JUMAMOSI
iliyopita (Mei 31), palifanyika jambo moja kihistoria, pale familia ya
mwimbaji nyota wa zamani Hemed Maneti, ilipoandamana na wadau wa
wamuziki wa dansi kutembelea hospitali ya Mwananyamala ambako ndiko
alipougulia mwimbaji huyo hadi kufariki dunia miaka 24 iliyopita.
Maneti
alifariki katika hospitali hiyo tarehe 31 Mei 1990 baada ya kuugua kwa
muda mrefu na kwenda kuzikwa kijijini kwao Mamboleo, wilaya ya Muheza
mkoani Tanga.
Familia
hiyo na wadau hao wa muziki wa dansi, ikaitumia tarehe hiyo ya
kumbukumbu ya kifo cha kipenzi chao, kwenda kuitembelea hospitali ya
Mwananyamala, hususan wodi aliyolazwa Maneti na kutoa misaada ya
mashuka, kufanya usafi pamoja na kuwasabahi wagonjwa wa wodi hiyo.
Mungu
ana miujiza yake! Unajua kitanda alicholazwa Maneti kilikutwa vipi?
Kilikutwa na maiti ya mgonjwa aliyekuwa amelazwa kitandani hapo na
kufariki muda mchache kabla ya ziara hiyo ya familia ya Maneti
iliyoongozwa na mzazi mwenzie, Kida Waziri, mwanae wa kike Komweta,
mtoto wake wa kiume Maneti Hemed na Sadru ambaye ni mkwewe.
Kwa
vile wadau na familia hiyo walikuwa wakitandika mashuka mapya katika
kila kitanda, wakalazimika kuuhamisha mwili waliokuta kwenye kitanda cha
Maneti na kutandika shuka jipya kisha kuurejesha tena mwili huo
kitandani hapo.
Hadi
anafariki, Maneti alikuwa ni kiongozi wa Vijana Orchestra “Air
Pambamoto”, bendi aliyoiongoza kwa takriban miaka 16, lakini cha ajabu
hakuna mwanamuziki hata mmoja wa bendi hiyo aliyeshiriki katika ziara
hiyo ya Mwananyamala Hospital licha ya kushirikishwa katika kila hatua.
Msafara huo ulijumuisha waandishi, watangazaji na mashabiki wa muziki wa dansi.
Msafara wa kuelekea wodini unaanza
Maria Nyaswa, Hamis Dacota na Sadru wakiandaa mashuka mapya
Msafara sasa uko wodini
Komweta Maneti na Kida Waziri wakitandika kitanda alichofia Maneti
Hiki ndicho kitanda alichofia Hemed Maneti
Usafi unaendelea
Ilikuwa ni simanzi kubwa
Huu ndio msafara mzima uliokwenda Mwananyamala Hospital
CREDIT: SALUTI5.COM
No comments:
Post a Comment