Maiti katika uwanja wa Heysel, Ubelgiji
Wanausalama wakiangalia jinsi uwanja ulivyobomoka na kusababisha vifo vya watu 39.
Uokoaji wa watu walioangukiwa na ukuta.
Na Juventus wakatwaa ubingwa kwa ushindi wa bao 1-0.
Tarehe kama ya leo, yaani Juni 2, 1985, Umoja
wa Vyama vya Soka Ulaya (UEFA) lilizifungia klabu za soka za England kushiriki
mashindano yote ya Ulaya. Adhabu hiyo ilifuatia vifo vya mashabiki 39 wa Italia
na Ubelgiji kwenye Uwanja wa Heysel jijini Brussels katika vurugu
zilizosababishwa na mashabiki wanazi wa England wakati wa mechi ya fainali ya
Ulaya.
Mchezo wa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mwaka
1985 ulizikutanisha timu za Juventus ya Italia na Liverpool ya England, ambayo
ilikuwa inatetea ubingwa wake. Majira ya saa 1 usiku, muda mfupi kabla ya
mchezo kuanza, kundi la mashabiki wa Liverpool waliokuwa wamelewa chakari,
ambao kutwa nzima walikuwa wanagida pombe kwenye baa za Brussels, wakawavamia
mashabiki wa Juventus.
Katika harakati hizo, ukuta wa uwanja
ukabomoka na kuwangukia baadhi ya watazamaji. Wengine walikanyagwa wakati
wakikimbia kutoka nje ya uwanja. Kwa ujumla, mashabiki 32 wa Juventus walikufa,
pamoja na watu wengine saba waliokuwa wakitazama. Mamia ya watu wengine
waliumia.
Ili kuepuka vurugu nyingine zisije zikatokea,
mchezo huo ukaendelea kama kawaida na Juventus wakaibuka mabingwa kwa ushindi
wa bao 1–0.
Baada ya tukio hilo, klabu zote za England
zikafungiwa kushiriki Klabu Bingwa laya na Kombe la UEFA kwa miaka mitano.
Adhabu ya Liverpool, ambayo awali ilikuwa ya muda usiojulikana, baadaye ikawa
kutoshiriki kwa miaka 10, na baadaye kupunguzwa hadi miaka sita.
Kuanzia mwaka 1977 hadi 1984, klabu za
England zilikuwa zimetwaa mataji saba kati ya nane ya Ulaya, na kuzuiliwa kwao
lilikuwa pigo kwa nchi na mchezo huo kwa ujumla.
Hata hivyo, wakati adhabu hiyo ilipotolewa,
Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher aliunga mkono kwa asilimia zote
akisema: "Lazima mchezo usafishwe kutokana na vujo za manazi hawa kuanzia
nyumbani na ndipo pengine tunaweza tukaenda ng’ambo tena."
Madhara hayo hayakuishia kwenye adhabu ya
kufungiwa, Liverpool ilijikuta mashabiki wake 14 wakipatikana na haia ya kuua
bila kukusudia nchini Berlin katika hukumu ya mwaka 1989 baada ya kesi hiyo
kuendeshwa kwa miezi mitano. Mashabiki hao wakafungwa miaka mitatu jela, huku
wakipunguziwa nusu ya kifungo hicho.
Klabu za England zilirejeshwa kwenye
mashindano ya Ulaya baada ya fainali za Kombe la Dunia 1990. Miaka 15 baadaye,
mnamo Aprili 5, 2005, Liverpool ikaichapa Juventus 2-1 kwenye mchezo wa kwanza
war obo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ilikuwa ni mechi ya kwanza tangu
timu hizo zilipopambana kwenye Uwanja wa Heysel. Mashabiki walisimama kimya kwa
muda mwanzoni mwa mchezo, kukumbuka watu 39 waliokufa mwaka 1985. Mechi ya
marudiano ilifanyika siku tisa baadaye Aprili 14 mjini Turin, ambapo Liverool
iliilazisha Juventus kwenda suluhu. Liverpool iliendelea hadi kutwaa ubingwa wa
Ulaya msimu huo.
Jun 2, 1953:
MALKIA ELIZABETH II ATAWAZWA
Mnamo
Juni 2, 1953,Malkia Elizabeth II alitawazwa rasmi kwenye taji la ufalme la
Uingereza katika sherehe kubwa. Askofu Mkuu wa Canterbury Geoffrey Fisher ndiye aliyemtawaza. Watu mashuhuri, viongozi na wageni elfu moja
walihudhuria sherehe hizo huko Westminster Abbey, jijini London na mamia kwa
mamilioni walisikiliza kupitia kwenye vituo vya radio na kwa mara ya kwanza
wakatazama kupitia kwenye luninga.
Baada ya
sherehe hizo, mamilioni ya watu walimshangilia malkia huyo aliyekuwa na miaka
27 na mumewe, Duke wa Edinburgh aliyekuwa na miaka 30, wakati walipopita
barabarani kwa umbali wa maili tano.
Elizabeth,
aliyezaliwa mwaka 1926, alikuwa binti wa kwanza wa Prince George, mtoto wa pili
wa kiume wa Mfalme George V. babu yake alifariki mwaka 1936, na baba yake
mkubwa akatawazwa Mfalme Edward VIII. Baadaye mwaka huo, Edward akaondolewa
kwenye ufalme kufuatia uamuzi wake wa kumuoa Wallis Warfield Simpson, Mmarekani
aliyekuwa ametalikiwa, na baba yake Elizabeth akatawazwa Mfalme George VI
badala yake.
Wakati
wa Vita vya Uingereza (Battle of Britain),
Princess Elizabeth na mdogo wake, Princess Margaret, walishi mafichoni nje ya
London, lakini wazazi wao waliingia matatizoni baada ya Hekalu la Kifalme
(Buchingham Palace) kupigwa mabomu na vikosi vya anga vya Ujerumani. Baadaye
wakati wa vita, Elizabeth akiwa amefundishwa na kuwa luteni usu katika vikosi
vya wanajeshi wanawake ambapo alikuwa akiendesha na kutengeneza malori.
Mwaka 1947,
aliolewa na binamu yake wa mbali, Philip Mountbatten, prince wa zamani wa
Ugiriki na Denmark ambaye aliachia taji lake ili amuoe Elizabeth. Akatawazwa
kuwa Duke wa Edinburgh wakati wa sherehe ya ndoa yao. Sherehe za ndoa yao
ziliamsha mizuka ya Waingereza, ambao walikuwa wakikabiliwa na uchumi mbovu
baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mtoto wao wa kwanza, Prince Charles, alizaliwa
mwaka 1948 hapo Buckingham Palace. Mtoto wa pili, Princess Anne, alizaliwa
mwaka 1950. Mnamo Februari 6, 1952, walikuwa nchini Kenya katika ziara wakati
waliposikia kwamba mfalme amekufa.
Mnamo Aprili
21, 2006, Malkia Elizabeth alitimiza miaka 80 (sasa ana miaka 88), na kuwa
Mwingireza wa tatu kushikilia taji la Uingereza.
Jun 2, 1865:
VITA VYA WENYEWE KWA WENYEWE MAREKANI VYAMALIZIKA
Katika
tukio lilionyesha kufikia mwisho wa Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe nchini
Marekani, Jenerali wa Confederate Edmund Kirby Smith, aliyekuwa akiongoza
vikosi vilivyokuwa magharibi mwa Mississippi, tarehe kama ya leo mwaka 1865
alisaini makubaliano ya kusalimu amri yaliyotolewa na wasuluhishi wa Muungano.
Baada ya Smith kusalimu amri, majeshi ya Confederates yakasambaratika na kuleta
utulivu katika vita vya umwagaji damu mkubwa nchini Marekani vilivyodumu kwa
miaka minne. Vita hivyo vilianza Aprili 12, 1861.
Jun 2, 1944:
MAREKANI YAANZA
‘KUSHUSHA MAKOMBORA’ KATIKA OPERESHENI FRANTIC
Tarehe kama ya leo mwaka 1944, warusha
makombora wa Marekani kutoka Kikosi cha 15 cha Jeshi la Anga walianzisha
Operesheni Frantic na kuanza kushusha makombora Ulaya ya Kati, wakitokea kwenye
kituo chao cha anga cha Italia, lakini yakarushwa kutokea vituo vya anga vya
Poltava, Urusi, katika kile ambacho kiliitwa "shuttle bombing."
Kikosi cha 15 cha Anga kiliundwa maalum kwa
ajili ya kuuvuruga uchumi wa Ujerumani kikiongozwa na Jenerali Carl Spaatz,
rubani mpiganaji wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Kikosi hiki kilianzishwa na Joseph Stalin kusaidia
Red Army katika kampeni zake nchini Romania. Katika kubadilishana na msaada wa
Kikosi cha 15, Stalin aliwaruhusu warusha makombora wa Marekani watue ndani ya
ardhi ya urusi wakati wakiendesha Operesheni Frantic, ukiwa ni mpango wa
kuuvuruga uchumi wa viwanda wa Ujerumani katika maeneo iliyokuwa imeyakalia ya Silesia,
Hungary, na Romania.
Jun 2, 1915:
VIKOSI VYA
AUSTRO-GERMAN VYWASHAMBULIA WARUSI HUKO PRZEMYSL
Mnamo Juni 2, 1915, vikosi vya Austro-Hungaria
na Ujerumani viliendelea na mashambulizi yao dhidi ya wanajeshi wa Russia
waliokuwa wakiushikilia mji wa Przemysl (sasa uko nchini Poland).
Vikosi vya Austro-German vilikuwa vinakaribia
kupata ushindi dhidi ya jeshi la Russia lililokuwa limechoka huko Przemysl; hata
hivyo mji huo uliangukia mikononi mwa Majeshi ya Kati chini ya Ujerumani siku
iliyofuata, ushindi ambao hatimaye uliifanya Russia ishindwe kuumiliki Galicia.
Jun 2, 1935:
BABE RUTH ASTAAFU
Tarehe
kama ya leo mwaka 1935, Babe Ruth, mmoja wa wacheza baseball hodari zaidi
katika historia, alistaafu kucheza akiwa na timu ya Boston Braves baada ya
kushiriki Major League kwa misimu 22. Mwaka uliofuata, Ruth, ambaye umbile lake
lilikuwa kumbwa mno, akawa mmoja wa wachezaji watano walioingizwa kwenye orodha
ya wachezaji mashuhuri (hall of fame).
George
Herman Ruth alizaliwa Februari 6, 1895, katika familia maskini huko Baltimore. Akasoma
shule ya wavulana ya St. Mary's
Industrial School iliyokuwa chini ya mapadre wa Kanisa Katoliki, huko ndiko
alikojifunza kucheza baseball. Akiwa na miaka 19 akasajiliwa na timu ya Baltimore
Orioles, ambayo ilikuwa ikishiriki ligi ndogo ya Boston Red Sox. Alichezea Red Sox hadi mwaka 1920
alipojiunga na New York Yankees na umaarufu wake ndio ulioifanya timu hiyo
ikafungua uwanja wake wa Yankees.
Jun 2, 1924:
COOLIDGE ASAINI
SHERIA YA RAIA WA INDIA
Tarehe kama ya leo mwaka 1924, Rais Calvin Coolidge
alisaini Sheria ya Raia wa India (Indian Citizen Act), iliyotoa uraia wa moja
kwa moja wa Marekani kwa wakazi wa Marekani waliozaliwa nchini humo.
Jun 2, 1886:
GROVER CLEVELAND AOA AKIWA IKULU
Rais Grover Cleveland anakuwa
rais wa kwanza aliyeko madarakani kuoa akiwa Ikulu (White House) katika tarehe
kama ya leo mwaka 1886.
Cleveland aliingia White House akiwa mseja (bachelor)
na akaondoka madarakani akiwa na mke na baba wa watoto wawili. Mkewe alikuwa
mwanamke mrembo aliyekuwa amemzidi kwa miaka 27, ambaye aliitwa Frances Folsom.
Frances alikuwa binti wa mwanasheria mwenza na msaidizi wake Cleveland. Wakati
binti huyo akiwa na miaka 11, baba yake akafariki na Cleveland akawa mlezi wake,
akiendelea kuwa rafiki wa karibu wa mama yake.
Watu wengi walidhani Cleveland angeweza
kumuoa mjane wa rafiki yake lakini badala yake wakashangazwa wakati alipomuoa
binti wa rafikiye mara tu alipofikisha umri wa miaka 21.
Katika tukio lingine la kwanza ndani ya White
House, binti wa pili wa Frances na Cleveland, Esther alikuwa mtoto wa kwanza
kuzaliwa katika chumba cha kulala cha White House.
Majanga
Jun 2, 1921:
MAFURIKO YALETA UHARIBIFU COLORADO
Mvua
kubwa yanyesha tarehe kama ya leo, mwaka 1921 huko Pueblo County jimboni Colorado, na kuleta mafuriko
makubwa yaliyosababisha vifo vya watu 120 na rasilimali na majengo yenye
thamani ya dola 25 milioni (sawa na Dola 230 milioni kwa fedha za sasa) vikiharibiwa.
Hadi kufikia wakati huo, haya yalikuwa mafuriko mabaya zaidi katika historia ya
jimbo hilo.
Mto Arkansas unapita katika uwanda wa kusini-magharibi
wa Colorado. Wananchi wa eneo hilo walikuwa wamejenga kingo
kando ya mto kuzuia mafuriko. Hata hivyo, kingo hizo hazikufaa kitu kwa
mafuriko hayo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kwenye eneo hilo Juni 1921. Mafuriko
haya yalidumu kwa wiki nzima.
Jun 2, 2012:
HOSNI MUBARAK AFUNGWA MAISHA
Tarehe kama ya leo mwaka 2012, rais wa zamani
wa Misri, Hosni Mubarak, anakutwa na hatia ya kushindwa kuzuia mauaji ya mamia
ya waandamanaji waliokuwa wakipinga serikali yake wakati wa machafuko makubwa
maarufu ya mwaka 2011 ambayo yalishuhudia mwisho wa utawala wake wa karibu
miaka 30.
Mubarak akiwa na miaka 84 alihukumiwa kifungo
cha maisha jela.
Mzaliwa wa Misri mwaka 1928, Mubarak alikuwa
kamanda wa jeshi la anga la Misri kabla ya kuteuliwa kuwa makamu wa rais mwaka
1975 chini ya Rais Anwar Sadat. Baada ya Sadat kuuawa na Waislamu wakati wa
gwaride la jeshi jijini Cairo Oktoba 1981, Mubarak akawa rais wa nne wa Misri.
Miongo mitatu kama mtawala wa taifa la Kiarabu lenye watu wengi zaidi
ilitawaliwa na rushwa kubwa serikalini, vurugu za kisiasa na kudumaa kwa
uchumi. Katika utawala wake wote, Misri ilikuwa chini ya “utawala wa hali ya
hatari”, ukiipa nguvu serikali kukamata na kuwaeka watu vizuizini vila
kuwafungulia mashtaka. Ukatili wa polisi uliripotiwa.
Maandamano yaliyosababisha Mubarak kung’oka
yalianza Januari 25, 2011, wakati wananchi walipotaka aachie ngazi huku
wakiandamana katika mitaa mbalimbali ya Cairo na miji mingine.
No comments:
Post a Comment