TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU ACHARUKA, AKATAA KUKAGUA JENGO LA ZAHANATI
*Ni baada ya wataalam kukiuka maagizo yake aliyotoa Machi mwaka huu
ILE
HALI ya kufanya kazi kwa mazoea (business as usual) iliyojengeka kwa
baadhi ya watendaji wa Serikali leo imewatokea puani watendaji wa
Manispaa ya Dodoma wakati Waziri Mkuu alipoamua kufanya ziara kukagua
miradi ya maendeleo.
Akiwa katika eneo la
kwanza ambalo alipangiwa kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Mkonze leo
asubuhi (Jumamosi, Juni 7, 2014) Waziri Mkuu alipokea taarifa ya ujenzi
wa kituo na kubaini kuwa hawajafanya chochote ili kutekeleza maagizo
yake aliyoyatoa Machi 22, 2014.
Katika taarifa
yake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe
alimweleza Waziri Mkuu kwamba walifanya tathmini ya ujenzi wa kituo
hicho na kubaini kuwa zinahitajika sh. Milioni 24.15 na kwamba maombi ya
matumizi hayo yamepangwa kujadiliwa kwenye kikao cha kamati ya fedha na
uongozi kitakachofanyika Juni 10, mwaka huu.
Akiwa
katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji ambayo Kitaifa
yalifanyika mkoani Dodoma, Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji jirani na
kituo cha afya cha Mkonze na kubaini kuwa kuna hitilafu za ujenzi.
Ndipo akaagiza kwamba ufanyike ukarabati na yeye akaahidi kuja kukagua
ukarabati huo mwezi Juni, 2014.
Mara baada ya
kusomewa taarifa ya mradi, Waziri Mkuu akahoji ni kwa nini hawajafanya
chochote tangu alipotoa maelekezo Machi, mwaka huu. Hakupata jibu la
kueleweka kutoka kwa viongozi wa wilaya na mkoa.
Waziri
Mkuu aliwasalimia wananchi waliokuwepo kwenye eneo hilo na kuwaeleza
kwamba hawezi kukagua kituo hicho ilhali hakuna kilichotekelezwa tangu
afike hapo Machi mwaka huu.
Alisema haiwezekani
yeye atoe maagizo katika kipindi chote hicho halafu kisifanyike kitu
chochote. Akaondoka na kuendelea na ziara hadi kijiji cha Manzase ambako
alikagua mradi wa kisima cha maji.
Mapema, katika taarifa
yake, Mhandisi Kilembe alisema kituo hicho cha afya kilijengwa chini ya
ufadhili wa ubalozi katika makubaliano yaliyofikiwa Novemba 11, 2009
kwamba ingetoa dola za marekani 84,307 sawa na sh. Milioni 152.86.
Hata
hivyo, mara baada ya ujenzi kukamilika Agosti 29, 2012, kituo hicho
kilipata nyufa nyingi hali iliyosababisha kifungwe na wananchi walitoa
malalamiko yao kwa Waziri Mkuu Machi mwaka huu wakati alipokwenda
kuzindua mradi wa maji kwenye kijiji cha Mkonze jirani na kituo hicho.
Akiwa
katika kijiji cha Manzase Waziri Mkuu aliridhishwa na ujenzi wa mradi
wa maji kwa ajili ya wakazi 9,000 wa eneo ambapo alielezwa kwamba
utakamilika Julai 16, 2014.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAMOSI, JUNI 7, 2014
No comments:
Post a Comment