Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akitoa hotuba juzi
jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu.
Arusha. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeelezwa kuwa mfano halisi
unaothibitisha uwezekano wa kuanzishwa na kudumu kwa Shirikisho la Afrika
Mashariki (EAC).
Wakuu wa nchi za EAC waliokutana jijini hapa jana waliipongeza
Tanzania kwa kuadhimisha miaka 50 ya Muungano huo Aprili 26, mwaka huu na
kusema huo ni mfano wa kuigwa kwa ajili ya kusonga mbele katika mikakati yao ya
kuunda shirikisho la EAC. Akizungumza wakati wa mkutano huo, Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya alisema kama Tanganyika na Zanzibar zimeweza kuungana kwa
miaka 50, hakuna sababu ya Shirikisho la EAC kushindikana.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania,
Rais Yoweri Mseveni wa Uganda, makamu wa kwanza wa rais wa Burundi, Prosper
Bozombaza na waziri mkuu wa Rwanda, Dk Pierre Habumuremy.
“Nachukua fursa hii kwa niaba ya viongozi wenzangu kuwapongeza
Rais Kikwete na Watanzania wote kwa kudumisha Muungano wao ambao ni wa kipekee
kwa bara la Afrika,” alisema Rais Kenyetta.
Kiongozi huyo aliwataka Watanzania kuulinda na kuudumisha
Muungano huo ambao ni darasa la namna ya kuungana wakati huu wa mchakato wa
kuanzisha shirikisho la kisiasa la nchi za Afrika Mashariki.
Kwa sasa Tanzania iko kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya na
suala la muundo wa Muungano ndio linaonekana kutawala mjadala huo kutokana na
baadhi ya watu kutaka muundo ubadilike na kuwa wa serikali tatu, huku kundi
linaloongoizwa na chama tawala, CCM likitaka kudumisha muundo wa serikali mbili
ulioboreshwa.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment