Siku mbili baada ya kufariki kwa mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars na klabu za Simba na Sigara, Gabriel 'Gebo' Peter, mashabiki wa soka Tanzania wamepata pigo jingine baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF) Kanali Ally Hassan Mwanakatwe kufariki ghafla leo asubuhi.
Inaelezwa kwamba, marehemu Mwanakatwe alifariki dunia wakati akiwa njiani kukimbizwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, baada ya kuzidiwa ghafla wakati akiwa bafuni.
Sababu za kifo chake bado hazijajulikana na msiba uko nyumbani kwake Mbezi Beach.
Mwanakatwe alikuwa Katibu wa FAT kuanzia mwaka 1992 baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika Kibaha, ambao ulishuhudia Muhidin Ndolanga akiwa mwenyekiti na Makamu wake akiwa Masalu Ngofilo.
Alianguka kwenye uchaguzi uliozua mizengwe mikubwa wa mwaka 1996, ambapo nafasi hiyo ilichukuliwa na Ismail Aden Rage.
Alikuwa miongoni mwa makamanda wa jeshi waliopenda sana kuendeleza michezo na enzi zake yeye alikuwa mrusha tufe. Kuibuka kwa timu nyingi za jeshi hata kwenye ligi kuu kulitokana na hamasa kubwa ya makamanda kama Mwanakatwe, ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Makumbusho ya Jeshi yaliyoko maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen.
No comments:
Post a Comment