INNOCENT A.
NDAYANSE (ZAGALLO)
0755 040 520 /
0653 593 546
Mauaji
ya kinyama ya Rwanda yanaanza ambayo ndiyo yaliyozua vita ya kimbari. Mzee
Ndayishimiye anashuhudia watu wengine wakiuawa. Lakini mara anaona akivamiwa na
askari wenye bunduki ambao wanamuelekezea mtutu kifuani. Wakakonyezana kwa
ishara. Je, nini kitaendelea? Fuatilia riwaya hii ya kusisimua….
Mara
mlipuko mkubwa ukaitawala sebule hiyo. Risasi mbili zikazama kifuani mwa mzee
Ndayishimiye. Akakata roho huku akishangaa vilevile, macho kayakaodoa,
akiwatazama watu hao ilhali hawaoni!
Mchezo
haukuishia hapo! Ukahamia kwa wanafamilia wengine. Alianzwa Martha, binti wa
pili kuzaliwa, ambaye alikuwa akikimbilia kwenye miaka 18. Huyo alilishwa
risasi ya kichwa!
John,
Abel na Ndiyokubwayo ambao walikuwa na umri wa kati ya miaka saba na kumi, wao
kabla hata hawajajua ni kipi kilichotokea, risasi kadhaa zikazama miilini mwao.
“Mungu
wangu wee!” mke wa mzee Ndayishimiye aliomboleza, na kilikuwa ni kilio chake
cha mwisho; mmoja wa wanaume wale hakumchelewesha, alimmiminia risasi mbili
usoni, risasi zilizokifumua kisogo na kuumwaga ubongo nje huku mwenyewe
akiuangukia mwili wa mumewe taratibu.
Aliyebaki
hai ni Judith, ambaye kwa wakati huo aliduwaa, huenda hata akili yake haikuwa
na uwezo wa kufikiri chochote. Aliyakodoa macho akiwatazama wageni hao ilhali
hawaoni! Tonge la ugali alilokuwa amelishika kabla ya uvamizi huo lilibaki
limetulia mkononi vilevile!
“Simama!”
mmoja wa wale watu alimwamuru.
Alisikia,
hakuelewa. Kwa jumla alikuwa ameathirika kisaikolojia kwa kiwango kikubwa.
Alikuwa nusu mfu! Kilichofuata siyo amri tena bali kono la mtoa amri lilimshika
kwenye ukosi wa blauzi na kumnyanyua kimsobemsobe, akaburutwa akipelekwa nje.
Ikawa
ni kama tamthilia fulani isiyopendeza akilini mwa Judith.
********
JUDITH
alikuwa ni binti ambaye tayari alitosha kuyavuta macho ya mwanamume yeyote
mpenda wanawake wazuri. Kifua chake kidogo, kilichoyabeba matiti yenye ukubwa
wastani yaliyovutia, kilikuwa kivutio machoni mwa wengi. Mapaja makubwa, na miguu minene iliyomeremeta, pia zilikuwa ni
taswira kuwa muumba aliikamilisha kazi yake kwa upendo na labda hisia za
wanadamu wengine zikawa ni kwamba ameifanya kazi yake kwa upendeleo.
Isitoshe,
kichwa chake ambacho hakikustahili kuitwa kidogo au kikubwa kilifunikwa na
nywele nyingi nyeusi tii, nywele zilizomwagika hadi mabegani na kuuongeza mvuto
ambao wengi wa mabinti wa rika lake hawakuwa nao.
Macho
yake yaliyorembuka muda wote kama yabembelezayo, pua ndefu na mdomo mdogo
ulioyahifadhi meno meupe yaliyopangika vizuri, ni miongoni mwa vigezo vilivyompandisha katika
chati ya juu kiasi cha kuwapagawisha wanaume wengi, Wahutu kwa Watutsi.
Makella
ni mmoja wa wanaume waliomtazama Judith kwa ‘macho mia.’ Akiwa ni mzaliwa wa mchanganyiko wa makabila hayo
mawili makubwa nchini Rwanda, Makella alijisikia kumpenda na zaidi kumtamani
Judith. Naye, kama wanaume wengine waliomtamani na kumhitaji Judith, hakumwachia hivihivi; alimtamkia
maneno mawili, matatu lakini akaambulia majibu yasiyomridhisha, na zaidi
yalikuwa ni majibu ya kumkatisha tamaa:
“Shaa…hivi
unaniona-aje?”
“Sina
muda wa kupendana na mtu…”
“Nina
malengo yangu ya maisha kwanza kwa miaka mitatu hivi mbele…”
“Sijui
nina ugonjwa gani…sijui kupenda ni nini…labda mpaka nikaombewe kanisani…” na
kadhalika na kadhalika.
Ndiyo,
yalikuwa ni majibu ya kumkatisha tamaa, lakini hakuwa mtu wa kukata tamaa wala kukubali kushindwa. Alijali kuwa mtu mwenye uvumilivu,
asiye na papara, akiamini kuwa ipo siku atafanikiwa. Mama yake Makella alikuwa
ni wa uzao wa Kitutsi na baba, Mhutu. Lakini hadi Makella anafikisha umri wa
kuijua historia ya wazazi wake, wenyewe walikwishafariki kitambo kutokana na
uhasama na mapigano hayohayo ya kikabila.
Makella
akatunzwa na baba yake mdogo hadi alipofikia hatua ya kuwa jasiri asiyeogopa
chochote wala kumwogopa yeyote. Aliweza kuua kwa risasi, kisu, panga hata kwa
mikono!
Katika
mfumo huo wa maisha, kikafikia kipindi ambacho alimsahau Judith kwa muda,
Judith ambaye ni mwanamke pekee aliyetokea kumwingia moyoni tangu siku
alipomtia machoni kwa mara ya kwanza, siku ambayo timu ya taifa ya soka ya
Rwanda (Amavubi) ilipocheza na timu ya taifa moja la ukanda wa Afrika ya
Magharibi katika Uwanja wa Amahoro.
Ni
mchana huo wa maafa, siku ambayo ilianza kwa sekeseke la risasi kurindima huku
na kule, visu kuchomwa kwa hawa na wale, mapanga na kila aina ya silaha kutua
miilini mwa raia wengi, ndipo kumbukumbu kuhusu Judith ilipomjia Makella.
Itaendelea kesho...
No comments:
Post a Comment