INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
Mauaji
ya Watutsi yamefanyika, na mbaya zaidi Makella, anayeongoza mauaji hayo,
ameamuru wenzake waue wanafamilia wote katika nyumba na Mzee Ndaishimiye na
aliyesalia ni Judith peke yake ambaye yeye anadai kwamba anampenda. Anamchukua na
kuondoka kuelekea kambini huku akimuahidi makubwa wakati ‘watakapochukua nchi’.
Je, Judith atakuwa salama? Nini kitaendelea katika riwaya hii? Ungana na
msimulizi wako…
Judith
hakujibu. Hakuwa na akili ya kujibu chochote. Kwa ujumla hakuwa timamu kiakili
kwa wakati huo.
“Mpenzi,
utakuwa na gari!” Makella aliendelea. “Kwa ufupi utaishi kama uko paradiso, ukiwa ni mke wa mwanajeshi, na
mwanajeshi mwenyewe ni mwenye madaraka makubwa jeshini na ana pesa! Nani kama
wewe?”
Yote
hayo yalipenya masikioni mwa Judith kwa utulivu mkubwa. Eneo hilo lilikuwa
tulivu na askari wengine walikuwa
wametangulia mbele kwa kiasi cha hatua kama hamsini hivi, hivyo kila
alichokisema Makella kilipenya masikioni mwa Judith kwa usahihi mkubwa.
Judith
alimsikia lakini hakumwelewa, na hakuwa ni mtu wa kuelewa chochote kutoka kwa Makella wakati huo. Baba, mama na wadogo zake
wameuawa kikatili na hawa watu waliomteka! Halafu eti huyu mmojawao anamliwaza
kwa maneno laini na kumwahidi maisha bora!
Ni
maisha gani bora atakayopata chini ya himaya ya huyu mtu ambaye moyo wake hautofautiani
na ule wa fashisti Adolph Hitler aliyedhamiria kukiteketeza kizazi cha Waisraeli
katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia? Katika vita vile Hitler aliwaua Waisraeli
zaidi ya milioni 6, huyu Makella na wenzake katika haka kanchi kadogo sana,
tayari wameshaua maelfu ya watu kwa muda mfupi tu! Ni kwa nini wasifananishwe
na Hitler?
Eti
Makella anamrai kwa maneno matamu! Akilini mwa Judith hiyo ilikuwa ni ndoto
nyingine, ndoto isiyopendeza, ndoto mbaya zaidi iliyomtabiria kifo kibaya,
zaidi ya vifo vilivyowakuta wazazi wake na wadogo zake.
Wakati
huo walikuwa wamesimama, mkono mmoja wa Makella ukiwa begani kwa Judith na
mwingine ukimtomasa matiti.
“Na
leo hutalala kambini,” Makella aliendelea. “Tutakwenda Kiyovu Hotel. Mrembo
kama wewe haustahili kulala sehemu duni na kulala na watu wengine wasiokuwa na
mpango. Eti mpenzi?”
Kama
ambavyo awali hakujibu, safari hii pia Judith alibaki kimya. Lakini pamoj na hayo kwa mbali alihisi ujasiri ukimwingia.
Na alitambua kuwa umakini ulipaswa kupewa kipaumbele vinginevyo maisha yake pia
yatakatishwa na mtu huyo kama mzaha!
Akakumbuka
kuwa mara kadhaa, siku kadha wa kadha zilizopita, Makella alimtongoza lakini
hakumkubalia ombi lake. Sababu? Hakumvutia!
Ile sura yake yenye makovu na kichwa ambacho ni kama kilifinyangwa na
msanii mchanga, kikiwa hakitofautiani na mchoro wa msanii maarufu wa katuni, msanii
achoraye picha za kutisha au kuchekesha, vilikuwa ni vigezo vya awali
vilivyomshusha hadhi na kumfanya Judih asimfikirie
kwa namna yoyote.
Mhutu!
Kabila hilo nalo, kwa Judith lilikuwa ni kabila lisilokubalika wala kuthaminika
nafsini mwake, ni kabila lisilostahili kuwepo duniani! Ni kabila ambalo ni
hatari zaidi ya hatari yenyewe! ‘Nimvulie
nguo Mhutu! Tena Mhutu mwenyewe anayetisha zaidi ya kifo!’ alijisemea
kimoyomoyo kwa kujiapiza.
Ndiyo,
hakuwa radhi kuwa na uhusiano wowote na Makella, iwe ni kwa mapenzi ya muda
mfupi au hata ya kudumu. Lakini usiku huo yuko naye. Wako wawili tu! Tena mbali
na kwao Judith! Ni Makella huyuhuyu ambaye tangu mchana hadi usiku huo tayari
alishatoa roho za watu ambao hata idadi yao haikumbuki! Roho za Watutsi! Baba,
mama na wadogo zake Judith wakiwa miongoni mwao.
Afanye
nini?
Ujasiri
ulihitajika katika kuulinda msimamo wake na ilihitajika hekima katika kuchukua
uamuzi wowote atakaoona unafaa kwa kuilinda hadhi yake na kuulinda uhai wake.
Itaendelea kesho...
No comments:
Post a Comment