SOTE NI WATANZANIA
Ndugu
Viongozi wa vyama vya siasa nchini, wanachama wa vyama mbali mbali vya
siasa nchini, wadau mbali mbali wa siasa nchini na watanzania wote kwa
ujumla; tunapenda kuwasalimu kwa salamu inayoashiria mabadiliko na
uwazi!
Chama cha ACT-Tanzania kinapenda kuwapa
salamu hizi kufuatia wasi wasi ambao umekuwa ukioneshwa na baadi ya
Viongozi wa vyama vya siasa, wanachama wao na hata washabiki wao juu ya
ujio wa Chama kipya cha ACT-Tanzania.Kumekuwa na wimbi la baadhi ya watu
kutoka vyama kadhaa vya kiaisa kulalamika kwamba eti chama cha
ACT-Tanzania kimekuja kuwamaliza kisiasa.
Chama
cha ACT-Tanzania kinapenda kutuma salamu kwa vyama vyote vya siasa
nchini na wanachama wao kwamba; Chama cha ACT-Tanzania hakijaja
Kuvimaliza vyama vyao wala kupambana na mtu yeyote wala chama chochote
cha siasa nchini, bali kimekuja kupambana na matatizo sugu yanayomkabili
mtanzania kupitia misingi, falsafa na itikadi zake.ACT-Tanzania
imeanzishwa katika misingi yake yenyewe, Inajijenga katika misingi yake
yenyewe,Itajiimarisha katika misingi yake yenyewe, Itatembea katika
misingi yake yenyewe, Itasimama katika misingi yake yenyewe na kama ni
kuanguka; basi itaanguka kwa kutokusimamia misingi yake yenyewe.Uwepo wa
ACT-Tanzania hautegemei wala hautatagemea uwepo wa vyama vingine au
operesheni za vyama vingine.Kwa lugha nyingine ni kwamba uwepo wa
ACT-Tanzania hautategemea matukio bali misingi yake yenyewe.
Hata
hivyo, kwa kuwa lengo kuu la ACT-Tanzania ni kupambana na matatizo sugu
yanayomkabili mtanzania ambayo bado yanasumbua sana na kuleta machungu
katika maisha ya watu, ili kuleta unafuu na furaha katika maisha ya
mtanzania; lengo hili litafikiwa kwa ukamilifu wake kwa chama kupewa
mamlaka ya kuiongoza nchi.Mamlaka hayo yatatoka kwa wananchi
watakaoikubali misingi itikadi na falsafa za chama.Kwa kuwa katika
uchaguzi chama kinachoshinda ni kimoja, ni wazi kwamba ACT-Tanzania
itakaposhinda; vyama vingine vyote vitabaki kuwa vyama vya upinzani
wakati ACT-Tanzania ikisimamia itikadi yake na ikitekeleza sera zake
lakini hii haimaanishi kwamba ACT-Tanzania imekuja kuvipoteza vyama
hivyo katika sura ya siasa za Tanzania! kwani hilo sio lengo la msingi
la ACT-Tanzania.
Kadhalika tunafahamu kwamba
kutokana na ubora wa falsafa, misingi na itikadi za ACT-Tanzania,
Uwajibikaji,uwazi na uadilifu wa viongozi wa chama tulionao na
tutakaokuwa nao, wanachama wengi kutoka vyama vyote nchini, watakuwa
wakijiunga na ACT-Tanzania makundi kwa makundi.Hata hivyo hiyo haitakuwa
inamaanisha kwamba tuna uadui na vyama wanakotoka wanachama
hao.Tutafanya nini sasa! katika hali hiyo ndipo tunaposisitiza kwamba
itatupasa tuwe na uvumilivu wa kisiasa.Tunawashauri wale watakaoona
kwamba chama chetu kinafanya vizuri, wasitujengee uadui bali watuunge
mkono au watuvumilie tu.
Kuhusu watu wanaotumia
mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kudai kwamba wao ni
wana ACT-Tanzania, na chama hiki kimekuja kupambana na watu fulani
fulani, nao wanasema kwa niaba ya chama! na watu wanaotunga habari na
kudai zimesemwa na viongozi wakuu wa chama kwamba ACT-Tanzania imekuja
kwa lengo kuu la kuua vyama vya watu fulani,Tunawaomba watanzania
muwasamehe kwani kuna siku watajua kwamba wanachokifanya si sahihi na
wakarudi kwenye njia ya ukweli na ustaarabu.
Mwisho,
ACT-Tanzania kupitia Ofisi yake ya Mawasiliano na Uenezi, Inajenga na
itaendelea kuimarisha mahusiano na vyama vyote nchini kwa kadiri
itakavyowezekana kwani chama kinaamini kwamba sote ni watanzania na
zaidi ya hapo sote ni watu.Chama kinakaribisha na kinapokea ushauri
wowote kutoka kwa yeyote bila kujali chama chake, kitaupitia na
kuuchambua na kila itakapoonekana unafaa, utafanyiwa kazi.Chama kiko
tayari kushirikiana na yeyote anayependa ushirikiano katika mambo mema
na yenye tija kwa taifa.ACT- Tanzania bado ndio chama kidogo zaidi
nchini, hivyo badala ya kukiogopa; ni bora kukishika mkono ili
kuimarisha demokrasia.Kadhaalilika Chama kupitia Ofisi ya Mawasiliano na
uenezi, kitajenga na kuimarisha uhusiano na vyama mbali mbali duniani
hasa vile vyenye muelekeo wa "Mrengo wa Kati Kushoto".
Ikumbukwe kuwa ACT-Tanzania ni kwa ajili ya taifa la leo na kesho.
ACT- Tanzania ..............Taifa kwanza!,
Mabadiliko na uwazi...........Chukjua hatua!
Imetolewa na Ofisi ya Mawasiliano na Uenezi ya Dar es Salaam leo tarehe 05/06/2014.
No comments:
Post a Comment