo na Kilimatinde. Jeshi la Mkwawa
katika mapigano ya Image, ambako wakeze pia walikuwa wametekwa na Wajerumani,
yaliongozwa na kaka yake, Chifu Malangalila Gamoto na kufanikiwa kuwakomboa.
Kwa bahati mbaya, pamoja na
kufanikiwa zoezi hilo la ukombozi, Malangalila Gamoto alijeruhiwa vibaya kwa
risasi. Chifu Mkwawa akaagiza kaka yake apelekwe Ubena ambako ndiko alikokuwa
anatawala, lakini walipofika eneo la Mbweni akafariki dunia. Mwili wake
haukuzikwa kwa sababu za kimila. Mahali hapo pamejengwa mnara.
Tutaendelea...
No comments:
Post a Comment