HOTUBA
YA WAZIRI WA FEDHA, MHESHIMIWA SAADA MKUYA SALUM (MB) AKIWASILISHA
BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA KWA MWAKA 2014/15
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa
hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi,
Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali
kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/15.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba ya
bajeti ya Wizara ya mwaka 2014/15. Aidha, natoa shukrani zangu za dhati
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Ninaahidi kwamba nitatekeleza
jukumu hili kwa weledi na uadilifu. Vile vile, nawapongeza Mhe. Mwigulu
Lameck Nchemba (Mb) na Mhe. Adam Kighoma Ali Malima (Mb) kwa kuteuliwa
kuwa Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha. Kadhalika, namshukuru pia
aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janeth Zebedayo Mbene (Mb) kwa
utendaji kazi wake mahiri na tunamuombea Mwenyezi Mungu ampe nguvu na
afya njema katika kazi zake mpya Wizara ya Viwanda na Biashara. Nichukue
pia fursa hii kumpongeza Bw. Rished M. Bade kwa kuteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe mwenyewe, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuongoza vyema majadiliano ya Bunge la Bajeti.
4. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuishukuru
kwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara
chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mbunge wa Kisesa) na
Makamu wake Mhe. Dunstan Luka Kitandula (Mbunge wa Mkinga) kwa maoni,
ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua
mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii
kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Mhe. Andrew John
Chenge (Mbunge wa Bariadi Magharibi) pamoja na Kamati nzima kwa ushauri
wao. Katika uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na
mapendekezo ya Kamati hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali
zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara kwa mwaka 2013/14.
5. Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, Wizara ilipata
pigo kwa kuondokewa na kiongozi wetu mkuu Marehemu Dkt. William
Augustao Mgimwa. Tunawashukuru Viongozi wa Serikali, Waheshimiwa
Wabunge, Washirika wa Maendeleo, Taasisi mbalimbali pamoja na wananchi
kwa ushirikiano waliotupa kipindi chote cha msiba. Tumeendelea kuenzi
misingi imara aliyotujengea marehemu katika kutekeleza majukumu ya
Wizara. Aidha, tunapenda kutoa pole kwa ndugu na jamaa
kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Chalinze Marehemu Saidi Ramadhani
Bwanamdogo. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
Amina.
6. Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza, Mhe. Yusuf
Salim Hussein Mbunge wa Chambani, Mhe. Godfrey William Mgimwa (Mbunge
wa Kalenga) na Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mbunge wa Chalinze) kwa
kuchaguliwa kwao.
7. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda
kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mhe. Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mpanda Mashariki kwa
hotuba yake nzuri ambayo imetoa mwelekeo wa shughuli za Serikali kwa
mwaka 2014/15.
8. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu nitaanza kuelezea
mapitio ya utekelezaji wa mipango ya Wizara katika mwaka 2013/14.
Nitaelezea pia mikakati mbalimbali ambayo Wizara imeweka kwa mwaka
2014/15 ili kuendelea kuboresha utekelezaji wa majukumu yake ya msingi
yakiwemo: usimamizi wa Bajeti ya Serikali; ukusanyaji mapato ya
Serikali; usimamizi wa misaada na mikopo; ulipaji wa Deni la Taifa;
usimamizi wa matumizi ya fedha za umma; usimamizi na udhibiti wa ununuzi
wa umma; usimamizi wa utekelezaji wa MKUKUTA; na usimamizi wa mashirika
na taasisi za umma.
9. Mheshimiwa Spika, mwisho
nitawasilisha bajeti ya mwaka 2014/15 kwa mafungu saba ya wizara ya
fedha ambayo ni fungu 7, 10, 13, 21, 22, 23 na fungu 50 pamoja na fungu
45 la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2013/14 NA MALENGO YA MWAKA 2014/15
10. Mheshimiwa Spika, uandaaji, utekelezaji na usimamizi
wa Mpango na Bajeti ya Wizara umezingatia malengo ya Mpango Mkakati wa
Wizara wa mwaka 2012/13 - 2016/17 ambao utaiwezesha Wizara kufikia
malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025; Mpango wa Maendeleo
wa miaka mitano 2011/12 - 2015/16; Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya
Milenia 2015; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) pamoja na
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma – PFMRP.
Aidha, Mpango na Bajeti ulizingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi ya Mwaka 2010 pamoja na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo
Makubwa (Big Results Now – BRN).
11. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara
ilipanga kutekeleza yafuatayo: kuongeza mapato ya ndani kufikia uwiano
wa Pato la Taifa wa asilimia 20.9 kwa mwaka 2013/14 ikilinganishwa na
asilimia 17.7 kwa mwaka 2012/13; kukamilisha Ripoti za Utafiti wa Mfumo
Bora wa Kodi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania; kuandaa na kusimamia utekelezaji wa bajeti ya Serikali;
kusimamia utekelezaji wa MKUKUTA-II; kufanya ukaguzi wa miradi ya
maendeleo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa watekelezaji wa miradi hiyo;
kukamilisha Sera ya Mali ya Umma; kufanya tathmini ya usimamizi na
utekelezaji wa malipo ya mishahara ya watumishi wa umma; kusimamia
utekelezaji wa mipango kazi ya ukaguzi na uzingatiwaji wa miongozo ya
ukaguzi katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, na
Mamlaka ya Serikali za Mitaa; kuratibu na kusimamia upatikanaji wa
misaada na mikopo nafuu kutoka Nchi Wahisani, Mashirika na Asasi za
Fedha za Kimataifa; kuidhinisha miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na
Binafsi (PPP); na kukamilisha Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma.
12. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi hicho, Wizara pia ilipanga kukamilisha miradi ya MCA-T na
kukabidhi miradi iliyokamilika kwa taasisi husika; kusimamia utekelezaji
wa Mpango Mkakati wa Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za
Umma Awamu ya nne (PFMRP IV); kufanya uhakiki wa Wastaafu waliopo katika
Daftari la Pensheni la Hazina; kuunganisha Hazina Ndogo na Sekretarieti
za Mikoa 24 katika mfumo wa malipo kwa njia ya elektroniki kupitia
Benki Kuu ya Tanzania (Tanzania Inter- Bank Settlement System - TISS); kuimarisha utendaji kazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina; na kuandaa na kuhuisha kanuni na miongozo ya utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi.
Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa
13. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, kupitia
Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Wizara ya Fedha katika maabara ya
utafutaji wa rasilimali fedha iliwekewa malengo yafuatayo: kuongeza
mapato mapya ya kodi ya shilingi trilioni 1.16; kuongeza mapato mapya
yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 96.7; kudhibiti matumizi; na kutafuta
fedha za utekelezaji wa miradi ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa
katika sekta zinazotekeleza miradi hiyo.
14. Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili 2014, ukusanyaji
wa mapato kutoka vyanzo vilivyoibuliwa chini ya BRN umefikia shilingi
bilioni 338 sawa na asilimia 29.14 ya lengo la kukusanya shilingi
trilioni
1.16. Matokeo
yasiyoridhisha yalisababishwa na baadhi ya mapendekezo ya BRN
kutokutekelezwa katika mwaka 2013/14. Mapendekezo hayo ni kubadilisha
mfumo wa ushuru wa bidhaa zisizo za petroli kutoka specific kwenda
advalorem (makisio shilingi bilioni 386) na kuanzisha kodi ya zuio ya
asilimia tano kwenye bidhaa zinazotoka nje ya nchi (makisio shilingi
bilioni 225.6). Kwa vile ukusanyaji wa mapato ndio msingi wa kufanikiwa
kwa BRN, Serikali inachambua vyanzo mbadala vya kufidia mapato haya ili
kuhakikisha lengo kuu la kuongeza mapato kwa shilingi trilioni 3.48
linafikiwa ifikapo mwaka 2015/16.
Mwenendo wa Uchumi
15. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara kupitia Benki Kuu iliendelea na jukumu la
kuandaa, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga
kuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei kwa ajili ya kuhakikisha
gharama za maisha haziongezeki. Kutokana na juhudi hizi, mfumuko wa bei
umeshuka kutoka wastani wa asilimia 16 mwaka 2012 hadi kufikia wastani
wa asilimia 7.9 mwaka 2013. Katika kipindi hiki uchumi umeendelea
kuimarika huku ukuaji halisi wa Pato la Taifa ukiongezeka kwa asilimia
7.0 katika kipindi cha mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 6.9 katika
mwaka 2012. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kiasi kikubwa ni pamoja
na mawasiliano asilimia 22.8, huduma za kifedha asilimia 12.2, ujenzi
asilimia 8.6, na uuzaji bidhaa wa jumla na rejareja asilimia 8.3. Katika
mwaka 2014/15, Wizara kupitia Benki Kuu itaendelea kushirikiana na
wadau wote katika kuhakikisha kwamba lengo la msingi la utulivu wa bei
na ukuaji wa uchumi linadumishwa.
Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali
16. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara imeratibu uandaaji wa Mwongozo wa Mpango na
Bajeti kwa kipindi cha 2014/15 – 2016/17 kwa Wizara, Idara
zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kusambaza kwa
wadau mwezi Desemba kama ilivyopangwa.
Aidha, Wizara imeandaa na kuchapisha vitabu vya bajeti ya Serikali vya
mwaka 2014/15 (Volume I, II, III na IV) kama vilivyowasilishwa Bungeni
kwa ajili ya mjadala wa Bunge la Bajeti la mwaka 2014/15 unaoendelea;
kitabu cha tafsiri rahisi ya bajeti ya Serikali (Citizen’s Budget) kwa
mwaka 2013/14; na Kitabu cha Budget Background and Medium Term Framework – 2013/14 – 201 5/16.
17. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuanza kutumia
mfumo wa Programu katika uandaaji, uidhinishaji na utekelezaji wa
Bajeti. Mfumo huu utasaidia Serikali kugawa rasilimali kwa kuzingatia
matokeo na kuweka viashiria vya kufikia malengo. Katika hatua za awali
za maandalizi ya utekelezaji wa mfumo huu katika mwaka 2013/14, Wizara
ilitenga fedha kwa ajili ya mafunzo kwa wataalam wa Wizara nane za
mfano. Maandalizi haya ya kimkakati na kimfumo yataendelea katika mwaka
2014/15. Wizara zilizotengwa kwa majaribio na ambazo tayari zimefanyiwa
mafunzo ni Wizara ya Maji, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara
ya Kilimo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya
Fedha. Wizara hizi kwa sasa zinaendelea na zoezi la kuandaa programu na
viashiria vya kupima utekelezaji kabla ya mfumo kuanza kutumika.
18. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu kikao kazi cha
wataalamu wa wizara, mikoa na halmashauri kuhusu mfumo wa ufuatiliaji,
tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Bajeti. Katika kipindi
hicho, Wizara
pia ilifanya kikao kazi kilichohusisha washiriki kutoka wizara, idara
za Serikali zinazojitegemea, mikoa na Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa kwa lengo la kutathmini uandaaji na uwasilishwaji wa Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2012/13 na kufanya mkutano wa mwaka wa wadau ambao
ulijumuisha Washirika wa Maendeleo kwa lengo la kutathmini utekelezaji
wa Bajeti ya Serikali.
19. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia na kudhibiti
utekelezaji wa bajeti ya Serikali ikiwemo kufuatilia matumizi ya fedha
za umma, Wizara ilifanya ufuatiliaji na ukaguzi wa matumizi ya fedha
zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwa miradi ya ASDP na DASIP
ikihusisha wizara nne, mikoa sita na halmashauri 33. Aidha, ufuatiliaji
na ukaguzi ulifanyika kwa mapato na matumizi ya Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) na kwa fedha zilizotolewa kuhudumia
vituo 16 vya Makazi ya Wazee katika mikoa 14 nchini.
20. Mheshimiwa Spika, katika ukaguzi huo, Wizara ilibaini
kuwapo kwa upungufu na changamoto katika maeneo haya ikiwa ni pamoja
na: fedha kutowafikia walengwa kwa wakati kama ilivyopangwa; udhaifu
kwenye udhibiti wa ndani wa matumizi na hivyo kusababisha kuwapo kwa
huduma duni; na miradi kutokamilika kwa wakati na kuwepo kwa bakaa ya
fedha za maendeleo. Aidha, zimekuwepo changamoto za kubadilika mara kwa
mara bei ya kununulia nafaka na gharama za usafirishaji, hivyo kuathiri
malengo yaliyopangwa ikiwemo kusababisha madeni. Wizara imewasiliana na
wahusika na kutoa nyaraka za maelekezo ya kuhakikisha kwamba udhibiti wa
ndani wa matumizi unaimarishwa katika ngazi zote za usimamizi na inapobidi hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.
21. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara inatarajia kutekeleza yafuatayo: kupitia mfumo wa
uwasilishaji wa bajeti za wizara, idara za Serikali, mikoa na
halmashauri na kuhakikisha kuwa sera na mipango ya kitaifa na ile ya
kisekta vyote vimezingatiwa ipasavyo katika Bajeti ya Serikali na
kutengewa fedha; kufanya tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali,
kuendelea kuboresha mfumo wa mpangilio wa Bajeti ya Serikali kwa
kuzingatia programu mbalimbali; kuimarisha mifumo ya kompyuta ya
uandaaji bajeti ili kukidhi mahitaji ya taarifa mbalimbali
zinazohitajika; kuendelea kujenga uwezo wa wizara, idara za Serikali,
mikoa na halmashauri katika uandaaji wa Bajeti ya Muda wa Kati,
usimamiaji wake na utoaji taarifa za utekelezaji ikiwa ni pamoja na
ufuatiliaji na tathmini kwa wakati; kutayarisha taarifa mbalimbali za
utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji
unazingatiwa; na kufuatilia matumizi ya fedha za umma zikiwemo fedha za
mishahara, matumizi mengineyo na fedha za miradi.
Usimamizi wa Misaada na Mikopo
22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara
ilifanikisha kusainiwa kwa mikataba 18 kwa ajili ya misaada na mikopo
nafuu yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 958.027 kutoka kwa
Washirika wa Maendeleo. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu ukamilishaji
wa Mwongozo mpya wa Ushirikiano wa Maendeleo - Development Cooperation Framework ambao utachukua nafasi ya Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA). Mwongozo huu una lengo
la kusimamia ushirikiano wa maendeleo baina ya Serikali na Wadau wa
Maendeleo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji
wa MPAMITA. Lengo la ujumla ni kupatikana ufanisi katika misaada kutoka
kwa Washirika wa maendeleo na kubainisha wajibu wa kila mdau wa
maendeleo wakiwemo raia, wabunge, asasi zisizo za kiserikali na sekta ya
habari.
23. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kuzindua Mwongozo wa
Ushirikiano wa Maendeleo na kuandaa mpango kazi wake pamoja na
kuhamasisha matumizi yake kwa Washirika wa Maendeleo, Wizara, Idara
Zinazojitegemea, Serikali za Mitaa, Taasisi Binafsi na Waheshimiwa
Wabunge; kutathmini utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali
inayotekelezwa kwa fedha toka Washirika wa Maendeleo kwa nia ya
kuhakikisha kwamba thamani ya fedha inapatikana katika miradi hiyo;
kushiriki kwenye majadiliano na Jumuiya za kikanda na kimataifa; na
kuendelea kutafuta fedha za misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na Misaada ya Kiufundi kutoka kwa
Mashirika ya Kimataifa na nchi wahisani.
24. Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeendelea kusimamiwa
na Sheria ya Madeni ya mwaka 1974 na marekebisho yake ya mwaka 2004.
Wizara imeendelea kutoa kipaumbele katika ulipaji wa madeni kwa wakati
ili kuepuka malimbikizo ya riba. Katika kipindi cha Julai, 2013 hadi
Aprili, 2014 malipo ya deni la ndani yalifikia shilingi bilioni 1,694.53
ambapo kati ya malipo hayo riba ni shilingi bilioni 581.20 na Mtaji
(principal rollover) ni shilingi bilioni 1,113.33. Aidha, deni la nje
limelipwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 340.22, kati ya kiasi hicho
malipo ya riba ni shilingi bilioni 201.52 na deni halisi - principal ni shilingi bilioni 138.70.
25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara
itaendelea kulipa madeni ya ndani na nje kwa wakati ikiwa ni pamoja na
kulipa kwa wakati madeni mbalimbali ambayo serikali imeingia mikataba
(Contractual Liabilities) na madai ya dharura (Contingent Liabilities)
pindi yanapotokea.
Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
26. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kujenga uwezo wa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma kwa
kudhamini mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 313 wa kada ya uhasibu,
ugavi na kompyuta kutoka kwenye wizara, idara za serikali, sekretariati
za mikoa, manispaa, halmashauri za miji na wilaya waliopo vyuoni na
watumishi 218 walipewa mafunzo ya muda mfupi kwa lengo la kuongeza
ufanisi katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma. Aidha, Wizara imeendelea kusambaza Mfumo wa Malipo wa Kielektroniki -TISS mikoani
ambapo hadi sasa jumla ya mikoa 20 imeunganishwa katika mtandao huo.
Mikoa iliyounganishwa kwenye mtandao huo ni Iringa, Morogoro, Pwani,
Tanga, Kilimanjaro, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Lindi, Simiyu, Mwanza, Kagera,
Geita, Mara, Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Njombe, Dar es Salaam na
Katavi. Vile vile, mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Katavi na Njombe
imeunganishwa kwenye mtandao wa malipo wa Serikali (Intergrated
Financial Management System).
27. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na mpango
wa kutekeleza mfumo wa uandaaji wa taarifa za hesabu kwa kuzingatia
Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Hesabu katika Sekta ya
Umma - IPSAS Accrual Basis ambapo hesabu za majumuisho za mwaka
2012/13 zimeandaliwa kwa kutumia mfumo huo kwa mara ya kwanza na
kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa
wakati.
28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, pamoja
na mambo mengine, Wizara itaendelea kuboresha usimamizi wa fedha za
umma kwa kufanya yafuatayo: kuendelea kutoa udhamini wa masomo ya muda
mrefu na mfupi kwa wahasibu, wakaguzi, maafisa ugavi na wataalamu wa
kompyuta kutoka Serikali Kuu na serikali za mitaa; kuweka mitambo katika
hazina ndogo zote ili kuwezesha sekretariati za mikoa na hazina ndogo
kufanya malipo kwa kutumia mifumo ya malipo ya kielektroniki -TISS/EFT; kuendelea kutoa mafunzo ya TISS/EFT kwa
wahasibu na watumishi wa kada zingine ili kuimarisha mfumo wa malipo;
na kuanza ujenzi wa jengo la ofisi ya Hazina Ndogo Arusha.
29. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15 ili kuinua kiwango cha fani ya uhasibu sambamba na
kuimarisha usimamizi wa fedha za umma Tanzania itakuwa mwenyeji wa
mkutano wa Wahasibu Wakuu wa Serikali wa nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika – ESAAG.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma – Public Finance Management Reform Programme (PFMRP)
30. Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma
imekamilisha utafiti wa mfumo wa kupeleka fedha kwenye Serikali za
Mitaa, mpango wa utekelezaji wa utafiti huo umeandaliwa na utekelezaji
wake utaanza mwaka wa fedha 2014/15. Aidha, utafiti juu ya mifumo ya
fedha inayotumiwa na Serikali kwa lengo la kuiunganisha mifumo hiyo ili
kuboresha usimamizi wake umekamilika. Vile vile, Wahasibu 522 kutoka
Wizara mbalimbali, hazina ndogo na sekretarieti za mikoa walipata
mafunzo juu ya Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Hesabu
katika Sekta ya Umma na watumishi wengine 34 ambao wanasimamia programu
hii kutoka katika wizara na taasisi walipata mafunzo ya kusimamia
Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change Management and Strategic Planning. Mafunzo haya yalilenga kuwajengea uwezo wa kuandaa mipango na bajeti inayolenga katika kutekeleza maboresho ya usimamizi wa fedha za umma.
31. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuboresha usimamizi wa fedha za umma
kwa kuendelea na utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Programu ya PFMRP kwa
kufanya yafuatayo: kupitia na kuboresha mifumo ya kifedha na kuangalia
njia bora ya kuiunganisha baada ya utafiti kukamilika; na kuwajengea
uwezo wakaguzi wa ndani katika wizara, idara, wakala za Serikali na
halmashauri za Serikali za Mitaa juu ya ukaguzi wa mifumo ya fedha,
usimamizi na ukaguzi wa vihatarishi, ukaguzi wa bajeti na mishahara, na
ukaguzi wa miradi.
Sera ya Ununuzi wa Umma
32. Mheshimiwa Spika, katika
kusimamia Sekta ya Ununuzi wa Umma nchini, Wizara imeendelea kutekeleza
yafuatayo: kuandaa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; kuandaa
mapendekezo ya muundo wa Vitengo vya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi
Serikalini; na kufanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo kwa maafisa
ununuzi na ugavi walioko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; na
kuendelea kuhuisha taarifa za maafisa ununuzi na ugavi Serikalini,
ambapo taarifa za maafisa 332 katika mikoa ya Shinyanga, Kagera, Mwanza
na Mara zimehakikiwa na kuingizwa katika daftari la maafisa ununuzi na
ugavi.
33. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kuandaa Mkakati wa
Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma na kusimamia utekelezaji
wa Sera hiyo; kuhuisha muundo wa vitengo vya usimamizi wa ununuzi na
ugavi serikalini; kuipitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.7 ya mwaka 2011
na kanuni zake za mwaka 2013; kukamilisha tathmini ya mahitaji ya
mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi Serikalini; na kufanya tathmini juu
ya ufanisi wa ununuzi wa umma nchini.
Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
34. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
imetoa mafunzo kuhusu sheria, kanuni na taratibu za ununuzi kwa taasisi
za umma 32 ambapo watumishi 747 walihudhuria mafunzo hayo. Aidha,
Mamlaka ilitoa mafunzo kuhusu mfumo wa upokeaji na usimamizi wa taarifa
za ununuzi nchini katika vituo vinne vya Morogoro, Arusha, Mwanza na
Mbeya ambapo jumla ya washiriki 330 kutoka taasisi 191 walishiriki. Vile
vile, Mamlaka imeendelea kusimamia mfumo wa upokeaji na usimamizi wa
taarifa za ununuzi nchini ambapo katika kipindi hicho, taasisi 191
ziliunganishwa na kupatiwa mafunzo ya kutumia mfumo huo na hivyo kufanya
jumla ya taasisi zilizounganishwa na kupatiwa mafunzo kufikia 364, sawa
na asilimia 80 ya taasisi zote.
35. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti
wa Ununuzi wa Umma imefanya ukaguzi kuhusu utoaji wa zabuni na
utekelezaji wa mikataba itokanayo na ununuzi wa umma katika Taasisi 120
zikiwemo wizara na idara zinazojitegemea 32, mashirika ya umma 46 na
serikali za mitaa 42. Ukaguzi huu uilihusisha mikataba 5,867 yenye
thamani ya shilingi bilioni 1,985.427 ikiwemo miradi 207 ya ujenzi yenye
thamani ya shilingi bilioni 777.2. Ripoti ya ukaguzi inaonesha wastani
wa uzingatiwaji wa sheria ya ununuzi ulikuwa ni asilimia 64 ambayo ni
chini ya lengo la asilimia 80. Maeneo yaliyobainika kuwa na udhaifu
mkubwa ni katika usimamizi wa mikataba na utunzaji wa nyaraka za
ununuzi.
36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara
imepanga kutekeleza yafuatayo: kuandaa mpango kazi wa usimamizi wa
utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011; kuelimisha wadau
mbalimbali kuhusu Sheria mpya na kanuni zake; kuendelea na maandalizi
ya kuanzisha mfumo wa ununuzi kwa njia ya kielektronic (e-procurement
system); kufungua ofisi za kanda Dodoma, Mbeya na Mwanza; kushirikiana
na TAMISEMI ili kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye vitengo vya
ununuzi vya halmashauri mbalimbali; kufanya kazi na Asasi za Kiraia na
Wanahabari ili kuongeza uelewa wa masuala ya Ununuzi wa Umma kwa
wananchi; na kuendelea kusimamia ununuzi katika sekta ya Umma.
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara
kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini imetekeleza yafuatayo:
kuongeza vifaa vya huduma mtambuka kutoka 86 vilivyokuwepo hadi 181;
kuendelea na ujenzi wa Ofisi na ghala katika mkoa wa Manyara; kuendelea
na ujenzi wa kituo cha mafuta mkoa wa Dodoma; na kununua magari mawili
makubwa yenye uwezo wa kubeba lita 45,000 za mafuta kila moja kwa ajili
ya kusafirisha mafuta toka kwa wazabuni kwenda mikoani. Aidha, Wakala wa
Huduma ya Ununuzi Serikalini, imeanza kufunga Mfumo wa Udhibiti na
Usimamizi wa Mafuta ya Magari ambao utaanza kwa majaribio Agosti, 2014
katika mkoa wa Dar es Salaam ili kudhibiti matumizi ya mafuta katika
magari ya Serikali.
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara
kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini imepanga kutekeleza
yafuatayo: kukamilisha kazi ya kufunga Mfumo wa Udhibiti na Usimamizi wa
Mafuta ya Magari katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma, Iringa na
Mbeya; kuanza kazi za Ujenzi wa Ofisi katika mikoa ya Njombe na Mara;
kukamilisha ujenzi wa visima vya mafuta katika mikoa ya Geita, Katavi na
Wilaya ya Ileje; na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kufikia wastani
wa lita 50,000 katika vituo vya mikoa ya Arusha, Mwanza, Kigoma, Mtwara,
Lindi, Tabora, Pwani, Tanga na Ruvuma. Aidha, Wakala wa Huduma ya
Ununuzi Serikalini itahuisha muundo wake ili kuweza kutoa huduma ngazi
ya wilaya na kuanza kutekeleza utaratibu wa ununuzi wa magari kwa pamoja.
Rufaa za Zabuni za Umma
39. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma imepokea jumla ya
mashauri 35, kati ya hayo mashauri matatu yaliondolewa na walalamikaji
kabla ya kusikilizwa; mashauri 17 walalamikaji walishinda; mashauri 11
walalamikaji walishindwa; mashauri mawili yalifutwa kufuatana na sheria;
shauri moja halikutolewa uamuzi kutokana na ukomo wa muda wa
kulisikiliza; na shauri moja lipo kwenye hatua ya kusikilizwa. Aidha,
katika mwaka 2014/15, Mamlaka itaendelea kusikiliza na kutolea maamuzi
malalamiko na rufaa katika Ununuzi wa Umma na kuelimisha umma na wadau
juu ya kuwasilisha pingamizi za zabuni kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi
wa Umma ya mwaka 2011.
Usimamizi wa Mali ya Serikali
40. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/14, Wizara iliendelea kuandaa Sera ya Mali ya Umma.
Lengo la sera hii ni kusimamia na kutoa miongozo ya udhibiti wa mali ya
umma. Aidha, Wizara ilifanya uthamini wa mali ya Serikali katika mikoa
mitano na wizara mbili, hivyo kufanya wizara, idara zinazojitegemea na
wakala wa Serikali zilizofanyiwa uthamini kufikia 42. Katika kipindi
hicho, usimikaji wa mfumo wa uhakiki wa mali ya umma ulikamilika. Vile
vile, Wizara iliendelea na zoezi la kuondosha mali chakavu
katika wizara na idara za Serikali ambapo jumla ya shilingi bilioni
1.58 zilikusanywa kutokana na mauzo ya vifaa hivyo na shilingi milioni
12.83 kutokana na utoaji wa leseni za udalali.
41. Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya uhakiki wa mali
ya Serikali katika wizara, idara zinazojitegemea na wakala za Serikali
kwa lengo la kudhibiti matumizi ya mali katika taasisi hizo. Aidha,
Wizara imefanya uhakiki maalum katika Bohari Kuu ya Madawa ambapo
ushauri ulitolewa wa namna ya kupunguza hasara inayotokana na madawa,
vifaa tiba na vitendanishi kuisha muda wake wa matumizi kabla ya
kutumika.
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka, 2014/15, Wizara
imepanga kukamilisha Sera ya Mali ya Umma na kuisambaza kwa wadau kwa
ajili ya kupata maoni kabla ya kuanza utekelezaji wake. Aidha, Wizara
imepanga kufanya uthamini wa mali katika mikoa saba na taarifa zake
kuingizwa kwenye Daftari la Mali ya Serikali. Vile vile, Wizara
itaendelea kuondosha mali chakavu, mali zilizokwisha muda wake na vifaa
sinzia kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha za Umma; kushughulikia
taarifa za ajali na potevu za mali ya Serikali; na kuendelea kuchambua,
kufanya majadiliano na wadai na kulipa madai ya fidia na kifuta machozi
yanayotokana na amri ya Mahakama. Kadhalika, Wizara itaendelea na
uhakiki wa mali katika wizara, idara zinazojitegememea na wakala za
Serikali.
Mpango wa Millenium Challenge Account – Tanzania (MCA-T)
Ukaguzi wa Ndani
44. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2013/14, Wizara imetekeleza yafuatayo: kutoa Mwongozo wa Kamati
za Ukaguzi katika Sekta ya Umma kwa lengo la kuhakikisha utendaji wenye
tija kwa Kamati zote za Ukaguzi; kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo
wakaguzi wa ndani 458, wajumbe wa Kamati za Ukaguzi na wadau wa ukaguzi
wa ndani wapatao 567; kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo 11; ukaguzi
wa orodha ya malipo ya mishahara; na kuhakiki madai mbalimbali
yaliyowasilishwa wizarani kabla ya kulipwa.
45. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza juhudi za Serikali
za kudhibiti ubora wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,
Wizara imenunua vifaa vya kuhakiki ubora wa miundombinu. Vifaa hivyo
vitatumika katika ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Wizara, Idara,
Wakala za Serikali na Halmashauri za Serikali za Mitaa katika
kuhakikisha kuwa miradi na miundombinu inayotekelezwa inakuwa na ubora
unaokidhi viwango na hatimaye kupata thamani ya fedha. Hatua hii itaenda
sambamba na kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani Serikalini katika
kufanya ukaguzi wa kiufundi kwa miradi inayotekelezwa katika taasisi
zao.
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara
itaendelea kusimamia kada ya ukaguzi wa ndani na kamati za ukaguzi;
kufanya ukaguzi wa Mfumo wa ulipaji Mishahara Serikalini; kuhakiki madai
mbalimbali ya Serikali kabla ya kuyalipa; na kufuatilia utekelezaji wa
miongozo mbalimbali iliyotolewa. Aidha, Wizara inatarajia kutoa miongozo
ifuatayo: Mwongozo wa Usimamizi wa Viashiria Vya Udanganyifu; Mwongozo
wa Udhibiti wa Ndani; Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Usimamizi
wa Vihatarishi; Mwongozo wa Ukaguzi wa Ununuzi; na Mwongozo wa Ukaguzi
wa Mikataba. Vile vile, wizara kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali
itaendelea kuimarisha ofisi za Mkaguzi Mkuu wa ndani kwa lengo la
kusimamia matumizi ya fedha.
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Ofisi ya
Taifa ya Ukaguzi imetekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria. Ofisi
imeendelea kuwa mshirika katika Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa
katika kukagua taasisi za Umoja wa Mataifa. Aidha, Ofisi imeendesha
mafunzo kwa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali na Kamati ya
Bajeti kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kuimarisha uwajibikaji na
utawala bora. Vile vile, ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vya
siasa vyenye usajili wa kudumu unaendelea.
48. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuondoa wakaguzi
katika majengo ya wakaguliwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imekodi majengo
ya ofisi katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Tanga, Iringa, Kagera na
Geita. Aidha, ujenzi wa ofisi katika mkoa wa Dodoma unaendelea ukiwa
katika hatua za mwisho. Vile vile, Ofisi imeendelea na uunganishaji wa
ofisi zake zilizoko mikoani na makao makuu kwa njia ya mtandao mpana.
Kwa mwaka huu ofisi 4 zimeunganishwa na hivyo kufanya ofisi
zilizounganishwa kufikia 14.
49. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/15, Ofisi inatarajia
kufanya yafuatayo: kukagua mafungu yote 49 ya Wizara na Idara za
serikali, hesabu za Mikoa yote 25 ya Tanzania Bara, Hesabu za
Halmashauri zote 161 za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, Mashirika ya
Umma 177, Balozi zote 32 zilizoko nje ya nchi na Wakala 33 za Serikali
pamoja na kufanya ukaguzi wa thamani ya fedha katika maeneo sita;
kuendelea na ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vyote vya siasa;
kuanza ukaguzi katika sekta ya gesi na mafuta pamoja na ukaguzi
wa miradi mikubwa inayoendeshwa kwa ubia wa sekta ya Umma na Sekta
binafsi; kuendelea kushiriki kikamilifu katika jukumu la kukagua taasisi
za Umoja wa Mataifa sanjari na wanachama wengine wanaounda Bodi ya
Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.
50. Mheshimiwa Spika, mambo
mengine yatakayotekelezwa katika mwaka 2014/15, ni pamoja na: kuendelea
na zoezi la kuwaondoa wakaguzi katika maeneo ya wakaguliwa katika
wizara zote na katika mikoa 6 iliyobaki; kuendelea kuzijengea uwezo kwa
njia ya mafunzo Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali na
Kamati ya Bajeti katika maeneo ya kuelewa kwa undani taarifa za ukaguzi
wa hesabu zinazoandaliwa na wakaguliwa; kukamilisha ujenzi wa ofisi
katika mkoa wa Rukwa pamoja na kuanza ujenzi wa ofisi katika mikoa ya
Mara na Iringa; na kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuimarisha uwezo wao
katika kutumia mfumo wa TeamMate ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika ukaguzi wa kisasa.
Uratibu wa Utekelezaji wa MKUKUTA
51. Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kuratibu utekelezaji wa MKUKUTA II kwa kufanya ufuatiliaji,
tafiti, na tathmini na kuandaa taarifa ya utekelezaji na hali ya
Umaskini nchini ili kuwezesha maamuzi ya kisera, kibajeti na
kiutekelezaji. Kazi ya uandaaji wa Taarifa ya Mwaka ya Utekelezaji wa
MKUKUTA II imekamilika na kuwekwa katika tovuti ya Wizara. Aidha, Wizara
inaendelea kukamilisha Taarifa ya Maendeleo
ya Malengo ya Milenia. Taarifa ya awali inaonesha kuwa umaskini wa
mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara ni asilimia 28.2 ambapo kwa Dar es
Salaam ni asilimia 4.2, maeneo mengine ya mjini ni asilimia 21.7 na
maeneo ya vijijini ni asilimia 33.3. Umaskini wa chakula ni asilimia 9.7
ambapo kwa Dar es Salaam ni asilimia 1.0, maeneo mengine ya mjini ni
asilimia 8.7 na maeneo ya vijijini ni asilimia 11.3.
52. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/15, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: kukusanya na
kuchambua taarifa mbalimbali kutoka katika Wizara, Idara na Wakala za
Serikali ili kuandaa Taarifa ya mwaka ya Utekelezaji wa MKUKUTA II;
kuandaa taarifa ya mwisho ya kutathimini utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia; kufanya mapitio ya MKUKUTA II; kukamilisha Mpango
wa Utekelezaji wa Kinga ya Jamii pamoja na kuainisha viashiria vya
upimaji juhudi za kinga ya jamii; na kuratibu mkutano wa kitaifa
wa kujadili sera za kupambana na Umaskini nchini. Pia Wizara kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali inaandaa mapendekezo ya hatua
zitakazofuata baada MKUKUTA II kufikia kikomo mwezi Juni, 2015.
53. Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Mradi wa SELF II imeendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali
ambapo hadi kufikia Aprili 2014, mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 8.6 ilikopeshwa kwa wajasiriamali 4,943 kupitia Asasi ndogo 103.
Kati ya waliokopeshwa, wanawake ni 2,040 sawa na asilimia 41 na wanaume
ni 2,903 sawa na asilimia 59. Kwa wastani, urejeshwaji wa Mikopo ya
Mradi wa SELF umeendelea kuwa wa ufanisi
No comments:
Post a Comment