INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
Mambo
yameanza, chuki baina ya makabila mawili makubwa nchini Rwanda – Wahuti na
Watutsi – imeshika kasi na mauaji yanaendelea. Lakini mapenzi nayo yanaingilia
kati. Je, nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako…
Kumbukumbu
hiyo ilimjia wakati yeye na wenzake wamebakiza mitaa mitatu tu kabla ya ule
alikoishi Judith, huku hiyo mitaa waliyokwishaipitia wakiwa wameziacha maiti
lukuki za Kitutsi, maiti ambazo Makella na wenzake walichekelea pale
walipoua kwa kutumia risasi, kunyonga
kwa mikono yao hata kwa kuchoma visu.
Ilikuwa
ni burudani kubwa kwao kushuhudia mtu akianguka chini na kukata roho kwa
maumivu japo baadhi ya hao wanauawa wakiomba
waachwe hai, wakitumia sauti za kusihi na macho ya kubembeleza.
Makella
na wenzake walifikia katika nyumba ya mzee Ndayishimiye saa 2 usiku, dhamira
yao ikiwa ni ileile, kukifutilia mbali kizazi cha Kitutsi katika ardhi ya
Rwanda. Wakiwa mbele ya nyumba ya mzee Ndayishimiye, walitulia, wakatazamana.
Dakika
iliyofuata ndipo wakachukua hatua na kufanikiwa kuingia ndani ambako walijikuta
kwenye varanda kubwa iliyosheheni sofa chakavu na mikeka. Eneo hilo lilitoa taswira
ya kuwa ni sehemu isiyo rasmi kwa wageni, zaidi palitumiwa na watoto au hata
watu wazima wa familia hiyo kwa kujipumzisha nyakati za mchana.
Mbele
kulikuwa na mlango mwingine. Na huo pia haukuwa umefungwa lakini pazia nene
lililojaa hapo liliwafanya Makella na wenzake wasiweze kuona ndani zaidi.
“Ni
humo,” hatimaye aliwaambia wenzake huku akitangulia kuelekea huko ndani.
Kama
awali, wenzake walimfuata.
**********
MZEE
Ndayishimiye na familia yake walikuwa ni Watutsi. Na zoezi la Makella na
wenzake lililenga kuwateketeza Watutsi pekee! Lakini Makella na kundi hilo
walipoifikia hii nyumba aliwahadharisha wenzake akiwaambia, “Humu kuna mwanamke
wangu…ninataka kumwoa! Huyo msimguse!”
“Ni
Mtutsi?!” mmoja wa watu waliomzunguka alimuuliza kwa mshangao.
“Ndiyo,
ni Mtutsi!” Makella alijibu kwa msisitizo, lakini sauti yake ikiwa ya chini.
Kauli
yake iliwafanya wenzake wote wamkodolee macho ya mshangao, wakionekana
kutoamini wakisikiacho.
“Unataka
kuoa Mtutsi?!” mwingine alimdaka.
“Hivyo
hivyo!” Makella aliwaka. “Hata kama sitamuoa, lakini ni afadhali hata…”
akaiacha sentensi hiyo ikielea.
Wenzake
wakakosa nguvu ya kuendeleza maswali au udadisi. Muda haukuwaruhusu. Wote
wakafuatana na kuingia kwa kishindo, bunduki zilizokamatwa na wawili zikiwa
zimewatangulia. Wenyeji wao walikuwa
mezani wakipata mlo wa usiku. Ilikuwa ni sebule yenye mvuto, sebule ambayo kwa
mgeni yeyote, wa hadhi yoyote lazima atajisikia burudani pindi
atakapokaribishwa.
Kulisheheni
samani aghali na zenye kuvutia. Seti
mbili za sofa zilikuwa zimeichukua robo tatu ya chumba hicho huku kabati kubwa
la vyombo vya kauri na televisheni kubwa ya kisasa, iliyokuwa kwenye kijimeza
chake maalumu vikiongeza ubora wa sebule hiyo. Pia kulikuwa na vijistuli kadhaa
hapa na pale vilivyowekwa kwa mpangilio mzuri na kuzidi kukifaharisha chumba
hicho.
Kule
alikokaa mzee Ndayishimiye na familia yake kulikuwa na meza kubwa na viti
maalum likiwa ni eneo maalum kwa maakuli. Kwa jumla ilikuwa ni sebule
iliyostahili kuitwa ‘sebule bora.”
Makella
na wenzake waliwakodolea macho yenye kila dalili ya kuua! Hawakuwa kama
binadamu wa kawaida, simama yao na tazama yao ilitosha kuonyesha kuwa wako
tayari kwa lolote na kwa yeyote
“Ni yule pale! Msimguse!” Makella alisema kwa
msisitizo huku akimnyooshea kidole mmoja wa wanafamilia hao, Judith.
Itaendelea kesho...
No comments:
Post a Comment