Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 22 December 2013

KAMA UNATEMBELEA HIFADHI MOJA TU AFRIKA, NJOO RUAHA


Na Daniel Mbega, Iringa

NI eneo kavu katikati ya Tanzania ambapo ardhi ni ya rangi ya udongo, nyasi za rangi ya simba huku miti ikionekana kana kwamba inaweza kutumia kiasi kidogo tu cha maji. Kila kitu ambacho unategemea Afrika iwe nacho kipo hapa: anga la bluu lenye mawingu kiasi, jua kali na harufu maalum ya hewa itokanayo na mambo mengi yakiwemo maua ya mikungugu (acacia), miti mikavu, vumbi jekundu na manyunyu kwa mbali.
Kila mtu na kila kitu kinasubiri mvua inyeshe. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni mojawapo ya maeneo makavu nyakati za kiangazi na yenye joto hasa nyakati za mchana. Kwa wale wanaotoka kwenye nchi za baridi, ambao wanahitaji halijoto kama hii, hapa ndipo mahali ambapo wanaweza kufurahia zaidi likizo na mapumziko yao ya kiangazi bila shida.
Kwa yeyote anayehitaji mapumziko, Ruaha ndiyo mahali pake, ambapo utulivu wake ni murua unaoweza kumpumbaza yeyote akasahau fadhaa zote za maisha na kujiona yuko katika ulimwengu mzima akisawiri utukufu wa Mungu kwa namna alivyoweka mandhari nzuri iliyojaa hayawani wa kutosha na wa kila namna.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ndiyo kubwa kuliko zote Tanzania, ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Hifadhi ya Kafue ya Zambia. Ni kubwa kiasi gani? Huwezi kuamini kwamba hifadhi hii ukubwa wake ni zaidi ya 2/3 (theluthi mbili) kwa ukubwa wan chi ya Ubelgiji ambayo eneo lake la mraba ni kilometa za mraba 30,528! Rwanda yenye eneo la ukubwa wa kilometa za maraba 26,338 na Burundi (27,834km2) zinaizidi kidogo hifadhi hii.
Utashangaa nikikwambia kwamba ukubwa wa hifadhi hii ni sawa na Jimbo la New Jersey la Marekani, ambao eneo lake ni kiliometa za mraba 22,608. Hifadhi ya Ruaha ina ukubwa wa kilometa za mraba 20,226!
John Nyamhanga ni Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambaye anasema hifadhi hiyo imezungukwa na hifadhi za kijamii na maeneo tengefu hivyo kuifanya iwe na eneo kubwa zaidi ya hilo kutokana na kutengeneza mfumo imara wa ikolojia unauruhusu kuwepo kwa wanyama wengi ingawa kuna changamoto nyingine nyingi zinazotokana na shughuli za kibinadamu.
“Mbali ya ukubwa wake, hifadhi ya Ruaha ina wanyama wengi wakiwemo mbwa mwitu ambao wamekuwa adimu katika maeneo mengi nchini. Makundi ya tembo hayakosekani kwani ni miongoni mwa maeneo yenye tembo wengi ikiwa nyuma ya pori tengefu la Selous,” anasema Nyamhanga.
Kwa mujibu wa Nyamahanga, hifadhi hiyo inayopitiwa na Bonde Kuu la Ufa inategemea mfumo wa maji wa Mto Ruaha Mkuu unaoshibishwa maji kutoka katika mito ya Mazombe, Mdonya, Mwagusi na Jongomero. Mto Ruaha Mkuu unatiririka kwa urefu wa kilometa 160 upande wa kaskazini mwa hifadhi hiyo.
Ndege wa kila aina wanapatikana katika hifadhi hiyo na kwa watalii, nyakati nzuri za kuona ndege hao ni majira ya masika.
“Ruaha imejaaliwa tembo wengi kuliko hifadhi yoyote Afrika Mashariki na ndipo mahali ambapo unaweza kuwaona wanyama wengi wa jamii ya swala kama Pofu, Kuro na hata digidigi bila kuwasahau samba, chui, duma, twiga, pundamilia, mbweha na mbwa mwitu,” anasema Nyamhanga.
Hifadhi hii inafahamika na wanahistoria kama ndiyo ardhi ya Chifu Mkwawa, na kwamba misafara ya awali ya watumwa iliyofanywa na Waarabu ilipitia hapo. Mkwawa pia alitumia njia hizo wakati alipokuwa anatembelea himaya za Wasangu, Wagogo na Wanywamwezi.
Miongoni mwa maeneo ya kihistoria ndani ya hifadhi hiyo ambayo zamani yalitumika kwa kutambikia ni pamoja na “Ganga la Mafunyo”, Nyanywa na Chahe, Jabali lililochorwa la Nyanywa, kaburi la Mtemi Mapenza wa Wagogo huko Mpululu na eneo la majimaji la Mkwawa ambalo linasadikiwa kuwa lilitumiwa na Chifu Mkwawa mwenyewe.

Kutambulika
Ofisa Utalii wa Tanapa wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Risala Kabongo, anasema ofisi yake imeanzisha mkakati wa kuhamasisha utalii wa ndani katika hifadhi za mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni pamoja na kukutana na watoa huduma mbalimbali wakiwemo wa hoteli na kuwapa elimu ya kuhudumia  wageni ili kukuza utalii.
Hata hivyo, anasema ili kuitangaza zaidi Hifadhi ya Ruaha, ni vyema kuitambulisha hifadhi hiyo kimataifa hasa kwa kuuita Uwanja wa Ndege wa Songwe, Mbeya kama Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Ruaha.
“Kama hifadhi za kaskazini zilivyotangazwa kwa kuupa uwanja wa kimataifa wa ndege jina la ‘Kilimanjaro’, ni wakati sasa wa kuuita uwanja wa Songwe kama ‘Ruaha’. Kwa namna hii tutaitangaza hifadhi hii pamoja na nyingine zilizo Nyanda za Juu Kusini,” anasema Kabongo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC), Frank Leonard, anasema wanahabari wanao wajibu mkubwa wa kuitangaza hifadhi hiyo pamoja na nyingine zilizoko ukanda huo ili kuhamasisha watalii wa ndani na wa kimataifa.
“Tumerejea hivi karibuni katika ziara ya mafunzo kanda ya kaskazini, tuliyoyaona ni changamoto kwetu wanahabari kuhakikisha tunatumia taaluma yetu kuutangaza utalii katika kanda hii,” anasema.
Pamoja na changamoto hiyo, amewahimiza vijana na wananchi wa mikoa hiyo kuchangamkia fursa nyingi zilizopo zinazoendana na uwekezaji katika sekta ya utalii.
“Ni vyema hoteli bora zikajengwa katika maeneo tulivu, siyo kubanana mjini, kwani watalii wanapenda kuja kupumzika. Lakini pia wakulima walime mazao bora ya chakula yatakayotumiwa kwenye hoteli hizo na mambo kadha wa kadha,” anasema Frank na kuongeza kwamba, ukuaji wa utalii uendane na kuboresha kipato cha wananchi.
Mkurugenzi wa Mipango na Utalii wa Tanapa, Dk. Ezekiel Dembe, anasema idadi ya watalii wa ndani na nje wanaotembelea Hifadhi ya Ruaha na hifadhi nyingine nchini ni kubwa zaidi japo lengo ni kufikisha watalii milioni 2.5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2015.
Hata hivyo, anasema lengo ni kuona idadi ya watalii katika hifadhi inakua kwa kuzingatia ubora siyo idadi kubwa ili kulinda ikolojia ya maeneo yaliyohifadhiwa.
“Pamoja na idadi ya watalii wa nje katika Hifadhi ya Ruaha inazidi kuongezeka kila mwaka, lakini changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa mafuta ya ndege katika Uwanja wa Nduli mjini Iringa, jambo ambalo linawalazimu watalii kujaza mafuta Dodoma kabla ya kwenda Iringa,” anasema Dk. Dembe.
Dk. Dembe alisema wanafanya mpango kuona mafuta ya ndege yanauzwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Seronera katika Hifadhi ya Serengeti ili watalii wakitoka huko waende moja kwa moja Ruaha na Katavi.
Aidha, amewataka wawekezaji kujitokeza kuwekeza katika sekta ya lodge na hoteli ndani ya hifadhi hiyo ili kuwapa fursa watalii wengi zaidi kupata mahali pa kupumzika.
Kwa sasa kuna lodge sita tu ndani ya Hifadhi ya Ruaha ambazo ni Tandala Tented Camps, Mwagusi Safari Camp, Mdonya Old River Camp, Ruaha River Lodge, Kwihale na Jongomero Camp.

Changamoto
Changamoto inayoikabili Hifadhi ya Ruaha ni shughuli za kibinadamu zinazoendelea katika maeneo mengi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hususan kilimo cha umwagiliaji, ambacho kinatumia maji mengi hivyo kukausha Mto Ruaha Mkuu ambao ndio tegemeo kubwa la uwepo wa hifadhi hiyo.
Godwell ole Meing'ataki ni Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneneo yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) ambaye anabainisha kwamba, shughuli hizo zilizopamba moto mwanzoni mwa miaka ya 1990, zinasababisha kupotea kwa viumbehai kwenye hifadhi hiyo wakiwemo wanyama na mimea.
“Hii ni changamoto kubwa na juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kila sekta iweze kunufaika bila kuathiri ikolojia ya asili,” anasema.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, eneo lote la Bonde la Usangu linaguswa na takriban wizara sita ambazo kila moja inapigania maslahi yake, hivyo kuzua mgongano wa sera.
Wizara ya Ardhi na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika zinaguswa moja kwa moja, lakini Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaonekana ndiyo iliyovuruga mfumo-ikolojia kwa kuhamaisha kilimo cha umwagiliaji wa mashamba makubwa ya mpunga katika maeneo ya Mbarali, ambako maji mengi ndiko yanakotumika.
Aidha, maeneo mengine ya mito inayomwaga maji yake kwenye Bonde la Usangu na Mto Ruaha Mkuu nayo yamevamiwa na kilimo cha umwagiliaji kutokana na serikali kuhimiza ‘Kilimo Kwanza’.
Wizara ya Nishati na Umeme inayotegemea maji hayo ya Mto Ruaha Mkuu kujaza Bwawa la Mtera ili kuzalisha umeme nayo imeathiriwa kwa sababu hata bwawa lenyewe limekauka, huku mwathirika mkuu akiwa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo wanyama wengi katika Hifadhi ya Ruaha wanakufa kwa ukame.

Historia ya Ruaha
Historia ya hifadhi hiyo, kwa mujibu wa taarifa za Tanapa, inaanzia mwaka 1910 wakati ilipotangazwa na serikali ya kikoloni chini ya Wajerumani kama Mbuga ya Wanyama ya Saba (Saba Game Reserve) lakini Waingereza walipoingia wakaibadilisha na kuiita Rungwa Game Reserve mwaka 1946.
Mnamo mwaka 1964 ndani ya Tanganyika huru, upande wa kusini wa mbuga hiyo ukatangazwa kwenye gazeti la serikali na kuitwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na mwaka 1974 sehemu ndogo ya kusini mashariki ya Mto Ruaha Mkuu ikaongezwa kwenye hifadhi. Hifadhi hii ni sehemu ya mfumo ikolojia wa Rungwa-Kizigo –Muhesi ambao unachukua eneo la kilometa za mraba 45,000. Mwaka 2008 Usangu Game Reserve na maeneo mengine oevu ya Bonde la Usangu yaliingizwa kwenye hifadhi, na kuifanya hifadhi hiyo kuwa kubwa zaidi Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla ikiwa na kilometa za mraba 20,226.
Hifadhi hii iliyoko katikati ya Tanzania ipo umbali wa kilometa 128 magharibi mwa mji wa Iringa na inafikika kwa usafiri wa barabara na hata ndege za kukodi. Magari hufika wakati wowote wa mwaka kutoka Dar es Salaam, takriban kilometa 625.

No comments:

Post a Comment