Joshua Nassari na Halima Mdee, mwaka 2012
Na Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Meru
UWEZEKANO wa kuwepo kwa ndoa baina ya mbunge kijana wa Chadema wa jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, na Mbunge wa Jimbo la Kawe (Chadema), Halima Mdee, umeota mbawa baada ya taarifa kubainisha kwamba Nassari sasa anatarajia 'kuvuta' jiko kesho katika kanisa moja huko Arumeru.
Mdada ambaye ameuvutia moyo wa Nassari ametajwa kwa jina na Anande Nko, na kwamba jana ndiyo ilikuwa 'Send Off' yake tayari kwa tukio kubwa la harusi.
Mahaba baina ya Nassari na Halima Mdee yalidaiwa kuchomoza mwaka 2012 wakati ule mbunge huyo akiwa ameteuliwa kuwania ubunge katika uchaguzi mdogo kufuatia kifo cha mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Solomon Sumari, ambaye pia alikuwa naibu waziri wa fedha.
Wakati wa kampeni zake, taarifa zilizagaa kwamba moyo wa Nassari ulikuwa umemdondokea Mdee na yeye mwenyewe hakuweza kulificha hilo.
Nassari alitangaza ndoa yake na Halima Mdee katika kipindi chote cha kampeni na hata baada ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo lake mwezi Aprili mwaka 2012.
Wachunguzi wa masuala ya siasa mkoani hapa wanasema hii pia ni mbinu mojawapo ya kujiandaa na kinyang’anyiro cha kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Katika uchaguzi uliopita, Nassari alipata shida kubwa sana kutoka kwa wapinzani wake waliodai kuwa kwa sababu ni kapera isingekuwa jambo la busara kwa wananchi wa jimbo hilo kumchagua.
Hatua hiyo ilisababisha mbunge huyo kuamua kumtangaza hadharani Mdee kama mchumba wake ambaye wangefunga naye ndoa mara tu baada ya kumalizika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
Hata baada ya ushindi wake, Nassari aliendelea kumnadi Halima Mdee kuwa ni mkewe mtarajiwa na anatarajia kufunga ndoa kubwa sana ambayo nayo ingeweza kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa kutoka ndani na hata nje ya Chadema.
Lakini baada ya uchaguzi huo mdogo kupita bado Nassari hakuweza kuizungumzia ndoa hiyo hali ambayo ilifanya wananchi wa jimbo hilo kubaki na mshangao.
Jitiada za kumpata mbunge azungumzie suala hilo ziligonga mwamba blogu hii kuwasiliana kupitia simu yake ya kiganjani na yeye kusema kwamba yuko kwenye kikao.
Aidha, blogu hii ilimtafuta Halima Mdee, lakini simu yake ya kiganjani haikuweza kupatikana.
Hii hapa ni habari iliyopamba magazeti Aprili 16, 2012:
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) amesema sasa yuko tayari kufunga ndoa na Mbunge mteule wa chama hicho wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
“Nafurahi kwamba Nassari hatimaye ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo,” alisema Mdee wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha na Meru juzi katika viwanja vya Leganga kusherehekea ushindi wa chama chake katika uchaguzi huo.
Mdee alifafanua, kwamba yeye na chama chake walikuwa wamebanwa na kampeni za kuhakikisha Chadema inatwaa jimbo la Arumeru Mashariki na ndiyo sababu hakujibu mara moja maombi ya Nassari ya kumwoa aliyoyatoa katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
“Naondoka kwenda Dar es Salaam kujiandaa kwa Mkutano ujao wa Bunge, kisha nitakwenda Dodoma ambako nitamsubiri Nassari na kwa pamoja tutafanya maandalizi,” alisema Mdee huku akishangiliwa na hadhira hiyo huku wakiimba na kucheza katikati ya mvua iliyokuwa ikinyesha.
Mdee alisema ndoa kati ya wabunge hao wawili wa Chadema ni wazo zuri na itatangazwa sana na kuandika historia.
Alipoona anashambuliwa sana na wapinzani wake juu ya useja wake katika kampeni hizo, Nassari hatimaye alitangaza kumwoa Mdee ambaye pia hajaolewa.
Na katika moja ya mikutano ya hadhara, alisimama naye jukwaani kukampeni.
“Kuna viongozi wengi wa kidini Dodoma, ikiwa ni pamoja na ndani ya Bunge ambao watatushauri jinsi ya kulitimiza hili,” alisema Mdee na kuongeza kwamba baba yake Joshua, Mchungaji Samuel Nassari alipata kusema, ‘mwanamke mzuri ni zawadi kutoka kwa Mungu’.
Chadema ina idadi kubwa ya wabunge vijana ambao hawajaoa, ikiwa ni pamoja na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’; wa Ubungo, John Mnyika; wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na sasa Nassari.
No comments:
Post a Comment