Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot.com, Arusha
MWENYEKITI kamati ya usafi mkoa wa Arusha Adolf Ulomi amesema kuwa zoezi la usafi wa Jiji la Arusha bado unakabiliwa na changamoto kubwa hasa ya baadhi ya wanasiasa kuingiza siasa kwenye usafi jambo ambalo wakati mwingine linafanya Jiji kuonekana bado chafu.
Ulomi aliyasema hayo jana katika eneo la Kwa Murombo wakati Kamati hiyo ikiendelea na usafi wa Jiji na kuhusisha wananchi pamoja na wafanyabiashara wa eneo hilo.
Alisema kuwa pamoja na kuwa kamati hiyo ya usafi imejidhatiti katika kuhakikisha kuwa Jiji la Arusha linakuwa safi lakini baadhi ya wanasiasa wa Mkoa wa Arusha wanatumia vyeo vyao kupotosha maana halisi ya Kamati hiyo lakini pia umuhimu wa jiji kuwa safi.
Alifafanua kuwa baadhi ya wanasiasa hao mara nyingine wanadai kuwa wanawaonea huruma wananchi hasa wale ambao wanaharibu mazingira huku baadhi ya wananchi hao nao wakitumia muda huo kuchafua hali ya usafi wa jiji kwa kisingizo kuwa wamepewa ruhusa na wanasiasa wao.
“Pamoja na kuwa kweli tunajitaidi sana katika kuhakikisha kuwa lakini tukipita tu na kufanya usafi kisha kuwaambia wananchi umuhimu wa kufanya mazingira na miji yao basi wanasiasa nao wanarudi na kuwapa moyo wananchi waendelee kuchafua kwani wanaonewa sasa hali hii kweli inatukwamisha sana," alisema Ulomi.
Pia alisema wanasisasa wanatakiwa kuiga mfano wa usafi kwenye miji mingine ambayo imeendelea duniani na hata baadhi ya Miji hapa Nchini ukiwemo mji wa Moshi jinsi ambavyo wameungana na kisha kuwabana baadhi ya wananchi wanaochafua mazingira jambo ambalo limekubalika na limejengeka kuwa usafi ni wa jamii na wala sio wa Serikali.
Aliishauri Serikali kuwa inatakiwa kuwa bunifu zaidi kwenye sekta ya uwekezaji kwani kama sekta hiyo ikiwa ni kubwa hata wafanyabiashara wadogowadogo(Machinga) ambao wakati mwingine wanauza bidhaa zao bila kujali usafi wa Mji wataweza kuwa na ajira.
Ulomi alifafanua kuwa kwa sasa katika mji wa Arusha asilimia kubwa ya wafanyabiashara wadogo wanafanya biashara zao kila kona ya Mji wa Arusha lakini kama kungekuwa na fursa za uwekezaji nyingi basi wangezitumia vema hivyo hata usafi ungeimarika zaidi.
Alimalizia kwa kusema kuwa hata wafanyabiashara hao ambao wanajitafutia riziki zao za kila siku pembezoni mwa Jiji wa Arusha wanatakiwa kuuza bidhaa zao lakini wakiwa wanazingatia kanuni za usafi ili kuweza kutoa sifa kwa mji wa Arusha ambao unasifika duniani kote.
No comments:
Post a Comment